Home Latest News Rekodi zilizowekwa EPL 2018-19

Rekodi zilizowekwa EPL 2018-19

2915
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

HATIMAYE msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL) ulifikia ukomo wake mwishoni mwa wiki iliyopita kwa Manchester City kutwaa ubingwa, ikiwa ni baada ya vita ya mrefu dhidi ya Liverpool.

Wakati ubingwa ukielekea jijini Manchester, tayari vigogo Man United na Arsenal walishathibitika kuwa nje ya timu nne za juu ‘top four’, wakizidiwa kete na Tottenham na Chelsea zilizo nyuma ya Liverpool na Man City.

Hivyo basi, ili kutinga Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, Arsenal watalazimika kulibeba taji la Ligi ya Europa kwa kuwadunda Chelsea katika mchezo wa fainali utakaochezwa Mei 29, mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa licha ya kutokuwa kwenye kiwango chao katikati ya msimu huu wa EPL, bado waliweza kumaliza wakiwa ndani ya zile nne za juu, hivyo hawana presha juu ya Ligi ya Mabingwa.

Lakini, hata kama hawana wasiwasi na tiketi yao katika michuano hiyo, ukweli ni kwamba watalihitaji taji la Ligi ya Europa kwa kuwa msimu huu umemalizika wakiwa hawana kikombe chochote.

Man City, ambao waliwachapa Brighton mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho, walilibeba taji wakiwa na pointi 98 dhidi ya 97 walizokuwa nazo Liverpool.

Wakati timu 20 zikiwa dimbani Jumapili ya wiki iliyopita, zipo rekodi nyingi zilizokuwa zikiwekwa kama zinavyoanikwa na makala haya.

Kwa kuanza, Liverpool imekuwa timu ya kwanza kumaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 97, idadi ambayo haijawahi kufikiwa na timu iliyokosa ubingwa katika historia ya EPL.

Pili, kwa mara ya kwanza, timu zinazofukuzia ubingwa zilibadilishana mara nyingi (32) pale kileleni. Kabla ya hapo, ni msimu 2001-2002 ndiyo ulioshuhudia timu zikipishana kileleni mara nyingi (28).

Tatu, ni kwa mara ya kwanza timu mbili za juu zimekusanya idadi kubwa zaidi ya pointi (195). Awali, rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na msimu wa 2017-2018, ambapo bingwa na ile iliyoshika nafasi ya pili zilikuwa na pointi 181.

Nne, imetokea kwa mara ya kwanza kuona idadi kubwa zaidi ya mabao (1,072), ikizingatiwa kuwa rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na msimu wa 2011-12 ni ligi kumalizika ikiwa na mabao 1,018.

Tano, akiwa na umri wa miaka 20 tu, beki wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee wa eneo hilo kumaliza msimu akiwa na pasi za mabao ‘asisti’ 13.

Sita, baada ya Mohamed Salah, Sadio Mane na Pierre-Emerick Aubameyang kugawana kiatu kwa kila mmoja kuzitikisa nyavu mara 21, ni kwa mara ya kwanza tangu miaka nane iliyopita kushuhudia tuzo hiyo ikichukuliwa kwa idadi ndogo ya mabao.

Saba, mkali wa Man City, Sergio Aguero, aliifikia rekodi ya mpachikaji mabao wa zamani wa Newcastle, Alan Shearer, baada ya kufikisha ‘hat-trick’ 11 ndani ya msimu mmoja wa EPL.

Nane, Mike Dean alifikisha kadi nyekundu 100, hivyo kuwa mwamuzi wa kwanza kuwa na idadi hiyo katika historia ya EPL.

Tisa, makocha sita walivicha vibarua vyao, Fulham wakifanya hivyo mara mbili, Southampton, Manchester United, Huddersfield na Leicester. Hiyo ni sawa na msimu wa 2009-10, ikiwa ni idadi ndogo tangu msimu wa 2005-06.

Mwisho, nyota wa Chelsea anayehusishwa na mpango wa kwenda Real Madrid, Eden Hazard, ndiye aliyenyakua tuzo ya mkali wa asisti msimu huu baada ya pasi zake za mwisho kuzaa mabao 15.