Home Uchambuzi SERIKALI ISHIRIKIANE NA SEKTA BINAFSI KUFUFUA ZAO LA MKONGE

SERIKALI ISHIRIKIANE NA SEKTA BINAFSI KUFUFUA ZAO LA MKONGE

2576
0
SHARE

TANZANIA ilikuwa ndiyo nchi pekee barani Afrika kupokea zao la mkonge kutoka Jimbo la Yucatan, nchini Mexico mwaka 1893. Mkoa wa Tanga ndio ulikuwa kinara wa kulima zao hilo kwa wingi kwa kuwa na mashamba makubwa ikifuatiwa na Morogoro.

Hadi kufikia mwaka 1964, uzalishaji wa mkonge nchini ulikuwa ni tani 235,000 kwa mwaka, hivyo kuifanya Tanzania kuwa ndiyo nchi pekee iliyokuwa ikifanya vizuri katika zao la mkonge barani Afrika.

Kutokana hali hiyo, sekta ya kilimo hicho ndiyo sekta ambayo ilikuwa imeajiri watu wengi hususani katika maeneo ya mashambani. Hivyo Mkoa wa Tanga ulikuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi kutokana na faida ya uwapo wa zao hilo ukitoa viwanda vilivyokuwepo enzi hizo.

Licha ya zao hilo kuwa na manufaa ya kiuchumi, ni bidhaa ya nyuzi pekee ndiyo ilikuwa ikisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya dunia. Hata hivyo, ujio wa kamba mbadala za nailoni katika miaka ya 1970 uliweza kuua soko la mkonge kwa kiasi kikubwa hali iliyolazimu kushusha uzalishaji na kufikia tani 32,000 pekee kwa mwaka.

Hali hiyo iliashiria anguko kubwa la zao la mkonge nchini Tanzania licha ya kuwepo kwa sababu nyinginezo kama mabadiliko na ukuaji wa teknolojia. Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na jitihada za makusudi zinazochukuliwa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kulifufua zao hilo kutokana na umuhimu wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Katani Ltd,  Salum Shamte, anasema jitihada zilizoanza kuchukuliwa tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2016, zao hilo limeanza kuonyesha mwelekeo wa kufufuka.

Anasema mwaka 2005 Serikali ilipata mapato ya kiasi cha Sh milioni 140 kwa kuuza kamba (singa) za mkonge nje ya nchi tani 849 huku mwaka 2016 ikipata Sh bilioni 3.6 kwa kuuza tani 4,837.

Anasema mafanikio hayo yanatokana na namna walivyoweza kuhamasisha wananchi hususani wakulima wadogo kulima mkonge katika maeneo yao.

“Mfumo wa ushindani pamoja na kuhusisha wakulima wadogo kumewezesha kulima zao hilo katika maeneo yao sambamba na kupanda mazao mengine ili kuongeza uzalishaji,” anasema Shamte.

Anasema zaidi ya hekta 8,263 za mashamba yao wamefanikiwa kupanda zao hilo huku zikibaki hekta 7,322 ambazo bado hazijapandwa zao hilo, lakini zipo kwenye mkakati wa kupandwa.

Anasema zao la mkonge katika masoko ya dunia lina thamani sana kwani ni moja ya zao ambalo unapovuna kila kitu kina thamani kutokana na maendeleo ya kiteknolojia yalivyo kwa sasa.

“Sisi Tanzania tunatumia asilimia mbili tu ya mmea wa mkonge wote na kutupa  asilimia 98 baada ya kuvuna wakati kwa sasa mmea huo unatumika wote katika kuzalisha vitu vingi.

“Mabaki ya zao hilo yanatumika katika kuzalishia bidhaa mbalimbali ikiwemo magari, vigae vya kujengea, chakula cha mifugo pamoja na nishati ya umeme.

“Kutokana na mahitaji makubwa ya zao hilo hususani katika nchi za Ulaya na Asia, tumelazimika kuanza kulitilia mkazo ili kuhakikisha tunaliteka soko.

“Nyuzi za mkonge kwa nchi za wenzetu zinatengeneza viatu, matofali, mabati na wakati wa kujenga zinatumika ili kudhibiti nyumba isiungue kunapotokea hitilafu ya umeme,” anasema.

Anaongeza kuwa moja ya malengo waliyokuwa nayo ni kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia tani milioni moja kwa mwaka ifikapo mwaka 2040 pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

“Kutokana na upigaji vita wa bidhaa zisizo rafiki kwa mazingira kama vile bidhaa za plastiki hivyo mkombozi pekee aliyebaki ni kujikita kuwekeza kwenye ulimaji na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge ambazo ni rafiki wa mazingira.

“Pia kutokana na utafiti tulioufanya hivi karibuni, tumegundua kuwa shina la zao hilo linaweza kutumika kuzalisha sukari pamoja na mvinyo.

“Jitihada zinaendelea kutafuta wawekezaji ambao tutaweza kuingia nao ubia ili tuweze kujenga viwanda vya sukari na mvinjo hapa nchini ili kuongeza fursa za ajira na pato kwa Serikali,” anasema.

Licha ya jitihada hizo, Shamte anaiomba Serikali pamoja na taasisi za fedha kuona namna bora ya kuwekeza wa zaidi ili sekta hiyo iendane na mapinduzi ya kiuchumi.

“Zao hilo lina fursa nyingi za uwekezaji hivyo jitihada zilizoanza kuchukuliwa ni lazima ziendane na kasi ya uwekezaji huo kidunia ili Tanzania nayo iweze kunufaika.

“Kwa sasa viwanda vingi vya kuzalisha kamba na bidhaa vinahitaji ufufuaji ikiwemo kuwepo kwa mashine za kisasa pamoja na mitaji ili kuongeza uzalishaji.

“Ili dhana ya Tanzania ya viwanda iwe ya vitendo ni wajibu wa taasisi za fedha kupunguza masharti pamoja na riba kubwa ili kuvisaidia viwanda vya ndani ya nchi,” anasema.

Naye Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Theodora Mtegeta, anasema kwa sasa kampuni hiyo ina jumla ya wakulima wadogo 1,273 ambao wanamiliki zaidi ya hekta 15,590.

Anasema kati ya hayo mkulima mdogo kabisa anamiliki hekta sita huku mkulima mkubwa akiwa anamiliki hekta 200 ya mashamba ya zao hilo.

Anasema licha ya shughuli za kilimo, kampuni hiyo inamiliki viwanda vya kuzalisha kamba za katani, kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na mkonge pamoja na kiwanda cha kuzalisha nishati ya umeme.

“Tunahitaji uwekezaji mkubwa katika kiwanda pekee cha kuzalisha nishati ya umeme inayotokana na mabaki ya mkonge pale Hale kwani sasa tunatekeleza sera ya viwanda na umeme ni muhimu sana,” anasema Meneja huyo.

Anasema kilimo hicho kinaweza kuwa na tija zaidi kama Serikali itaweza kuingia ubia na sekta binafsi ili kusaidia mitaji ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji.

“Sasa kilimo kinafanywa na wakulima wadogo lakini kama kutakuwa na ubia zao hilo linaweza kulimwa kwa ufanisi na kuongeza uzalishaji wake kwa kiasi kikubwa,” anasema Mtegeta.