Home Habari RIPOTI YA CAG: ACT-Wazalendo haiko salama

RIPOTI YA CAG: ACT-Wazalendo haiko salama

395
0
SHARE

LEONARD MANG’OHA

CHAMA cha ACT-Wazalendo hakiko salama sana kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG), iliyowekwa hadharani wiki iliyopita, kutokana na hesabu zake za mwaka wa fedha 2017/18 kupata hati yenye shaka.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ukurasa wa 68, sura ya pili imeonesha kuwa mapato na matumizi ya ACT-Wazalendo hayakuwa na nyaraka muhimu.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa mapato na matumizi hayakuwa na nyaraka muhimu, taarifa ya utendaji wa fedha pamoja na nukuu namba12 ya taarifa za fedha ilionesha michango ya hiari yashilingi 8,875,000; hata hivyo kiasi hicho hakikuwa na nyaraka na vielelezo muhimu vya kuthibitisha usahihi wake.

Vilevile taarifa za fedha zilionesha malipo ya shilingi 1,200,000 kwenda Zanzibari, lakini hakukuwa na nyaraka yeyote iliyowezesha kuthibitisha usahihi na uhalali wake.

Mbali na ACT-Wazalendo pia chama cha NCCR-Mageuzi kinachoongozwa na Mwenyekiti wake James Mbatia nacho kimekumbana na hati yenye shaka kutokana na taarifa zake za  fedha pamoja na nukuu namba 7 ya taarifa hizo kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2018 kuonesha bakaa ya pesa taslimu kiasi cha Shilingi2,777,975, hata hivyo hakukuwa na nyaraka yeyote iliyowezesha kuthibitisha kama kweli kiasi hicho kilikuwepo tarehe hiyo.

“Taarifa ya mizania ya hesabu kufikia tarehe 30 June 2018 ilionesha madeni ya kiasi cha shilingi 85,366,000; madeni hayo hayakuwa na nyaraka zozote za kuweza kuthibitisha uhalali wake kama vile hati za madai, n.k. Kiasi cha shilingi 1,500,000 kililipwa kwa Kituo cha Demokrasia Tanzania kama marejesho ya mkopo, hata hivyo hakukuwa na nyaraka zozote zinazoonyesha uhalali wa mkopo huo na marejesho yake.

Kwa upande wake chama cha Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kinachoongozwa na Hashim Rungwe chenywe kimekutwa na mapungufu kwenye taarifa za fedha Jedwali la mabadiliko ya mali, mitambo na vifaa (nukuu namba12) ilionesha kiasi cha uchakavu cha shilingi 1,350,000 ambacho kilitakuwa kitolewe kwenye gharama ya mali, mitambo na vifaa, badala yake kilijumlishwa.

Pia, kiasi cha uchakavu kilichoripotiwa kwenye taarifa ya utendaji wa fedha kilikuwa shilingi 1, 300,000 badala ya shilingi 1350,000 kama kilivyokuwa kwenye nukuu namba 12.

Aidha chama hicho hakikuandaa taarifa ya mabadiliko ya mtaji, pia taarifa za ulinganisho za mwaka jana hazikuoneshwa kwenye taarifa za fedha kama inavyotakiwa na Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu (IAS 1). Baadhi ya taarifa zilizooneshwa kwenye uso wa taarifa za fedha hazikuwa na mchanganuo (nukuu) wa kuelezea taarifa hizo, mfano, hakukuwa na mchanganuo wa wadaiwa wa kiasi cha Shilingi 2,600,000 walioripotiwa kwenye taarifa za fedha.

Viambatisho356Viambatisho -Sura ya PiliMalipo ya shilingi 7,069,000 hayakuwa na hatiza malipo, hivyo hatukuweza kuthibitisha uhalali wa malipo hayo.

Ripoti ya CAG kwa upande wa vyama vya siasa imeweka wazi kuwa katika hati za ukaguzi za vyama vya Siasa 19 vyenye usajili wa kudumu ni vyama 14 pekee ndivyo vilivyoandaa na kuwasilisha taarifa zake za Fedha kwa ajili ya Ukaguzi kwa mwaka huu wa fedha ikilinganisha na vyama 10 vilivyokaguliwa mwaka uliopita, 2016/17.

Kati ya vyama vya Siasa 10 vilivyowasilisha Taarifa za Fedha mwaka uliopita, vyama vitatu (3) havikuwasilisha Taarifa za Fedha mwaka huu. Kwa upande mwingine, vyama vitatu (3) vya siasa ambavyo havikuwahi kukaguliwa miaka ya nyuma lakini vimekaguliwa mwaka huu havikuandaa Taarifa za Fedha kwa miaka hiyo ya nyuma isipokuwa kwa vyama vinne (4).

Ripoti imefafanua kuwa kwa sababu ya mpishano huo, imekuwa vigumu sana kuandaa mwenendo ili kubainisha kama kuna maboresho ya maandalizi ya taarifa za fedha au la.

Pia, kuwasilisha taarifa za fedha za miaka ya nyuma pamoja na za mwaka huu kumeongeza mzigo wa ziada katika kufanya ukaguzi wa miamala ya miaka miwili au mitatu.

Mpishano huo unahitaji hatua za haraka kutoka Serikalini (Msajili wa Vyama vya Siasa) kuhakikisha kuwa, vyama vya siasa vilivyosajiliwa vinaandaa na kuwasilisha taarifa za fedha kama inavyotakiwa kisheria.

Kwa ujumla, vyama vya siasa vimeendelea kufanya vibaya katika maandalizi ya taarifa za fedha ambapo kati ya vyama 14 vilivyokaguliwa mwaka huu wa fedha, ni vyama vitatu (3) tu vimepata Hati inayoridhisha (safi), ikiwa ni idadi sawa na mwaka uliopita. Vyama vinne (4) vimepata hati yenye shaka, hii ni sawa na mwaka uliopita. Vyama vitano (5) vimepata hati mbaya; wakati vyama viwili (2) vimepata Hati isiyoridhisha.

Hati mbaya na hati isiyoridhisha ni hati chafu ambazo zinaonesha kuwa taarifa za fedha zilizoandaliwa haziwezi kutumiwa kwa ajili ya kufanya maamuzi mbalimbali kwani zinakuwa sio sahihi.

Matokeo mabaya ya vyama vya siasa kwa kiasi kikubwa yalisababishwa na ukosefu wa mwongozo kwa vyama vya siasa.

Vyama vilivyokaguliwa ni Chadema, UDP, CCM, DP, CCK, ADC, TLP, Demokrasia Makini, ADA- TADEA, AAFP, SAU, NLD, NRA, UMD, CHAUMA, UDP, ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi

ACT-WAKIRI

Katibu Mwenezi wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu,  alisema wanakubaliana na ripoti ya CAG na wanachokifanya wao ni kuhakikisha wanazifanyia kazi changamoto hizo kwa manufaa ya chama chao na siasa za nchi kwa ujumla.

Alisema wao  kama chama kinachoitetea na kuilinda ofisi ya CAG hakiwezi kupinga mambo yaliyoibuliwa katika ripoti hiyo kuhusu chama chao bali wanayachukua kama changamoto ili wayafanyie kazi.

Shaibu alisema chama chao kimeyapokea mambo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuimarisha mifumo ya ndani ya chama ili kipate hati safi.

“Sisi kama chama cha siasa ambacho kinaitetea na kuilinda ofisi ya CAG, hakiwezi kika-over defend’ mambo ambayo yameibuliwa kama ni kweli katika ripoti ya CAG. Tunalipokea tutajiimarisha ili mbeleni tuwe na hati safi.

 “Labda tujipe moyo hatujapata hati chafu kwa sababu tukitaja katika mlolongo wa hati isiyoridhisha haimaanishi hati uliyonayo ni chafu. Ukitazama mwaka jana tulikuwa na hati inayoridhisha, mwaka juzi tulikuwa na hati inayoridhisha, wakati huu tuna isiyoridhisha kwa hiyo mambo hayo tutayafanyia kazi” alisema Shaibu.

Akizungumzia  baadhi ya mambo yaliyosababisha chama hicho kupata hati isiyoridhisha ambayo ni  kutotumia risiti za kielektroniki katika shughuli mbalimbali za chama hicho, alisema  jambo hawawezi kulikataa bali wanalichukua kama changamoto ya kuimarisha utendaji kazi wa chama hicho.

Shaibu alisema kwa bahati mbaya baadhi ya huduma zinazotolewa na vyama vya siasa ni vigumu kupata risiti za kielektroniki hasa pale wanapokuwa katika shughuli za uenezi wa chama maeneo mbalimbali nchini.

Sababu nyingine aliyoitolea ufafanuzi ni ya kutofanyika vikao vya mara kwa mara vya bodi ya wadhamini ambao ndiyo wanaosimamia rasilimali na madeni ya chama jambo ambalo amedai kuwa wanalipokea kama changamoto ya kuitisha vikao hivyo.

Shaibu alisema hadi sasa chama hicho kimepata mhutasari wa ripoti hiyo ya CAG lakini hakijaipata ripoti yenyewe ili kuipitia kwa mapana zaidi kuona ni mambo gani mengine yaliyosababisha wapate hati isiyoridhisha kwa sababu baadhi ya masuala ya ukaguzi ni ya kitaalamu.

WASOMI WASHAURI

Wakizungumzia mvutano wa Spika wa Bunge Job Nduga na CAG, Profesa Mussa Assad uliosababisha kuibuika kwa shinikizo la kujiuzulu kwa CAG kwa madai kuwa anampa wakati mgumu Rais wasomi wamesema msimamo huo hauna tioja kwa taifa.

Katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam hivi karibuni Spika Ndugai alidai kuwa hana chuki binafsi na Profesa Assad na ni rafiki yake lakini ugomvi wao uko katika matamshi na lugha za udhalilishaji na kwamba kitendo chake cha kuendelea kutumia neno dhaifu ni kielelezo kuwa hiyo ni dharau na kejeli kwa mhimili huo.

Ndugai alisema tatizo lao ni maneno ambayo Profesa Assad aliyasema alipokuwa nchini Marekani na na kuyarudia hivi karibuni katika mkutano na waandishi na kusisitiza kuwa ataendelea kuyatumia maneno ambayo wao waliyakataa.

Spika Ndugai alimtaka Profesa Assad kuacha matusi anayoyatoa ama kwa kujua au kwa kutokujua kwa sababu anampa Rais wakati mgumu.

DK. BISIMBA

Mkurugenzi Mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema Spika hakupaswa kushutumu CAG kwa sababu kama Rais angekuwa anataka CAG ajiuzulu angefanya hivyo yeye mwenyewe.

Dk. Bisimba alisema Spika anamshutumu CAG kwa sababu katika ripoti yake ya ukaguzi kuna mamo yanayomhusu yeye binafsi yamegushwa.

“Hiyo inaonesha moja kwa moja kwamba hayuko ojective. Shida siyo hilo neno dhaifu shida. Ni kwamba wamekamatwa sana na hawajazoea viongozi wa nchini hii mtu kuonesha maovu yao kweupe hicho ndicho ninachodhani kuwa kinamsumbua kuliko hilo neno dhaifu.

“Hilo neno dhaifu halibadilishi chochote kwa Bunge. Kama Bunge siyo dhaifu na huyo bwana akasema Bunge ni dhaifu mimi sioni kama ni tatizo la kufanya mtu mpaka aambiwe ajiuzulu.

“Hiyo ndiyo picha iliyopo kwa sababu hilo neno dhaifu lina shida gani hadi lifanye CAG aambiwe ajiuzulu wakati anafanya kazi zake vizuri na watu tunaiona ni nzuiri inasaidia kufichua mambo ambayo tunayaona hayakukaa vizuri na ndiyo kazi ya CAG kuangalia yale ambayo hayakukaa vizuri,” alisema Dk. Bisimba.

Dk. Bisimba alisema tangu ofisi ya CAG imaenza kufanya kazi vizuri yameshuhudiwa mabadiliko mbalimbali i8kiwamo halmashauri zilizokuwa na hati chafu za ukaguzi zimefanikiwa kupata hati nsafi baada ya uoneshwa kasoro zao.

“Kama CAG anafanya kazi yake vizuri alafu mtu ambaye na yeye yuko implicated kwenye hiyo ripoti anasema hivyo, inaonesha kwamba ndicho kimnachomfanya azungumze siyo hilo neno dhaifu isipokuwa ni kwa sababu tu wamekamatwa” alisema Dk. Bisimba.

Alisema ili kumaliza mgogoro huo inampasa Spika arudishe akili yake nyuma na afahamu kuwa CAG yuko kazini na ikiwa hilo neno linamuuma yeye ndiye ajiuzulu na si kumtaka CAG ajiuzulu.

PROF. MPANGALA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha, (Ruco), Gaudence Mpangala, alisema yawezekana nyuma ya pazia ya suala hilo la CAG kuwa na msimamo na kuwa mkweli katika kuibua mambo dhaifu ya Serikali, kuna shinikizo ang’olewe ili awekwe ambaye hatakuwa tishio kwa Serikali.

Profesa Mpangala alisema nyuma ya pazia jambo hilo linawezekana kwa sababu ripoti za nyuma na hii ya sasa zote zimekuwa na mwelekeo huo.

“Sina hakika kuwa mgogoro huu unatokana ripoti yake ya hivi karibuni. Nafikiri tu tarajio la Spika kwamba huyu bwana ajiuluzu kutokana na mgongano wao, sasa huu mgongano umeshambuliwa umeonyesha madhaifu mengi ya Serikali.

“Lakini hiyo siyo sababu ya kumfanya yeye ajiuzulu kwa sababu hilo ndilo linaloonesha kuwa yeye ni mkaguzi mwenye msimamo asiyefanya kazi kwa kuogopa bali kwa maslahi ya Taifa,” alisema Mpangala.

Alisema kwa sababu Bunge ni chombo cha wananchi hivyo kwa chombo hicho wangemshukuru na kumwomba atoe ufafanuzi wao ukoje ili waweze kujisahihisha na si kumshutumu CAG.

 “Kama Bunge ambalo lina misingi ya demokrasia na utawala bora wangemshukuru kwamba awaelekeze udhaifu wao ukoje wajisahihishe, sasa kuanza kugombana nao mara wamwite wamhoji, mara watoe maamuzi lakini wadau wengi utakuta wanamsapoti CAG.

“Tegemeo la Ndugai ilikuwa ni wao wakichukua hatua hizo basi atajiuzulu kwa hiyo wakaamua kufanya ule uamuzi wa kutofanya kazi na Assad wakitegemea kwa hatua hiyo atajiuzulu, atachaguliwa mwingine. Sasa kule kutojiuzulu na kuona wadau wengi wanamsapoti nafikiri kunalichanganya zaidi Bunge hasa Spika.

“Ndiyo maana ‘anaropokaropoka’ maneno mengi mara akaripoti kwa Rais, anamsumbua Rais anampa wakati mgumu, hivi jukumu lake ni kumzungumzia Rais, hilo siyo jukumu lake. Labda yeye alitarajia kwa kuchukua hizo hatua kwa Assad basi Assad ama atajiuzulu ama Rais atamtumbua ndilo lilikuwa tegemeo lake.

Sasa kwa sababu hajajiuzulu na wala Rais hajamtumbua hilo linamchanganya zaidi, na ukiangalia ripoti alishindwa kuikataa, sasa unaposema hufanyi kazi na Assad maana yake nini na ripoti yake ameipokea,” alisema Profesa Mpangala.

Ili kumaliza mzozo huo Profesa Mpangala alisema kinachopaswa kufanyika ni Bunge kuamua kuwa jambo hilo liishe na waafikiane na Profesa Assad kwamba wafanye kazi pamoja kwa sababu sasa ni kama wanajichanganya zaidi.

Alisema kwa sababu Bunge ni chombo cha wananchi kinapaswa kilinda heshima yake, kwa kuonesha kuwa siyo chombo dhaifu badala ya kuendelea kufanya uamuzi ambao wananchi wanaowawakilisha wanabaki wanashangaa.

DK. BANA: CAG ANGEKUBALI YAISHE

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema kinachoendelea si shinikizo la kumtaka kiongozi huyo ajiuzulu bali ni suala la maadili, kauli na nidhamu na kwamba endapo CAG alipoitwa bungeni angekubali kufuta kauli yake lingekwisha.

“Suala si ripoti kwa sababu Spika anazifanyia kazi na Serikali inazifanyia kazi, suala lililoleta songombingo hii ni suala na kimaadili na msimamo kama CAG angefika bungeni akafuta kauli ya Bunge ni dhaifu. Kwa sababu neno dhaifu ndilo lililowakera wabunge na ndilo chimbuko ya haya yote,” alisema Dk. Bana.

Dk. Bana alisema neno hilo limemkera zaidi Spika kwa sababu hata alipokuwa akiwasilisha ripoti yake alisisitiza kuwa ataendelea kulitumia.

“Hata ungekuwa wewe ungeweza ‘ku-react’ vingingevyo. Nadhani suala ni CAG kutokuwa na msimamo ambao ni reflexible kidogo na kufahamu kwamba anafanya kazi na wanasiasa na ushindani katika hili hauna tija.  Sawa una msimamo ujumbe umekwisha ufikisha.

“Wewe ni mtumishi wa umma si mwanasiasa zingatia maadili na viapo vyako kama mtumishi wa umma. Mtumishi wa umma aina ya CAG anafanya kazi kwa maagizo zaidi ya wanasiasa, unateuliwa na wanasiasa na ukishateuliwa unawajibika kwa wanasiasa” alisema Dk. Bana.