Home KIMATAIFA Senegal ya Aliou Cisse ni darasa la soka kwa Tanzania

Senegal ya Aliou Cisse ni darasa la soka kwa Tanzania

447
0
SHARE

NA MAWAZO LUSONZO

FAINALI  za  Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2019, maarufu kama mashindano ya Afcon zinaendelea kutimua  vumbi nchini  Misri, ambapo sasa inasubiriwa  hatua fainali.

Ni  fainali kati ya mataifa mawili ya Algeria dhidi ya Senegal ambayo  yametinga hatua  hiyo.

Kila mdau anayependa soka anatumia macho na masikio yake katika mashindano hayo, ambayo yanabakiza mechi  chache kabla ya kujulikana kwa  taifa  litakalotwaa  ubingwa wa  Afcon, ambayo ni mashindano makubwa kabisa kwa ngazi ya timu za taifa barani Afrika.

Wakati huu ambapo tunasubiri kujua Kombe la  Afrika kwa  ngazi ya  timu za  taifa  linatoa  ama Senegal au Algeria,kuna mengi ya kujifunza kwa  timu zote 24 zizoshiriki mashindano haya ya mwaka huu.

Funzo halitabakia kwa  timu zinazofanya  vyema tu, bali  hata zilizoboronga,  pia  kuna  jambo la kujifunza kutoka kwao.

Katika mengi yanayoendelea  katika fainali hizo za  mwaka  huu, mimi nimeliona  hili suala la makocha wazawa waliopewa  majukumu ya  kuzisimamia  timu za mataifa yao, ambalo  tulitazame kwa  jicho la tatu la darasa letu  la soka.

Achana  na makocha  wengi wanaoziongoza  timu za mataifa yao, wakiwa wazalendo, mimi nimemtupia  jicho huyu Aliou Cisse, ambaye analiongoza  jahazi la  Senegal, iliyotinga  fainali. Huyu ni  kocha mzawa.

Kocha  huyu nimemtaza kwa  jicho la tatu na kubaini ya kwamba, kupitia kwake kuna darasa  kubwa ,  hasa katika suala la kuaminika kwa wanandinga wetu wa zamani kwa mustakabali wa soka letu la ngazi ya kimataifa.

Simtazami Aliou Cisse kwa matokeo ya mechi zake zote hadi kuifikisha Senegal katika  hatua  hiyo, bali ni kocha mzawa aliyeonesha kuaminiwa na  taifa lake.

Kuaminiwa kwake ndiko  kunakomfanya aendelee kujiamini na kuaminika pia mbele ya  Wasenegal waliompa  jukumu  hilo.

Ikumbukwe kuwa,  ni Aliou Cisse  huyu  ndiye aliyeiwezesha  Senegal  kushiriki  fainali za  Kombe la  Dunia zilizofanyika mwaka huu nchini Urusi.

Kupitia mashindano ya Afcon ya mwaka  huu,  tunaliona  tena  jina la kocha huyo likiendelea  kutajwa kwa mafanikio na hivyo kutoa  funzo kuwa,  wanandinga wa zamani wakiaminiwa, wanaweza  wakayafikisha mbali mataifa   yao.

Walio na kumbukumbu watamtambua  Cisse huyu ambaye wakati  Senegal  ilipofuzu kwa mara ya  kwanza kabisa  kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2002, yeye alikuwa  nahodha wa kikosi hicho.

Cisse  mwenye umri wa 43, alianzia taaluma yake ya kucheza kandanda  katika klabu ya Lille OSC kabla ya kuhamia CS Sedan na kisha Paris Saint-Germain.

Alipanda ngazi kutoka kuwa naibu meneja hadi kaimu meneja na sasa amechukua usukani kamili wa timu.

Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Senegal kilichochukua nafasi ya pili katika  mashindano ya Afcon mwaka 2002 lakini alikuwa mmoja wa wachezaji waliopoteza penalti wakati wa fainali na kupoteza dhidi ya Cameroon.

Cisse aliteuliwa kuwa,  kocha msaidizi wa timu ya  taifa ya Senega mwaka 2010 na mwaka  2018 alipewa jukumu la kuwa Kocha Mkuu akiwa na timu hiyo nchini Urusi.

Ukiangalia kumbukumbu hii fupi, unapata picha ya namna wachezaji waliowahi kusakata  soka miaka ya nyuma  walivyo na  nafasi kubwa ya  kuchangia mafanikio katika  timu  zetu za  taifa.

Wanaweza kwasababu, wamepitia huko na  hata uzoefu wao unaweza kuwa  darasa  kubwa kwa wanandinga wa sasa, ama kwa kuwapa majukumu ya ukocha au kwa kuwatumia kama washauri.

Bahati tuliyonayo hapa nchini Tanzania,  hii ya kuwapo kwa wacheza  soka wengi waliolitumikia taifa kwa mafanikio.

Hawa ni baadhi ya wadau  tunaoweza kuwatumia katika kuendelea  kusaka maendeleo ya  timu zetu za taifa.

Kuna wengi wa kuwatolea mfano, wakiwemo akina Charles Boniface Mkwasa, Abdallah ‘King’ Kibadeni, Zamoyoni Mogella, Mohamed Adolf Richard, Malota  Soma, Peter Tino,Makumbi Juma na Hamis Kinye.

Hawa  niliwataja ni mfano tu wa namna ambavyo tunaweza kuwatumia wachezaji wa zamani kama wanavyofanya baadhi ya  wenzetu wa  mataifa  ya Afrika, wakiwemo Senegal  tunayoiangalia kwa  jicho la mafanikio ikiwa na mchezaji wa  zamani katika  benchi lake la  ufundi..

Ninachoendelea kuamini ni  kwamba, wachezaji wengi wa zamani  ni kama  darasa la kusaka mafanikio na matunda ya  soka la Tanzania katika medani ya kimataifa kwa ngazi ya  timu zetu za   taifa za rika mbalimbali.

Bahati njema ni kwamba ,wengi wao  bado wako hai na wameweka historia kama hawa wachache niliowataja, wakitumika vema wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa soka la Tanzania.

Kama  ilivyo kwa makocha kama Aliou Cisse anavyoweza kuwaongoza  Wasenegal katika michuano mkubwa kama hii ya  Afcon, naamini hata hawa wa  kwetu wanaweza.

Kinachohitajika hapa ni kuendelea kuwaamini na kuwatumia  pindi tunapoona  inafaa, kwasababu wana  uzoefu unaoweza kuwa darasa kwa ama viongozi wa  soka letu au kwa wachezaji wetu wa kizazi cha sasa.

Yote kwa yote, ninachoweza kusema kupitia mada hii ya  leo ni kwamba, wakati huu wa kuendelea kushuhudia  uhondo wa  soka wa fainali za Afcon, tuyachukulie mashindano hayo kama darasa hasa kwa wanaofanya  vyema.

Hivyo, wakati huu  tukimjadili  Aliou Cisse  katika jicho la  mafanikio kama  kocha mzawa, ni kipindi  pia cha  wenye mamlaka na soka la  Tanzania  kuendelea  kujifunza  kupitia mashindano ya  Afcon,  hasa kwa aina ya makocha.

Ninachoendelea kuamini ni  kwamba, wachezaji wengi wa zamani  ni kama  darasa la kusaka mafanikio na matunda ya  soka la Tanzania katika medani ya kimataifa kwa ngazi ya  timu zetu za   taifa za rika mbalimbali.

Wakiruhusiwa kutoa ushauri wao wanaweza kutusaidia hata kutueleza tumekwama wapi. Ni kweli wengine wametangulia mbele ya haki, lakini hawa walioko hai tumewatumia?

Kinachohitajika  hapa ni kuendelea kuwaamini na kuwatumia  pindi tunapoona  inafaa, kwasababu wana  uzoefu unaoweza kuwa darasa kwa ama viongozi wa  soka letu au  kwa wachezaji wetu wa kizazi cha sasa.

Wakati huu ambao Afcon  inakaribia kumalizika, ni kipindi mwafaka kwa  walio na mamlaka ya soka tukajifunza mengi kupitia mashindano  hayo, ikiwa pamoja na kumtazama Kocha Aliou Cisse kama  darasa.

Darasa la kutujengea  utamaduni wa  kuendelea kuwapa   fursa  baadhi ya wanandinga wa zamani ili waje kuwa msaada kwa  soka letu kuanzia ngazi ya  klabu na  timu za taifa za rika zote.

Hivyo,Senegal  iliyo  chini ya kocha  Aliou Cisse inaweza  kuwa  somo la  soka  letu  sambamba na kujifunza  yote mazuri  tuliyoyashuhudia kupitia mashindano  haya ya Afcon ya  mwaka  2019, ambayo  Tanzania tulishiriki na kuishia  hatua ya makundi.

Wahenga wamewahi kunena ya kwamba, Historia ni mwalimu mzuri wa kujifunza  kutoka humo. Waliocheza  soka zamani ni kilelezo  cha historia hii. Tusisite kuwatumia katika kusaka matunda  ya soka letu katika ngazi ya kimataifa.