Home Habari kuu SAKATA LA TRILIONI 1.5 LAKUMBUSHA ESCROW

SAKATA LA TRILIONI 1.5 LAKUMBUSHA ESCROW

6139
0
SHARE
NA GABRIEL MUSHI, DODOMA    |   

MWENENDO mzima wa sakata la ni wapi zilipo Sh. trilioni 1.5, unatajwa kufanana kwa kiasi kikubwa na hali ilivyokuwa wakati wa kashfa ya uchotwaji wa Sh. bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow. RAI linachambua.

Sakata hili la sasa la Trilioni 1.5 ambazo ni zaidi ya mara tatu ya fedha za Escrow linahusishwa moja kwa moja na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyoitoa hivi karibuni.

Wakati sakata la Trilioni 1.5 likitajwa kuibuliwa na ripoti ya CAG, kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow iliibuliwa Mei, 2014 na iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa lengo la kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na Kampuni ya IPTL na suala hilo kupelekwa mahakamani.

Taswira ya masakata haya mawili zinawiana kwenye namna yanavyojadiliwa, kujibiwa na wakati mwingine kutolewa maamuzi.

Kama ilivyokuwa sakata la Escrow ndivyo ilivyo kwenye sakata hili la sasa la Sh. Trilioni 1.5, ambapo kwa kiasi kikubwa mhusika Mkuu ni Serikali kwa upande mmoja na wabunge hasa wa upinzani kwa upande wa pili.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo), wakati akifanya uchambuzi wa ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha unaoishia June 2017 ndio aliyeliibua sakata hili bila hofu kama alivyopata kufanya wakati wa sakata la Escrow wakati huo akiwa sambamba na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) David Kafulila.

ZITTO YULE YULE

Kama ilivyokuwa kwa kashfa ya Escrow, Zitto ameendelea kuwa kitovu cha mjadala kuhusu zilipo Sh trilioni 1.5 ambapo Aprili 16 mwaka huu aliibua hoja hiyo baada ya kufanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, ambapo alisema ripoti inaonyesha asilimia sita ya fedha zilizokusanywa na Serikali hazijulikani zilipokwenda.

“CAG ameonyesha kuwa katika bajeti ya Sh trilioni 29.5 iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya Sh trilioni 25.3 tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo.

“Serikali ilishindwa kukusanya Sh trilioni 4.2 sawa na asilimia 15 ya bajeti yote ya mwaka 2016/17.

“Katika fedha zote zilizokusanywa Sh trilioni 25.3, ni Sh trilioni 23.8 tu ndizo zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali na riba. Sh trilioni 1.5 zilizobaki hazijulikani zimekwenda wapi, hii ni asilimia 6 ya fedha zote zilizokusanywa mwaka huo,” alisema Zitto.

Hoja hiyo ya Zitto kwenye Trilioni 1.5 inashabihiana na ile iliyotolewa na Kafulila kwenye Bunge la 10 juu ya sakata la Escrow.

Kafulila ambaye sasa ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa karibu kabisa na Zitto ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa PAC, alisema baadhi ya maafisa wa ngazi za juu serikalini walihusika katika ushawishi wa kuchotwa kwa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow, na kumfanya aliyekuwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu kushindwa kuzuia fedha kuchukuliwa.

Sakata hilo lilipamba moto, ukweli wa mambo uliaanza kufichuka hatua kwa hatua baada ya Bunge kuipa PAC kupitia ripoti ya uchunguzi uliofanywa na CAG ili kuwasilisha taarifa itakayotoa ukweli.

Kamati hiyo na Bunge ilitoa mapendekezo manane ambayo yalimtaka, Rais wa awamu ya Nnne, Jakaya Kikwete ayafanyie maamuzi ambapo baadhi ya mapendekezo hayo ni kuchukuliwa hatua kwa vyombo vya uchunguzi na kuwajibishwa kwa watumishi wa serikali waliotajwa kushiriki katika kadhia hiyo, wakiwemo mawaziri.

KAULI YA JPM

Mfanano wa kimwenendo wa masakata haya mawili unakolezwa zaidi na kauli ya hivi karibuni ya Rais Dk. John Magufuli kuwa hakuna upotevu wa kiasi hicho cha fedha na kwamba kinachofanyika ni upotoshaji wa kwenye mitandao.

Aprili 20 mwaka huu Rais John Magufuli akiwa Ikulu kwenye hafla ya kumwapisha Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Edson Makallo, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Clement Mashamba, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi na majaji 10 wa Mahakama Kuu alisema habari zinazosambazwa kuwa kuna upotevu wa Sh trilioni 1.5 uliodaiwa kuainishwa katika ripoti ya CAG, si za kweli na kama zingekuwepo angechukua hatua za kumfukuza kazi waziri husika mara tu baada ya kupokea ripoti hiyo Machi 27 mwaka huu.

“Nilisikia Serikali imeiba shilingi trilioni moja nukta tano, nikampigia CAG nikamwambia mbona hukuniambia huu wizi wa trilioni moja pointi tano, maana ungeniambia siku hiyo hiyo ningefukuza mtu hata kama waziri, akanijibu hakuna kitu kama hicho.

“Aliniambia hakuna fedha iliyoibwa na Serikali, nikaamua kunyamaza nikasema huku mitandaoni tulishaambiwa hata ndege ni mbovu kwa sababu tu ya uhuru wa kutumia mitandao uliopo,” alisema Dk. Magufuli.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Dk. Magufuli, alimuuliza CAG, Profesa Assad, kama kweli kuna upotevu wa Sh trilioni 1.5 katika hesabu za Serikali ambapo alisimama na kujibu: “Hapana Mheshimiwa.”

Swali hilo hilo pia alimuuliza Katibu Mkuu wa Hazina, Dotto James, ambaye pia alijibu hapana. Baada ya kupata majibu hayo, Dk. Magufuli, alisema Watanzania kwa sasa wamekuwa na ugonjwa wa kuamini vitu vinavyoandikwa katika mitandao hata kama vya uongo. Alisema watu wamekuwa wakizungumza na kuandika vitu katika mitandao ya kijamii bila aibu kwa sababu Serikali haina nguvu ya kudhibiti mitandao.

“Yaani mimi nitafute fedha halafu waibe, nadhani ifike mahali wananchi wanapaswa kuacha kupotosha, ukipotosha angalia kitu husika kina masilahi gani katika nchi,” alisema Dk. Magufuli.

Kauli ya utetezi kama hiyo pia ilipata kutolewa na Rais mstaafu, Kikwete wakati akitetea madai ya kuchotwa fedha hizo za Tegeta Escrow kwa kudai kuwa fedha hizo hazikuwa za umma bali ni mali ya IPTL.

KAULI YA JK

Desemba 22,2014, Rais Kikwete alitoa ufafanuzi wa uhalali wa fedha za Escrow ambazo ziliibua mjadala wa je, ni fedha za umma au za IPTL.

…Maelezo haya kwa kiasi fulani yanasaidia kwenye kupata jibu la swali maarufu, fedha hizi hasa mwenyewe nani? Akaunti ya Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa ajili ya sababu maalum, kufanya kazi maalum, kwa masharti maalum na kazi hiyo ikiisha na  akaunti yenyewe inafungwa… Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akasema aaah.. nyinyi si mliletewa madai? Si mmelipa?  Hata kama hazijaenda kwa mwenyewe msizihesabu kuwa ni zenu, hizi sio zenu…”

“Fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni mali ya Tanesco, hivyo marekebisho yamefanywa ili kutotambua mali na madeni yanayohusu fedha hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow… Ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow sio za Tanesco na hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu vya Tanesco kama mali yake… Kama si za Tanesco ni za IPTL…“ alisema Rais Kikwete.

KUUNGANA KWA WABUNGE

Bila kujali itikadi zao za kisiasa baadhi ya wabunge wa pande zote mbili kwa maana ya CCM na upinzani waliungana na kusimama kidete kulijadili sakata la Escrow na hivyo ndivyo ilivyo sasa kwenye sakata la Trilioni 1.5.

Kwenye sakata la Escrow baadhi ya wabunge wakiongozwa na aliyekuwa Spika Anne Makinda na aliyekuwa Naibu Spika sasa Spika, Job Ndugai walitoa uhuru kwa wabunge kukubali kujadiliwa au kutokujadiliwa kwa hoja hiyo ambayo ilidaiwa kuwa kuna katazo la Mahakama.

Aidha kumbukumbu zinaonesha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa PAC, Hayati Deo Filikunjombe (CCM) alikuwa kinara katika kulishghulikia sakata hilo, ambalo liliwaangusha baadhi ya vigogo Serikalini.

Aliyekuwa mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka nae alihoji kwa kujiamini: “Serikali lazima ifanye uchunguzi wa kina kuwabaini na kuwachukulia hatua wale waliochukua mabilioni ya fedha taslim kutoka Benki ya Stanbic na kubeba katika mifuko ya sulfate kwa siku mbili…kinyume na taratibu zote za kibenki.”

Katika sakata hili la sasa tayari Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM) Omary Mgumba alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango (kwa niaba ya serikali) kutoa ufafanuzi wa taarifa ya upotevu wa Trilioni 1.5 ambazo zinadaiwa kutofahamika matumizi yake kwa mujibu wa ripoti ya CAG.

“Kuna upungufu, lazima nikiri ni kweli kuna mapungufu, Sh trilioni 1,5 haionekani, tusiposema kweli hatuitendei haki serikali. CAG ndio jicho la wabunge, anaposema CAG anatusemea sisi wabunge, sasa leo amesema kuna pesa hazionekani sisi wenye mali tukishabikia tunakosea sana na kuna upotoshaji mkubwa kwenye mitandao.

Kama alivyofanya Mgumba, ndivyo walivyofanya wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Selasini (Rombo) na Halima Mdee (Kawe), ambao kila mmoja kwa nafasi yake alihoji zilipo fedha hizo.

HOJA ZA SELASINI

Selasini alimwandikia waraka Rais Dk. Magufuli kuhusiana na sakata hilo, akisema alimsikiliza alichosema kuhusu Sh trilioni 1.5 na hata alipomsimamisha CAG na kumhoji kama fedha hizo zimeibiwa na kumjibu kuwa hakuna.

Selasini anasema hata na yeye ameisoma ripoti hiyo na hakuna mahali ambako CAG amesema fedha hizo zimeibiwa, bali anachokisema matumizi yake hayaonekani. Katika kuthibitisha hilo, Mbunge huyo anasema, ukurasa wa 34 wa ripoti hiyo ambayo hata yeye ameisoma CAG aligundua ni kweli yanayosemwa.

Selasini alisema kwa mantiki hiyo, inawezekana kweli fedha hizo zimeibwa au zimetumika kwa uzembe bila kufuata sheria au zipo mahali fulani.

“Kama wakishindwa kuifunga PAC na CAG sasa wanaweza kuomba msaada wa Polisi na au Takukuru kutafuta wezi au wabadhirifu,” linasomeka andiko la Selasin.

MDEE

Kwa upande wake, Mdee, mbali na kuhoji kile alichodai kuwa ni bakaa ya shilingi trilioni 1.5, alihoji pia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Baraza la Rufaa la Kodi na Mahakama kushindwa kukusanya baadhi ya mapato, halikadhalika kuongezeka kwa gharama za matibabu nje ya nchi, na ukiukwaji wa sheria ya manunuzi, licha ya serikali kujinasibu kupambana na mambo hayo.

TAARIFA MPYA KILA MUDA

Kama ilivyokuwa kwenye sakata la Escrow, suala la zilipo Sh trilioni 1.5 limekuwa likiibua taarifa mpya kila mara kwani kabla ya kauli hiyo ya Rais Magufuli, Serikali kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ililazimika kulifafanua suala hilo bungeni, akikanusha kupotea kwa fedha hizo.

Akifafanua ilipo hiyo Sh trilioni 1.5, Dk. Kijaji alisema Sh bilioni 697.9 zilitumika kulipa hati fungani, Sh bilioni 689.3 mapato tarajiwa na Sh bilioni 203.9 ni mapato yaliyokusanywa kwa niaba ya Zanzibar.

“Kuanzia mwaka 2016/2017, TRA ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual, hivyo kati ya mapato haya ya Sh trilioni 25.3, yalikuwepo pia mapato tarajiwa kama mapato ya kodi ya Sh bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar ya Sh bilioni 203.92,” alisema Dk. Kijaji.

Alisema katika uandishi wa taarifa yake, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taarifa za utekelezaji wa bajeti, ambapo hadi Juni 2017, mapato yaliyokusanywa yalikuwa Sh trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa Sh trilioni 23.79.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva, matumizi haya yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika, hivyo basi baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia ridhaa za matumizi (exchequer issues) yalikuwa Sh trilioni 24.4,” alisema Kijaji.

Kauli hiyo ya Dk. Kijaji inarandana na ile iliyotolewa mwanzo kabisa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Pamoja na ufafanuzi huo wote, Zitto yeye amesisitiza kwamba, fedha hizo Sh trilioni 1.5 kati ya Sh trilioni 25.3 za mapato yaliyokusanywa katika uchambuzi wake wa ripoti hiyo ya CAG umeonyesha hazina nyaraka zinazothibitisha katika matumizi ya serikali.

CHIMBUKO LA KASHFA YA ESCROW

Escrow ni akaunti iliyofunguliwa ilipotokea wabia wawili walipokuwa na ugomvi kuhusiana na mapato yao.

Kampuni ya VIP Engineering inayomilikiwa na James Rugemalila na Kampuni ya Mechmar walikuwa wabia walioanzisha biashara pamoja kupitia kampuni ya IPTL. Mradi huu harufu yake ilianza mwaka 1994, ukawa na mgogoro mkubwa, ukachelewa kuanza rasmi hadi mwaka 2000.

Mwaka 2006 waliingia mgogoro, hivyo ikabidi wapelekane mahakamani na kadiri siku zilivyokwenda wakalazimika kufungua akaunti ya kuhifadhi fedha zilizotoka Tanesco kutokana na kuzalisha umeme zijulikanazo kama ‘capacity charge’.

Uchunguzi wa kuchotwa zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow na kuuzwa mitambo ya kufua umeme ya IPTL kwa Kampuni ya Pan Africa Power (Tanzania) Limited (PAP), umefikisha miaka miwili sasa.

Vigogo wa Kampuni ya PAP mpaka sasa wanaendelea kusota rumbande kutokana na tuhuma za uchotwaji wa fedha hizo kwenye akaunti ya Escrow.

MKURURO WA KASHFA

Katika kuamua sakata hili la Trilioni 1.5, Bunge hili la 11 litakuwa na kazi nzito ya kupita kwenye njia ilizopita mabunge mawili yaliyotangulia ambayo ni Bunge la 10 na lile la tisa ambayo kwa pamoja walijadili kashfa zilizoikumba Serikali kwa weledi wa hali ya juu na kutoa maazimio yaliyosaidia kuwajibisha baadhi ya vigogo.

Itakumbukwa kuwa Bunge la tisa lililofahamika kwa sifa ya kasi na viwango lilifanya maamuzi mazito dhidi ya kashfa ya Richmond, huku Bunge la 10 likishughulikia kwa weledi kashfa ya Tegeta Escrow.