Home Makala Serikali isitumie ukubwa kudhalilisha watu

Serikali isitumie ukubwa kudhalilisha watu

998
0
SHARE

Na Markus Mpangala

MILA na desturi za Watanzania zinafanana na baadhi ya mataifa ya barani Afrika pamoja na Amerika Kusini. Kwa mujibu wa Profesa Ivan Sertima, aliyeandika kitabu cha ‘They Came Before Columbus’, alisema kwamba baadhi ya mila na desturi za wananchi wa Mexico, hususani utamaduni wao na imani za asili, zinashabihiana mno na watu wa Bara la Afrika.

Profesa Sertima alitoa ushuhuda kuanzia mifumo wa majina, mila na desturi za wenyeji wa Mexico na baadhi ya wakazi wa Amerika Kusini ambao wana nasaba za moja kwa moja na Afrika.

Aidha, alieleza namna Waafrika waliovyoweza kufanya safari za Amerika kabla ya baharia Christipher Columbus ambaye anatajwa kuivumbua Ameka.

Kwa maana hiyo, mifumo ya maisha waliyojijengea Waafrika katika jamii zao, ni pamoja na kuwaheshimu, kuwatii na kuamini kuwa wakubwa hawakosei. Hayo ni makuzi ambayo Watanzania wengi tumeyapitia.

Askofu Placide Temple, naye aliandika ‘Falsafa za Wabantu’ au kwa lugha ya kimombo ‘Bantu Philosophy’, ambayo ni tafsiri ya lugha ya Kifaransa ‘La Philosophie Bantoue’ (1945) akiwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Askofu Temple ameeleza mifumo ya maisha ya Waafrika ilivyojengwa kwa mujibu wa taratibu za kuheshimu mababu. Kwamba mifumo hiyo haibadiliki na mtiririko kutoka kwa wakubwa hadi wa ngazi za chini, ni kitu ambacho kinaitambulisha jamii ya Kiafrika—utii, kuheshimu wakubwa, na imani juu ya viumbe wa kale.

Sasa tugeikie maana ya maneno utii, heshima na adabu. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Oxford Toleo la Pili (uk.2), neno ‘adabu’ limeelezwa kuwa ni tabia njema, nidhamu, heshima na staha.

Neno ‘heshima’ limeelezwa kuwa ni thamani ya utu, utukufu, daraja la juu. Aidha, neno heshimu, limeelezwa kuwa ni staha, adabu nidhamu na kitu kinachopewa mtu kama alama ya kuthaminiwa kwake (uk.114).

Nimetangulia kusema hayo baada ya tukio la hivi karibuni linalomhusu Emile Ntakamulenga ambaye alikutwa na kadhia ya kutoheshimiwa na Serikali yake  na ndani ya taifa lake.

Emile Ntakamulenga alitangazwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara. Uteuzi wake ulifutwa dakika chache akiwa ukumbini Ikulu ya Rais akisubiri kula kiapo pamoja na wakuu wengine wa wilaya 139 waliotakiwa kuapishwa siku hiyo na Jaji (mstaafu) Salome Kaganda,  Kamishina wa Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma.

Emile alikwenda Ikulu kutimiza wajibu wake wa kula kiapo, lakini cha kushangaza alitakiwa kuondoka kwa maelezo kwamba hakuwa mhusika kwa kuwa jina lake lilikosewa. Aliambiwa shughuli haimhusu.

Baada ya kuondolewa, ilitangazwa kuwa aliyestahili nafasi yake ni Nurdin Babu, ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Kwahiyo Nurdin Babu alihamishwa wilaya tu.

Hadi ninaandika katika safu hii, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa umma ya kuombwa radhi kutokana na tukio hilo. Wapo Watanzania wanadai kuwa tukio hilo ni makosa ya kibindamu—kwamba  halipaswi kukuzwa mno.

Wanaoamini hilo siwazuii, waendelee kufikiri hivyo, lakini ninayo sababu ya kukemea kwa nguvu, akili na uwezo nilionao—kwamba tukio hilo, linaudhi, linakera na ni ukosefu wa heshima kwa mtu mwenzetu.

Nimetumia siku nyingi mno kulifikiria hili. Najiuliza kwa nini limetokea wakati lingeweza kuzuilika? Nimefuatilia kwa kina taarifa za kuapishwa Wakuu wa Wilaya wapya. Nimefikiria mengi na kusubiri ni namna gani Serikali inaweza kusema hadharani juu ya makosa haya.

Kwamba mnataka kuniambia hadi leo Ntakamulenga hajaombwa radhi? Hivi ni nani anataka na kupenda kufedheheshwa ama kusumbuliwa hadharani namna ile?

Hivi adabu na heshima hii ionyeshwe kwa mdogo tu, kwamba mtu mkubwa hastahili kuonyesha na kuthamini adabu na heshima kwa wadogo aliowazidi umri, madaraka na hata elimu?

Labda tuseme Ntakamulenga ameombwa radhi kisisiri. Lakini mbona ninyi mlimwambia hadharani juu ya kukosewa jina na kumwondoa kwa kumwambia shughuli haikuhusu?
Ina maana yule aliyekosea jina naye ameambiwa nini ili nasi walalhoi tukajua?

Mnaniambia kuwa akikososewa mdogo asiombwe radhi, ila mkubwa haombi radhi na huombwa radhi punde akikosewa? Nafsi ya mkosewa iko katika hali gani kukosa thamani ya utu? Ni nani atafidia huzuni na maumivu na fadhaa yake?

Najua nitaambiwa, je, ni lazima kuombwa hadharani, na kwamaba pengine pale aliondoka na barua mikononi mwake Serikali ikimtaka radhi?

Swali hilo ninalijibu ifuatavyo: Ni kwa nini haukufanyika utaratibu wa kumzuia Ntakamulenga asiingie kabisa ukumbini? Kwahiyo tunapoambiwa kuwa walifanya kazi kubwa kuwatafuta watu wa kuteuliwa kuwa Wakuu wa Wilaya, walimaanisha nini au ilikuwa ni urongo?

Kama aliyestahili kuteuliwa alipewa taarifa na kufika eneo la kuapishwa, mbona aliyekosewa hakuambiwa asiende? Watawala wetu walishindwaje hata kumtuma mesenja amwite pembeni na  wamwambie kimya kimya?

Labda tuseme Mheshimiwa Rais Magufuli alipotoshwa na washauri wake, ikabidi jipu litumbuliwe. Nitawauliza swali: Utamtumbuaje jipu mtu (Ntakamulenga) asiyekuwa nalo? Jipu anatumbuliwa aliyeitwa au waliomshauri na kumweka kwenye orodha?

Tuliambiwa kuwa Anne Kilango alidanganya aliposema mkoani kwake Shinyanga hakukuwa na watumishi hewa. Nami nakiri kumdanganya Rais ni kosa linalostahili adhabu. Je, walioweka jina la Emile Ntakamulenga hawajamdanganya Rais?

Naamini hekima ya mwanadamu kama kiongozi, ni pamoja na kutoa adhabu au kuwaadhibu wakosaji. Nani ameadhibiwa na umma umeambiwa kama tulivyoambiwa kukosewa jina la mwapishwaji mpya? Ukuu wetu na nguvu zetu, zisitumike kudhalilisha watu.