SHARE

ERICK SHIGONGO NA MITANDAO

Wimbi la wanasiasa kuhama vyama vya upinzani na kuelekea vyama tawala limezidi kushika kasi Barani Afrika na kuleta tafsiri hasi kwamba sasa ukuaji wa siasa katika bara hili umeanza kudumaa.

Ukuaji wa kisiasa huchanua pindi jamii inaposhuhudia uwapo wa demokrasia ndani ya Taifa husika hivyo kuleta amani na ushirikiano ndani ya jamii.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, hali imekuwa tofauti ndani ya baadhi ya nchi za Tanzania na Tunisia ambazo kwa kipindi kifupi cha miaka miwili kumeshuhudiwa wimbi la wabunge kuhama kutoka upande mmoja kuelekea upande mwingine.

Ndani ya Tanzania pekee hadi sasa kumeshuhudiwa zaidi ya madiwani 146 wakihama vyama vya upinzani na kuhamia chama tawala cha CCM, pia wabunge sita wamehama upinzani na kuelekea CCM huku mbunge mmoja wa CCM akihamia upinzani.

Wimbi hilo pia limepiga hodi nchini Tunisia, Taifa ambalo lipo Kaskazini mwa Bara la Afrika ambapo tangu Agosti mwaka huu wabunge 20 wamekihama chama tawala nchini humo na kuhamia mrengo wa upinzani.

Hali hii imeanza kutafsirika kuwa ni sawa na siasa za mataifa haya kunasa ndani ya tope zito kutokana na sababu  zisizo na mashiko wanazozitoa wahamaji hao.

Kubwa linaloonekana kushika kasi ni wahamaji kushindwa kumudu hoja za chama alichopo na kuamua kuhamia katika mrengo mwingine kwa sababu tu ameshindwa kushindana kwa hoja.

Tanzania

Tangu kuingia kwa utawala mpya wa Rais John Magufuli mwaka 2015 hadi sasa umeshuhudia wabunge wanne wa Chadema, Dk. Godwin Mollel (Siha), Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), James Ole Milya (Simanjiro)  ambao wamehamia CCM na kuteuliwa tena kugombea majimbo hayo katika uchaguzi mdogo.

Wabunge wengine ni Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Mohamed (Liwale) wote kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao wamehamia CCM.

Vilevile CCM kilimpoteza Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye alihamia Chadema.

Licha ya hamahama hiyo kuruhusiwa kikatiba, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa wamegawanyika kuhusu wimbi hilo kwa upande wa Tanzania.

Kundi la kwanza ni lile linaloamini kuwa wanasiasa hao wamenunuliwa. Kwamba wanasiasa hao wamekubali kununuliwa kama bidhaa sokoni kutokana na kuwa wepesi kupokeafedha, jambo ambalo halijathibitishwa hadi leo kwa nyaraka zozote rasmi au kauli.

Kundi la pili linaamini kuwa wimbi hilo linasukumwa na hotuba ya Rais Magufuli Julai 28 mwaka huu wakati akitangaza uteuzi wa Makatibu tawala,wizara na wakuu wa wilaya, kuwa haiwezekani awateua yeye halafu kwenye matokeo ya uchaguzi wawatangaze washinde kutoka upande wa upinzani.

Hatua hiyo inatafsiriwa kwakuwa yeye ni Mwenyekiti wa CCM, maana yake anataka kuona washindi wanaotangazwa ni wale wanaotokana na chama chake sio kinyume.

Kundi la tatu nalo linaamini ni vuguvugu la kisiasa linalotokea ndani ya vyama tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi. Kundi hili linatolea mfano uamuzi wa aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu wa zamani, Augustine Mrema aliyeihama CCM na kujiunga chama cha NCCR-Mageuzi mwaka 1995, kisha kutikisa katika uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na madiwani mwaka huo.

Pia mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye ambao walihama CCM na kwenda Chadema miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani mwaka 2015 pamoja na wimbi la wanasiasa waliohamia upinzani mwaka huo.

Wakati kundi la nne linatazama hama hama hizo kuwa ndani ya vyama vya upinzani kuna migogoro ambayo huchochea baadhi ya wanasiasa kuhama.

Hoja kubwa wanayoitoa wanasiasa hao ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika utendaji wake, lakini pia wanadai uwapo wa migogoro ya kimadarakani ndani ya vyama vyao ni moja ya sababu ya wao kuhamia upande wa pili.

Tunisia

Wabunge 20 wa Chama tawala cha Nidaa Tounes ambacho ndicho kilichomweka madaraka Rais wa sasa wa nchi hiyo, Beji Caid Essebsi wamejiuzulua na kujiunga na mrengo mwingine katika Bunge la nchi hiyo kwa jina la Muungano wa Kitaifa (al Watani) unaomuunga mkono Waziri Mkuu wa Tunisia Youssef Chahed.

Chama cha Nidaa Tounes kilikuwa chama cha upinzani hadi kiliposhinda uchaguzi wa wabunge nchini humo Oktoba mwaka 2014 kwa kupata viti 85 kati ya viti vyote 217 vya bunge jipya.

Hata hivyo, kutokana na chama hicho kutopata viti zaidi ya nusu, kilishirikiana na vyama vingine kuunda baraza la mawaziri ambaye Waziri Mkuu wake ni Youssef Chahed.

Wabunge hao kutoka chama cha Nidaa Tounes  wamekuwa wakijiuzulu kwa kasi tangu Agosti mwaka huu kwa madai kuwa misimamo ya chama hicho ni ya upande mmoja.

Wabunge hao waliojiuzulu wanatarajiwa kujiunga na mrengo wa Muungano wa Kitaifa unamuunga mkono Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Youssef Chahed ambaye alikuwa anasakamwa na makada wa chama cha Nidaa Tounes kwa kumtaka ajiuzulu nafasi yake ya uwaziri mkuu.

Hitilafu za kisiasa hizo zimeshika kasi nchini Tunisia katika miezi ya karibuni kutokana na kuongezeka matatizo ya kiuchumi na maandamano ya mara kwa mara ya wananchi.

Wakosoaji wa Chahed wanasema kuwa serikali yake imeshindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi unaoisumbua Tunisia na kwa sababu hiyo wamemtaka Waziri Mkuu na baraza lake la mawaziri wajiuzulu.

Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo anaandamwa kwa madai kuwa ndiye aliyewashawishi wabunge hao kujiuzulu katika chama hicho tawala na kujiunga na mrengo wa muungano wa al Watani. Mrengo wa al Watani uliasisiwa Agosti mwaka huu na wabunge 33 wa kujitegemea na wale waliojizulu kutoka vyama vingine.