Home Latest News SHIMON PERES (1923–2016): ‘Mpenda amani’ aliyewakumbatia makaburu wa A. Kusini

SHIMON PERES (1923–2016): ‘Mpenda amani’ aliyewakumbatia makaburu wa A. Kusini

943
0
SHARE

NA HILAL K. SUED

Wiki iliyopita, aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Israel na baadaye kuwa Rais wa nchi hiyo, Shimon Peres alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 93.

Peres alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kwa vipindi vitatu tofauti na baadaye kuwa rais, na ni miongoni mwa waasisi waliokuwa wamebakia wa taifa la Israel.

Ingawa duniani alikuwa akitambulika kama kiongozi mpenda amani na kuwa tayari kuipata amani hiyo kwa njia ya mazungumzo, lakini kiukweli anakumbukwa zaidi kwa kuendelea kutwaa na kuyatawala maeneo ya Wapalestina na pia katika kuasisi mradi wa nyuklia wa Israel.

Aidha, wafuasi wake watamkumbuka kwa kupigania uwepo wa taifa la Palestina na kama mmoja wa waanzilishi wa chama cha Labour chenye mrengo wa kushoto.

Kabla ya kuanza kuundwa kwa taifa la Israel muda mwingi wa ujana wake alikuwa anajihusisha na uhamasishaji wa itikadi ya kisoshalisti na kuunda asasi za itikadi hiyo.

Kwa juhudi zake binafsi akiwa miongoni mwa mawaziri wa kwanza kwanza wa ulinzi alisaidia sana katika uundwaji wa jeshi imara la nchi hiyo, jeshi ambalo baadaye likaja kuwa na nguvu mno.

Hata hivyo, alihusika sana katika mikataba miwili ya amani ya eneo hilo na ameandika vitabu 11 kuhusu visheni yake ya Mashariki ya Kati, ambayo iliiona Israel ikijenga mahusianio makubwa ya kiuchumi na nchi za Mashariki ya Kati.

Lakini kwa wengi, Shimon Peres atakumbukwa kama ‘tai’ (Kiingereza ‘hawk’) wa kijeshi, ingawa yeye mwenyewe hakuwahi kuvaa sare za kijeshi au kupigana katika vita yoyote baina ya nchi yake na mataifa ya Kiarabu. Hivyo alitumia hadhi yake kama mtu wa kupigania amani ili kuuhadaa ulimwengu tu, wakati nyuma ya pazia alikuwa anahusika sana katika kujenga nguvu za kijeshi za Israel.

Mwaka 1996 wakati akiwa Waziri Mkuu na pia Waziri wa Ulinzi, alianzisha mapambano yaliyoitwa “Operation Grapes of Wrath” dhidi ya Lebanon.

Aprili 18, 1996 vikosi vya anga vya Israel vilishambulia kwa mabomu eneo la Umoja wa mataifa la Qana ambamo zaidi ya wakimbizi 800 walikuwa wamechukua hifadhi na hapo hapo kuwauwa zaidi ya 100. Mauaji haya yaliibua upinzani mkubwa kila alipokuwa akihutubia.

Katika miaka ya baadaye Peres hakuonyesha dalili yoyote ya kujutia kuhusu operesheni ile ya kijeshi, na alidiriki hata kusema kwamba ilikuwa haimuondolei amani.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa kila mara ulikuwa unaiambia Israel kwamba eneo la Qana lilikuwa linahifadhi wakimbizi. Robert Fisk, mwandishi mmoja maarufu wa Uingereza kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati anaeandikia gazeti la The Independent, aliandika wakati huo kwamba, Peres binafsi alibariki shambulio lile ili kujiongezea hadhi ya kisiasa nchini mwake. Shambulio hilo lilifanyika siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa kuziba pengo lilioachwa wazi baada ya kuuawa kwa Waziri Mkuu aliyetangulia – Yitzhak Rabin.

Msimamo wake dhidi ya Wapalestina ulikuwa unajulikana – miaka minne iliyopita aliwahi kunukuliwa akisema Wapalestina walikuwa wanajiangamiza wenyewe.

Kama ilivoelezwa hapo juu Shimon Peres ndiye alikuwa muasisi wa mradi wa nyuklia wa nchi hiyo – mradi ambao hadi sasa nchi hiyo haijaukubali rasmi.

Akiwa Waziri wa Ulinzi chini ya Yitzhak Rabin, alitaka kuiuzia Afrika ya Kusini zana za nyuklia kinyume cha vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa. Novemba mwaka 1974 Peres alisafiri hadi Pretoria, Afrika ya Kusini kuonana na viongozi wa utawala wa kibaguzi.

Baada ya ziara hiyo Peres aliwaandikia wenyeji wake akiwashukuru kwa kusaidia katika kuanzisha kile alichokiita  ‘mahusiano makubwa’ baina ya serikali zao mbili.

Hata hivyo Peres mara kwa mara alikuwa akilaani sana hadharani siasa za kibaguzi za Afrika ya Kusini, lakini baada ya ziara hii alisema: “uhusiano huu na Afrika ya Kusini ulikuwa umejengwa si tu katika masilahi yetu yanayofanana, bali hasa katika juhudi zetu za kupambana na adui zetu, na pia kulinda misingi imara ya kupigania haki na kupingana na uonevu wa aina yoyote.”

Mahusiano ya kijeshi baina ya Israel na Afrika ya Kusini yalishamiri sana katika miaka iliyofuatia na alipoulizwa na gazeti la Guardian la Uingereza hivi karibuni kuhusu ushiriki wake katika kudumisha mahusiano yale alisema: “Huwa sirudishi fikra zangu nyuma. Kama sina uwezo wa kubadili mambo yaliyopita, kwa nini nijishughulishe nayo?”

Wakati hadhi ya Peres ulimwenguni ilipanda chati baada ya kutiwa sahihi Mkataba wa Oslo – mkataba wa amani na Wapalestina, Peres alikuwa wa kwanza kushabikia sera ya utwaaji wa ardhi ya Wapalestina kwa ajili ya kujenga makazi ya Wayahudi.

Aidha ikumbukwe kwamba baada ya Mkataba wa Oslo, mwaka 1994 Peres, Rabin na Kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat walitunukiwa pamoja medali ya Amani ya Nobel.

Lakini sera ya utwaaji wa ardhi, kama ilivyoelezwa hapo juu, Peres aliiasisi tangu akiwa Waziri wa Ulinzi katika miaka ya 70, kufuatana na hati za kimaandishi zilizochapishwa katika tovuti ya Gershom Gorenberg.

Hati hizo za tangu mwaka 1976 zinaonyesha hata ramani ya mji wa Jerusalem namna utakavyokuwa na makazi ya Wayahudi baada ya ardhi kutwaliwa.

Na miaka miwili iliyopita Peres aliwahi kuliambia gazeti maarufu nchini humo la Jereusalem Post kwamba, Waziri Mkuu wa sasa wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu alikuwa tayari kuishambulia kijeshi Iran lakini yeye (Peres) alimwambia “achana na kitu hicho kabisa.”

Agosti 2014 Peres, alidaiwa kusema hivyo katika mahojiano na wahariri Steve Linden na david Brinn kwamba, aliwakataza wanahabari hao wasichapishe habari hizo hadi Peres atakapokuwa amefariki.

Ikumbukwa kwamba mwaka 2011, Netanyahu na Waziri wake wa Ulinzi wakati huo Ehud Barak, walikuwa wanajenga hoja ya kuishambulia kijeshi Iran kutokana na kwamba Jamhuri hiyo ya Kiisilamu ilikuwa imedhamiria kuiangamiza Israel kwa silaha za nyuklia.

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa vyanzo mbali mbali vya Intaneti.