Home kitaifa SABABU ZA KUDORORA UTUMISHI WA UMMA

SABABU ZA KUDORORA UTUMISHI WA UMMA

3793
0
SHARE
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu), George Mkuchika akisalimiana na watumishi wa ofisi yake.
NA MARKUS MPANGALA    |     

KILA kazi inakuwa na vigezo vyake ili uipate. Kila idara inakuwa na vigezo vyake ili mwombaji afanikiwe kuajiriwa. Vilevile kila shughuli inakuwa na kanuni zake ambazo mhusika anatakiwa kuzifuata pamoja na kubuni zile ambazo hazihitaji mwongozo rasmi wa kiutumishi.

Ninazungumzia suala la biashara kwa mfano, zipo kanuni za asili ambazo kila mmoja anaweza kubuni kama njia ya kuongeza ufanisi. lakini zipo zile ambazo hazipaswi kuondolewa kwakuwa zimekuwa msingi wa ufanisi.

Ukahiki wa vyetu vya watumishi wa umma umekwisha. Awamu ya mbili muhimu zilishafanyika kwa watumishi wa umma, awamu ya mwisho ilianza Julai mwaka 2017. Sijui zoezi la kuhakiki vyeti limefikia wapi, kwani nimeona limeyoyoma kimya kimya kiasi kwamba imebaki kukisia tu nini kilichotokea kwa baadhi ya watumishi wa umma.

Ninawafahamu baadhi kama 20 ambao wameondolewa kazini kutokana na suala hilo, hali ambayo nami ilinishangaza wao kukutwa nalo na wakawa hawana mpango wa kukata rufaa.

Kuna watumishi walikatisha likizo zao kwasababu wanatakiwa kwenda vituo vya kazi kukamilisha suala la uhakiki wa vyeti na utumishi wao.

Leo katika mazungumzo yangu na msomaji mmoja ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake gazetini, napenda kuwashirikisha mawaidha yake ambayo yanafaa kutekelezwa na wakubwa. Endelea kumsoma..

“Nataka tujiulize je, kuzorota kwa ufanisi serikalini ikiwa ni pamoja na idara, wizara, taasisi na mashirika ya umma unasababishwa na vyeti feki peke yake?

Binafsi naona kuna sababu nyingine ambazo nazo zinapaswa kushughulikiwa ili matarajio yafikiwe. Mbali na vyeti vya kufoji kuna haya mambo yanachangia sana kudhoofisha utumishi wa umma. Nayajadili kwa ufupi;

MOSI; Watu kufanya kazi wasizokuwa na ujuzi nazo. Kwamba watu wenye vyeti vyao halali wanapangiwa kazi ambazo sio walizosomea au watu wenye vyeti vya kufoji wanapangiwa kazi ambazo hawazimudu wala kuzijua, lakini wanatakiwa kuzifanya kwa kiwango bora!

Tukumbuke kuna watu wana vyeti vya kufoji lakini wanamudu kazi walizopangiwa! Wanastahili kufutwa lakini ukweli ni kuwa wanamudu kazi walizopangiwa hadi twaweza kudhania wamezisomea.

PILI; Watu kupangiwa kazi ambazo ni chini mno ya utaalamu waliobobea au kusomea. Jaribu kufikiri Profesa aliyesomea elimu apangiwe kufundisha chekechea. Bila shaka Profesa huyo ataharibu kazi hiyo na kuzidiwa na Mwalimu mwenye cheti cha ualimu toka Chuo cha Ualimu. Hawa mara nyingi hawapendi kazi maana iko chini mno ya kiwango chao. Wapo sehemu ya kazi kama “kuzuga”. Bada yake wanachojali wao ni mshahara na marupurupu yakiingia kwenye akaunti zao za benki.

Niwapeni mfano, kwenye jeshi la Marekani hii wanaita “Counting the Dolphins’” na kule Uingereza wanaita “Counting the Snow”. Kwamba mtaalamu kwelikweli lakini kazi anayopewa haihitaji utaalamu wa hali ya juu. Ufanisi unapungua mno. Kila saa ana hasira na kazi yake wala haelekei kukomesha hilo. Kwa mfano anaweza kuja mteja, lakini mapokeo yake yakawa tofauti kabisa, ni kama vile anamsumbua. Huyu ni mwepesi kubwatukia wateja.

Binafsi nakiri hili kukutana nalo mwezi Machi mwaka huu 2018 katika Benki moja ya umma Tawi la Kariakoo. Nilibwatukiwa badala ya kuelekezwa kiasi kwamba niliduwaa, na kukiri nilikuwa sahihi kufunga akaunti zangu katika benki hiyo. Hapo ndipo nilikumbuka hilo la “Counting the Snow”.

TATU; Kumpa madaraka ya usimamizi mtu bila kuzingatia ujuzi au elimu baina yake na anaotakiwa kuwasimamia. Unakuta mtu ana shahada ya Uzamili anasimamiwa na kuelekezwa kazi na mtu mwenye cheti, pengine cheti cha kufoji. Anayemsimamia akijaribu kumkosoa au kumshauri kitaalamu inakuwa nongwa. Tofauti hii haijazingatiwa kiasi cha kutosha hali ambayo inasababisha kuzorotesha utumishi wa umma.

Na makazini mwetu kuna wasimamizi wa aina wengi sana. Na zaidi wanadhani wakikosoeolewa basi hukimbilia kujibu, “unadhani naogopa elimu yako”. Wana vyeti halali lakini wanawasimamia wenye vyeti vikubwa kuliko vyao.

NNE; Kufa kwa mfumo wa kusimamia na tathimini makazini. Huko nyuma mabaraza ya wafanyakazi yalikuwa na nguvu sana. Wakati mwingine nguvu kupita kiasi. Mambo haya hayakupendwa sana na Mawaziri, Makatibu wakuu, mameneja wa mashirika ya umma, wakurugenzi, wakuu wa idara na viongozi wengine. Yalikuwa yanawaondolea mamlaka ya kutenda watakavyo.

Ukweli ni kuwa pamoja na matatizo yaliyokuwepo kuhusu haya mabaraza lakini yaliweza kuwasimamia watu sehemu za kazi watu wasigeuke miungu watu.

Mabaraza yalikuwa kizingiti kwa wahujumu na mafisadi. Ujio wa utandawazi umeua au kudhoofisha mabaraza haya. Miungu watu wakajichomoza kwa wingi na kuamua mambo watakavyo. Hakuna wa kuwahoji tena.

Lakini pia enzi ya mfumo wa chama kimoja chama kilichokuwepo nacho kilisaidia katika kusimamia na kutathimini. Ujio wa vyama vingi ukaondoa jukumu hili. Ni vyema itafutwe namna ya kurejesha jukumu hili kwa kuzingatia mfumo wa vyama vingi. Binafsi sioni ni kwa nini chama kilichounda serikali kisipewe jukumu hili. Ufanisi serikalini ukizorota si chenyewe ndio kitabeba lawama?

Nadhani tulijidanganya kudhani jukumu hili litabebwa na bunge! Kila mmoja wetu ni shahidi wa jinsi bunge letu lilivyofeli kwenye jukumu hili! Tunasikia wenyewe wakituhumiana kuwa wanahongwa wakati wakitekeleza jukumu hili! Mbwa tuliyemtuma kuchunga duka analipwa alale!

TANO; Tabia ya kutoadhibu imeota mizizi mno. Mathalani Mkaguzi mkuu kila mwaka anatoa ripoti yenye madudu ya kutisha. Imekuwa kama wimbo mzuri lakini umekosa wachezaji au mapromota. Hata wanaotajwa katika ripoti wamejenga kiburi kuwa wimbo hauziki! Kutokana na kutoadhibiwa wamejaa kiburi kiasi kwamba ufanisi sehemu zao za kazi umeshuka mno. Na mtumishi yeyoote amabye anahisiwa kuwa alihusika kutoa taarifa kwa Mkaguzi wa Serikali anaonyeshwa mlango.

Wengine wote waliosalia wanaufyata! Wanaona njia muhimu ni kushiriki uhuni wa bosi! Enzi za Mwalimu wizi ulikuwepo lakini hata mijizi ilijua kuwa za mwizi ni arobaini.

Watumishi wakikaguliwa hata nyumba au viwanja au unywaji bia uliopitiliza. Ndio maana enzi zake walisomeshwa, kutibiwa na kupatiwa huduma bila matatizo makubwa. Sasa watu mshahara unajulikana lakini anamiliki majumba na magari na hakuna wakumuuliza nyumbani kwako una mtambo wa kutengeza noti au vipi?

Najua kuna sababu nyingine nyingi zinazochangia kushusha ufanisi sehemu zetu za kazi lakini kwa leo niishie hapa ili niwape nafasi na wengine wachangie.

Ili hii vita ya vyeti feki izae matunda inatupasa tushughulkie na haya mengine la sivyo linalotarajiwa halitapatikana.