Home KIMATAIFA SADC, EAC bingo kwa Tanzania

SADC, EAC bingo kwa Tanzania

522
0
SHARE

Na MWANDISHI WETU

WAKATI vuguvugu la kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) likipamba moto, Tanzania ndio nchi pekee yenye kufaidika na uanachama wa jumuiya mbili tofauti.

Mbali ya kuwa muasisi na mwanachama wa SADC, Tanzania pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), yenye Makao Makuu yake jijini Arusha.

Mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za SADC unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Agosti 17 na 18, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, atakabidhiwa uenyekiti.

Uzito na umuhimu wa mkutano wa SADC ni mkubwa na unalinganishwa na ule wa EAC, ambao huwakutanisha wakuu wa nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda na Sudan Kusini.

Pia EAC huwakutanisha mawaziri wanaoshughulikia masuala ya jumuiya, wabunge wanaounda Bunge la Afrika Mashariki na wadau wengine mbalimbali.

Faida za uanachama:

Jumuiya zote mbili ambazo ni za kikanda zinatajwa kuwa ni chanzo cha Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo, uchumi, diplomasia, usalama, demokrasia pamoja na mahusiano ya kijamii kati yake na SADC na EAC, kwa kuangalia misingi ya malengo ya kuanzishwa kwake.

SADC na EAC zote zimeanzishwa kwa malengo ya kuimarisha uchumi na usalama wa nchi wanachama wake, ambapo zimezindua mikakati na kuingia mikataba mbalimbali yenye tija, ili kuinua hali ya wananchi wao.

SADC ni Jumuiya iliyoanzishwa mwaka 1992 ikiwa na malengo ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kuratibu masuala ya maendeleo kwa nchi wanachama wake.

Wakati Tanzania inajitoa kwenye jumuiya ya soko la pamoja kwa nchi za kusini mwa Afrika (COMESA), katika utawala awa Awamu ya Pili, mjadala mkubwa ulihusu nini mwelekeo wa nchi katika kujitafutia ushirikiano na maendeleo.

Faida za uanachama wa SADC:

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa SADC ambaye ni Mtanzania, Stregomena Tax, jumuiya hiyo imeondoa vikwazo na baadhi ya tozo za kibiashara, pamoja na kuchagiza juhudi za utekelezaji wa miradi ya umeme na miundombinu ya usafiri, kama vile reli na barabara inayofanywa na Serikali ya Tanzania.

Mikakati ya Sera ya Viwanda ya SADC imejikita katika kuongeza kasi, kuimarisha ushirikiano na ushindani wa kiuchumi kutoka nchi zisizokuwa wanachama wa jumuiya hiyo.

Sera ya Viwanda ni ndio kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani mwaka 2015.

Sera hiyo Sustainable Industrial Development Policy (SIDP) ya mwaka 1996 inaonyesha kuwa Tanzania hadi mwaka 2015 ilitakiwa kuwa na viwanda vya kati.

Sera hiyo ilipitishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara wa wakati huo alikuwa Dk. Abdallah Kigoda.

Katika kipindi chote hicho, kampeni ya ujenzi wa viwanda au kusisitiza sera utekelezaji wa sera yenye haikuwa kubwa. Tangu mwaka 2015 tumejionea kampeni hiyo, huku wawekezaji mbalimbali wakiomba nafasi za kuwekeza pamoja na kuanzishwa viwanda nchini.

Hapo ndipo yalipo mafungamano kati ya Sera ya Viwanda ya SADC na Tanzania. Sera hiyo ni miongoni mwa mambo yanayozungumzwa kwenye vikao vya maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za SADC.

Rais Dk. Magufuli wakati akifungua rasmi maonyesho ya viwanda na biashara siku chache zilizopita, alisema; “Tumekuwa waagizaji wa bidhaa kutoka nje, ambazo zimekuwa za gharama kubwa. Pia nchi za Afrika zimekuwa wazalishaji wa nguvu kazi. Wanaikimbia Afrika ili kwenda Ulaya na Marekani kufanya kazi. Tukizitumia fursa za ndani ya Afrika tutapiga hatua kubwa.”

Ajira:

Ajira ni miongoni mwa maeneo ambayo yameleta manufaa makubwa kwa Tanzania. Baadhi ya wataalamu wa Kitanzania wamepata nafasi za kufanya kazi katika asasi mbalimbali kwenye nchi za SADC, kwenye sekta za elimu, afya, diplomasia, uchumi na ulinzi na usalama.

Fadhy Mtanga, Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Restless Development kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Ruvuma na Iringa) ambaye pia amewahi kuishi na kufanya kazi nchini Zambia na kutembelea karibu nchi zoteza SADC, alisema; “Jumuiya za kikanda ni muhimu.

“Zina manufaa makubwa sana, hii ya SADC, kwa mfano, huhitaji kulipia viza kuingia nchi hizo, jambo ambalo linapunguza. Pia kwenye jumuiya hizo wananchi bila kujali rangi, tabaka, na vipato wanawezeshwa kwa urahisi kupata ajira pamoja na kufanya biashara.”

Usalama:

Tanzania kwa sasa ndiye Makamu Mwenyekiti Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama (Troika).

Akizungumzia suala la usalama, Mwanasheria kutoka kampuni ya Finkleys Advocated ya jijini Dar es Salaam, Ambroce Nkwera, alisema; “Suala la usalama pia ni muhimu sana, kwa kuwa nchi hizo ni majirani zetu, mataifa ya nje hayawezi kupitia huko kuhatarisha usalama wetu, kwa kuwa ni wana-jumuiya wao.

“Ni watu ambao tunashirikiana katika mambo mengi likiwamo la usalama wa raia wetu, mfano wakati mwingine kunakuwa na mafunzo ya pamoja kwa wanausalama wetu.”

Alisema, malengo makuu ya SADC ni kuwa chombo cha amani na usalama, uchumi na maendeleo, pamoja na kuendeleza diplomasia miongoni mwa wanachama, huku Tanzania ikibeba sifa kubwa ya kuzipigania nchi hizo katika vita vya ukombozi. Manufaa ya usalama ni pamoja kubadilishana wataalamu wa masuala ya ulinzi na usalama.

Kiswahili:

Afrika Kusini ni mwanachama wa jumuiya ambaye ametangaza kufundisha somo la Kiswahili katika mitaala ya elimu. Tanzania itatoa msaada mkubwa kwa nchi hiyo kwa kuipatia wataalamu, vitabu na nyenzo zote muhimu katika kukamilisha mpango huo.

Hatua hiyo ya Afrika Kusini kuamua kufundisha Kiswahili katika ngazi mbali za elimu, inaweza kutumika kama chachu katika kueneza Kiswahili kwa nchi wanachama wa SADC.

Itakumbukwa kuwa, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Rais wa zamani wa Msumbiji (ambayo ni nchi mwanachama wa SADC), Joachim Chissano, aliwahi kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili katika mojawapo ya mikutano AU, hatua ambayo inadhirisha ukubwa wa Kiswahili.

Mtwara Corridor:

Ni mpango mwingine ambao unaziunganisha nchi za SADC na Tanzania. Ujenzi unaoendelea wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay mkoani Ruvuma kwa kiwango cha lami, ni kiunganishi cha nchi za Msumbiji na Malawi.

Katika ziara yake nchini Malawi mapema mwaka huu, Rais Dk. Magufuli aliwaomba wafanyabiashara na Serikali ya nchi hiyo kuanza kutumia Bandari ya Mbamba Bay, mara baada ya kukamilika barabara hiyo.

Tanzania itaweza kupitisha mizigo ya nchi za Msumbiji na Malawi kupitia bandari za Mtwara na Mbamba Bay. Msumbiji na Malawi wote ni wanachama wa SADC.

Tanzania ndani ya EAC:

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilifufuliwa mwaka 1996 chini ya ushawishi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, pamoja na marais wenzake Daniel arap Moi (Kenya) na Yoweri Museveni (Uganda), baada ya kuvunjika mwaka 1977.

Baada ya kufufuliwa na hatimaye kuanzishwa upya Januari, 2001, imekuwa na vipaumbele vya maendeleo ambavyo Tanzania ni moja ya wanufaika wakubwa.

Tanzania imekuwa na historia ya amani tangu ilipopata Uhuru 1961, ikilinganishwa na fujo na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoshuhudiwa katika mataifa ya Kenya, Rwanda, Burundi, na Uganda.

Hata sasa Afrika Mashariki inajaribu kudumisha utulivu na amani katika ya migogoro inayoendelea katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.

Pia Tanzania ni nchi pekee yenye ardhi kubwa kuliko mataifa mengine 3 yakiunganishwa (Uganda, Rwanda na Burundi), na baadhi ya Watanzania wamekuwa na hofu ya kupokwa ardhi na wakazi wa mataifa mengine wanachama wa EAC.

Uhaba wa ardhi ni suala nyeti katika eneo la Afrika Mashariki, hasa nchini Kenya, ambako mapigano ya wenyewe kwa wenyewe upande wa Mlima Elgon mwaka 2007 yaliwaacha zaidi ya watu 150 wakiwa wamekufa na kulazimisha takriban watu wengine 60,000 kukimbia Mahakama ya Afrika Mashariki:

Mahakama ya Afrika Mashariki ndiyo Mahakama inayosimamia kesi zote katika eneo hilo. Mahakama hiyo ina makao yake jijini Arusha.

Bunge la Afrika Mashariki

Bunge la Afrika Mashariki ndicho chombo cha kutunga sheria katika eneo la Afrika Mashariki. Lina na wajumbe 27 ambao wote wamechaguliwa na mabunge ya nchi wanachama.

Linahusika na masuala yote ambayo yanahusu jumuiya kama vile kujadili bajeti ya EAC na masuala yote ya jumuiya na kutoa mapendekezo kwa asasi nyingine kuhusu utekelezaji wa mkataba mbalimbali ya ushirikiano.

Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2001, Bunge hilo limekuwa na vikao kadhaa mjini Arusha, Kampala na Nairobi. Makao yake pia yapo jijini Arusha

Jiografika ya eneo la EAC:

Jiografia ya nchi wanachama wa EAC imeiweka Tanzania katika sehemu nzuri kuweza kufaidika zaidi kiuchumi, ambapo Ziwa Victoria Lake sehemu kubwa ipo nchini.

Ziwa Victoria linaunganisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania na ni la pili duniani kwa eneo.

Pia Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko yote Afrika pia upo Tanzania.

Nchi za Sudan Kusini, Uganda, Rwanda na Burundi hazina bahari, hivyo zinategemea bandari za Tanga na Dar es Salaam, pamoja na Mombasa nchini Kenya.