Home Habari SAADA MKUYA: KODI ILINITOA MACHOZI ZANZIBAR

SAADA MKUYA: KODI ILINITOA MACHOZI ZANZIBAR

2120
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


WAZIRI wa zamani wa Fedha, Saada Mkuya ameweka wazi kuwa kodi kubwa kwenye umeme wa Zanzibar, ulimfanya kutoa machozi bungeni, jijini Dodoma.

Mkuya alimwaga machozi wakati wa mjadala wa vikao vya Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.

Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa mwanamke wa pili Mzanzibari kuongoza Wizara ya Fedha, baada ya Zakia Meghji, alifikia hatua ya kutokwa machozi baada Serikali kuweka wazi kuwa ufumbuzi wa tatizo la Zanzibar kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya umeme mara mbili halitapata ufumbuzi kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018.

Katika mazungumzo yake na RAI wiki iliyopita, pamoja na mambo mengine alisema suala hilo lilimuumiza kiasi cha kumfanya amwage machozi.

Yafuatayo ni mahojiano maalum na mwanasiasa huyo:

RAI: Unaweza kueleza ni nini kilikusibu hadi kufikia hatua ya kutokwa machozi bungeni wakati wa Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 unapitishwa?

SAADA: Ni kwamba Zanzibar inaponunua umeme inatatozwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sehemu ambayo umeme unanunuliwa, ingawa sio sheria ya kodi hiyo  inavyoelekeza kufanywa. Kwa sababu inasema ikiwa utanunua umeme Tanzania Bara ambao unakwenda kutumika Tanzania Bara, utatozwa VAT palepale Tanzania Bara. Ila umeme huo ukienda kuutumia nje ya Jamhuri ya Muungano, ile VAT itatozwa Tanzania Bara.

Sasa kigugumizi ni kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, na inanunua umeme Tanzania Bara, haipaswi kutozwa VAT kwa sababu inanunua umeme mbichi (umeme usioongezwa thamani), ambao unakuja kuongezewa thamani hapa Zanzibar kwa kupitia miundombinu yake. Mwenye haki ya kutoza ni Zanzibar ni sawa na umenunua nyama mbichi umeenda kutengeneza mishkaki, ule mshkaki ndio unapaswa wewe utoze kodi kwa sababu ndio bidhaa ya mwisho.

Sasa nilitokwa na machozi ya majonzi kwa sababu nilijiuliza kwa nini jambo hili linapigwa dana dana! Kwa nini ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo lilianza tangu mwaka 2016 usipatikane?

Kwa nini tuwe wagumu kukubaliana kuwa hii VAT itozwe Zanzibar? Mpaka mwisho likawa halijapita, ndio nilijisikia majonzi, na mpaka sasa bado tunaendelea kujadiliana. Tunataka umeme Zanzibar uwe nafuu.

DENI LA TAIFA

RAI: Ipo hoja ya kukua kwa deni la Taifa, hili inalizungumziaje?

SAADA: Sasa hivi tunaweza kuona limekua kwa kasi kwa sababu ya kushuka kwa shilingi, lakini kuna matokeo chanya kwa sababu fedha ambayo tunakopa tunawekeza katika uzalishaji zaidi na hayo ni masharti ya wakopeshaji wote kwamba hawawezi kukukopesha fedha ili ukatumia katika matumizi ya kawaida. Ni sawa kama tunapokwenda kukopa benki, masharti ni lazima uanzishe biashara, ili baadaye izalishe faida. Unakopa kukuza au kuanzisha biashara ambayo wanakuja kukufanyia tathmini, ndipo wanakupa mkopo. Kwa hiyo, wanakukopesha ili uweze kuzalisha na utakachozalisha ndio utumie kuwalipa. Tunawekeza kwenye masuala ya umeme, barabara, reli na mengine. Ni jambo zuri.

Wananchi wana hofu, au wanapotoshwa, kwa sababu kwanza mkopeshaji yaani IMF, huwa wanakuja kutufanyia tathmini kwa mwaka mara mbili na kupata thamani ambayo tunaweza kukopa. Kwa hiyo ni vigezo vya kimataifa kulingana na mikopo ambayo tunakopa kwa malengo ya uzalishaji. Uwezo wa kukopa bado upo tunaweza kuendelea kukopa.

RAI: Unafikiri ni sababu gani za msingi zinasababisha thamani ya shilingi kushuka na unatoa ushauri gani kwa serikali, ili kukabiliana na hali hiyo?

SAADA: Kushuka kwa shilingi kuna sababu nyingi, ila kubwa, sisi tunaponunua zaidi bidhaa kutoka nje kuliko tunavyouza. Kwa hiyo, mahitaji ya Dola yamekuwa makubwa, yaani tunakusanya pesa kwa ajili ya ununuzi wa Dola ili kutafuta bidhaa. Lakini pia inaleta mshituko (shock) kwa sababu bei ya mafuta inazidi kupanda.

Mwonekano mwingine ni uwekezaji unaoendelea bado si wa kutosha, pia kipindi cha siku kuu na mapumziko, watu wengi wanakusanya zaidi fedha au Dola kwa matumizi.

Pamoja na hayo, naamini udhibiti holela wa maduka ya fedha za kigeni kama ilivyofanywa kule Arusha, Dola inaweza kuwa katika mzungumzo mzuri zaidi na sahihi. Jambo zuri ni kwamba bado tuna akiba nzuri, kwa hiyo si jambo la kutisha sana kwani ni changamoto za kawaida. Kwa sababu tupo katika harakati za kutengeneza uchumi wetu.

SAKATA LA KOROSHO

RAI: Katika siku za karibuni kumekuwapo na sakata la korosho ambalo baadaye serikali imeamua kuzinunua baada ya wafanyabiashara kudaiwa kuwanyonya wakulima, unatoa ushauri gani kwa serikali kusimamia suala hili ili kusiwepo na mgongano wa kimasilahi kati ya pande zote?

SAADA: Kwanza lazima nimpongeza Rais Magufuli kwa kuingilia suala hili, kwa sababu mara nyingi tukiacha mifumo ya soko huria peke yake, wananchi wanaumizwa. Kwa hiyo, katika sera za kiuchumi  uamuazi wa serikali kuingilia ni muhimu sana kama rais alivyofanya sasa.

Awali, hofu kubwa ilianzisha kwenye yale mabadiliko ya Sheria ya Korosho, wengi walidhani pengine serikali inachukua zile fedha, hivyo urejeshaji wake ungeweza kusuasua na kuathiri fedha za mfuko wa korosho… kwa hiyo kulikuwa na ubishani kidogo kutokana na ununuzu wa pembejeo ndio maana wakulima kupitia wabunge wao walikuwa wanapinga.

Lakini sasa tumeona wamezalisha korosho, kawaida tunategemea bei ya soko ambalo lilikuwa limepanda. Korosho ni katika bidhaa zinazouzwa ghali duniani. Cha kushangaza wanunuzi walikuja kuwapa bei ndogo wakulima, ndio maana  wakagoma. Nadhani hii intervention ya rais, ni sahihi na sasa itatengeneza mfumo madhubuti zaidi kwa serikali kuzichukua korosho na kuziuza moja kwa moja katika soko la duniani.

Jambo kama hili Zanzibar tumelipatia uzoefu katika zao la karafuu, kulikuwa na changamoto ya usimamizi, ambapo Serikali ya Mapinduzi ilipoamua kusimamia sasa tunaona matunda yake, wakulima wanapata bei nzuri na serikali inapata mapato.

Kwa hiyo Serikali ya Bara inaweza kujifunza kwa Serikali ya Zanzibar, kwani hadi sasa Serikali ya Mapinduzi inakopesha hata wakulima vifaa wanavyohitaji wakati wa matayarisho ya mashamba ya karafuu. Na wakati wa kurejesha wanarejesha kwa utaratibu mzuri ambao mkulima haumii, na zile karafuu anaziuza moja kwa moja kwa serikali.

Naamini tunakoenda tutaweka mfumo mzuri zaidi wa serikali kuzinunua na moja kwa moja kwenda kutafuta soko kuliko kuwaachia middle men ambao wanawaumiza wakulima. Ni utaratibu mzuri, changamoto hazikosekani. Pia natarajia serikali itapeleka kwa wakati pembejeo.

Kiujumla, changamoto hii itapelekea kuundwa kwa mfumo madhubuti zaidi wa ununuzi wa korosho, pamoja na mazao mengine, pengine serikali ya Jamhuri itakuwa na changamoto kwani yapo mazao mengi ya biashara,  kama vile pamba, tumbaku, nadhani hii itakuwa funzo. Naamini kutakuwa na mfumo mzuri zaidi, ila tumepata funzo kutokana na hili la korosho.

Niseme kwamba sakata hili, limetokea kwa mara ya kwanza, biashara iliachiliwa kwenye soko huria, hatuwezi kusema kuna ubaya kwa serikali kuingilia kwa sababu ni mojawapo ya theory ya uchumi. Zamani kina Adam Smith wao walikuwa wakisisitiza tuwaache soko huria, ila miaka ya 1930 nchi nyingi za Ulaya uchumi ulipokufa, serikali ndio ziliingilia kati.

Hii inadhihirisha kuwa sio kila kitu ni lazima kuachia Sekta Binafsi moja kwa moja, hapana! Kuna wanaoumia, hasa wananchi. Kuingilia huku ni busara, lakini bila shaka ndio chanzo cha kuweka mfumo mzuri zaidi pia katika mazao mengine, ili kuwepo na win win situation, kusiwepo na hali ya mkulima kuminywa na wengine wanatajirika.

Kwa hiyo changamoto hii itasababisha kuwepo na mfumo mzuri zaidi, kwa pande zote tatu. Si jambo la kulaumiwa kwani ilikuwa muda muafaka kwa serikali kuingilia.

RAI: Mwaka 2020, Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla, kunatarajiwa kufanyika Uchaguzi Mkuu, lakini pia mwaka ujao kutafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Je, unatazama vipi chaguzi hizo na wewe umejiandaaje?

JOTO LA URAIS ZANZIBAR

SAADA: Uchaguzi unaokuja si uchaguzi mgumu kwa sababu kuna mageuzi mengi yamefanyika ambayo yamerudisha matumaini kwa wananchi. Wamepata yale waliyoyataka, yaani CCM imevaa viatu vya wananchi na kuleta matuamini zaidi. Ila binafsi bado sijaamua nitakuaje 2020.

RAI: Hata hivyo, joto la nafasi ya urais Zanzibar linazidi kupanda, hasa ikizingatiwa Dk. Shein anamaliza mihula yake, Je, unatarajia kuwania nafasi hiyo?

SAADA: Suala la joto kupanda Zanzibar ni vizuri kwa sababu Zanzibar ni ndogo, Ila SMZ imefanya vizuri katika nyanja mbalimbali hivyo tunategemea tupate rais hodari, mchapakazi, ambaye ataendeleza miundombinu ya kiuchumi ambayo imeanzishwa na awamu zilizopita. Kikubwa Zanzibar tubadilike zaidi kutumia fursa hizo.

Unajua mwaka 2020 ni mwaka ambao Zanzibar inakamilisha mpango wake wa mendeleo ya kiuchumi.

RAI: Kwa kuwa tangu ulipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete na kushika nyadhifa mbalimbali hukuwa Mbunge wa jimbo, lakini sasa ni Mbunge wa Welezo. Je, ni mambo gani unajivunia kuyatekeleza kwa kipindi kifupi ulichokaa madarakani?

SAADA:  Kipindi hiki ni Mbunge wa wananchi, ni tofauti na mwaka 2015, sasa nimevaa viatu vya wananchi. Kipindi kile kuanzia mwaka 2015 wananchi walikuwa na shauku kubwa kutokana na changamoto nyingi walizokuwa nazo, ila nimedhamiria kuzitatua kwa sababu mimi pia ni mwenzao.

Kwanza jimbo la Uwelezo ni jimbo jipya, lilitokana na Magogoni na jimbo la Dole. Kwa hiyo kulikuwa na changamoto nyingi sana, ila kubwa ni upatikanaji wa maji safi na salama, ukiangalia Welezo ndio penye vyanzo vya maji  ikiwamo miundombinu mikubwa ya maji ipo hapo,  ila cha ajabu wananchi wa hapo wana shida ya maji ndio maana nikaanza nalo hilo.

Tumechimba visima wananchi wanapata maji, tumeipunguza changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa.

Pia kulikuwa na changamoto ya barabara, hususani za ndani zilikuwa hazipitiki. Kwa kuwa ujenzi wa barabara ni gharama kubwa, tumejitahidi kupunguza tatizo hilo kwa zile barabara korofi zaidi huku tukisubiri serikali imalizie.

Wananchi wa Welezo pia wanajishughulisha na biashara ndogondogo, kwa hiyo wengi walikuwa wanategemea tuwawezeshe kimitaji na tumefanikiwa katika hilo.

Tumeboresha baadhi ya shule kwa kuwapatia madawati ingawa hatujafanikiwa kumaliza tatizo hilo kabisa. Lakini pia tumeendelea kufanyia ukarabati baadhi ya shule kwa sababu nyingi ni za zamani kidogo.

Ila baadhi ya Diaspora wametusaidcia ujenzi wa hospitali ambayo sasa pia imeanza kuzidiwa na idadi ya watu wanaotegemea kwa sababu inatoa huduma ya mama na mtoto. Changamoto ni rasilimali fedha ila tunasonga.

Tutaendelea kushirikiana kupunguza hizi changamoto. Zipo na nyingine ni ahadi za Rais ambazo tumempekelea na  ataanza kuzitekeleza kabla ya 2020. Ninachoomba ni ushirikiano wao.