Home Makala SERA YA UONGOZI WA NCHI NA USIMAMIZI WA MASILAHI YA TAIFA

SERA YA UONGOZI WA NCHI NA USIMAMIZI WA MASILAHI YA TAIFA

747
0
SHARE

NA ABBAS MWALIMU,

KATIKA miaka ya karibuni kumejitokeza changamoto nyingi za kiuongozi na kiutawala ikiwa ni pamoja na usimamizi hafifu wa mambo au vitu vyote vinavyobeba masilahi ya Taifa kwa baadhi ya wale waliopewa dhamana hiyo. Kuanzia utawala wa awamu ya tatu tumeshuhudia kuibuka kwa kashfa mbalimbali dhidi ya baadhi ya viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia na kuendeleza masilahi hayo ya Taifa.

Mambo kama vile rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa mali za uma, uhujumu uchumi, madawa ya kulevya, kuwepo kwa baadhi ya viongozi wasiokidhi matakwa ya idara, mamlaka, taasisi ama wizara husika kwa ujumla vimepelekea kufanyika kwa mabadiliko ya mara kwa mara katika maeneo tofauti ya Serikali. Awamu hii ya tano mabadiliko haya yamekuwa na jina maarufu ya ‘Utumbuaji majipu’.

Baada ya wiki iliyopita kuelezea namna ambavyo Taifa linaweza kurudi katika mstari mnyoofu kwa kuandaa sera ya Taifa ya uongozi wa nchi ambayo italenga katika kuwaongoza wale watakaopata mamlaka ama madaraka ya kuongoza na kusimamia masilahi ya Taifa kizalendo. Huu ni muendelezo wa sehemu ya mwisho kuhusu ufafanuzi wa sera hiyo ya Taifa.

Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na maono ya kipekee sana katika kuongoza nchi. Ninasema ni maono ya kipekee kwa maana tukumbuke kuwa mwaka 1962 mwaka mmoja tu baada ya Uhuru wa Tanganyika, Mwalimu aliandika Chapisho la Ujamaa na Misingi yake ikijieleza kuwa Ujamaa ni imani iliyojijenga ndani ya misingi ya Uzalendo. Hapa tunagundua kuwa Mwalimu Nyerere alitaka tuwe na sera ya ndani ya kutuongoza kama nchi. Andiko hili ndilo ambalo baadaye Februari 5, mwaka 1967 ikiwa ni miaka sita baada ya Uhuru, lilitangazwa na kupitishwa kama Azimio la Arusha.

Kimsingi, Mwalimu Nyerere baada ya Tanganyika kupata Uhuru aliona kama Taifa tunapaswa kuwa na sera yetu ya ndani itakayotuongoza katika kusimamia na kuyaendeleza masilahi yetu na ndiyo maana lengo kuu la Azimio la Arusha lilikuwa kuleta ukombozi wa kiuchumi  (Masilahi ya Taifa) chini ya misingi ya Ujamaa na Kujitegemea.

Miiko ya uongozi iliyoainishwa katika andiko la Mwalimu Nyerere la mwaka 1962 ambayo baadaye ilirithiwa na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) inaonesha dhahiri kuwa Mwalimu Nyerere alitaka Azimio la Arusha liwe ndiyo Sera ya ndani ya Taifa inayolenga pia kutuongoza namna ya kupata viongozi waadilifu na usimamizi bora wa masilahi ya Taifa.

Kwa bahati mbaya mnamo mwaka 1992, Azimio la Arusha lilikuja kufifishwa na Azimio la Zanzibar ambalo lililenga kuiongoza nchi katika uchumi wa soko  huria kufuatia masharti ya kisera yaliyotolewa na taasisi za kimataifa za Bretton Woods yaani Benki ya Dunia (World Bank) na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa yaani IMF.

Miongoni mwa masharti ya taasisi za Bretton Woods ambayo kwa namna moja ama nyingine yalikuwa ni magumu kwa nchi yetu kuweza kuyatekeleza na kupelekea athari katika utekelezaji wa Azimio la Arusha, ni pamoja na kuzilazimisha nchi zote zinazotaka misaada, kufanya uchumi wa soko huria ikiwa na maana ya kuwa Serikali kutofanya biashara wala kuingilia na kuweka vikwazo vya kiforodha na visivyo vya kiforodha kwenye biashara, kuwa na demokrasia ya vyama vingi yenye kufuata misingi ya uchaguzi huru na wa haki pamoja na uhuru wa kujieleza, kubinafsisha viwanda pamoja na kushusha thamani ya sarafu.

Tukumbuke kuwa sarafu yetu kwenye miaka ya 1970 hadi 1980 ilikuwa na nguvu kiasi kwamba ilifika wakati pauni moja ya Uingereza ilikuwa sawa na Sh 20 ambayo kwa wakati ule mtaani ilijulikana kama Pauni. Si hiyo tu, hata Dola moja ya Marekani kipindi hicho ilikuwa sawa na Sh tano ya Tanzania na ndiyo sababu iliyopelekea mabasi ya abiria kwenye Mji wa Dar es Salaam wakati ule mpaka sasa kujulikana kama daladala kwa kuwa nauli yake ilikuwa Sh tano ambayo ni sawa na Dola moja kwa wakati huo. Hapo utagundua ni jinsi gani sarafu yetu ilikuwa na thamani ukilinganisha na sasa.

Masharti mengine yalikuwa kama vile uwazi katika uongozi na matumizi ya Serikali (Transparency), ndiyo maana tuliona kipindi cha utawala wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali iliingia na kusaini mkataba wa uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi yaani Open Government Partnership kwa kifupi OGP. Sambamba na hilo, suala la kufuatwa kwa Utawala wa Sheria kwa kingereza Rule of Law pia lilikuwa sehemu ya masharti hayo.

Tukumbuke kuwa nchi yetu kipindi hicho ilikuwa imetoka kuathiriwa vibaya kiuchumi na vita na nchi ya Uganda katika kulikomboa eneo la Kagera mnamo mwaka 1978 hadi 1979, hivyo kuhitaji misaada ya namna ya kipekee kuweza kuhuisha uchumi wetu.

Kutokana na masharti hayo ya kimuundo na kisera yaliyotolewa na taasisi za Bretton Woods, iliilazimu Tanzania kuandaa mpango wa kurekebisha muundo wa kiuchumi uliofahamika kama Structural Adjustment Program (S.A.P) ambao nao kimsingi iliutohoa kutoka kwenye taasisi hizo.

Wapo wanaodhani na kuamini kuwa masharti yaliyowekwa na taasisi za Bretton Woods ndiyo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuamua kuachia madaraka na kupumzika kwa kuamini kwamba sera ya ndani ya Taifa ya Azimio la Arusha ambayo alitamani iwe ndiyo msingi wa kuongoza nchi imekufa, kitu ambacho kwangu sidhani kama ni sahihi. Kimsingi Mwalimu Nyerere aliona ipo haja ya kuwapa nafasi wengine baada ya kuongoza nchi kwa miaka 20 na tatu toka tulipopata uhuru mwaka 1961.

Kimantiki tunagundua kwamba baada ya kuletwa kwa masharti ya kimuundo na kisera ya Bretton Woods sambamba na Azimio la Zanzibar la mwaka 1992 lililoshadihisha nchi kuingia katika uchumi wa soko huria Azimio la Arusha la mwaka 1967 ambalo ndilo limebeba sera halisi ya ndani ya Taifa (Domestic Policy) lilififishwa nguvu yake ama kupotea kabisa, hivyo kuifanya nchi yetu kukosa chombo kutuongoza kama dola kwa maana ya sera ya ndani.

Nikiri wazi tu kuwa ninafurahishwa sana na juhudi za kizalendo za Rais wetu wa Awamu ya Tano, John Magufuli katika kusimamia masilahi ya Taifa, ingawa anakumbana na changamoto mbalimbali. Mfano mzuri ni hivi karibuni jinsi alivyoliendea suala la mchanga unaosadikiwa kuwa na madini, inaonesha dhahiri anavyoguswa na upotevu wa rasilimali zetu ambazo ni sehemu ya masilahi ya Taifa. Ninadhani ipo haja kwa Serikali kupitia upya mikataba yote ya madini sambamba na mikataba mingine inayobeba masilahi mapana ya Taifa.

Licha ya juhudi zote zionazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, bado ukweli unabaki kuwa ni muhimu sana kwa Taifa kuwa na sera ya ndani ya uongozi wa nchi na usimamizi wa masilahi ya taifa ambayo itaainisha vigezo kuwa ni kiongozi wa aina gani, mwenye tabia na hulka zipi Taifa linapaswa kuongozwa naye. Miongoni mwa vigezo ambavyo hata kwenye miiko na maadili ya TANU vimeainishwa ni kama vile utu, uzalendo, uadilifu, ukweli, mwenye kuweza kulinda umoja wetu wa kitaifa, mwenye kutambua wanadamu wote ni sawa, uchapakazi na uwajibikaji. Vigezo kama hivi vitawaongoza wale wote wenye nia ya kugombea uongozi katika ngazi yoyote ya kisiasa ama kijamii kujipima navyo na kuona kama wanatosha kuongoza ama hawatoshi. Lakini pia hata wale wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali nao wapimwe kwa vigezo hivi. Ninatambua kuwa Serikali inapotaka kupata ama kuteua viongozi kushika nyadhifa mbalimbali hutumia wataalamu wake kubaini wale wanaotarajiwa kabla ya kuteuliwa lakini bado ninaamini uwepo wa sera hii na sheria yake utarahisisha maamuzi ya Serikali kufanyika kwa urahisi mno.

Sera hii pia ibainishe ni vipi viongozi hao watawajibika kusimamia, kutetea, kuyapigania na kuendeleza masilahi ya Taifa. Kwa msingi huu tutakuwa na viongozi wenye karima na tajiriba zinazofanana katika kuongoza na hivyo kurahisisha kusukuma gurudumu la maendeleo yetu mbele kwa urahisi mno. Sambamba na hilo tutakuwa tumeepuka kuwa na viongozi wenye lengo la kujinufaisha kupitia mamlaka na madaraka wanayoyapata, tabia za ulaji rushwa, kuhujumu uchumi na mengine mengi yasiyofaa.

Ni imani yangu kuwa Serikali inaweza kuangalia ni namna gani ya kuirekebisha Sheria namba 13 ya Mwaka 1995 ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kuangalia uwezekano wa kutohoa baadhi ya vipengele vya kwenye Azimio la Arusha la mwaka 1967 ili kupata sera mpya ya Sera ya Taifa ya Uongozi wa Nchi na Usimamizi wa Masilahi ya Taifa ambayo itatafsiriwa na sheria mpya ya Uongozi wa Nchi, Maadili ya Viongozi wa Umma na Usimamizi wa Masilahi ya Taifa ambayo itakuwa imejumuisha vitu vyote yaani uongozi wa nchi, maadili, miiko na masilahi ya Taifa.

Makala haya yameandaliwa na:

Abbas Mwalimu (Abbas Abdul Mwalimu)

Mchambuzi wa Masuala ya Siasa za Kimataifa na Diplomasia.

Anapatikana kwa namba 0719 258 484