Home Latest News REA: TURNKEY III ITAFAIDISHA VIJIJI 7,873 KWA UMEME

REA: TURNKEY III ITAFAIDISHA VIJIJI 7,873 KWA UMEME

1369
0
SHARE
Mojawapo ya nyumba zilizounganishiwa umeme maeneo ya vijijini

NA MWANDISHI WETU,

ILI kukabiliana na dha ya usambazaji wa nishati ya umeme vijijini Serikali ilianzisha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao ulianza rasmi kufanya kazi Oktoba 2007, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2003.

Kwa mujibu wa taarifa ya maeneo rasmi ya kiserikali kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tanzania Bara ina jumla ya vijiji 12,268 ambapo vilivyofikiwa na umeme hadi Juni 2016 vilikuwa 4,395 sawa na asilimia thelathini na sita  asilimia 35.

REA hadi sasa imetekeleza miradi kabambe ya usambazaji nishati vijijini ambako katika mradi wa awamu ya pili ulioanza Oktoba 2013 hadi Disemba mwaka jana umewezesha jumla ya vijiji 4,395 kuunganishwa na huduma ya umeme sawa na asilimia 36 ya vijiji vyote 12,268 vya Tanzania Bara wakati lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara ifikapo mwaka 2021; na kuongeza idadi ya wanachi waopata huduma ya umeme hadi asilimia 85 mwaka 2025 na asilimia 100 Mwaka 2030.

Hata hivyo sasa, mradi wa awamu ya tatu umeanza kutekelezwa  kwa ushirikiano kati ya TANESCO na REA. Katika mpango huo serikali ilielekeza mpango wa awamu ya tatu ufikishe huduma ya umeme kwenye vijiji vyote nchini ambavyo bado havijafikiwa na umeme.

Akifafanua kwa kina namna mradi huo wa awamu ya tatu utakavyotekelezwa, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Boniface Nyamo Hanga anasema wakala umeweka lengo la kufikisha umeme wa gridi na nje ya gridi (off-grid) kwenye vijiji 7,873 ambavyo bado havijafikiwa na umeme katika kipindi cha miaka mitano (2016/17-2020/21).

Anasema kati ya vijiji hivyo, vijiji 7,697 vimepangwa kupelekewa umeme wa gridi na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi (off-grid) utokanao na nishati jadidifu kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuvipelekea umeme kwa gharama nafuu kwa sasa. Maeneo kwenye vijiji ambavyo tayari vina miundombinu ya msingi lakini wananchi au baadhi ya vitongoji/mitaa havijapatiwa umeme wataunganishwa kwenye mradi wa Densification utakaotekelezwa kama sehemu ya Mradi Kabambe wa Awamu ya Tatu.

Aidha, anaongeza kuwa miradi ya mpango kabambe wa awamu ya tatu inajumuisha: miradi mkubwa wa Grid Extension unaolenga kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa kabisa na miundombinu ya umeme wa gridi, Miradi ya Densification ya kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo miundombinu ya kupelekak umeme imefika.

“Pia mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyo pembezoni mwa miradi ya kusafirisha umeme mkubwa (High Voltage Transmission Lines) ya Backborne Transmission Investment Project (BTIP) kutoka Iringa hadi Shinyanga katika wilaya za Iringa, Mpwapwa, Chamwino, Bahi, Manyoni, Singida, Iramba, Igunga, Kishapu na Shinyanga. Mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyo pembezoni mwa miradi ya kusafirisha umeme mkubwa kutoka Makambako hadi Songea na kuhusisha wilaya za Wanging’ombe, Njombe, Songea, Ludewa, Nambumbo na Mbinga na Miradi ya kuendeleza na kusambaza nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi ambayo ni vigumu kufikiwa na umeme wa gridi,” anasema.

Hata hivyo, anasema hadi sasa maandalizi na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa chini ya mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya Tatu yapo katika hatua mbalimbali ambayo ni mradi wa kupeleka umeme wa gridi kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme:

“Orodha ya vijiji hivyo imekamilika na taratibu za ununuzi zimeanza ambapo tathmini ya Prequalification imekamilika na kupitishwa na Bodi ya Zabuni kwa ajili ya hatua zaidi za ununuzi. Mradi wa Densification unahusu kuongeza wigo wa kusambaza umeke kwenye maeneo ambayo tayari  yamefikiwa na miundombinu ya umeme wa gridi. Awamu ya kwanza inatekelezwa kwenye mikoa 6 ya Pwani, Tanga, Arusha, Iringa, Mbeya na Mara kwa ufadhili wa Serikali ya Norway.

“Tayari wakandarasi wameshasaini mikataba ya utekelezaji wa miradi umeanza. Maandalizi ya Awamu ya Pili ya Densification kwa ushirikiano kati ya TANESCO na Wakala. Mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyo pembezoni mwa Mkuza wa Mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV kutoka Iringa hadi Shinyanga  (BTIP) utatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali ya Sweden na Norway; na tayari taratibu za ununuzi zimeanza.

“Zabuni zimeshapokelewa na kufanyiwa uchambuzi, na inatarajiwa kuwa wakandarazi wataanza kazi mwezi Februari 2017. Ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme vijijini chini ya mradi wa Makambako hadi Songea umekwishaanza. Miradi ya kuendeleza na kusambaza nishati jadidifu kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi – Wakala ulitoa tangazo la kwanza (1st Call for Proposals) Novemba, 4 mwaka jana kwa ajili ya kushindanisha uendelezaji nishati jadidifu kwenye maeneo ya nje ya Gridi (off-grid mini grids) unaofadhiriwa na Serikali za Sweden na Uingereza. Jumla ya waombaji takribani 300 wamewasilisha maombi yao na uchambuzi wa maombi yaliyopokelewa umekamilika,” anasema.

 Jinsi ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mradi

Mkurugenzi huyo anasema ili kufanikisha utekelezaji wa Mradi Kabambe wa kusambaza umeme vijijini – Awamu ya Tatu (Turnkey III), wakala unatekeleza yafuatayo kukabili changamoto zilizojitokeza na kuchelewesha kukamilika kwa mradi wa Awamu ya Pili.

  1. Kuimarisha usanifu wa mradi na usimamizi wa mradi kuwa kuingia Mikataba na Kampuni za usimamizi ambao kila kanda ya TANESCO Kikanda na mikoa katika Kanda husika. Wakala umeingia Mkataba na Kampuni ya  SMEC International Ltd kwa ajili ya usanifu wa mradi, upimaji wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni ya miradi ya Awamu ya Tatu.
  2. Kuzishirikisha serikali za vijiji katika ktuenga maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme ili kuondoa madai ya fidia.
  3. Kushirikisha viongozi na wananchi kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu ikizingatiwa imejengwa kwa fedha za wananchi wenyewe (Walipa Kodi).
  4. REA, TANESCO na wakandarasi pamoja na viongozi wa wananchi kuhamasisha wananchi kutenga fedha ili kutandaza nyaya katika majengo yao.
  5. Kuhamasisha uunganishaji wateja ikiwa ni pamoja na matumizi ya UMETA (Ready Board), na matumizi ya umeme kwa shughuli za kijamii na uzalishaji mali; na
  6. Ujenzi wa miundombinu ya misongo ya kilovolti 220kV na 132kV (High Vokltage Backbone Transmission Lines) pamoja na vito vya kupozea umeme (Distribution Sub-Stations) kwa ajili ya kuboresha umeme unaosambazwa vijijini hasa maeneo ambayo miundombinu ya kilovolti 33 imeelemewa.

Uhaba wa fedha changamoto inayozorotesha ufanisi

Anasema pamoja na mafanikio yaliyopatikana wakala unakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa fedha za kutosha kugharamia utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini ili kukidhi ongezeko kutokana na mahitaji ya wananchi, Kuongeza kasi ya uunganishaji wateja kwenye maeneo ambapo ujenzi wa miundombinu umekamilika, Kuhamasisha wananchi kutenga maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme yasiyohitaji fidia ili kuharakisha  huduma ya umeme kuwafikia na kwa gharama nafuu.

“Kuhamasisha ongezeko la ushiriki wa sekta binafsi kwenye miradi ya nishati. Kuhamasisha wananchi kutumia umeme kwa ajili ya shughuli za usalishaji mali ili kuboresha maisha yao; na kuhakiki usalama wa miundombinu iliyokamilika kutokana na vitendo vya uharibifu. Wakala unaomba ushiriki wa vyombo vya habari ili kuepusha uharibifu wa miundombinu hii ambayo ni mali ya umma.

Kwa sababu inakadiriwa kuwa miradi ya kusambaza umeme wa gridi itagharimu takribani sh bilioni 7,000. Kati ya fedha hizo kiasi cha sh bilioni 4,000 ni kwa ajili ya kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikishiwa umeme katika mikoa na wilaya zote; na kiasi cha sh bilioni 3,000 kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo yameshafikiwa na miundombinu ya umeme lakini baadhi ya vitongoji na taasisi bado havijafikiwa na umeme.

“Gharama halisi zitabainishwa baada ya zabuni kupokelewa na kuchambuliwa. Fedha hizi zitatoka kwenye Bajeti ya Maendeleo ya Serikali kila Mwaka; tozo kwenye petroli na mafuta ya taa, tozo ya umeme na michango ya Washirika wa Maendeleo.