Home Latest News SERENGETI BOYS YAPANIA MAKUBWA GABON

SERENGETI BOYS YAPANIA MAKUBWA GABON

1828
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

WAKATI kikosi cha Serengeti Boys, kikiwa kinajiandaa kwenda kushiriki fainali za Afrika kwa vijana nchini Gabon mapema mwezi Mei mwaka huu, wachezaji wamekuwa na matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa.

nahodha wa kikosi hicho Dickson Nickson, ameonekana kuwa na matumaini kibao juu ya kikosi hicho kuibuka mabingwa kwenye kundi B.

Katika michuano hiyo, Tanzania imepangwa kundi B ikiungana na timu kutoka Mali, Angola pamoja na Nigeria.

Mbali na kujituma ipasavyo kuhakikisha Tanzania inaibuka kidedea katika fainali hizo nahodha wa Serengeti Boys, Dickson Nickson ameweka wazi mkakati wao wa kuhakikisha wanapigana kufa na kupona ili waandike historia kwa kutwaa kombe hilo.

Dickson alitoa msimamo huo katika mahojiano maalum na RAI hivi karibuni.

Katika mahijiano hayo nyota huyo amefunguka mambo mengi juu ya safari yake ya soka kule alipotoka, alipo hivi sasa na anapoelekea.

RAI: Unaizungumziaje safari yako ya soka kwa muda mfupi uliojikita kwenye mchezo huu?

DICKSON: Safari yangu sio ndefu sana wala fupi, lakini namshukuru Mungu mpaka hapa nilipofikia kwani nisingekuwa Serengeti Boys mapenzi ya muumba.

RAI: Njia gani umepita kufika hapo ulipo?

DICKSON: Njia nilizopita mimi kufika hapa nilizianza mwaka 2015 kupitia mashindano ya Shule za Sekondari ( UMISETA) nikiwa mkoani Morogoro katika shule ya Academic na baadaye kuitwa katika kombaini ya wilaya na baadaye mkoa.

RAI: Kipi kilikusababishia kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Serengeti Boys?

Dickson: Sababu kubwa ni kutokana na uwezo niliouonesha kipindi chote nacheza, naamini wapo wadau mbalimbali wenye kufuatilia soka ndani na nje ya mkoa wa Dar, hao ndio waliona kipaji changu na kunitunuku.

RAI: Zipi changamoto ulizokutana nazo kipindi chote unacheza soka?

Dickson: Changamoto zipo nyingi sana, kwanza kabisa ushindani wa namba, kama unavyojua mimi ni beki wa kati nafasi ambayo sichezi peke yangu wapo wenzangu ambao kila mmoja anapigana kufa na kupona kupata namba.

RAI: Yapi matarajio yako kwenye soka?

DICKSON:Matarajio yangu kwenye mchezo huu ni makubwa sana, kwanza nataka kucheza kwa bidii katika kila michuano ili timu yangu ipae kimataifa.

Mbali na hilo, nina ndoto za kuwa mchezaji mkubwa kimataifa, nataka ifike siku moja na mimi nisajiliwe kucheza timu za Ligi Kuu barani Ulaya, naamini nitaipa sifa nchi yangu.

RAI: Hivi karibuni tumeshuhudia mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga kwa upande wako uzi rangi gani unaukubali hapo?

Dickson: Kwa kweli mimi timu zote nazikubali, na nina amini kila mchezaji hapo ana kiwango kikubwa ndio maana kasajiliwa kwenye klabu hizo kubwa, natoa pongezi tu kwa Simba kwa kuibuka mabingwa pia niwasifu Yanga kwa kucheza kwa kiwango cha hali ya juu.

RAI: Mchezaji gani wa ndani unakubali kiwango chake?

Dickson: Namkubali sana mchezaji wa zamani wa klabu ya Azam, Serge Pascal ‘Wawa’, huyu jamaa ana kiwango cha Kimataifa, pongezi nyingi kutoka kwangu zimfikie.

RAI: Vipi kura yako Kimataifa unaidondosha kwa mchezaji gani?

Dicson: Kimataifa namkubali sana mchezaji Leonardo Bonucci, ananivutia sana na kunifanya nijitume kwenye kazi yangu kwakuamini siku moja nitafika pale alipo.

RAI:Tueleze mipango ya kikosi chako kuelekea safari ya Gabon?

Dickson: Safari ya Gabon naweza kusema ipo vizuri, niwaahidi Watanzania tutajituma kuhakikisha tunaipeperusha vema bendera ya nchi na kuiletea heshima nchi yetu.

RAI:Baada ya kupata taarifa juu ya nchi mtakazokutana nazo kwenye michuano hiyo kundi B yapi maandalizi ya mapema mlioanza nayo kujiweka tayari na wapinzani wenu?

Dickson: Moja ya harakati tulizofanya ni kuangalia ‘CD’ za timu tutakazokutana nazo tuna amini zitatusaidia kumjua mchezaji mmoja mmoja ili tuweze kuwamiliki kikamulifu tutakapokutana nao.

RAI: Katika harakati zenu za kuwafuatilia wapinzani wenu nchi gani mnaihofia na mchezaji yupi anayekupa joto kuelekea michuano hiyo?

Dickson: Kwa upande wetu mpaka sasa hakuna nchi yoyote inayotunyima usingizi kikubwa tunajipanga kuhakikisha tunafanya vema, kwa upande wa mchezaji yupo mmoja kutoka Mali anayevaa jezi namba 19, pamoja na hilo nitahakikisha namzidi maarifa ili tufanye vizuri.