Home Makala SHIRLEY CHISHOLM: MWANAMKE WA KWANZA KWA KILA KITU KWENYE SIASA ZA MAREKANI

SHIRLEY CHISHOLM: MWANAMKE WA KWANZA KWA KILA KITU KWENYE SIASA ZA MAREKANI

977
0
SHARE

LUQMAN MALOTO,

HUTOKEA mtu kufanya mengi na asikumbukwe. Wakati mwingine binadamu huamua kutoa kipaumbele kwa jinsi wanavyopendezwa wao. Ni vipaumbele kutokana na matakwa, siyo kwa hali halisi.

Unafanya kazi kubwa na haipewi kipaumbele? Unaona watu hawaioni? Wala usijali, unachotakiwa ni kuendelea kufanya kazi nzuri kila siku. Wengi wasipoithamini wapo wachache wataitetea.

Historia ina kawaida ya kutoa upendeleo. Matakwa ya watunza kumbukumbu na waandishi wa historia, huamua nani mkubwa. Hii ni sababu kwamba watu wengi waliofanya mambo makubwa duniani hawatambuliki kwa thamani yao.

Hillary Rodham Clinton aliweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa na chama chake, Democrats, kuwa Mgombea Urais wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba 2016 lakini akashindwa.

Sifa nyingi zinampamba Hillary kama mwanamke mwenye uthubutu mkubwa na kwa uthubutu wake aliweza. Anatazamwa kama raia wa Marekani aliyekaribia kwenda kuyafanya makazi yake Ikulu ya nchi hiyo, White House.

Hillary alipambana na mwanasiasa, vilevile mfanyabiashara mtata, Donald Trump wa Chama cha Republican ambacho hujulikana pia kama Grand Old Party (GOP). Trump ndiye Rais wa Marekani kwa sasa.

Safari ya Hillary inapambwa pia kwa sifa kwamba ni mwanamke wa kwanza akitokea kuwa mke wa rais (first lady), kugombea uongozi na kushinda. Kati ya Januari 2001 na Januari 2009, Hillary alikuwa Seneta wa Jimbo la New York.

Mwaka 2008, Hillary alijitosa kwenye Uchaguzi wa Rais kupitia Democrats lakini alikutana na ushindani mkubwa dhidi ya Rais Barack Obama ambaye alishinda. Hillary alitoka wa pili.

Hillary mke wa Rais wa 42 wa Marekani, William Jefferson Clinton ‘Bill Clinton’, anapewa ukubwa kwa mambo hayo tu. Ila yupo mwanamke ambaye ameshafanya uthubutu mkubwa tena katika kipindi kigumu zaidi kisiasa lakini hakumbukwi.

Rais Obama anapewa sifa kuwa mtu mwenye uthubutu, akiwa Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyefanikiwa kuishawishi jamii kubwa ya Wazungu kumpigia kura na kuandika historia yake ya kuwa Rais wa Marekani.

Katika dunia ambayo inaendelea kukumbwa na uasili wa mfumo dume, Obama ni mwanaume. Na kama kielelezo ni ubaguzi wa rangi, basi Obama ni nusu Mzungu, nusu Mwafrika. Kwamba baba yake ni Mjaluo wa Kenya, mama yake Mzungu wa Marekani.

Miongo minne kabla ya Obama na Hillary, alikuwepo Shirley Chisholm. Huyu ndiye mwanamke wa kwanza, tena mwenye asili ya Bara la Afrika kwa baba na mama, kuthubutu kisha kuingia kwenye mchakato wa kuwania nafasi ya uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Democrats.

Mwaka huu 2017, rudi miaka 45 nyuma, Shirley aliweka historia pale alipowashangaza wengi, alipotangaza azma yake kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuelekea White House.

Nia yake hiyo ya kuiwania nafasi kuu ya utumishi (top job) kwa Marekani, ilikuwa na uhai mfupi lakini ndiyo iliyoweka rekodi ambayo imefungua milango. Ni tangu kwa Shirley ndipo ilipoonekana kumbe wanawake wanaweza, zaidi Waafrika wakiota ndoto kubwa watazifikia.

Shirley ni mfungua njia (pioneer) kuanzia kizazi chake, cha sasa na kijacho, kwa wanawake kufikiria ngazi kubwa za kiutumishi basipo kuhofia chochote. Zaidi aliwafungulia njia wanawake wa Kimarekani wenye asili ya Afrika kutamani na kuthubutu mambo makubwa bila woga.

Chukua hii; Bila kuonesha uthubutu kuwa unaweza kufanya vitu ambavyo watu wanaamini huwezi, basi kila siku utarukwa na watafikiriwa au kufuatwa na kupewa nafasi wengine wenye kuonekana wanaweza.

Unaweza jambo? Usikae pembeni umejikunyata au kuhofia kuwa hutaeleweka na utadharauliwa. Simama nao mstari wa mbele, jipambanue kuwa unaweza kuliko wao. Wathibitishie kwamba viwango vyako ni bora zaidi ya wanaofikiriwa na kupewa nafasi. Uwezo ni lazima uanze kwa kuoneshwa.

Shirley ni mwanamke wa nafasi nyingi za kwanza (woman of many firsts). Ndiye mwanamke wa kwanza menye asili ya Afrika nchini Marekani kushinda ujumbe wa Bunge la Marekani (Congress). Kwa lugha rahisi ni kuwa Shirley ni mbunge wa kwanza mwanamke mwenye asili ya Afrika nchini Marekani.

Shirley ndiye Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika, kwa jinisa zote kuwania Urais wa Marekani. Kabla yake hakuna aliyethubutu japo kuifikiria nafasi hiyo kubwa nchini.

Ongezea pia kuwa Shirley ndiye mwanamke wa kwanza kwa rangi zote, kuwania uteuzi wa kuwa Mgombea Urais wa Marekani kupitia Chama cha Democrats. Hapa ndiyo kuonesha kuwa Hillary anafuata baada ya Shirley kutoa changamoto.

Nafasi ya ujumbe wa Congress (congresswoman) aliipata baada ya kushinda ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa vipindi saba mfululizo. Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi huwa na mihula ya miaka miwili miwili, kwa hiyo alidumu kwenye nafasi hiyo miaka 14 mfululizo.

Shirley alikuwa mwanachama wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, akiwakilisha Jimbo la New York, Wilaya ya 12, kuanzia Januari 3, 1969 mpaka January 3, 1983 na alikuwa Katibu wa Kambi ya Chama cha Democrats (House Democratic Caucus) ndani ya Congress kati ya Januari 3, 1977 mpaka Januari 3, 1981.

ALIVYOGOMBEA URAIS MWAKA 1972

Shirley alianza kuzunguka na kueleza dhamira ya kugombea Urais Julai 1971, kisha kwa urasmi kabisa, alitangaza nia yake Januari 25, 1972, mtaani kwao jijini Brooklyn.

Kampeni yake ya kuuelekea Urais wa Marekani mwaka huo, aliita Mapinduzi Bila Damu (Bloodless Revolution). Na alijitahidi kupambana kuzipa hadhi mbio zake ili aonekane ni mgombea mwenye nguvu na siyo msindikizaji.

Katika kampeni zake hizo, Shirley alitumia dola 300,000 amabazo kama zingebadilishwa kwa thamani ya sarafu ya Tanzania kwa sasa, ingefika zaidi ya shilingi milioni 600.

Hata hivyo, alipuuzwa sana na wanachama wa Democrats hasa wanaume, hali hiyo ilimvunja moyo kisha akeleza kuwa changamoto aliyokutana nayo siyo kwa sababu ya Uafrika wake bali jinsia yake ya kike.

Shirley alisema: “Nilipogombea kwa ajili ya Congress, nilipogombea kwa ajili ya urais, nilikutana na ubaguzi mkubwa zaidi kama mwanamke kuliko kuwa mtu mweusi. Wanaume ni wanaume tu.”

Katika hilo, Shirley aliwaponda wanaume wa Kimarekani wenye asili ya Afrika, hasa wale waliokuwepo ndani ya Democrats: “Wanafikiri najaribu kuchukua mamlaka kutoka kwao.

Mwanaume wa Kiafrika lazima apige hatua mbele lakini haimaanishi mwanamke wa Kiafrika apige hatua nyuma.”

ALINUSURIKA KUUAWA MARA TATU

Pamoja na dharau dhidi yake lakini bado Shirley alionekana ni mwanamke hatari kwa ushupavu wake. Wakati anawania tiketi ya Democrats kuwa Mgombea Urais wa Marekani, alinusurika kuuawa mara tatu.

Hali hiyo ilisababisha mume wa Shirley, Conrad Chisholm aache majumuku yake mengine na kusimama kama mlinzi wa mke wake ili kumwepusha na hatari ambayo ingeweza kujitokeza kutokana na majaribio hayo ya kumuua.

Conrad alifanya kazi hiyo mpaka Mei 1972, Idara ya Siri ya Usalama Marekani, ilipomuwekea ulinzi Shirley, baada ya hatari kuonekana imeshakuwa kubwa.

Mwisho wa mbio hizo za kuwania uteuzi wa chama chake kuwa Mgombea Urais, Shirley alitoka wa nne. Baada ya matokeo hayo alisema: “Pamoja na kila aina ya changamoto, niligombea bila kuwa na matumaini.”

Katika mchakato huo, Shirley aliongoza kwenye majimbo matatu kwa jumla ya kura, New Jersey, Louisiana na Mississippi, hivyo kumthibitisha kama mwanamke shupavu na ambaye alikuwa anakaribia kuweka mapinduzi makubwa.

ALIFUNGUA NJIA YA OBAMA, HILLARY

Wachambuzi mbalimbali wanamuelezea Shirley kama mwanamke aliyefungua njia kwa wanawake wengine ndani ya siasa za Marekani, vilevile ni ufunguo wa wanaume kuwania utumishi wa ofisi kuu ya Marekani.

Wachambulizi wanaeleza kuwa mwanzo uliowekwa na Shirley mwaka 1972 ndiyo uliofungua njia za kampeni za Hillary na Obama mwaka 2008 ndani ya Democrats. Hillary kwa uanamke wake na Obama kwa Uafrika wake.

Kwamba mchuano wa Obama na Hillary ulijengwa zaidi na matokeo ya Shirley, jinsi alivyocheza na siasa mwaka 1972.

Akiwa mjumbe wa Congress, Shirley alianzisha Kambi ya Wajumbe Weusi, yaani Wamarekani wenye asili ya Afrika ambayo imesaidia mambo mengi, kwanza kutengeneza ajenda za Waafrika, vilevile kutoa urahisi kwa wanafunzi wa Kiafrika wanaotaka kujifunza kwa vitendo mambo ya Kibunge.

Hapo kabla, haikuwa rahisi kwa wanafunzi wa Kiafrika kupata nafasi ya kwenda Congress kupata mafunzo ya vitendo (internship).

“Shirley alitengeneza njia rahisi kwetu sisi kiasi kwamba tunaweza kupanda mlima mkali,” Kimaya Davis, mwenye umri wa miaka 22, anayefanya kazi kwenye kamati ya Congress, anamuelezea Shirley.

Kimaya ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika, alisema kuwa amepata kazi hiyo baada ya kusoma kwa vitendo kupitia Kambi ya Wajumbe Weusi wa Congress (Congressional Black Caucus) iliyoasisiwa na Shirley.

Ni kwa sababu ya msingi ambao Shirley aliutengeneza ndiyo niliweza kupata nafasi ya mafunzo ya vitendo. Inasaidia sana kuwezesha vijana wa Kimarekani wenye asili ya Afrika.

Vijana wengi kama mimi hatuna mtandao wa kifamilia ambao unaweza kutupa nafasi lakini tunapata kwa sababu kuwepo kwa kambi ya wausi,” anasema Kimaya.

SALUTI KWA KILA ALIYEMUONA

Kwa wale ambao walimfahamu, wanaeleza kuwa Shirley alikuwa zaidi ya mfano wa kuigwa, alikuwa ni nembo akistahili heshima na kumbukumbu zenye thamani kuliko ambavyo imekuwa.

“Alijulikana zaidi mwishoni mwa miaka 1960 na 1970, lakini kama hukuwepo nyakati hizo ni rahisi kusahaulika,” anasema Ky Ekinci, mjasiriamali wa kijamii, anayeishi Florida, Palm Coast.

Ekinci aliwahi kufanya tukio la heshima kwa kuratibu Siku ya Shirley Chisholm, takriban watu 50 walihudhuria kufurahia maisha ya Shirley.

ASILI YAKE

Jina lake kutoka kwa wazazi wake ni Shirley Anita St. Hill. Alizaliwa Novemba 30, 1924, Brooklyn, New York. Wazazi wake ni wahamiaji wa Marekani waliotokea Caribbean.

Alikuwa na wadogo watatu wa kike, wawili walizaliwa ndani ya miaka mitatu tangu kuzaliwa kwake, baadaye mmoja alifuata. Baba yao Charles Christopher St. Hill, alizaliwa British Guiana na kuishi Barbados kabla kufika Marekani kupitia Antilla, Cuba, April 10, 1923.

Mama yao, Ruby Seale, alizaliwa Christ Church, Barbados, na alifika Marekani, jijini New York, Machi 8, 1921. Baba yake alifanya kazi kama kibarua kiwandani, vivyo hivyo kwa mama yake.

Shirley alisoma Chuo cha Brooklyn na baadaye Chuo Kikuu cha Columbia na kupata Shahada ya Kwanza ya Sanaa (BA) kisha Shahada ya Pili ya Sanaa (MA).

Alikuwa mwalimu kitaaluma na kipindi akifundisha ndipo alipopata hamu ya kufanya siasa. Kabla ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, alikuwa Mjumbe wa Bunge la New York kuanzia mwaka 1965 mpaka 1968 kisha mwaka uliofuata ndipo aliingia Congress.

NUKUU YA SHIRLEY: “Vipaji vikubwa na vilivyotuka vinapotea kwenye jamii yetu kwa sababu vipaji hivyo vinavaa sketi.”

Tafsiri: Hapo Shirley anamaanisha kuwa wanawake wengi wenye vipaji vikubwa, wanadidimizwa na vipaji vyao vinapotea bila kuonekana kwa sababu ya ukandamizaji kwa mwanamke.

“Hisia, ngono na mgamizo wa kisaikolojia kwa mwanamke huanza pale daktari anaposema, ni msichana,” anasema Shirley.

Shirley na Conrad walitengana mwaka 1977, baada ya kuwa kwenye ndoa kwa takriban miaka 30. Baada ya hapo, Shirley aliolewa na Arthur Hardwick, Jr ambaye ni mjumbe wa zamani wa Bunge la New York. Shirley alifariki dunia Januari Mosi, 2005.