Home Makala Serikali itie mkono medali Mbio za Nyika, Olimpiki

Serikali itie mkono medali Mbio za Nyika, Olimpiki

1811
0
SHARE

HASSAN DAUDI

WANARIADHA 28 wamechaguliwa kuingia kambini jijini Arusha kujiwinda na michuano ya Mbio za Nyika itakayofanyika mwaka huu nchini Denmark na zile za mwakani za Olimpiki huko Tokyo, Japan.

Itakumbukwa kuwa wanariadha walipatikana baada ya mashindao ya taifa yaliyofanyika hivi karibuni mjini Moshi, Kilimanjaro.

Wawakilishi hao wa Tanzania walitarajiwa kuingia kambini wiki hii, ambapo watachujwa na kubaki 20 wakakaokwenda kwenye mashindano hayo.

Watakaokwenda Denmark, kwa maana ya kushiriki Mbio za Nyika zitakazoanza Machi 30, ni wale wenye umri wa chini ya miaka 18, huku wengine wakiwa na kibarua kigumu cha kurudi na medali huko Japan.

Ikiwa chini ya jopo la wataalamu nane, akiwamo mwanaridha mstaafu, Marcellina Gwandu, binafsi naiona kambi ya Arusha kuwa ni yenye matumaini makubwa kuelekea michuano hiyo ya kimataifa.

Hata hivyo, licha ya juhudi kubwa za Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) chini ya Katibu Mkuu wake, Wilhelm Gidabuday, hiyo haindoi shaka kuwa Tanzania inaweza kuvurunda kama ambavyo imekuwa katika miaka ya hivi karibuni.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba bado kumekuwa na umbali mrefu kati ya Serikali na mchezo wa riadha, ambapo mara nyingi uongozi wa RT umekuwa ukiachiwa mzigo huo.

Tofauti na ilivyo katika soka, ambapo nguvu kubwa ya uwekezaji imekuwa ikielekezwa huko, ushiriki wa wanariadha katika mashindano ya nje ya mipaka ya Tanzania umekuwa si wa kupewa nguvu.

Mfano mzuri katika hilo, imeshuhudiwa namna Serikali, kupitia Wizara ya Michezo, imekuwa ‘bize’ na fainali za Mataifa Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Afcon U-17).

Hivi, nini kinachozuia uzito wa mashindano hayo usielekezwe pia kwa wanariadha wanaotarajiwa kuipeleka bendera ya Tanzania huko Denmark na Japan?

Ukiacha hiyo, ni kawaida kuona viongozi wenye dhamana ya michezo nchini wakiipa kipaumbele Taifa Stars inapokuwa ikikabiliwa na michuano ya kimataifa, kama ilivyo sasa, ambapo inawania kwenda Afcon 2019.

Ilikuwapo kampeni ya ‘Zamu Yetu’ kuhamasisha Stars kufuzu kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980. Wakati huo huo, ni mwezi mmoja tu umebaki kabla ya wanaridha kwenda Denmark lakini hakuna mikakati ya aina hiyo kuwajenga kisaikojia wawakilishi watakaokwenda.

Aidha, licha ya kwamba bado ni mapema, huenda siku chache tu za kambi ya Arusha zikatosha kusikia kilio cha ukata, jambo ambalo huwezi kulisikia kwa wachezaji wa Taifa Stars.

Kwa maana nyingine, uwekezaji katika kandanda umekuwa ukipewa sapoti ya moja kwa moja na Serikali, huku michezo mingine, ikiwamo riadha, ikibaki hoi, yaani ikiendeshwa kwa ‘bakuli’.

Ni kweli soka linaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi duniani lakini je, ni utafiti gani uliobaini kuwa umeiwakilisha Tanzania vema zaidi kuliko michezo mingine?