Home Habari Serikali kupeleka neema vijijini

Serikali kupeleka neema vijijini

983
0
SHARE

MWANDISHI WETU

HARAKATI za serikali kufikia uchumi wa kati kwa wananchi wake huenda zikazaa matunda kutokana na mkakati unaoandaliwa sasa wa kupeleka viwanda vidogo vijijini.

Mpango wa serikali uliopo sasa ambao umekuwa ukinadiwa mara kwa mara na Wizara ya Viwanda na Biashara ni kuhakikisha kila mkoa unakuwa na viwanda 100.

Wakati mpango huo ukiwa unaendelea kwa kasi, tayari serikali imeiona haja ya kuhakikisha rasilimali zilizopo katika kila kijiji nchini zinatumika kwa uharaka.

Njia pekee ya kulifanikisha hilo ni kuhakikisha viwanda vingi viodogo vinajengwa kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).

Hatua hiyo imetajwa kuwa  itakuwa ni msaada mkubwa kwa kila kijiji kuzalisha bidhaa itakayouzwa kwenye vijiji vingine kwa kutumia viwanda hivyo vidogo kwa lengo la kuhakikisha nchi inakuwa ya viwanda vya kutosha na kuwafikia wananchi wote mpaka vijijini.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara

ndiye aliyeitangaza neema hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Aliyesema hayo  kwenye mkutano wa kuangalia changamoto za uwekezaji kati ya Tanzania na China.

Aliweka wazi kuwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha nchi inafikia lengo la kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Alisema awali ilikuwa watu wanakuwa na viwanda tu, lakini kwa sasa wanahakikisha viwanda vyote vinavyojengwa vinakuwa na tija kwa kutumia rasilimali zinazozunguka wananchi, hivyo kupata wateja nje ya kijiji, mkoa na hata nchi.

Alisema lengo la kuwa na uchumi wa kati, linakwenda sambamba na lengo namba tisa la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa, hivyo kwa sasa kwa kutumia SIDO wanafanya utafiti kufahamu rasilimali kwa kila kijiji ili kuhakikisha kunakuwa na kiwanda kimoja katika eneo hilo.

Alibainisha kuwa kila kijiji kinatakiwa kujitathimini, kwa kuwa na kiwanda himilivu, kitakachozaliwa, kukua na kuwa na tija kwa maendeleo ya sehemu hiyo, mkoa na nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo kama mazao, miti na mengineyo.

Manyanya alisema wizara yake imejizatiti kurejesha viwanda vyote, vilivyochukuliwa na wawekezaji, akiwemo kiongozi mstaafu aliyetajwa na Rais John Magufuli wakati wa ziara yake mikoa ya kusini.

“Ni lazima akirejeshe kwani ile ni amri na kama alikopa fedha kutumia kiwanda hicho na kuwekeza katika masuala mengine, atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika mahakama ya mafisadi,“ alisema.

Alisema kwa sasa viwanda vinachangia kwa asilimia nane katika Pato la Ndani la Taifa (GDP), hivyo wamejipanga zaidi kwa mwaka 2025 kuchangia zaidi kulingana na nchi yenye uchumi wa kati.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana viwanda vilivyokuwa vimejengwa kwa nchi nzima vilikuwa 4,777, sawa na asilimia 183.73 ya lengo la kujenga viwanda 2,600.

Jafo alisema hayo wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa viwanda 100 kwa kila mkoa kwa kipindi kinachoishia Desemba 2018.

Alisema viwanda 1,285, kati ya 2,600, vimejengwa katika mikoa mbalimbali tangu atoe agizo la ujenzi wa viwanda 100 kwa kila mkoa.

Hata hivyo, alieleza kuwa baadhi ya mikoa haijafikia lengo. Alisema hataitaja mikoa isiyofikia malengo hadi Juni mwaka huu, kama watakuwa hawajafikia lengo.

Alisisitiza kuwa hajafurahishwa na hali hiyo.

“Sijafurahishwa na mikoa hiyo na inajijua haijafikia malengo ya ujenzi wa viwanda 100, nawapa muda hadi mwezi wa sita mwaka huu, mhakikishe mmefikia malengo mliyowekewa, sitaitaja nimetumia busara za uongozi ingawa kiukweli sijafurahishwa sana, mkishindwa kufikia lengo nitawataja hadharani,” alisema Jafo.

Waziri Jafo alisema ujenzi huo ni utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017-2020/2021, unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, ambao kwa kuanza kila mkoa ulitakiwa kuanzisha viwanda 100.

Alisema viwanda hivyo viligawanywa katika makundi manne ambayo ni viwanda vikubwa 108, viwanda vya kati 236, viwanda vidogo ni 2,422, na viwanda vidogo kabisa 2,010, ambavyo vilikuwa vimetoa ajira kwa wananchi 36,796 kwa nchi nzima.

Aidha, Jafo aliutaja Mkoa wa Dar es Salaam kuwa ndio ulioongoza kwa upande wa mikoa iliyofanikiwa kujenga viwanda vikubwa kwa kujenga viwanda vikubwa 46 kati ya 108 vilivyojengwa nchi nzima.

Unaofuatia ni mkoa wa Pwani uliojenga viwanda vinane na nafasi ya tatu ni mikoa mitatu ya Mwanza, Lindi na Simiyu, ambayo kila mmoja ulijenga viwanda vikubwa saba.

Alisema mikoa na serikali za mitaa ina wajibu wa kuwatumia kikamilifu wataalamu, hasa maofisa maendeleo ya jamii na maofisa biashara waliopo ili kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na upatikanaji wa malighafi za kutosha.

MALENGO YA NCHI

Miongoni mwa malengo makuu ya Tanzania kiuchumi ni kuwa nchi ya uchumi wa kati. Lengo hili limeelezwa katika maeneo mbalimbali kama vile katika Dira ya Maendeleo 2025. Chini ya lengo la kuwa na uchumi imara wenye ushindani.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya wadau wakuu wa uchumi wa Tanzania hawaelewi maana ya nchi kuelekea katika uchumi wa kati.

Wadau hawa wanaweza kuwa baadhi ya viongozi wanaotaka ‘kuivusha’ nchi kwenda uchumi wa kati na wananchi ‘watakaovushwa’ kuelekea huko.

Kati ya mambo muhimu ya kufahamu ni maana ya uchumi wa kati kwa maana ya kujua uchumi huu unafananaje, nini kinatakiwa ili kuufikia, tunaufikia kutoka uchumi upi, kuna faida gani kuwa katika ngazi hii ya uchumi na kadhalika. Makala haya inajibu baadhi ya maswali haya.

UCHUMI WA KATI

Inawezekana kuwa baadhi ya wadau hawaelewi tunataka kwenda katika uchumi wa kati kutoka katika uchumi gani. Kwa sasa Tanzania ipo katika uchumi wa chini.

Uchumi huu unazijumuisha nchi zenye kipato cha wastani kwa kila mtu cha Dola za Marekani 1,025 (wastani wa Shilingi 2,194,000) au chini ya hapo kwa mwaka kwa takwimu za mwaka 2015.

Katika orodha ya Benki ya Dunia, kuna nchi 31 katika kundi hili la nchi. Pamoja na Tanzania, nyingine ni kama vile Afghanistan, Burundi, Congo, Ethiopia, Liberia, Malawi, Msumbiji, Nepal, Somalia, Zimabwe, Uganda na kadhalika.

Matabaka ya uchumi wa kati

Katika juhudi za kuelekea uchumi wa kati ni muhimu kwa wadau wote kuelewa huu uchumi ni wa namna gani na nini kinatakiwa kuufikia.

Kwa kadiri ya vigezo vya Benki ya Dunia uchumi wa kati una matabaka mawili makubwa. La kwanza ni lile la uchumi wa kati wa ngazi ya chini na la pili ni uchumi wa kati wa ngazi ya juu.

Hivyo katika ‘kuvushana’ kuelekea uchumi wa kati ni vema ‘watakaotuvusha’ na ‘tutakaovushwa’ kuelewa kama safari ni ya kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya chini au ule wa ngazi ya juu. Maandishi na mazungumzo mengi yanaonyesha Tanzania inataka kuwa uchumi wa kati. Hii haitoshelezi.

Uchumi wa kati ngazi ya chini

Ni muhimu kuweka wazi kuwa maadam tupo katika uchumi wa chini lengo katika awamu ya kwanza linapaswa kuwa kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya chini.

Huu ni uchumi ambapo wastani wa kipato cha kila mtu kwa mwaka ni kati ya Dola za Marekani 1,026 na 4,035, yaani wastani wa kati ya Shilingi 2,195,640 na Shilingi 8,634,900.

Nchi zilizopo katika kundi hili ni 51. Hizi ni pamoja na India, Ghana, Indonesia, Morocco, Sudan, Tunisia, Pakistani, Bangladesh, Kosovo, Lesotho, Misri, Kenya, Nigeria, Zambia, Syria na kadhalika.

Hivyo juhudi za Tanzania za kuelekea katika uchumi wa kati wa ngazi ya chini ni juhudi za kufanana na nchi hizi kiuchumi.

Uchumi wa kati ngazi ya juu

Baada ya kufikia uchumi wa kati wa ngazi ya chini ndipo tunapaswa kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya juu.

Nchi zilizopo katika uchumi wa kati wa ngazi ya juu zinakuwa na wastani wa kipato kwa mwaka kwa kila mtu cha Dola za Marekani 4,036 na 12,475 yaani wastani wa kati ya Shilingi 8,637,040 na Shilingi 26,696,500.

Kwa kadiri ya Benki ya Dunia kuna nchi 55 katika kundi hili. Nchi hizi ni pamoja na Algeria, Angola, Botswana, Brazil, China, Irani, Jamaica, Namibia, Urusi, Afrika Kusini, Cuba, Libya, Iraki, Uturuki na kadhalika.

Hivyo tutakapoanza safari ya kuelekea uchumi wa kati wa ngazi ya juu tutakuwa tunataka kufanana na nchi hizi ikiwemo kila Mtanzania kuwa na kipato cha wastani wa Shilingi 8,637,040 na Shilingi 26,696,500 kwa mwaka yaani wastani wa kati ya Shilingi 719,753 na Shilingi 2,224,708 kwa mwezi. Kwa viwango vingi vya leo, hizi sio fedha kidogo.