Home Makala Siasa za sukari zimeangusha mawaziri

Siasa za sukari zimeangusha mawaziri

903
0
SHARE

Idd SimbaNa Gabriel Mwang’onda

SUKARI imekuwa janga nchini Tanzania. Sukari imekuwa siasa hapa kwetu lakini si Tanzania pekee ambapo sukari imekuwa kete ya kisiasa. Na siasa ya sukari ni kali kiasi cha Mwenyekiti wa Wazalishaji wa Sukari, Balozi Ami Mpungwe, anadiriki kuifananisha sukari na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Kwa kuwa Balozi Ami Mpungwe yupo nadhani atakuwa anajua vita iliyopo ndani ya siasa ya sukari. Hapa kwetu kuna mawaziri wengi tu wamewahi kujiuzulu kwa sababu ya sukari, akiwemo Idd Simba.

Hata serikali zingine nyingi za Afrika zimewahi kutikiswa kisa sukari. Mara ya mwisho ilikuwa kwa watani wetu wa jadi hapo Kenya ilikuwa almanusura mawaziri waende na maji kwa sakata la sukari na shinikizo lilienda hadi kwa rais.

Mtu anaweza kujiuliza  kuna nini kwenye hii biashara. Jibu la haraka ni kwamba kuna fedha nyingi mno inayopatikana kutokana na biashara ya sukari.

Kuna urahisi mno wa kupata fedha kwenye baishara ya nzima ya sukari, yaani mfanyabiashara akifanikiwa kupata kibali basi yeye hujiona amepata faida, na kwa  vijana basi wangesema ‘ametusua’.

Mfano zile tani 4,500 zinazosemekana zimeonekana kwa mfanyabiashara mmoja zina thamani ya takribani shilingi bilioni 9 na huo mzigo unaisha ndani ya muda mfupi sana au tunaweza kukadiria unakwisha ndani ya siku 7 tu.

Ripoti ya Kamati ya Kdumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (POAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa zamani wa Kigoma Kaskazini na sasa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ya Januari mwaka 2015, iliwanukuu wataalamu wakidai kuwa kati ya mwaka 2009 hadi 2012 serikali ilipoteza mapato zaidi ya Sh. bilioni 460 kwa waagizaji kuwa na ubavu wa kukwepa kodi. Bila shaka msomaji hapa utakuwa umeona ni kwanini basi sukari inakuwa biashara ya wakubwa.

Biashara ya sukari si kama nguo, viatu ama bidhaa nyingine za kawaida kwamba mtu anaweza akaichezea upatu kwa kuweza kuficha ili ikiadimika aweze kuuza kwa faida si hivyo.

Serikali inavyowapatia vibali watu wachache ni kama mtu katumwa na kijiji chenye njaa kwenda kutafuta chakula halafu akikipata anaanza kula mwenyewe ama anawanyima waliomruhusu ili wapate shida sana aje kuwauzia bei ghali.

Hii biashara inahitaji watu wazalendo sana na si walafi kabisa. Kuna sababu ya kuwapa watu wachache vibali lakini hao waliaminiwa na kubahatika wakiwa wanataka faida maradufu bila kujali raia wenye nchi ambao kimsingi ndio wamewapa hiyo fursa si sawa kabisa mbele ya wanadamu wenzako hata Mungu.

Ndio maana katika kuingiza sukari si kila mtu anaweza kuleta kama atakavyo. Kwa kulitambua hilo serikali ikaamua kutumia vibali kutoa ruhusa kwa watu wachache tu ili wasije wakaua viwanda vya ndani kwa kuwa kwa sasa mahitaji ni takribani tani  600,000 na viwanda vya ndani havizalishi zaidi ya tani 320,00.

Kwa minajili hiyo basi hilo pengo lazima lizibwe kwa kuagiza hicho kiasi cha nakisi suluhu ambayo iwe ni suluhu ya haraka na ya muda mfupi lakini la pili na suluhu ya kudumu ni kujenga kiwanda kitakachoziba hii nakisi.

Kulikuwa na mradi mkubwa sana wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari ni matumaini yangu kuwa serikali hii itaufufua ule mradi. Ule mradi ulishindikana kwa sababu ambazo ni aibu hata kuelezea. Kukosa fedha kidogo ya kuwalipa fidia watu ni fedheha kubwa ukilinganisha na faida za mradi wenyewe.

Lakini kwa kuwa miwa haioti kama uyoga kwa siku mbili ama tatu, basi hatuna budi kuagiza sukari nje ya nchi. Sasa kuweka udhibiti kwenye suala hili ni jambo muhimu kupita maelezo. Rai yangu kwa serikali kama ifuatavyo kama njia rahisi ya haraka ya kuondokana na siasa ya sukari.

Kwa kuwa hii bidhaa ina umuhimu kwa raia na inagusa takribani asilimia 95 ya raia wote basi ni vyema serikali ikatumia mfumo wa ‘bulk procurement’ kama inavyofanya sasa kwenye mafuta. Sote tunakumbuka jinsi wachuuzi wa mafuta hapo nyuma kabla ya mfumo huu walivyokuwa wakitusumbua hadi nchi inasimama.

Faida ya bulk procurement kwenye ni kama ifuatavyo;-

  1. Ubora wa mlaji uzingatiwe, iwe tofauti na ilivyo sasa wachuuzi wanatulisha sukari iliyokwisha muda wake wa matumizi. Uwezo wa kudhibiti ni mdogo sana kwenye hii biashara.
  2. Bei ya kudhibitiwa vizuri kabisa na kuna uwezekano ikapungua sana. Kwa kuwa kutakuwa na ushindanishaji na taarifa ya bei ya duniani ziko wazi na zinajulikana. Bei elekezi zitatolewa kama ifanyikavyo kwenye mafuta. Hili litafanyika kwa umakini kuepusha viwanda vya ndani kushindwa ushindani.
  3. Wingi au kiasi kitachoruhusiwa kuingizwa kitakuwa ni rahisi sana kukimudu kama ifanyikavyo kwenye mafuta. Hii itaondoa kabisa uhaba bandia wa sukari unaosababisha bei zipande na matokeo yake badala ya kuwa soko huru linakuwa soko holela.
  4. Itarahisisha sana utozaji kodi kwasababu kiwango na kiasi kinachoingizwa kilichokubalika kinajulikana na mwingizaji anajulikana vilevile.
  5. Itaondoa kabisa ubabaishaji wa watu kupata vibali holela kisha wanauza vibali kwa watu wengine , yaani hiyo ‘chain’ inaweza kufika watu wanne, matokeo yake bei inakwenda juu kijinga kabisa.

Ikumbukwe kuwa kuagiza sukari iwe ni suluhu ya muda mfupi lakini njia ya kudumu ya kumaliza tatizo hili ni kujenga viwanda vitavyoziba pengo na zaidi ili tuweze kuuza hata nje ya nchi yetu.