Home Michezo SERENGETI BOYS YAWEKA HISTORIA

SERENGETI BOYS YAWEKA HISTORIA

1547
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

NI historia nyingine tena inawekwa na vijana wadogo katika ulimwengu wa soka wakionekana dhahiri kutaka kuwafuta machozi watanzania kupitia mchezo huo unaopendwa zaidi siyo tu Tanzania bali ulimwenguni kote.

Kwa mara nyingine ni Timu ya soka ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambayo kwa mara ya kwanza inashiriki fainali za Afrika katika michuano inayoanza mwishoni wma wiki hii nchini Gabon.

Serengeti Boys ilipata nafasi hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2003 lakini kabla ya kutua katika fainali hizo ikaenguliwa baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kubaini udanganyifu wa umri kwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo akiwemo Nurdin Bakari.

Ilikuwa ni pigo kubwa sana katika historia ya soka la Tanzania na toka wakati ule ilizima kabisa ndoto na hata hamasa ya vijana kupamba kuisaka nafasi hiyo, kabla ya kuipata tena mapema mwaka huu baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Congo Brazaville waliyemchezesha mchezaji ‘kijeba’ Langa Lesse Bercy.

katika mchezo baina yao uliomalizika kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini hivyo kutupwa nje ya mashindano.

Miezi miwili iliyopita CAF iliridhika na ukiukwaji wa kanuni hizo hivyo kuipa nafasi Tanzania ambayo toka ipewe nafasi hiyo imeonekana kuwa ‘bize’ kwa kufanya jitihada za dhati kabisa katika maandalizi ya timu hiyo kuwa ya ushindi.

Safari ya kwenda Gabon haikuwa rahisi kwani katika mchezo wao wa kwanza walipambana na kufanikiwa kuishinda Shelisheli kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza kabla ya kurudiana ugenini na kushinda mabao 6-0. Wakapangiwa kucheza na Afrika Kusini na kutoka sare ya bao 1-1 ugenini lakini wakashinda mabao 2-0 nyumbani.

Mchezo wao wa mwisho kufuzu ulikuwa dhidi ya Congo ambapo wakiwa nyumbani walishinda kwa mabao 3-2 lakini wakiwa ugenini wakapoteza kwa bao 1-0 na kuamua kumkatia rufaa mchezaji Langa Lesse Bercy na hatimaye kuikwaa nafasi hiyo.

Katika mechi za kimataifa za kirafiki saba ilizocheza kujiandaa na fainali hizo Serengeti Boys imeshinda mechi tano, sare moja na kupoteza moja. Iliifunga Burundi katika mechi zote mbili kwa mabao 2-0 na kisha 3-0, kabla ya kutoka sare na Ghana kwa mabao 2-2.

Baadaye ikaishushia kipigo Gabon kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza na idadi kama hiyo katika mechi ya pili na kufuatia na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cameroon katika mechi ya kwanza na klisha kukubali kipigo cha bao 1-0 katika mechi ya marudiano.

Bila shaka sasa watanzania wanaelekeza macho na masikio yao nchini humo huku wakiiombea dua Serengeti Boys iweze kufanya maajabu zaidi kwa kutwaa ubingwa wa Afrika na kuandika historia mpya itayodumu milele katika historia ya soka Tanzania katika anga la kimataifa.

Licha ya ugumu wa michuano hiyo inayotarajiwa kushirikisha jumla ya mataifa nane ukweli unabaki kuwa Serengeti Boys wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika fainali hiyo huku wakilindwa na rekodi nzuri waliyonayo.

Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa imeonesha kutoa sapoti kubwa katika kuhakikisha historia mpya inaandikwa. Kupitia kiongozi huyo aliendesha kampeni ya kuisapoti timu kwa kuhamasisha watanzania kuichangia zoezi ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana licha ya Shirikisho la Soka Tanzania kutoweka wazi michango ambayo tayari wameshakusanya.

Kupitia harambee iliyofanyika wiki mbili zilizopita wadau mbalimbali kuanzia kampuni, vikundi na hata wanamichezo mmoja mmoja walijitokeza kuchangia zoezi ambalo lilitoa taswira ya mafanikio.

Pengine hiyo inakua matumaini pekee kutokana na ukweli kuwa katika historia ya soka nchini hakuna timu kuanzia ya klabu hadi taifa iliyowahi kutwaa ubingwa katika mashindano makubwa ya kimataifa yanayoatambuliwa au kuandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Timu ya Taifa ya Tanzania ilijaribu na kufanikiwa kucheza fainali za Afrika wakati huo michuano ikijulikana kama Kombe la Mataifa Huru ya Afrika (sasa Afcon) mwaka 1980 na kushindwa kuwika hivyo kutolewa katika hatua za awali za makundi.

Taifa Stars kwa mara nyingine ikiwa chini ya Kocha, Marcio Maximo ilifuzu kucheza fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ‘CHAN’ mwaka 2009 lakini hata hivyo nayo ikatolewa mapema katika fainali hizo.

Toka wakati huo hadi sasa imekuwa ikijaribu mara kadhaa bila ya mafanikio achilia mbali pia kutafuta nafasi ya kucheza fainali za Dunia.

Timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ nayo ilipata nafasi kama hiyo mwaka 2010 ilipofuzu kucheza fainali za Afrika upande wa wanawake huku ikipangwa kundi moja na timu za Nigeria, Mali na wenyeji Afrika Kusini iliambulia patupu na kutolewa katika hatua ya makundi.

Sasa ni zamu ya Serengeti Boys kufanya kile ambacho kimeshindwa kufanywa na wakubwa zao ‘Taifa Stars’ pamoja na Twiga Stars.

Ikiwa kundi moja na timu za Mali, Angola na Niger kuna kila sababu nguvu kubwa kuendelea kuwekwa nchini Gabon kuhakikisha Serengeti Boys inaweka historia mpya.

Mchezo wake wa kwanza katika fainali hizo dhidi ya Mali wiki ijayo bila shaka utatoa mwanga ya itakachokifanya nchini humo na pemngine kuwa faraja kwa soka la Tanzania.

Ubora wa kikosi hicho kilicho chini ya mdenmark Kim Paulsen na Bakari Shime ni uimara wa karibu safu zote muhimu kama vile ushambuliaji, kiungo na ulinzi ambapo katika mechi hizo saba za kimataifa za kirafiki imefunga mabao 12 na kufungwa matano tu.

Kikosi kinachoipeperusha bendera ya Tanzania nchini Gabon kinaundwa Ramadhan Kabwili, Samwel Edward na Kelvin Kayego (makipa). Walinzi ni Nickson Kibabage, Israel Mwenda, Issa Makamba, Kibwana Shomari, Ally Msengi, Enrick Vitalis Nkosi na Dikson Job.

Wengine ni Kelvin Nashon Naftali, said Mussa, Mathias Juan, Najim Mussa, Marco Gerald, Abdulhamn Suleiman, Cyprian Mtasigwa, Shaban Ada, Mohammed Rashid Ng’anzi (Viungo) huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Yohana Mkomola, Muhsin Makame, Ibrahim Abdallah, Abdul Suleiman na Assad Juma.

Ni rekodi nzuri kwa timu ambayo ndiyo kwanza imetengenezwa kufuatiwa msingi ulioanza kuwekwa na Rais wa zamani wa TFF, Leodeger Tenga kuaniza mwaka 2004 ambapo alizuia ushiriki wa timu za vijana ili kwanza kutengeneza msingi pamoja na mfumo mzuri.

Katika msingi huo ndiyo sasa matokeo yanaanza kuonekana kwa timu hiyo ambayo hakika imepata matunzo mazuri kutoka wka uongozi wa sasa TFF chini ya Jamal Malinzi.

Kila la kheri Serengeti Boys, kila la kheri Tanzania.