Home Michezo SIASA ZINAVYOLITAFUNA SOKA TANZANIA

SIASA ZINAVYOLITAFUNA SOKA TANZANIA

1532
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU,

KWA sasa kila kitu kinachofanyika na kuendelea hapa nchini kinahusika na siasa. Hakuna anayebisha kama sote tunaiishi siasa lakini kwa upande wa michezo kuna athari nyingi ikiwa itapewa nafasi kubwa zaidi.

Wakati Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ikiweka sheria za kutaka masuala ya soka kutohusishwa na siasa kupigwa marufu bila shaka iliangalia mbali.

Soka ndiyo mchezo unaopendwa zaidi Duniani achilia mbali hata hapa nchini. Kwa sasa mchezo huo umehama kutoka kwua sehemu ya burudani na kuwa ni biashara kubwa pale tu utakapotumika vizuri.

Kipato kikubwa kimekuwa kikipatikana kupitia mchezo huo ndani ya muda mfupi sana. Nani asiyejua ndani ya wiki moja tu Christiano Ronaldo analipwa pauni 375,000 (zaidi ya bilioni 1 za kitanzania), Carlos Tevez pauni 615,000 ( sawa na bilioni 1.7), Messi pauni 336,000 sawa na bilioni 1 na ushee za kitanzania wakati hapa nchini wapo wachezaji wanaolipwa kati ya shilingi milioni 14 hadi milioni mbili kwa mwezi.

Leo hii soka imekuwa sehemu ya kuibeba siasa lakini ajabu kubwa kuona siasa hiyo hiyo ikishindwa kuukomboa mchezo huo. Nani asiyejua mchezo huu unavyotumika kuwaingiza madarakani baadhi ya wanasiasa? Lakini je baada ya kupata madaraka wanausaidiaje mchezo huo?.

Timu kubwa zikiwemo za Simba na Yanga mara kadhaa zimekuwa ngazi ya wanasiasa kuingia madarakan. Kuna kundi kubwa sana la wanasiasa limekuwa likijibanza nyuma ya pazia kupitia soka, wengi wameutumia kupatia udiwani au ubunge na hatimaye uwaziri.

Ukweli ulio wazi ni kwamba kuna wanasiasa wengi wamejibanza kupitia mchezo huu kimsingi wanautumia sawa na ule msemo wa ‘kutumia toileti paper pale unapoihitaji kisha kuitupa’.

Kama hiyo haitoshi bado taasisi inayosimamia mchezo wa soka nchini inashindwa kabisa kujinasua katika mtego huo na badala yake sasa nayo inajikita humo humo aidha kwa kujua au kutokujua.

Kwa Tanzania haishangazi kuona maamuzi yenye mlengo wa kisiasa yakishika nafasi kubwa. Hata maamuzi ya hivi karibuni ya kuwapelekea wabunge na viongozi wa Serikali fainali ya Kombe la FA ‘Azam Federation Cup’ yana mlengo huo huo.

Dalili za kutaka kuihamisha fainali hiyo ilianza kuonekana mapema hata kabla ya sababu za msingi kujulikana.

Awali fununu zilidai ingefanyika jijini Mwanza kabla ya kubadilisha kauli na kudai ingefanyika ‘droo’ ya kuchagua uwanja kabla ya kuja na taarifa rasmi kuwa sasa itafanyika mkoani Dodoma. Kwa TFF imejiingiza katika mtego ambao kung’atuka itakuwa ngumu sana kwao.

Akikaririwa wakati wa kutoa maamuzi hayo, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema uamuzi wa kuipeleka mkoani humo umetokana na kutaka kuwapa burudani wakazi wa mkoa huo ambao kwa sasa uko katika pilika pilika za vikao vya Bunge la Bajeti hivyo ni wazi sehemu ya waliokusudiwa ni wabunge, mawaziri na watendaji wengine wa serikali.

Ipo sababu nyingine kuwa TFF inaunga mkono mpango wa serikali wa kuhamia Dodoma hivyo kuipeleka fainali hiyo mkoani humo. Inaweza kuwa sababu nzuri lakini ilitegemewa kabla ya kutangaza uamuzi huo vema shirikisho hilo lingeanza kutangaza ni lini wao kama taasisi ya kusimamia soka watahamishia ofisi zao mkoani humo. Pengine hilo lingeanza ingekuwa nia jambo jema zaidi.

Licha ya sababu kubwa ya mchezo huo kuhamishwa kutoka Dar es Salaam ambapo ndipo mara zote fainali hiyo hufanyika kutokana na Uwanja wa taifa kufungwa kwa matengenezo bado TFF walipaswa kuwa na vigezo vingine muhimu kabla ya kufikia tamati ya wapi ikafanyike.

Lakini je ni kweli Uwanja wa Dodoma ni bora kuliko viwanja vingine kama vile Sokoine Mbeya, Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha au CCM Kirumba huko Mwanza?

Hapa nafasi kubwa ya kiushauri alipaswa kupewa mdhamini wa michuano ambaye siyo siri amekuwa akitumia fedha nyingi kuhakikisha inafanyika, swali ni je alishirikishwa katika kuamua uwanja wa mechi ya fainali? Je kulingana na mahitaji yake atafanikiwa kama mdhamini?

Binafsi sintoshangaa kusikia mdhamini hajashirikishwa katika suala hilo na badala yake wakashirikishwa zaidi viongozi wengine wa kisiasa.

Lakini vipi mahitaji ya pambano hilo kuhusu usalama wa mashabiki ndani na nje ya uwanja kwa muda wote wa pambano? Vipi kuhusu mahitaji halisi ya uwanja kwa maana ya idadi ya mashabiki je utakidhi kiu ya mashabiki? Vilevile viingilio vitalenga kipato cha wakati wa mji husika?

Kulingana na ugumu wa mchezo huo sio tu bingwa apatikane lakini mazingira ya timu zinazokutana inaonesha mechi hiyo itakuwa na pilikapilika nyingi ambazo kama TFF haitakuwa makini ni wazi wanaweza kuitia doa michuano husika.

Pengine suala hilo linaweza kuamsha kamjadala kidogo kuhusiana na jinsi soka la Tanzania linavyoendeshwa kwa maamuzi ya kukurupuka na kusahau kanuni zake.

Klabu kongwe za Simba na Yanga zimekuwa zikikingiwa kifua sana na hoja ya kisiasa. Maamuzi mengi yanayozihusu timu hizo yamekwua ya kisiasa zaidi.

Ukichunguza kwa makini utabaini kuwa hali hii si mara ya kwanza kutokea kwani viongozi wengine wa kisiasa wakiwemo mawaziri waliwahi kuingilia kati maamuzi ya kisoka na hata kusababisha matatizo kadhaa.

Profesa Juma Kapuya akiwa Waziri mwenye dhamana ya michezo mwanzoni mwa mwaka 1999 alisababisha Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kusitisha mkataba wake wa udhamini wa Ligi Kuu wakati huo ikijulikana Ligi daraja la kwanza ‘Ligi ya Safari Lager’ baada ya wadhamini hao kutofurahishwa na kitendo cha kiongozi huyo kupandisha idadi ya timu bila ya kushauriana nao kama mdhamini mkuu.

Katika sakata hilo lililofanyika mwishoni wma mwaka 1998, Profesa Kapuya alidaiwa kuingilia kati madaraka hayo kwa kupandisha daraja timu nne badala ya tatu kucheza Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) ili tu ‘aibebe’ timu ya Milambo ya Tabora ya mkoani kwake. Msimu huu zilipadishwa timu za Reli Morogoro, Kariakoo Lindi, AFC ya Arusha pamoja na Milambo.

Lakini pia mara kadhaa FIFA imetishia kuifungia Tanzania kujihusisha na mchezo huo baada ya Serikali kuingilia masuala ya ndani ya utendaji wa mchezo huo.

Mwaka 2000 kupitia Waziri huyo huyo mwenye dhamana ya Michezo alisimamia kuondolewa madarakani kwa waliokuwa viongozi wa TFF wakati huo ikijulikana kama FAT, Muhidin Ndolanga na katibu wake Ismail Rage na kuundwa kwa kamati ya muda ambapo viongozi hao walilalamika FIFA na kutishia shirikisho hilo kutishia kutua rungu lake Tanzania.

Kama hiyo haitoshi mwaka 2013 FIFA hiyo hiyo ilitishia tena kuifungia Tanzania kufuatia Serikali kuingilia kati maamuzi ya TFF kwa kuishinikiza kurejesha jina la Jamal Malinzi kugombea baada ya kuenguliwa kwa madai ya kutokuwa na sifa. Katika sakata hilo uongozi uliokuwa madarakani ulikubali kutii amri ya serikali na kunusuru nchi kufungiwa na shirikisho hilo la kimataifa.

Hivi karibuni imeshuhudiwa Waziri wa Michezo Dr Harison Mwakiyembe akitoa kauli nzito kuhusiana na klabu ya Yanga baada ya kushindwa kupeleka kikosi cha kwanza mkoani Dodoma kucheza mechi ya kirafiki na badala yake kupeleka kikosi B. Mechi ya kirafiki iliyoandaliwa na Chama cha Soka cha Mkoa Waziri anahusikaje kutaka kuchukua hatua?

Hali hiyo imekuwa ikidumaza harakati za kukuza mchezo huo hasa ikizingatiwa kuwa mara zote maamuzi huwa kuwanufaisha wasiohusika na mchezo wa soka.