Home Afrika Mashariki Seneta Seneta Mike Sonko ajitangaza Rais Kenya

Seneta Seneta Mike Sonko ajitangaza Rais Kenya

1470
0
SHARE

Machakos, Kenya

Ni kweli imetokea. Inawezekana kuchekesha au kufikirisha lakini wiki iliyopita Seneta asiyeisha vituko wa Nairobi, nchini Kenya alijitangaza kuwa ndiye Kaimu Rais hali iliyozua mtafaruku katika msiba. Seneta Sonko alikuwa katika msiba wa marehemu Dolamu Oduwole, aliyekuwa mume wa Wavinya Ndeti, Naibu Waziri wa zamani wa Vijana na Michezo.

Mwanamama Ndeti anatajwa pia kuwa anaweza kukalia kiti cha Ugavana wa Kaunti ya Machakos. Pia ni kiongozi wa chama cha CCU na mbunge wa zamani wa jimbo la Kathiani. Marehemu Oduwole, raia wa Nigeria aliyekuwa mfanyabiashara mkubwa pamoja na kutoka katika ukoo wa kifalme, alifariki kutokana na shinikizo la damu.

Wakati akihutubia Sonko alisema: “Rais Uhuru yuko nchini Togo, Kaimu Rais William Ruto yuko Ufaransa. Mimi ni namba tatu katika mamlaka kisiasa na kijamii. Sasa mimi ni Kaimu Rais wa Jamhuri ya watu wa Kenya,” alisema na kuongeza:

“Polisi wote waliopo hapa na magari yote ya serikali mnayoyaona hapa yameletwa kwa sababu mimi nakaimu nafasi ya Rais.”

Awali Sonko aliambiwa na Msimamizi wa shughuli hiyo kufupisha hotuba yake kufuatia muda wake wa dakika 10 kuisha na kisha akazimiwa kipaza sauti. Kuona vile, Sonko akaanza kumshambulia kwa maneno msimamizi wa shughuli hiyo, akimtaka amuache aendelee na hotuba yake. Tukio hilo liliambatana na Sonko kutoka sehemu kilipokuwa kipaza sauti na kumfata msimamizi wa shughului hiyo na kumrushia konde ambalo alilikwepa.

“Huwezi kunifanyia hivyo mimi, huwezi kunizimia kipaza sauti. Mbona wakati Raila anazungumza hakuna aliyemkatisha,” Sonko alisikika akipayuka na kuendelea.

“Hapana shika mimi..Taka taka ghasia nyinyi. Wasituletee kwendeni kabisa huko,” alisikika akipayuka. Baada ya muda Sonko anayetajwa pia kuwa na nia ya kuwania kiti cha nafasi ya Gavana katika Kaunti ya Nairobi alitakiwa kusoma hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta na mara alipoanza kusoma, watu wakaanza kumzomea na wengine wakipiga kelele.

“Unadhani hapa ni Jubelee. Kwenda huko,” watu walisikika wakisema huku umati wa watu wengine wakinyanyuka katika viti vyao na kuanza kuondoka. Katika kundi hilo la walioondoka ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa Upinzani nchini Kenya Raila Odinga, ambaye alionekana kunyanyuka na kisha kuondoka akifuatana na walinzi wake.

Baada ya tukio hilo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya Keriako Tobiko alitoa amri kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Joseph Boinett kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kisha kumpatia majibu ya uchunguzi huo ili achukue hatua. Kwa mujibu wa Tobiko, tukio hilo alilolifanya Sonko linaangukia katika kosa la uhaini na hivyo aliagiza uchunguzi ufanyike ili sheria ichukue mkondo wake.

Wafuatiliaji wa mambo na wanaomfahamu Seneta Sonko wanaeleza kuwa Seneta huyo alikuwa kapata kilevi kabla ya kuja hapo Msibani. Hata hivyo mke wa Marehemu Naibu Waziri wa zamani wa Vijana na Michezo Bibi Ndeti alisikika baada ya mazishi akimtetea Seneta Sonko licha ya ghasia aliyoisababisha katika msiba wa mumewe.

“Hakufanya kosa na wala hakusababisha ghasia. Sina tatizo naye kabisa. Alikaa hadi baada ya mazishi akabaki na familia yangu na gari lake lilitumika kuwapeleka majumbani baadhi ya waombolezaji,” alisema Bi. Ndeti.

Naye Sonko baada ya kuona hali ya hatari iko mbele yake, alianza kutoa sababu za kusingizia wapinzani wa Cord kuwa walichukua video ile na kuitengeneza kwa lengo la kumchafua na kusababisha ashtakiwe. “Mimi sikusema kuwa ni rais, bali nilisema ninakaimu nafasi hiyo kisiasa na kijamii na sio urais kwa mapana yake,” Sonko alisikika akizungumza huku akilaani wabaya wake walioko katika Muungano wa Cord kuwa ndio waliolikuza jambo hilo kwa lengo la kumchafua kisiasa.

Kabla ya Sonko, Raila alizungumza na kuelezea bayana kuwa hakutakuwa na mambo ya kisiasa katika msiba huo. “Tumekuja hapa kwa ajili ya mazishi. Mnaweza kuona Kalonzo Musyoka yuko hapa, Wetangula yupo na mimi nipo. Tuko pamoja. Ni vyombo vya habari vinavyosambaza habari za kutunga kwamba Muungano wa Cord utavunjika,” alisema Raila na kuongeza:

“Wanasema Wetangula atakimbia nje ya Cord, na kwamba Kalonzo naye pia ataondoka. Tena wanasema kwamba nitabaka peke yangu katika Cord. Haya yote ni uzushi tu.”

Baada ya habari hiyo kuchapishwa na gazeti la The Star, wachangiaji wengi katika mtandao wa gazeti hilo walionesha kukerwa kwao na tabia mbaya za Seneta Sonko, huku wengine wakielezea kuwa, wananchi wa Nairobi wameweka fedha mbele badala ya kuangalia uhalisi wa maisha na tabia ya kiongozi kabla ya kumchagua.

Mmoja wa wachangiaji hao, Sialo Sururu aliandika: “Sonko anaamini anayo haki ya kuzungumza namna yoyote vile anayotaka na kuishi anavyotaka. Anaweza kutoheshimu yeyote na hata kudharau hadhi ya urais. Hata hivyo ni sisi wananchi wa Nairobi ambao tulimpatia nafasi ya kutuongoza huku tukifahamu fika kuwa mipaka ya Sonko inatokana na uwezo wake wa fedha.

“Hatuna sababu ya kulalamika tumuache tu aendelee kufanya maana sisi ndio tuliompatia mamlaka na kubwa ni kuonesha jeuri ya fedha zake. Tusilalamike na wala tusiwaze kuhusu heshima kutoka kwake. Pia tusitarajia kuona viwango vyua uongozi bora kutoka kwake. Tumuache aendelee kutuongoza kwa fedha zake.”

Mchangiaji mwingine aliandika: “haya ndiyo matokeo ya Rais Uhuru kuchukua watu aina ya Sonko na kwenda nao kwenye nyama choma…baada ya nyama choma naye anajiona yuko nafasi ya tatu katika utawala wa Kenya. Huyu ni seneta anayelipwa Shilingi milioni moja ya Kenya kwa mwezi na bado hajui itifaki ya uongozi serikalini.”