Home kitaifa SADC imerudi nyumbani

SADC imerudi nyumbani

662
0
SHARE

Na NASHON KENNEDY

JUMUIYA ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imerejea kwenye chanzo chake baada ya kupitishwa kwa Mkutano wa Jumuiya hiyo ambao unafanyika jijini Dar es Salaam.

Kihistoria, SADC chanzo chake ni mawazo yaliyoanzia kwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu, Julius Nyerere, katika jitihada zake za kuimarisha jumuiya hiyo kiuchumi kwa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa Bara la Afrika ambao makao yake makuu ya kudumu yalikuwa jijini Dar es Salaam sambamba na wazo la uanzishwaji na ufadhili mkuu ambao ulikuwa ama ulitokana na dhamira ya kimawazo ya Mwalimu Nyerere ambaye ni Baba wa Taifa na Mhandisi Mkuu wa fikra na mikakati ya ukombozi wa bara letu.

SADC ilianzishwa rasmi April Mosi mwaka 1980 mjini Lusaka nchini Zambia, ikiwa na wanachama 16 ambao ni Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagaska, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zambia na Zimbabwe na makao makuu yake yapo Gaborone nchini Botswana.

Na sababu za kuundwa kwa SADC ni kuleta ulinzi na usalama, mshikamano baina ya nchi wanachama na kuongeza na kukuza biashara katika nchi hizo.

 Tangu awali Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais wa Zambia, Keneth Kaunda na marehemu Abeid Karume walijua kuwa vita ya panga haiamuliwi kwa fimbo, lakini pia vita ni mchakato wenye kubeba hisia na uhalisia hivyo kuwa ni chombo cha kiuchumi cha mataifa yaliyokuwa huru tayari na yale yaliyokombolewa baadaye lilikuwa ni jambo lisilokwepeka.

Kwa msingi huo ndipo SADC ilipoundwa ili kuzalisha fedha na rasilimali nyingine ambazo zingesaidia kuhuisha harakati za uhuru wa kisiasa lakini pia ukombozi wa kiuchumi kwa mataifa wanachama.

Mataifa ya kibeberu yaliyofurisha awali jukumu la kuyatunza makoloni yaliyokuwa chini yake, yasingeacha salama nchi zilizokuwa zinatawaliwa bila athari za uchumi wenye mwelekeo wa utegemezi kwa Watawala wao ili mataifa hayo hata baada ya uhuru wa kisiasa na kinachoitwa kujitawala wenyewe bila athari za kimfumo katika uchumi, hali ambayo ingeendelea kuyafanya mataifa hayo machanga kuendelea kufuata matakwa ya watawala wao wa zamani na hivyo kuendeleza mfumo wa Ukoloni Mamboleo (Neo- Colonialism)!

Huu ni Mkutano wa 39 wa SADC na mikutano yote tangu kuanzishwa kwake imezaa mafanikio mengi ikiwamo kiunganishi cha mashirika mengine ya kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Preference Trade Area (PTA) na Great Lakes States kwa kutaja machache.

Kutokana na mfumo huo nchi za Tanzania, Malawi, Zimbabwe, Swaziland, Lesotho, Angola, Namibia, Afrika Kusini, Msumbiji na Kongo DRC na Madagscar zimeunganishwa katika mtandao huu wa ushirikiano wa kibiashara ambao kimsingi unateng’eneza soko kubwa la kibiashara lenye watu zaidi ya milioni 300, hakika hili ni soko kubwa la kibiashara kwa minajiri ya kuuza na kununuliana bidhaa za aina mbalimbali.

Kuimarika kwa jumuiya hii sio jambo lenye kuwafurahisha mabwana wakubwa waliotawala mataifa yetu kisiasa hapo zamani na hata kiuchumi kwa sasa, kwani kunawanyima fursa katika kutimiza nia zao za kutawala milele nchi za Bara la Afrika.

Kukosekana kwa fursa hizi kunateng’eneza chuki na hivyo kuimarisha njama za jinsi ya kusambaratisha nguvu hii ya pamoja katika uchumi, ili kwa namna moja ama nyingine nchi hizi ziendelee kuyategemea mataifa yaliyozitawala zamani kama paka anavyojenga urafiki na mwanamama ili anufaike na ukaangizaji unaofanyika mekoni, hakika huu ni urafiki wa mashaka kama ulivyo uswahiba wa chui na mbuzi!

Mkutano huu unafanyika Tanzania mara hii chini ya Rais Dk. John Magufuli, anayeamini katika falsafa ya kujitegemea kwa mataifa ya Afrika kiuchumi na kama mwarobaini wa kumaliza umaskini katika Bara la Afrika kupitia katika mfumo wenye kutegemea viwanda kwa ajili ya kuiingiza Afrika katika mtandao wa uchumi wa kati kufikia 2025.

Chini ya Dk. John Magufuli ambaye katika kilele cha mkutano huu atakabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa SADC, mawazo na dhana aliyoaiasisi ya uchumi wa viwanda kwa nchi za Afrika itatekelezwa kirahisi na mataifa wanachama wa SADC, kwani mwenyekiti atakuwa na nafasi bora zaidi kushawishi mawazo yake kutekelezwa bila kuzunguka mbuyu na hivyo basi kusaidia kwa kiwango kikubwa kuimarika kwa uchumi wa mataifa husika.

Kuna maazimio mengi yamewahi kupitishwa katika vikao mbalimbali vya mashirika ya Bara la Afrika, likiwamo Azimio la Maputo lililokuwa linashauri kwamba angalau bajeti zote za mataifa yaliyo Kusini mwa Afrika zitenge asilimia 15 kwa ajili ya kilimo kwa sababu asilimia kubwa ya Waafrika walioko vijijini wanategemea kilimo, azimio ambalo kwa bahati mbaya halijawahi kutekelezwa hii ikiwa ni kutaja kwa uchache kati ya maazimio mengi yaliyopitishwa bila kutekelezwa.

Hali hii pengine na sina hakika huenda ilitokana na uimara usioyumukunika wa viongozi waliopita katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

Walatini walisema zamani kuwa sauti ya watu ni sauti ya Mungu “Voxy Populi” maoni mengi ya watu katika nchi wanachama wa SADC yanahusisha kudharauliwa na kutokutiliwa maanani kwa sekta ya kilimo kwani kwa kiasi kikubwa ndio msingi thabiti na chanzo cha umaskini, njaa, maradhi, mashaka ya maisha, vita na mifarakano, lakini pengine hata vurugu za utawala na mapinduzi ya umwagaji damu, vita ya wenyewe kwa wenyewe, usaliti dhidi ya nchi zao na kukosekana kwa uzalendo miongoni mwa wananchi katika mataifa mengi ya Afrika.

Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa, uchumi na jamii katika Afrika wanaona kwamba kukosekana kwa ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Afrika ndiko kunakoyapa nafasi mataifa ya kibeberu kuingilia masuala ya ndani ya Afrika na hivyo nchi hizo za kiafrika kukosa uthibiti wa maamuzi na usimamizi sahihi wa uchumi na usalama wa mataifa yao.

SADC kama Jumuiya inayoelekea kuwa imara zaidi Kusini mwa Afrika ikiungana na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) zina nafasi kubwa ya kuimarisha uthabiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Kuimarika kwa SADC kama chombo cha kikanda Kusini mwa Afrika kunapunguza lawama na jukumu la AU katika kusimamia umoja na amani pamoja na utulivu wa kisiasa katika eneo hili muhimu na la kimkakati kwani Angola, Afrika Kusini, Kongo zimo katika mwambao wa Bahari ya Pacific, lakini Tanzania, Msumbiji, Madagascan na Afrika Kusini zimo katika ukanda wa Bahari ya Hindi na kila mmoja anajua umuhimu wa kanda hizi kiuchumi  na kijeshi zinazotegemewa na mataifa yenye nguvu ya kijeshi duniani sambamba na nguvu za kiuchumi, lakini pia ushawishi wa kidiplomasia kutokana na historia za mataifa haya.

Ni matarajio ya wananchi wengi waliomo katika nchi zinazounda SADC kwamba viongozi watu wanaohudhuria mkutano huu hawatachukulia mkutano huo kama utalii na mapumziko kwa ajili ya kujipunguzia mbinyo wa mawazo yanayotokana na matatizo katika nchi zao bali uwe mkutano wa kazi, kubadilishana ujuzi(Skills), uzoefu, mapambano ya fikra za kiuchumi juu ya maendeleo ya jumuiya na mchango wa mbinu bora zinazowakilisha matakwa halisi ya kuondoa unyonge wa kiuchumi na umaskini wa fikra unaotokana na utegemezi wa mataifa yaliyotawala nchi za Bara la Afrika kwa miaka mingi iliyopita.

Ni wakati muafaka katika mkutano huu bila kupepesa macho wala kumung’unya maneno kwa viongozi wetu kujitambua na kujua matakwa halisi ya Waafrika katika masuala yanayohusu maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huu wa Afrika na SADC kwa ujumla.

Bravo viongozi wa Mataifa wanachama wa SADC, Bravo Rais Dk. John Magufuli kama mwenyeji wa mkutano huu muhimu na mwenyekiti ajaye wa SADC. Hakika Mkutano huu wa SADC umerudi nyumbani! Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0756 823 420/ 0684 214 114/ 0718 392 711 au email: nashonkennedy@gmail.com