Home Makala SENETI ‘YAMTUMBUA’ MAGU

SENETI ‘YAMTUMBUA’ MAGU

1356
0
SHARE

ABUJA- NIGERIA


Seneti ya Nigeria wiki iliyopita imekataa kumuidhinisha Ibrahim Magu, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Rushwa na Ufisadi (Economic and Financial Crimes Commission (EFCC), kutokana na sababu za kiusalama.

Katika ripoti yao ya siri kwenda kwa Rais Muhammadu Buhari, yenye kurasa 14, Seneti imefafanua kuwa Magu ameonekana kukosa maadili yanayomhitaji mtu wa kukalia nafasi hiyo. Ripoti hiyo inafafanua zaidi kuwa kumpatia nafasi hiyo Magu, ni kusababisha mazingira magumu ya uchunguzi wa rushwa na ufisadi katika nchi hiyo.

Seneti hiyo, licha ya kumuweka pembeni Magu, imethibitisha teuzi za majina manne ya wajumbe wa bodi ya EFCC ambayo yaliwasilishwa pamoja na jina la Magu kutoka kwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo Yemi Osinbanjo. Majina hayo yaliwasilishwa na Makamu huyo wa Rais mwezi Julai, wakati Rais Buhari akiwa nje ya nchi kwa matibabu.

Taarifa ya siri kutoka katika Idara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, pamoja na masuala mengine, ilionesha kuwa Magu anapata kitita cha fedha za Nigeria Naira milioni 20 kwa ajili ya kulipia makazi yake katika nyumba aliyokodisha na mfanyabiashara mmoja ambaye EFCC inamchunguza kwa tuhuma za rushwa.

Masuala mengine anayohusishwa nayo Magu, ni aina ya maisha ya anasa pamoja na kukaidi amri ya Rais Buhari iliyopinga maafisa wa Nigeria kusafiri Daraja la Kwanza katika ndege wanapo kwenda nje ya nchi. Magu alitumia daraja hilo wakati akienda kuhiji Makka.

Hata hivyo msemaji Kamati ya Habari na Mahusiano ya Seneti, Seneta Aliyu Abdullahi, alipata wakati mgumu kutoka kwa mashabiki wa Magu ambao hawakutaka kusikia chochote kutoka kwa viongozi wa Senate, huku wakilalama kuwa madai hayo hayana msingi na kwamba yana nia ovu dhidi ya Magu.

Mashabiki wa Magu wanaeleza kuwa, Magu katika kipindi chake ambacho amekaimu nafasi hiyo, amefanya mengi katika kukabiliana na ufisadi na rushwa nchini humo. Ikumbukwe pia kuwa kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi, ilikuwa ni moja ya mambo makubwa aliyoahidi Rais Buhari kukabiliana nayo katika serikali yake.

Seneta Abdullahi aliwaambia waandishi kuwa: “Seneti baada ya kupata taarifa na kujiridhisha kuwa yapo matendo ambayo yanamuondolea hadhi Magu, imeamua kutoendelea na mjadala na kutomthibitisha Magu na kwamba inarejesha jina lake kwa mamlaka ya uteuzi.

Gazeti la Vanguard la Nigeria, lilifanikiwa kupata ripoti ya paragrafu 14 iliyotoka kwa Mkurugenzi wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Folashade Bello, ambayo aliikabidhi kwenye Seneti na kusomwa na Seneta Bukola Saraki. Nakala ya taarifa hiyo hata hivyo, haikusambazwa kwa Maseneta wote, bali ilitolewa kwa ajili ya Katibu wa Seneti ikiandikwa kuhusu ombi la kufanya ukaguzi wa mteuliwa Magu.

Taarifa hiyo ilisema, Mwezi Agosti mwaka 2008, kufuatia ukaguzi katika makazi ya Mteuliwa wa nafasi ya Mwenyekiti, yaani Magu, walifanikiwa kukuta taarifa za EFCC ambazo hazikupaswa kuwa katika mikono ya Magu zikiwa katika makazi yake. Kufuatia tukio hilo, alikamatwa na kuhojiwa na Polisi, na baadaye akafukuzwa kazi. Mwezi Desemba 2010, Polisi ilimtia hatiani Magu kwa makosa ya kuweka usalama wa nchi katika mashaka, na hivyo kutakiwa kupewa adhabu kali.

Lakini cha kushangaza, mwaka 2011, baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti mpya wa EFCC, Ibrahim Lamorde, alimrejesha Magu EFCC kwa hitaji maalumu. Wawili hawa walikuwa wamehudumu pamoja huko nyuma, wakati Lamorde akiwa Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji. Magu aliendelea kuwa afisa wa juu wa kitengo hicho, hadi alipoteuliwa kukaimu nafasi ya Lamorde

“Magu kwa sasa anakalia nyumba inayolipwa  Naira 40 millioni ambazo ni sawa na Naira 480 millioni kwa mwaka. Makazi hayo yanaelezwa kuwa hayakulipiwa na fedha za EFCC. Tena Magu ameonekana mara kwa mara akifanya safari rasmi na binafsi akitumia ndege binafsi, Easy Jet.

Katika safari mojawapo, Magu alisafiri kwenda Maiduguri akiwa na Mkurugenzi wa Benki, ambaye amekuwa akichunguzwa na EFCC kwa madai ya kutakatisha fedha zilizopotea kipindi cha Waziri wa Mafuta Alison-Madueke.

“Pia Kaimu huyu wa EFCC ameendelea kuishi maisha ya anasa, na akakaidi amri ya Rais Buhari iliyokataza watumishi wa umma kupanda ndege Daraja la Kwanza. Juni 24, 2016, Magu alipanda Daraja la Kwanza ndege ya Shirika la Emirates kuelekea Hijja nchini Saudi Arabia. Gharama za Hijja hiyo zilikuwa kiasi cha Naira 2,990,196.00.

Kutokana na ripoti hiyo, Magu amekuwa akiwatumia Polisi alio karibu nao, kufunika au kuficha mambo yake na kwamba oparesheni zake nyingi amekuwa akiwatumia hao. Kutokana na hali hiyo, uchunguzi umegundua kuwa kuna kundi la Polisi linalomiliki mali nyingi na  kuhusishwa na polisi watiiifu wa Magu.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Seneti haukufikiwa kirahisi. Kulikuwepo hali ya kutupiana maneno kati ya Maseneta, ambapo Kiongozi wa Maseneta, Ali Ndume, ilimpasa kukabiliana vilivyo na Seneta Dino Melaye, ambaye anatoka jimbo la Borno anakotoka Magu.

Upande wa Ofisi ya Rais, umeendelea kusisitiza kuwa, haukuwa katika wakati wa kutoa majibu na kwamba ulikuwa ukisubiri taarifa rasmi ya Seneti, huku pia Seneti ikitoa majibu kwa Magu kuwa, suala lake linarudishwa kwa Rais.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Rais kuhusu masuala ya Rushwa, Itse Sagay, alisikika akisema kuwa, kutomthibitsha kulikofanywa na Seneti, kusitarajiwe kuwa ndio kuondoka kwa Magu katika nafasi yake.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Vanguard, Sagay alisema: “Wamtake au wamkatae, Magu ataendelea kuwa katika nafasi hiyo. Nafasi yake ya Uenyekiti wa itaendelea kuwepo. Tangu Nuhu Ribadu aondoke katika nafasi hiyo, hatujapata mtu mwenye uwezo mkubwa katika nafasi hiyo zaidi ya Magu. Atakuwa katika nafasi hiyo hadi amalize muda wake,” alisema Sagay kabla Seneti haijapitisha maamuzi ya kukataa jina lake.

Tume hiyo inayokabiliana na masuala ya ufisadi na rushwa, imeanzishwa kwa sheria iliyopitishwa mwaka 2004, na katika sheria hiyo, suala la uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, liko kimya katika suala la kukaimu nafasi hiyo. Ibara ya 2 (3) ya uanzishaji wa EFCC, inaelezea kuwa Mwenyekiti wa EFCC na makamishna wa tume hiyo, watateuliwa na Rais na kisha uteuzi huo utapaswa kuthibitishwa na Seneti.

Ibara ya 3 (1), inaeleza kuwa, wateule hao wakishathibitishwa na Seneti, watatumikia nafasi zao kwa miaka mine, na wanaweza kuteuliwa tena kwa kipindi cha miaka mingine mine na sio vinginevyo.