Home Uchambuzi RC Paul Makonda ameonyesha njia,tuifuate!

RC Paul Makonda ameonyesha njia,tuifuate!

2429
0
SHARE

MakondaNA JOSEPH SHALUWA

NI fikra mgando kudhani kwamba ili uwe kiongozi ni lazima awe mtu mzima ama mzee. Katika zama hizi uongozi una fursa kubwa hususan kwa vijana. Kipimo cha kuwa kiongozi ni weledi katika utendaji na si vinginevyo.

Nafasi ya kijana katika kuongoza ni kubwa sana zama hizi. Muhimu ni kuwa na uwezo na nia thabiti ya kuongoza. Wapo vijana wengi huko mitaani wana kiu ya kuwa viongozi, lakini wanawaza, itawezekanaje?

Vipo vikwazo mbalimbali vichwani mwao, wanafikiri hili au lile, lakini kubwa zaidi wanajikatisha tamaa kwa sababu mbalimbali. Nataka kuwaambia vijana wenzangu, hakuna sababu ya kujikatisha tamaa. Vijana tuna nguvu na ndiyo taifa la leo na kesho.

Usijishushe thamani kwa namna yoyote ile, jipe moyo kwamba ndani yako kipo kitu kikubwa ambacho unaweza kukifanya kwa ajili ya jamii na nchi yako kwa jumla. Kama kichwani mwako unawaza kwamba kwa sababu wewe ni kijana huna nafasi ya kuongoza, badili fikra hizo kuanzia leo.

Kama unawaza kuwa siasa ni fedha na huwezi kupata nafasi ya kuongoza kwa sababu ya umasikini wako, utakuwa unawaza tofauti sana, tena uko nje ya boksi.

TAZAMA MIFANO

Taarifa za bunge zinaeleza kuwa katika bunge hili la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  idadi ya wabunge vijana wenye kati ya umri wa miaka 21 – 35 ni 47 kati ya wabunge 441 waliopo bungeni hivi sasa.

Hiyo siyo idadi mbaya, maana hapo bado kuna wale ‘vijana walioendelea’ ambao wana kati ya miaka 36 – 45. Wabunge hao ambao wapo wa kuteuliwa na kuchaguliwa na wananchi katika majimbo mbalimbali nchini, wanatoa taswira kwamba kumbe inawezekana kwa kijana kuwa kiongozi katika nchi hii.

Hofu yako ya nini? Hebu fikiria, ikiwa vijana wanaoimba Bongo Fleva, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini) na Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mikumi) wameweza kuuza sera zao kwa wananchi na wakaingia bungeni, inashindikana vipi kwako?

Nimewataja hao, maana wanatoka kwenye muziki wa Bongo Fleva ambao bado kuna fikra kwamba ni muziki wa kihuni. Hiyo itoshe kukufanya ujiamini na uchukue hatua.

Unataka uthubutu wa namna gani? Vijana wameonyesha njia za wazi kabisa kuwa inawezekana kuwa viongozi. Inafurahisha kuona kuwa wapo vijana wengi waliojaribu kurusha karata zao katika chaguzi mbili zilizopita (mwaka 2010 na 2015).

Mbunge wa Kigoma Mjini, kupitia Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Zubeir Kabwe anaweza kuwa mfano mwingine wenye tija. Zitto aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 akitokea Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema.

Alikuwa kijana mdogo sana. Nakumbuka wakati huo, wabunge wadogo zaidi walikuwa wawili – yeye na marehemu Amina Chifupa ambaye aliingia kwa nafasi ya Viti Maalum kutoka Umoja wa Vijana wa CCM  (UVCCM).

Wakati huo, Halima Mdee ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kawe kwa msimu wa pili, aliingia katika chombo hicho cha kutunga sheria kwa tiketi ya Viti Maalum (Wanawake) ndani ya Chadema.

Zitto ndiye aliyeleta mwamko mkubwa zaidi kwa vijana kuingia katika uongozi. Akiwa bungeni, pamoja na umri wake mdogo aliibua hoja nyingi zenye faida kwa serikali na wananchi wa Tanzania.

Mwaka 2010 ndipo idadi kubwa zaidi ya wabunge vijana ilipoongezeka. Felix Mkosamali (Muhambwe – NCCR – Mageuzi), David Kafulila (Kigoma Kusini – NCCR – Mageuzi), Moses Machali (Kasulu Mjini – NCCR – Mageuzi), Dk. Hamisi Kingwangala (Nzega – CCM), Livingstone Lusinde (Mtera – CCM) na wengine wengi.

Kwa bahati nzuri, vijana wote hao waliopata kuwa wabunge (wengine wameingia tena katika bunge hili) wamefanya kazi kubwa wakiwa bungeni na hata majimboni mwao.

Itakumbukwa namna Zitto, Kafulila na marehemu Deo Filikunjombe (Mungu amrehemu), aliyekuwa Mbunge wa Ludewa walivyosimama kidete kwenye sakata la Tegeta Escrow, mwaka jana.

PAUL MAKONDA NI SOMO

Nilipata kumsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kauli yake mwenyewe namna alivyosota katika uongozi. Lakini pia nilimsikia akisimulia namna alivyopitia kwenye changamoto ngumu za kimaisha kutokana na umasikini mkubwa wa familia yake.

Simulizi za Makonda nilizisikia wakati akiwa hana nafasi yoyote ndani ya serikali. Alikuwa Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi katika Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Katika simulizi zake, Makonda alisema hajakata tamaa na hatakata tamaa akiwa na imani ipo siku atakuwa kiongozi mkubwa katika nchi hii.

Miezi michache tu baadaye, Makonda aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, wengi walihoji: kijana mdogo hivi, ataweza kweli? Ataweza kupambana na mikikimikiki katika wilaya hiyo kubwa akiwa hana uzoefu? Wenye kubeza walibeza, wenye kusifia walisifia.

Hata alivyoanza kazi kwa kasi, watu waliishia kusema ni nguvu ya soda tu na asingeweza! Leo hii yuko wapi? Makonda hakumwangusha Rais Jakaya Kikwete aliyemteua wakati ule, akaonyesha namna ambavyo vijana wanaweza kufanya kazi.

Akiwa mkuu wa wilaya, aliwaza zaidi na kufikiria pia kuhusu watoto wa masikini wenye vipaji. Hapo ndipo alipoanzisha Shindano la Kinondoni Star Search ambalo lilisaidia kuinua vipaji vya vijana wengi.

Utendaji wake ulimkuna Rais John Magufuli na akamteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nafasi ambayo anaitumikia mpaka sasa kwa mafanikio makubwa. Kila siku anabuni namna ya kuufaya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa wa mfano.

Bila shaka kwa namna Makonda anavyofanya kazi, inampa moyo Rais na hata wananchi kwa jumla kuwa kumbe vijana wakipewa nafasi wanaweza kufanya makubwa kwa ajili ya nchi yetu. Hii ikupe moyo wewe kijana ambaye unaamini ndani yako kuna mbegu ya uongozi, kuchukua hatua na kuingia kwenye siasa.

Lakini kumbuka, huwezi kuingia kwenye siasa kwa kufuata mkumbo. Zipo sifa za kiongozi. Uzijue na ujitathimini kama kweli unazo na unaweza kuongoza.

Unao ushawishi katika jamii? Unao ufahamu wa mambo na namna ya kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili jamii? Ikiwa majibu yako ni ndiyo, basi unachotakiwa kufanya ni kuchukua hatua!