Home Makala SERIKALI IJITAHIDI KUIIMARISHA TANESCO

SERIKALI IJITAHIDI KUIIMARISHA TANESCO

2008
0
SHARE

NA HILAL K SUED


Nakumbuka vizuri mwaka 1974 baada ya kufunguliwa kwa mtambo wa kufua umeme wa maji wa Kidatu, mmiliki wa mtambo huo – Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) liliweka punguzo kubwa la gharama ya nishati hiyo kwa watumiaji wa nyumbani (domestic consumers) katika jedwali waliyoitoa.

Kwa ujumla ilikuwa ni kwamba kadri mtumiaji anavyotumia uniti nyingi za umeme ndiyo bei ya umeme kwa uniti moja inapungua. Lengo la mfumo huu – kwa Kiingereza “tapering system” lilikuwa ni kuwapa motisha watumiaji wa umeme kutumia umeme mwingi kadiri walivyoweza.

Tanesco waliweza kufanya hivyo miaka 30 hadi 40 iliyopita kwa sababu walikuwa wanazalisha umeme mwingi kuliko matumizi, na bila shaka hali ilichangiwa na uwepo wa watumiaji wachache pamoja na viwamda.

Sasa hivi ni kinyume chake – mtumiaji wa majumbani analazimika kulipa gharama kubwa zaidi kwa kila uniti kadri jinsi anavyotumia uniti nyingi kila mwezi, lengo ni kuhimiza matumizi madogo ya umeme. Kwa maneno mengine uzalishaji wa nishati hiyo ni mdogo kuliko watumiaji. Na hii ndiyo sababu ya kuwa na mgao wa umeme mara kwa mara.

Katikati mwa Novemba mwaka jana (2017) Waziri wa Nishati Medard Kalemani alitangaza kwamba ifikapo 15 Desemba 2017 kukatika katika kwa umeme nchini kungekuwa historia. Ni dhahiri hakujakuwa historia kama alivyoahidi na pengine kukatika katika ndiyo kumeongezeka bila ya maelezo ya yanayoeleweka kutoka kwa waziri huyo. Na athari ya hili suala nimelishuhudia wiki mbili zilizopita.

Siku moja nilikuwa maeneo ya Kariakoo Mtaa wa Congo, na mitaa mingine jirani yenye harakati nyingi za kibiashara, hasa kuwepo maduka mengi ya nguo na biashara nyingi za kimachinga za barabarani. Hizi biashara za barabarani zimeongezeka sana siku hizi na athari zake zingine nilishazizungumza katika safu hii wiki kadha zilizopita.

Kitu kimoja kilichojionyesha mara moja ni uwingi wa majenereta yaliyojipanga kwenye mabaraza ya takriban kila duka yakinguruma, huku watembea kwa miguu wakipata shida kuyakwepa, na hata mara nyingi hulazimika kuziruka nyaya zake zilizosambaa. Majenereta haya huwashwa pindi unapokatika umeme kwa ajili ya maduka.

Nikawa nawaza tena kwa hofu kubwa – je iwapo hutilafu yoyote ikitokea kwenye moja ya majenereta hayo kama vile tanki mojawapo la petrol linavuja na mpita njia akatupia kipande cha sigara? Mtaa mzima unaweza kuteketea, lakini Mungu apishe mbali mambo haya. Hata hivyo hii ni changamoto tumekuwa tukiishi nayo kwa miongo mingi tu sasa.

Ninaposema miongo mingi nina maana tangu mapema miaka ya 90 pale serikali ya Awamu ya Pili ya ali Hassan Mwinyi ilipotiliana mkataba na kampuni ya IPTL ya mwanahisa mkuu kutoka Malaysia na wadau wengine kufua umeme na kuiuzia Tanesco. Mkataba huo ulikuwa wa kinyonyaji kwani Tanesco ilikuwa inalazimika kuilipa kampuni hiyo fedha hata kama ilikuwa haihitaji umeme.

Kikubwa kilichopelekea serikali kuingia mkataba huo na IPTL ilikuwa ni mgao mkubwa wa umeme nchini wakati huo uliotokana na hali ya ukame, hja;li ambayo iliathiri mitambo ya kufua umeme wa maji ambayo ndiyo ilikuwa inatoa kiasi kikubwa cha umeme katika gridi ya taifa.

Sote twafahamu athari ya mikataba ya aina hii na yote yaliyotokea hadi sasa kwa Tanesco na kwa Tanzania nzima kwani shirika hilo la umma ililazimishwa kuingia katika mikataba ya aina hii na makampuni mengine kadha.

Ni mara ngapi, katika kipindi chote cha zaidi ya miongo miwili iliyopita, Watanzania wamekuwa wakisikia kauli kutoka kwa watawala kwamba “Kuanzia sasa tatizo la mgao wa umeme litakuwa ni historia?”

Ni mara nyingi sana, hususan kila baada ya mtambo mpya binafsi wa kufua umeme unapozinduliwa. Na kama nilivyosema, mitambo yote hii iliyozinduliwa katika kipindi hicho si mali ya Tanesco – ni mali ya watu (wawekezaji) binafsi ambao huliuzia nishati hiyo kwa shirika katika mikataba ya utata mkubwa.

Mapema mwaka jana alipokuwa anawasilisha kwa Rais John Magufuli Ripoti yake ya kila mwaka ya mahesabu ya serikali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) Profesa Mussa Assad alisema Rais aangalie ile aliyoiita “biashara kichaa” – jinsi Tanesco inavyokamuliwa – inanunua umeme kutoka kwa kampuni hizo kwa bei ya juu na kulazimika kuuza nishati hiyo kwa wateja wake kwa bei ya chini.

Kwa maneno mengine Tanesco ilikuwa imegeuzwa kuwa “ng’ombe wa maziwa” na watu wachache wenye nafasi za juu katika utawala na maswahiba wao katika sekta binafsi. Na inaonyesha kwamba utamaduni huu umesitishwa na Rais Magufuli na hivyo kurudia hali ilivyokuwa zamani na huenda matatizo ya umeme sasa hivi ni kutokana na kipindi hiki kigumu cha mpito.

Aidha kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa Tanesco haijaongeza gharama za umeme kwa watumiaji wake kutokana na katazo la Rais Magufuli la mapema mwaka jana. Huko nyuma takriban kila mwaka Tanesco ilikuwa inaongeza bei na ni rahisi kuhisi kwamba kuongezeka huku kunatokana na kufidia gharama ambazo shirika hilo lilikuwa likilipa kwa wafua umeme binafsi.

Hali ya zamani ni kwamba Tanesco imiliki mitambo yake ya kufua umeme – kwa mfani mtambo huu mpya wa Kinerezi nje kidogo jiji la Dar es Salaam. Utawala wa Awamu ya Kwanza wa Mwalimu Julius Nyerere ulijenga mitambo minne ya kufua umeme ya maji – Nyumba ya Mungu, Kidatu, Mtera, na Kihansi.

Mitambo yote hii na ile ya mingine kadha ya mafuta (thermal) takriban katika kili mji mkubwa mchini ilikuwa mali ya Tanesco. Kulikuwa hakuna mgao wa umeme, na kama ulikuwapo, basi haukuwa wa kiwango kikubwa. Kuna kila sababu ya kuifanya mitambo ya kufua umeme ya binafsi kuwa historia.