Home Makala RIPOTI HASI ZA CAG: WANANCHI WENGI HAWAJALI AU HAWAELEWI MAANA YAKE

RIPOTI HASI ZA CAG: WANANCHI WENGI HAWAJALI AU HAWAELEWI MAANA YAKE

644
0
SHARE
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Juma Assad akikabidhi ripoti kwa Rais John Magufuli

NA HILAL K. SUED


Wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli anafungua miradi kadhaa ya maendeleo jijini Dar es Salaam, ukiwemo ule mradi mkubwa wa Reli ya Standard Gauge Railway (SGR), Watanzania walikuwa wakitafakari Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) kwa mwaka 2015-2016.

Ripoti hii kama kawaida ya zile zilizotangulia miaka nenda miaka rudi, ilibeba ujumbe wa hali hasi kuhusu utawala; jinsi wachache wenye ushawishi mkubwa wanavyowaibia wananchi fedha na mali nyingine zilizopatikana kwa kodi zao, wakiwasababishia kukosa huduma bora za jamii kama vile elimu, afya na maji.

Wanafanya hivi bila mamlaka husika kukomesha tabia hii au kujali chochote. Kwa kifupi ripoti hizo zimekuwa zikionyesha uozo uliopitiliza katika mfumo wa udhibiti wa fedha na mali za umma na namna Serikali inavyougua ukiziwi na upofu.

Itakuwa vyema kueleza kwamba uozo huo unatoa sababu ya ugumu uliopo kwa nchi kupiga hatua za maana za maendeleo na kupunguza umasikini, ukiachilia mbali kuwa ushahidi mkubwa wa kuwepo ufisadi hasa katika safu za juu za utawala, hali ambayo Serikali huwa inapata kigugumizi kuikubali, achilia mbali kuchukua hatua.

Na haitashangaza iwapo huko mbele hiyo miradi aliyozindua Rais Magufuli wiki iliyopita, ikaainishwa katika ripoti zijazo za CAG kwamba sehemu ya fedha zake zilifisadiwa na wachache. Kama haitashangaza kutokana na huu mwenendo.

Kujua namna vigogo katika utawala walivyo na ndimi mbili katika kuyaelezea madudu ya ufisadi kwa upande mmoja na kuyashughulikia kwa upande mwingine, naomba niwarudishe zaidi ya miaka miwili nyuma hadi mwishoni mwa mwaka 2014, wakati ule Ludovick Utouh, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali wa zamani alipostaafu.

Wiki mbili baada ya kustaafu, Utouh alitoa kauli iliyoshtua sana jamii yetu  hasa kwa wale wanaochukizwa na vitendo vya rushwa na ufisadi na hata kuifanya vita dhidi ya kansa hiyo inayoendeshwa na vyombo vya Serikali kuonekana ni dhihaka kubwa.

Katika mahojiano na gazeti la Nipashe, Utouh alisema wakati alipokuwa analichunguza suala la wizi wa mabilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje ya EPA, alikuwa akitafutwa na mmoja wa watuhumiwa wa mabilioni hayo ili ampe mlungula wa Sh 30 bilioni ili amkabidhi nakala ya ripoti ya uchunguzi huo kabla hajaiwasilisha serikalini.

Alisema hiyo hali ya ‘kutafutwa na mtoa mlungula’ ili akabidhiwe ‘mzigo mnono’ kwa kazi iliyoonekana ni rahisi tu, ilimtia hofu sana na hadi akawa ni mtu wa kujifichaficha tu kwa kuogopa kudhurika kutokana na kitendo chake cha kukataa rushwa hiyo iliyokaa nje nje.

Nilipatwa ugumu sana kuamini kauli yake hiyo, hasa kutokana na kiwango kikubwa sana cha mlungula wenyewe, lakini baada ya kutafakari sana hasa mazingira ya mpango mzima wa wizi wa EPA ulivyokuwa ukiibuliwa na jinsi hapo awali ulivyokuwa unafunikwa, nikaona inawezekana ni kweli.

Kwanza kabisa suala hili la Utouh linaonyesha jinsi gani baadhi ya watu katika jamii walivyokuwa tayari kutapanya fedha kwa lengo la kuficha uovu wao unaochangia umasikini nchini.

Lakini kikubwa zaidi ni jinsi maovu haya yanayotanda katika ngazi za juu kabisa za uongozi hunyamaziwa wakati yanapotokea. Kwani bado sijapata mantiki ya kuridhisha kabisa kwa vipi Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anyamazie mpango huo uliokuwa unaandaliwa kuhusu yeye bila kuripoti katika vyombo husika, hususan Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)?

Hapa nataka kusema kwamba kama kweli kazi kuu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni kuchunguza wizi wa fedha na mali za umma na kuhimiza ukomeshaji wa tabia hiyo, kwa vipi alizinyamazia njama zilizokuwa zinasukwa na mmoja wa wezi wa fedha za umma kwa lengo la kumnasua mwizi huyo?

Busara na uadilifu kwa ofisa mkuu wa idara hiyo nyeti ya Serikali ilimpasa aripoti tukio hilo kwa vyombo husika; TAKUKURU, Polisi au hata Usalama wa Taifa (TISS). Aidha, mtego mahsusi na madhubuti ungeweza kusukwa na vyombo husika nilivyovitaja kwa lengo la kumnasa huyo mtoa rushwa mtarajiwa.

Lakini hili halikufanyika ingawa mitego ya aina hii hufanyika sana katika ishu zinazotokea katika ngazi za chini na kwa viwango vidogo vya fedha zinazofisidiwa.

Na hapo hapo linakuja swali: ni nani huikagua taasisi hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali? Wenyewe ndiyo huyakagua mahesabu yao?

Tukirudi kwenye mada husika ya madudu katika ripoti za kila mwaka za taasisi hiyo, huwa najiuliza iwapo wananchi wanaelewa maana yake.Katika kampeni za uchaguzi za mwaka juzi (2015), baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani walikuwa wanagusia suala hili  kwa namna ya kuwaambia wapiga kura umuhimu wa kwamba muda umefika kutaka mabadiliko.

Ujumbe ulikuwa ni kwamba Serikali ya chama kilichopo madarakani kinaonekana kushindwa kudhibiti ufisadi na wizi wa fedha na mali za umma na hivyo wananchi waliombwa kujiletea mabadiliko kupitia sanduku la kura. Ni vigumu kupinga kuwepo kwa hali hii ya ‘kushindwa’ kwani tungekuwa tumeshaanza kuona kuimarika kwa udhibiti wa fedha na mali za umma katika ripoti za kila mwaka za CAG. Badala yake hali inazidi kuwa mbaya.

Kwa nchi nyingine zenye demokrasia iliyopevuka, ni vigumu kuamini kwamba chama tawala kingekuwa kinashinda uchaguzi katika hali ya namna hii labda tu sababu ni kwamba ama wananchi  kama nilivyosema hapo juu, hawaelewi kabisa haya mambo na athari kwao ama huwa wanaibiwa katika chaguzi.