Home Tukumbushane SHERIA MPYA IRUHUSU VYAMA KUUNGANA, KUSHIRIKIANA RASMI

SHERIA MPYA IRUHUSU VYAMA KUUNGANA, KUSHIRIKIANA RASMI

1563
0
SHARE

HILAL K SUED

Wiki iliyopita Msajili wa Vyama vya Siasa aliandika barua kwa vyama vya siasa na asasi za kiraia kuwasilisha mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria mpya ya vyama vya siasa ambayo amesema mchakato wake ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu 2020.

Sheria hiyo mpya itafuta sheria iliyopo (No 5) ya mwaka 1992, na tayari mapendekezo ya sheria mpya yamepingwa na vyama hivyo vikisema hayakuwa na lengo jema kwao.

Pendekezo jipya linaloonekana kuwa mwiba kwa vyama vingi ni kuweka ukomo wa kukaa madarakani kwa viongozi wa vyama na adhabu kwa viongozi wanaokiuka Katiba.

Pia, sheria hiyo inapendekeza kupigwa marufuku kwa vikundi vya ulinzi na usalama vya vyama pamoja na kutoa mafunzo ya nguvu kwa vikundi hivyo.

Kifungu kingine kinahusu muda maalumu kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha pingamizi la mkutano wa chama cha siasa, tofauti na sasa ambapo hakuna muda huo.

Chini ya sheria hiyo, mtu binafsi, kiongozi, shabiki au mwanachama anayetenda kosa anaweza kupewa adhabu.

Tofauti na sheria ya sasa inayovipa hadhi sawa vyama vyote vyenye usajili wa kudumu isipokuwa katika suala la kupata ruzuku, kutakuwa na utaratibu wa kuvipanga kwenye madaraja – vyenye uwakilishi, visivyo na uwakilishi kabisa na vyenye uwakilishi mdogo.

Kwa mtazamo mmoja haiwezekani kwa marekebisho yoyote katika Sheria hiyo kutoa nafuu kwa vyama vya siasa – na mara nyingi ni kuongezea tu namna ya kuvidhibiti kama ambavyo viongozi wa baadhi ya vyama tayari wamelalamika.

Haitarajiwi kwa sheria hiyo, au sheria yoyote nyingine kuhusu masuala ya siasa na uchaguzi kutoa nafuu kubwa kwa vyama vya siasa ili viweze kuja kukiondoa chama tawala (CCM) madarakani.

Hata hivyo si mara kwanza kwa ofisi ya Msajili wa Vyama kupendekeza mabadiliko ya Sheria hiyo, kwani huko nyuma kulikuwapo pendekezo la mabadiliko ya sheria hiyo ya vyama kutoa nafuu kwa vyama vya upinzani  ingawa baadaye pendekezo hilo lilikuwa geresha tu.

Mapema mwaka 2009 kabla kabisa ya kesi ile ya Mchungaji Mtikila kuhusu wagombea binafsi kutolewa maamuzi, na kabla mchakato wa kuwepo Katiba mpya haujaanza, mtangulizi wa Jaji Mutungi katika ofisi hiyo, John Tendwa aliwahi kutamka kwamba anatayarisha muswada wa kurekebisha sheria ya Vyama vya Siasa.

Moja miongoni mwa mapendekezo yake ilikuwa kuweka urahisi kwa vyama kuungana (mergers) kwa jina jipya, au angalau kushirikiana (alliances) unaotambulika rasmi. Pendekezo jingine la marekebisho ya Tendwa ni kusukuma kuwepo kwa wagombea binafsi katika ngazi zote za kugombea nafasi.

Wengi Walijiuliza: Mapendekezo haya yalikuwa ya dhati kutoka moyoni mwake na kwamba alikuwa na lengo la kuacha jina lake (legacy) katika kusimamia na kuendeleza demokrasia ya kweli hapa nchini?

Huenda pengine ndiyo lilikuwa lengo lake ingawa msukumo huo aliokuwa nao ulionekana ni hatari sana kwa chama tawala ambacho Mkuu wake ndiye aliyemteua katika wadhifa huo. Kwani demokrasia kweli ni ile ya haki, kitu ambacho kitaweza kutishia ukiritimba wa chama kimoja kukaa madarakani. Hebu fikiria tu uwepo hapa nchini wa Msajili wa vyama wa haki, Tume haki ya Uchaguzi na kadhalika.

Hatari ya kuwepo kwa muungano au ushirikiano rasmi wa vyama upande wa upinzani ulionekana katika uchaguzi uliopita wa 2015 pale ushirikiano usio trasmi chini ya mwavuli wa UKAWA uliweza kukitikisa chama tawala, na nchi nzima kwa ujumla.

Na ndiyo maana katika mapendekezo yake wiki iliyopita Msajili wa Vyama hakuliweka hili, kwani anajua halitakubalika. Aidha inasadikiwa vyama vya upinzani katika mapendekezo yao wataliweka lakini halitakuwepo katika rasimu ya mwisho ya muswada wa mabadiliko.

Ofisi ya Msajili wa Vyama taasisi ambayo imekuwa ikiibua mijadala mikubwa. Sasa hivi kwa mfano Ofisi hiyo inakabiliwa na kesi kadha mahakamani zilizofunguliwa na uongozi wa Chama cha Wananch CUF.

Lakini katika zote hizo kesi ya msingi inalenga madaraka halisi ya Msajili chini ya sheria hiyo hiyo ya sasa na inataka mahakama itamke iwapo anayo madaraka kuingilia migogoro ndani ya vyama na hivyo yeye mwenyewe kuamua na kutoa maamuzi yenye nguvu – yaani kama vile ya mahakama. Huenda katika marekebisho ya sheria inayopendekezwa hili litawekwa rasmi na hivyo kumpa Msajili nguvu kubwa.

Katika nchi zilizoendelea kidemokrasia ya vyama vingi, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kama ipo, huwa haionekani kabisa. Na kama ipo, basi kazi kubwa ya msajili huyo ni kukisajili chama kipya cha siasa katika daftari lake baada ya muombaji kujaza fomu husika na kutimiza masharti machache yasiyo magumu. Baada ya hapo anaenda likizo.

Nazungumzia nchi kama Marekani, Uingereza, Sweden, Denmark na kadhalika. Marekani kwa mfano, daftari la msajili wa vyama, kama lipo, lina majina mawili au matatu tu.

Kenya, nchi jirani yetu na ambayo imepitia misukosuko mikubwa ya kisiasa kuliko sisi, msajili wake wa vyama vya siasa huwa hasikiki kabisa katika malumbano ya kisiasa pamoja na jina linaloendana na wadhifa wake. Ni hivi karibuni tu nimegundua kuwa yeye ni mwanamama Lucy Ndung’u.

Mama huyu anaweza kusajili chama cha siasa katika muda wa wiki moja tu. Anaruhusu vyama kushirikiana (alliances) bila tabu yoyote. Na haya yote yalikuwapo hata kabla ya ujio wa katiba mpya nchini humo. Sina hakika katiba yao mpya inasemaje kuhusu masuala haya, lakini bila shaka taratibu hizo zimekuwa rahisi zaidi.

Ni kweli, sheria zilizopo nchini Kenya zinaruhusu yote hayo, lakini napenda tu kusema kwamba wanaoshikilia nyadhifa hizo wapo katika sayari hii na hufanya kazi yao kwa njia njema kwa masilahi ya nchi.