Home Makala SERIKALI IACHANE NA WAFUA UMEME BINAFSI

SERIKALI IACHANE NA WAFUA UMEME BINAFSI

892
0
SHARE
Mradi wa umeme wa Kinyerezi unaomilikiwa na Tanesco ukiwa katika ujenzi.

HILAL K. SUED,

Inaelezwa, na si wengi wako tayari kupinga, kwamba eneo la kifahari la Mikocheni jijini Dar es Salaam liliendelezwa na fedha chafu zilizotokana na mashirika ya umma ya zamani – walizofisidi wakuu wa mashirika hayo wakishirikiana na maswahiba wao wa kibiashara.

Lakini kama vile msemo mmoja wa Kiingereza usemavyo: “It takes two to Tango” – yaani mchezo wa dansi wa Tango (maarufu katika nchi za Amerika ya Kusini), hushirikisha watu wawili. Hivyo maafisa wa ngazi za kati na chini ya mashirika hayo nao walinufaika – walijichotea chao na kuendeleza eneo la Sinza.

Hivyo iwapo watu watahoji ni urithi (legacy) gani chanya ulioletwa nchini na mamia ya mashirika yale ya umma, jibu sahihi, lakini lisilozungumzwa — ni kuendelezwa mandhari ya baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam. Lakini fedha chafu nyingi pia zilivunwa wakati wa kuachana na mashirika hayo – katika ule mchakato maarufu wa ubinafsishaji, kuanzia miaka ya mwanzoni ya 90.

Kuna watu walivuna mabilioni kirahisi tu kutoka mashirika haya, mashirika ambayo katika kipindi kifupi yaliifanya nchi kujisikia na kusifika kwa kuzalisha bidhaa nyingi kwa matumizi ya ndani, kuuza nje, bila ya kusahau kutoa ajira kwa maelfu ya vijana – wengiine wakitokea shuleni moja kwa moja.

Bidhaa zilizokuwa zikizalishwa na baadhi ya mashirika hayo ya umma ni pamoja na nguo, vifaa vya kilimo, magurudumu ya magari, redio na santuri, viatu, bidhaa za karatasi, pombe kali na mvinyo, nyama zilizosindikwa na kadhalika.

Lakini kutokana na sababu ambazo zinaweza tu kuhusishwa na uongozi mbaya, ufisadi, mashirika haya ya uzalishaji yalianza kuporomoka.

Hivyo ilipoonekana kwamba hakuna kingine cha kufanya isipokuwa kuyabinafsisha, basi yaliuzwa kwa “wawekezaji” kwa bei iliyokaribiana na bure – kwa sharti moja kali kwa wanunuzi: wawekeze fedha zao kwa lengo la kuyafufua mashirika hayo.

Wengi wa wawekezaji hawa walitanguliza malipo ya fedha na hadi sasa haijulikani iwapo wote walionunua mashirika hayo walilipa fedha zote.

Katika mfano mmoja, shirika moja la uzalishaji lilibinafsishwa kwa mwanafamilia mmoja wa Rais aliyekuwapo madarakani, kwa bei poa, na hata hivyo ni fedha kiduchu ya hizo ndizo zililipwa.

Na badala ya kuyaendeleza mashirika hayo,  wawekezaji hao wapya walianza kuuza mitambo na mashine kama chuma chakavu – hasa vile viwanda vya nguo na vya vifaa vya kilimo.

Kibaya zaidi ni kwamba, Serikali ilishindwa kusimamia na kuhimiza masharti ya ubiafsishaji, achilia mbali kudai albaki ya fedha.

Changamoto zote hizi na nyinginezo ziliwekwa katika ripoti ya kurasa 99 iliyotayarishwa na shirika hodhi – Consolidated Holding Corporation (CHC), liliopewa jukumu la kumaliza kazi zilizosazwa na Tume ya Rais ya Urekebishaji wa Mashirika ya Umma (PSRC) – Presidential Sector Reform Commission. Na kulikuwapo msukumo mkubwa kutaka CHC livunjwe.

Wengi wanasena iwapo habari kamili kuhusu ubinafsishaji wa mashirika yetu itaandikwa na kuwekwa wazi, basi nchi itakuja kufahamishwa ufisadi uliokithiri wa viongozi wao, kulindana kwa wahusika, na hasara kubwa kwa Serikali isiyowahi kutokea katika historia yake tangu nchi ipate uhuru.

Itakumbukwa wakati iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ilipobinafsishwa kwa Benki ya Absa ya Afrika ya Kusini kwa Tsh 15 bilioni, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere (angali yuhai), alikuwa karibu ya kulia machozi.

Vivyo hivyo ilivyokuwa kwa ubinafsishaji wa kampuni ya Sigara (TCC) na nyingine. Nyerere alishangaa kuona kwamba viongozi wa Serikali hawakuona mahala pengine pa kuchota fedha isipokuwa kutoka mashirika ya umma, yalipokuwa hai na wakati wa mchakato wa kuyauza.

Lakini kuna mashirika machache ya umma yaliyokwepa shoka la ubinafsishaji, na moja ndilo linaendelea kukamuliwa hadi sasa —Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Ni vigumu kujua ni mara ngapi neno hili ‘Tanesco’ limetokea magazetini, au kuzungumzwa na watu kuanzia zaidi ya miaka 10 iliyopita – tangu Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete aingie madarakani.

Na mara zote ni kwa mtazamo hasi – kama vile mgao wa umeme, mikataba mibovu kati yake na makamupni ya kuzalisha nishati ya umeme, kuchotwa kwa fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow na kadhalika.

Tanesco inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Sababu moja kubwa inayotajwa rasmi ya kutouzwa  shirika hilo kwa wawekezaji ni kwamba ni taasisi nyeti ambayo haiwezi kuachiwa katika mikono binafsi na nchi ikabaki salama, kwa sababu ni kama ‘moyo’ unaotoa uhai kwa uchumi wa nchi.

Lakini wananchi tayari wameona ni wapi ile ‘mikono salama’ ya Serikali ilivyokuwa inalipeleka shirika hilo – na tukisema korongoni ni kusema kidogo. Taasisi iligeuzwa kama ng’ombe wa kukamuliwa na wenye uwezo – viongozi wa Serikali wakishirikiana na maswahiba wao wa kibiashara.

Hadi sasa haijulikani Tanesco imepata hasara kiasi gani katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 tangu makampuni binafsi ya kufua umeme yaruhusiwe na Serikali kupitia mikataba kamuzi ya kuuza umeme kwa Tanesco.

Tukiachilia mbali kushindikana kulimaliza suala la mgao wa umeme, bei ya nishati hiyo kwa walaji imekuwa ikipanda kila mara – imepanda kwa zaidi ya asilimia 400 tangu 1990.

Akizindua Awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi mwaka jana, mtambo ambao utakuwa wa kwanza kujengwa na kumilikiwa na Tanesco tangu ile ya kutumia maji iliyojengwa katika awamu ya Mwalimu Nyerere zaidi ya miaka 30 iliyopita, Rais John Magufuli aliisemea miradi ya wawekezaji kwamba ilikuwa inalikamua taifa na kwamba ataachana nayo.

Na wiki mbili zilizopita tu, akiwasilisha Ripoti yake ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Serikali kwa Rais Magufuli, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG), Prof Mussa Asad, alimtahadharisha Rais kuhusu ‘biashara kichaa’ inayofanya Tanesco na makampuni ya kufua numeme binafsi.

Hivyo ni wakati sasa kwa Rais Magufuli kusimamia alichokisema mwaka jana, na alichosema CAG mwaka huu – kusema biashara hiyo sasa basi. Ingefaa Rais atoe ratiba ya kuachana kabisa na wawekezaji hao.