Home Latest News SIASA SAFI, DEMOKRASIA NA DINI DAMU DAMU

SIASA SAFI, DEMOKRASIA NA DINI DAMU DAMU

1400
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA

 SI mara haba tumemsikia Rais wetu, John Magufuli (JPM) akitutaka Watanzania katika kipindi cha uongozi wake, wenye harakati nyingi zikiwamo vita dhidi ya rushwa, ufisadi na maovu mengine ya kijamii, tumwombee kwa Mungu amalize salama na kwa mafanikio.  Maana yake nini?

Ni kwamba, kwake uwapo wake madarakani ni tunda la siasa safi; kuwataka watu wamwombee kwa Mungu ni ishara ya uongozi shirikishi kwa maana ya demokrasia na imani juu ya nguvu ishindayo nguvu zote, ikimwongoza, kwa maana ya Mungu; imani inayozaa kile kinachoitwa “dini” na ibada.

Kwa kuwa kauli hii haipingiki kwa vigezo vyote na yenye kuheshimika kwa jamii yoyote inayoitwa ya “kistaarabu”, tunaweza kusema siku zote, siasa safi, demokrasia na dini ni damu damu na kuwasuta wote wenye kushikilia dhana potofu kwamba “siasa na dini hazichanganyiki”; au lile katazo potofu la “kutochanganya dini na siasa”. Mambo haya matatu; siasa, demokrasia na dini, yana lengo moja, “maisha na ustawi wa mwanadamu”.

Zaidi ya miaka 100 iliyopita, mwanaharakati wa siasa za mapambano, Karl Marx, alidai kwamba, “dini” ni bangi inayolevya na kupumbaza watu wasiweze kujua adui wao wala kupigania haki zao.  Kwa mtizamo huo, Marx aliona dini kama taasisi inayopinga mapinduzi ya wanyonge, wenye kuonewa na kunyanyaswa, akatangaza vita dhidi yake.

Ni kwa sababu hii, mpaka leo dini (kanisa) havikai meza moja na itikadi za Ki-Karl Marx, (Ukomunisti) na dhana nyingine za kimapinduzi.

Zaidi ya miaka 2000 iliyopita, Yesu Kristo (Nabii Issa), wakati akijibu mashtaka dhidi yake kwenye kesi ya uhaini, alipotuhumiwa kutaka kupindua Serikali ya Kaisari, aliulizwa kwa mtego, aeleze ni kwa mamlaka yapi alielekeza utii wake kwa Mungu wake au kwa Kaisari?  Naye akajibu, “Cha Kaisari apewe Kaisari na cha Mungu apewe Mungu”.  Hapo ndipo ikazaliwa dhana ya kutochanganya dini na siasa, tafsiri ambayo mara nyingi imewasilishwa kwa kupotoshwa katika jamii.

Katika makala haya nitatumia neno “kanisa” kumaanisha jumuiya za waumini wa dini wa madhehebu mbali mbali katika jamii pana inayotawaliwa bila ubaguzi wa ki-madhehebu.  Kwa kifupi, kanisa ni waumini wa dini na si majengo ya kuabudia.

Kwa fikra za enzi za Karl Marx, dini na kanisa vilikuwa  vyombo vya watawala na vya wenye elimu, vilivyotumika kuwakandamiza na kuwaogofya (juu ya moto wa milele), kuwadhibiti na kuwapumbaza wanyonge kwa ahadi ya “ufalme wa mbingu”, kwa kuwaamuru Wajikani wenyewe, wasijifahamu wala kujipeleleza kujua chanzo cha matatizo yao yenye kusababishwa na binadamu wenzao.

Kilicho wazi hapa ni kwamba, upofu wa Karl Marx haukuwa juu ya dini, bali ugomvi wake ulikuwa juu ya watawala na kanisa kutekwa na ubinafsi wa watawala, waiochanganya dini na utawala kuzaa dhana na utawala wa Kiotheokrasia kwa nchi kuongozwa kwa misingi ya kidini; kwa dini huwa sehemu ya mfumo wa utawala wa nchi kuwa na “Kaisari – Mungu”.

Wapo watu waliomtangulia Karl Marx waliogundua udhaifu huo wa kanisa pekee la Roma la wakati huo (lililotekwa nyara na watawala tangu enzi za Mfalme Constantine wa I), lakini hawakushambulia dini, badala yake walishinikiza kufanyika marekebisho katika mfumo na mwenendo wa kanisa bila kuathiri imani na nafasi ya dini katika jamii.

Hawa ni pamoja na Mchungaji Martin Luther (1483 – 1534) aliyeanzisha Tawi la Kilutheri la Kanisa Katoliki la Roma; Mfalme Henry wa VIII wa Uingereza aliyejiengua kutoka Kanisa la Roma na kutangaza Kanisa lake la Anglikana; na John Calvin (1509 – 1547) aliyebuni Ukristo wa mapokeo ya Ki-Kalvin, kwa kutaja matukio machache tu.

Enzi za Karl Marx, kulikuwa na dini mbili za kimataifa: Ukristo na Uislamu.  Misahafu ya dini hizi ni Biblia (Ukristo) na Kurani kwa Uislamu.  Misahafu yote miwili inatetea wanyonge na kupiga vita uonevu, ukandamizaji na unyonyaji na kuwataka wanaoonewa kuasi dhidi ya vyanzo vya uovu na maovu.  Kama Marx angeisoma vizuri misahafu hiyo bila kuyumbishwa na matendo ya watawala walioliteka Kanisa, wakaitumia dini kwa manufaa yao, bila shaka asingejenga uhasama wala ukinzani na dini; badala yake angekuwa mtetezi mkubwa wa dini na Kanisa la kweli.

Tuchukue mfano wa harakati na uanamapinduzi wa Kristo: Kuna wakati alizua tafrani na ukinzani na watawala kwa kuwataka wajisafishe maovu yao, uonevu na dhuluma kwa wanyonge, kitendo kilichosababisha akamatwe na kusulubiwa kwa tuhuma za kuchochea maasi dhidi ya utawala wa nchi.  Kati ya wanafunzi wake 12, wawili kati yao, Simon na Yuda, kabla ya kumfuata, walikuwa wanaharakati wakereketwa (zealots) wa haki za binadamu na wapiganaji dhidi ya utawala wa kikoloni wa Kirumi nchini Uyahudi.

Uanamapinduzi wa Kristo unathibitishwa na maneno kama, “Nimekuja kutupa moto duniani”; au, “Sikuleta amani, bali upanga” (Luka 12: 49 – 53) kwa maana ya  mapambano ya ana kwa ana dhidi ya udhalimu katika jamii.

Na kwa sababu jamii ya wakati huo ilikuwa imejaa maovu, kama ambavyo Taifa letu lilivyogubikwa na rushwa na ufisadi, palitakiwa wachache kujitoa mhanga kwa manufaa ya walio wengi kama Kristo alivyojitoa na kama afanyavyo sasa JPM.   Na ili mtu aungane naye Kristo alisema, “Mtu ajikane mwenyewe na anifuate”.  Hata siku ya kusulubiwa msalabani, hakujutia vita aliyoianzisha; akawaagiza wafuasi wake wauze kanzu (nguo) zao, ili wanunue mapanga kuendeleza harakati za kuwakomboa wanyonge.

Kuhusu utajiri wa kinyonyaji, aliwaonya watawala wenye uchu wa kutajirika, kwamba hawawezi kutumikia mabwana wawili, Mungu (watu) na mali (utajiri) bila kuteteresha ukweli na haki; akasema, ni rahisi ngamia kupita kwenye tundu ya sindano, kuliko tajiri kuuona ufalme wa mbingu. Leo, tunapoambiwa kutenganisha madaraka na biashara, tunataharuki kama vile tumemwagiwa upupu.

Aliwanyuka mijeledi wezi na wafanyabiashara, walioweka mbele masilahi yao binafsi kuliko utu, alipowakuta wakiuza bidhaa kwa ulanguzi hekaluni.  Ikulu, kama lilivyo hekalu na msikiti ni mahali patakatifu; kwa sababu ndipo maamuzi makuu hutokea.  Ni dhambi kubwa kwa wanasiasa, kama ilivyo kwa waumini wa dini, kupageuza mahali patakatifu kuwa pango la walanguzi, kama alivyoonya Mwalimu Nyerere mwaka 1990.

Usawa wa binadamu katika jamii umesisitizwa pia katika Kurani tukufu kwa kuhusishwa na zaka (zakat) na sala kuwawezesha masikini kuendesha maisha mazuri kama binadamu wengine (LXX: 24 – 25). Kurani tukufu inasisitiza utu na wajibu wa kila mtu kwa jamii (jamaa), mshikamano katika usawa, na ushirikiano kwa jamii nzima (XVII: 70).

Uislamu, kama ulivyo Ukristo, unasisitiza haki, wema, usawa na ukweli kwa watu wote, hata kama hayo hayatamfurahisha muumini mwenyewe, wazazi au ndugu zake (IV: 135).

Karl Marx hakuyaona hayo, na hakuweza kuzitekeleza kwa vitendo nadharia zake, kwani alifia uhamishoni kama mkimbizi na kuacha mabunda lukuki ya vitabu vya fikra zake.

Katika zama zetu hizi, je, dini ina nafasi yoyote katika maendeleo ya jamii au bado ni yale yale ya mtazamo wa Karl Marx?   Ni kipi hicho kinachoitwa kuchanganya dini na siasa?

Ukichunguza kwa makini, utaona kuwa mambo yanayopigiwa kelele na viongozi wa dini, na ambayo watawala wanadai ni kuchanganya siasa na dini, ni pamoja na mambo kama:  tofauti kubwa ya umilikaji mali na utajiri wa nchi, kati ya wageni wahamiaji wachache na wazawa; ufukara unaoendelea kukithiri hasa kwa wananchi waishio vijijini; kupanuka kwa ufa kati ya “walio nacho” na wasio nacho; ubaguzi na kashfa za kidini.

Mengine ni kukosa kazi kwa vijana mijini; kuongezeka kwa maovu kama vile rushwa, madawa ya kulevya na ufisadi; kuongezeka kwa siasa za kujuana kwa namna ya mshikamano kati ya matajiri wakubwa na kada ya watawala, na mengine mengi.

Kanisa kama sehemu ya jamii, linaguswa na yote yanayotokea katika jamii. Kama tulivyoona hapo mwanzo,  wajibu wa dini na kanisa ni kutetea haki katika jamii kwa maendeleo ya wote, hasa wale wanaoathirika kutokana na matendo ya wengine (wachache) wasiojali.  Kwa sababu hii Kanisa na  binadamu yeyote mwenye kujali utu, haliwezi kunyamazia maovu  haya.

Vivyo hivyo, Kanisa makini haliwezi kuhubiri Injili ya amani na upendo, wakati waumini wake na jamii kwa ujumla, ni wenye njaa, wenye kuandamwa na magonjwa na umasikini uliokithiri ndani ya nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali, wanaonewa na kunyanyaswa na kunyimwa haki ya kuishi maisha bora na kushiriki katika kutoa maamuzi ya nchi yanayogusa jamii pana.

Kanisa (waumini) ni sehemu ya jamii na jamii ni sehemu ya kanisa.  Kwa mfano, Waumini wa dini wanashiriki kulipa kodi; wanashiriki chaguzi za kuweka viongozi madarakani; na wanashirki pia kazi za maendeleo ya nchi kwa jasho na damu.  Kwa nini wasitumie haki yao, kama wananchi wengine, kuonya, kukemea na kupigia kelele maovu yanayoisakama nchi yao?  Kwa nini kufanya hivyo kuitwe ni kuchanganya dini na siasa?

Nchi inapodidimia katika maisha ya rushwa umasikini wa kulazimishwa, kuvunjika kwa maadili mema, ufisadi na uporaji rasilimali za Taifa na kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi; Kanisa haliwezi kukaa kimya.  Likifanya hivyo, litakuwa linakwepa wajibu wake wa kinabii (Prophetic ministry) na hivyo litapashwa kulaumiwa kwani maovu ni chanzo cha kuvunjika kwa amani.  Ni Mungu yupi anayetaka maovu na vurugu zitawale miongoni mwa watu wake?

Wala si sahihi enzi zetu kudai kwamba watawala huwekwa madarakani na Mungu,  eti kwamba kuwahoji kwa matendo yao ni kupingana na Mungu, au kuchanganya siasa na dini. Mtazamo huu, unaoitwa kwa Kiingereza “The Positivistic view”, unawakweza watawala waovu waonekane kufanana na Mungu kimamlaka ili tuwaogope.  Ni dhana ya kale iliyoasisiwa na Mfalme Constantine wa I wa Rumi ya kale, alipoingiza dini kuwa sehemu ya mfumo wa Serikali (Theocratic state) kuwalinda watawala wasiguswe wala kuhojiwa na jamii, kwa madai ya kuwekwa madarakani na Mungu.

Mtizamo huo ulianza kupoteza ngvu wakati wa utawala wa fashisti Adolf Hitler (Ujerumani) na swahiba wake Benito Mussolini wa Italia karne ya 20, pale watu walipoanza kuhoji, kama kweli hao nao waliwekwa madarakani na Mungu.  Na katika enzi zetu tunaendelea kuhoji, kama kweli madikteta kama Idi Amin (Uganda), Jean Badel Bokassa (Afrika ya Kati), Marcias Nguema (Equatorial Guinea), Mobutu Seseseko (Zaire/DRC), nao waliwekwa madarakani na Mungu?

Mtizamo wa “Positivistic view” na dhana nzima ya watawala kuwekwa madarakani na Mungu (Warumi 13), unapingwa vikali na waumini wa mapokeo ya Ki-Kalvin  (Calvinistic view) kwa maelezo kwamba, anachoagiza Mungu na kuweka madarakani si Serikali yenyewe, bali Mungu anaamuru mfumo wa Serikali inayofaa. Ni kwamba, Serikali inayotimiza matakwa ya demokrasia na utawala bora na kukubalika na wengi, ndiyo Serikali inayostahili kuitwa imewekwa na Mungu, kwani sauti ya wengi ni sauti ya Mungu; na hiyo inayokwenda kinyume chake hupoteza mamlaka na uhalali wa kutawala, na hivyo haiwezi kudai kuwa imewekwa na Mungu.

Kanisa halipaswi kukaa kimya kueleza ukweli, kwani ni jukumu lake kusimamia mfumo wa aina bora ya Serikali itakiwayo na Mungu kwa watu wake.  Kufanya hivyo si kuchanganya dini na siasa, bali ni wajibu wake wa kiunabii usioepukika.

Peter Merkle, anabainisha pande mbili za siasa, za uzuri na ubaya; kwamba, uzuri wa siasa bora ni ile shauku ya mwanasiasa ya kutaka kuona kuwapo kwa haki na utaratibu mzuri wa utawala unaojali. Na kwa upande wa ubaya, ni ile tamaa mbaya ya madaraka, utukufu na utajiri.  Hili la mwisho lazima lipigwe vita na waumini wa dini zote, kwa maana haliwakilishi mapenzi ya Mungu kwa watu wake.

Kwa hili, Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius K. Nyerere, analiweka wazi katika kitabu chake “Binadamu na Maendeleo”, akisema: “Ikiwa (waumini) hatutashiriki kwa vitendo katika kuondoa utaratibu wa maisha na uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge; basi, Kanisa (dini) litakuwa halina uhusiano na maisha ya binadamu, na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu. Na ikiwa hivyo, Kanisa litakufa, maana litakuwa halina maana inayoeleweka kwa mtu wa (leo) kisasa”.

Mwalimu anaelezea namna watawala walivyogeuka kuwa miungu watu mathili enzi za Mfalme Constantine; anasema:  “Tunasema kwamba binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Mimi nakataa kumfikiria Mungu aliye fukara, mjinga, mshirikina mwoga, dhalili, ambayo ndiyo hali ya walio wengi aliowaumba kwa mfano wake mwenyewe.  Binadamu wenyewe ni waumbaji, hujitengenezea hali zao za maisha; lakini tulivyo sasa tu viumbe, tena si viumbe wa Mungu, bali wa binadamu wenzetu”.

 

Hoja ya Mwalimu hapa ni kwamba, binadamu anapotawaliwa na tamaa mbaya ya madaraka, utukufu na utajiri (Peter Merkle), hujitengenezea hali ya maisha kwa kuwageuza wengine kuwa viumbe vyake, waonekane duni ili aweze kuwatawala vizuri; wamtukuze yeye na wawe tegemezi kwake kwa fikra na kimaisha. Kanisa linapoingia kati na kusimama upande wa wanaoonewa na kunyanyaswa na kwa kulaani dhuluma na uonevu huo, hapo suala la kuchanganya siasa na dini linatoka wapi?

jmihangwa@yahoo.com/0713-526972