Home Tukumbushane SERIKALI HAIKUWATENDEA HAKI WASTAAFU EAC

SERIKALI HAIKUWATENDEA HAKI WASTAAFU EAC

1144
0
SHARE

 

NA HILAL K SUED

SABABU kubwa inayopelekea Serikali hii kutokubali madai ya waajiriwa wake, mfano madaktari na walimu na wa sekta nyingine inatokana na tabia au tuseme utamaduni uliojengeka kwa watendaji katika Serikali hiyo na haitokani na zile sababu zinazotajwa kila siku, kama vile Serikali kutokuwa na fedha.

Baadhi ya watendaji wa Serikali yetu wana tabia ya unyimi, au kwa maneno mengine ubakhili. Hawapendezwi na watu wengine, kumiliki pesa nyingi. Na hii iwe katika kuwalipa mafao yao stahiki au fidia kutokana na ardhi yao kutwaliwa na Serikali kwa shughuli zake za miradi ya maendeleo au hata kumpatia mwekezaji. Hapo ni hata kama fedha husika za fidia ilitoka kwa mwekezaji kupitia Serikali.

Historia inatueleza kwamba ulimwenguni kote nchi mbalimbali zimekuwa zinakabiliwa na changamoto ya jinsi Serikali inavyoweza kukidhi mahitaji ya watu wake. Hili lina ukweli zaidi kwa ulimwengu wa leo ambapo elimu ikichangiwa na teknohama inasambaa kwa kasi hivyo kuweka shinikizo kwa tawala kusikiliza sauti za wananchi wake na  kutimiza mahitaji yao.

Hivyo basi ingawa kuna umuhimu kwa serikali kubakia imara, lakini ni lazima pia zishughulikie kwa uchangamfu unaostahili masuala muhimu yanayowagusa wananchi wake, na pia kuzihimiza taasisi zake kutimiza wajibu wao kwa wananchi.

Hapa Tanzania siku zote kumekuwapo malalamiko kwamba mishahara na malipo mengine stahiki kwa wananchi ni midogo sana ukilinganisha na nchi nyingine za jirani, hususan zile zilizomo katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki au hata katika nchi za SADC.

Viwango vya malipo vimekuwa havikidhi mahitaji ya wanaolipwa, na hali hii imekuwa hivyo tangu wakati wa uhuru nusu karne iliyopita. Swali kubwa hadi lini hali hii itaendelea kuwa hivyo?

Hakika, kumekuwepo, kwa mfano, nyongeza za mishahara ya mara kwa mara kwa watumishi wa umma na sekta binafsi, wakati kima cha chini cha mishahara kimekuwa kikipanda kutoka Sh 45 kwa mwezi wakati wa uhuru hadi kufikia Sh 250,000 sasa hivi, ongezeko la zaidi ya asilimia 3,500.

Lakimi muulize sasa hivi mtu yoyote aliyekuwa hai miaka 50 iliyopita iwapo watu waliishi vipi kwa hizo sh 45 kwa mwezi. Bila kusita atakujibu ilikuwa rahisi kwa familia kuishi mwezi mzima kwa hizo sh 45 kuliko sh 250,000 sasa hivi. Anayepata sh 250,000 kwa mwezi sasa hivi atakupa simulizi ya kusikitisha sana jinsi anavyojitahidi kujihimu kimaisha.

Cha ajabu ni kwamba serikali inalifahamu hili lakini watendaji wake huamua kupiga danadana tu madai halali ya wananchi wake.

Kuna methali ya Kiingereza isemayo “Stinginess does not enrich and generosity does not impoverish” yaani ‘Ubahili hautajirishi mtu na wala ukarimu hauitii mtu umasikini.’ Kila Serikali duniani, hutanguliza tabia ya kubana matumizi, lakini nathubutu kusema kwamba serikali hii imejijengea rekodi mbaya sana ya ubanaji matumizi hadi nadiriki kusema ni unyimi uliovuka mipaka. Awamu hii ya Nne ndiyo usipime.

Si tu kwamba imekuwa inaburuza miguu kuchangamkia suala la ulipaji wananchi wake malipo yao stahiki punde inapotakiwa kufanya hivyo, bali pia huwa tayari hata kubadilisha sheria au kanuni za nchi katika kuwanyima wananchi stahiki hizo.

Lakini kama nilivyotanguliza kusema hapo mbele, pengine si haki kuilaumu serikali yenyewe kwa hili, bali watendaji wake, wale wakuu wenye nyadhifa za kutoa maamuzi. Na wao hufanya hivyo si kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa wivu tu.

Kwa mfano, iwapo mwananchi tu wa kawaida anayo haki ya kulipwa kutoka serikalini, tuseme sh 40 milioni, kuna watendaji wakuu ndani ya serikali hukataa kukubaliana na wazo kama hilo. Huonekana kuhoji: vipi wewe, mtu usie mbele wala nyuma, umiliki hela nyingi kama hizo?

Kwa maneno mengine, watendaji hawa wamejijengea akilini mwao fikra kwamba Watanzania wa kawaida wamelelewa katika mazingira kwamba hawapaswi kuwa wamiliki wa pesa nyingi na wanaona hakuna sababu za msingi kuibadilisha hali hiyo.

Pengine hili hutoa maelezo ya hulka ya Watanzania kwa ujumla wao – kwamba ni watu wapole, hawanung’uniki sana, huwa tayari kumeza kila kinachowachukiza, na mara nyingi, badala ya kuanzisha vurugu, kimya kimya hutafu njia nyingine kufidia. Ni hulka ambayo watawala wametokea kuiafiki sana na ndiyo hupenda kuitumia katika kuendelea kuwanyima haki zao.

Lakini hakuna mfano mzuri wa kuuelezea unyimi wa serikali kama lile suala la malipo stahiki ya mafao ya wastaafu (wa Tanzania) wa iliyokuwa Jumuiya ya Mashariki iliyovunjika mwaka 1977. Hili ni suala ambalo serikali ya Tanzania iko hatiani mara 10,000. Na inashangaza ni kwa nini hadi sasa haitaki kurekebisha.

Mwanzoni mwa miaka ya 80 serikali za nchi tatu ziliunda tume ya kusimamia mgawanyo wa mali za Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 chini ya msuluhishi Dk Umbricht ambaye ripoti yake ilikuwa Msingi wa Maridhiano (Mediation Agreement) ya mwaka 1984.

Makubaliano hayo yalikuwa ndiyo msingi wa Mgawanyo wa Mali na madeni ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mkataba huo wa Maridhiano ulipitishwa katika mabunge ya kila nchi husika na kuwa sheria. Miongoni mwa madeni hayo ni mafao ya wafanyakazi kwa kipindi cha uhai wa Jumuiya hiyo hadi ilipovunjika na kila nchi iliwekewa fedha hizi katika akaunti ya Crown Agents nchini Uingereza.

Ripoti hiyo iliweka wazi kabisa fomula itakayotumika katika kupata hesabu kamili ya mafao hayo ya wastaafu na kwamba ucheleweshaji wowote katika kuwalipa utalazimisha riba ya asilimia saba kila mwaka na kwamba bei ya dollar ya Kimarekani wakati wa kuwalipa ndiyo itatumika katika kupata thamani halisi kwa sarafu ya Tanzania.

Serikali ya Kenya mara moja iliwalipa wafanyakazi wake waliokuwa wakifanya kazi katika Jumuiya, wakati Uganda, ingawa ilikawia hadi mwanzoni mwa miaka 90, iliwalipa wafanyakazi wake mafao yao yote kwa fomula iliyokubaliwa.

Lakini haikuwa hivyo kwa serikali ya Tanzania ambayo badala ya kuwalipa walianza kuonyesha dalili za kuwadhulumu. Kwanza kabisa

serikali ya Tanzania ilipitisha sheria yake nyingine Bungeni iliyobainisha kwamba mafao ya wastaafu hao yataingizwa katika mfumo wa pensheni wa watumishi wa umma (Government Pension Scheme) na watalipwa baada ya kustaafu kwao kwa kawaida.

Hawa ni kwa wale wafanyakazi wa Jumuiya ambao walikubali kuingia katika wizara/idara mbali mbali za Serikali ya Tanzania kwa mikataba mipya. Lakini kuna wale ambao hawakutaka kufanya hivyo, waliamua kwenda kufanya kazi katika sekta binafsi, au wale waliofariki nk.

Isitoshe, ilikuwa imewekwa wazi kwamba wanaonufaika na mafao hayo ni waliokuwa wafanyakazi wa Jumuiya ile katika kipindi cha uhai wake, yaani kutoka 1967 hadi 30 Juni 1977 ilipovunjika na waliokuwa kazini tarehe hiyo ilipovunjika. Hayo ya serikali kuwarithi wafanyakazi hao kwa mikataba mingine hayahusiani kabisa na mchakato wa kuwalipa wafanyakazi hao mafao ya Jumuiya kama ilivyokubalikakatika mkataba wa kugawana mali na madeni.

Sababu kubwa ya serikali ya Tanzania kutowalipa wafanyakazi hao mafao yao stahiki ilitokana na kwamba jumla ya fedha ilikuwa kubwa mno kutokana na kupungua thamani kwa sarafu (depreciation) na deni kukaa miaka mingi bila kulipwa hivyo kusababisha riba kubwa, makosa ya serikali, siyo ya walipwa.

Lakini ilikuwa ni malipo stahiki kwa wastaafu hao na hivyo watendaji wa serikali waliona itakuwaje aiyekuwa kuli tu wa lililokuwa Shrika la Bandari Afrika Mashariki (EAHC) kulipwa milioni 40 hivi hivi? Waliona hapaswi kumiliki fedha nyingi kama hizo.

Ni kweli wafanyakazi hao walilipwa mafao yao katika vipindi viwili tofauti, lakini mara zote hizo haikuwa katika fomyula iliyokubalika. Mwaka 1999 serikali iliamua ‘kuwalipa’ lakini baada ya mahesabu waliambulia kiduchu mno kufuatana na ile sheria yake iliyopitisha kwamba mafao yao yaliingizwa katika mfumo wa penseni wa utumishi wa umma.

Lakini wengi waliona kwamba uamuzi huu wa kuwalipa ulitokana na ujio, mwaka uliofuata, wa hafla ya kutia sahihi mkataba wa kuanzisha jumuiya mpya ya Afrika Mashariki. Serikali ya Tanzania haikujisikia vizuri kuingia mkataba wa Jumuiya mpya huku wastaafu wake walikuwa bado hawajalipwa mafao ya Jumuiya ya zamani.

Mara ya pili ilikuwa ni mwaka 2005 wakati wa miezi ya mwisho ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa na ilikuwa wakati wafanyakazi hao wqalikuwa wameipeleka serikali mahakamani. Serikali ilikubali kuwalipa sharti ya kuondoa kesi mahakamani na hilo lilipofanyika, malipo yaliolipwa hayakufuata fomula ya Dk Umbricht.

Baadaye wafanyakazi walirudi mahakamani tena kudai urekebishwaji wa kasoro hiyo lakini baada ya muda mrefu hatimaye Mahakama ya Rufaa mwaka 2014 iliamua kwamba wafanyakazi hao walishalipwa tangu 2005 kutokana na Mkataba wa Makubaliano (Deed of Settlement) kati ya viongozi wa chama chao na Serikali.

Lakini unyimi au ubakhili huu wa serikali huelekezwa zaidi kwa watu wa ngazi za chini, na siyo kwa vigogo serikalini, ambao hujiamulia kulipana mishahara/posho kubwa kubwa, mara nyingine katika taratibu na kanuni zisizobainishwa popote serikalini, ingawa hili sasa hivi limeanza kubanwa na utawala wa Awanu ya Tano ya John Magufuli.

Kwa mfano tumekuwa tukishuhudia wabunge wanavyojipandishia mishahara na posho bila kujali hali halisi ya ufukara inayowakabili Watanzania walio wengi. Cha kushangaza ni kwamba wakubwa hawa hawaelewi jinsi wananchi wanavyochukizwa na mambo hayo.