Home Latest News Siku ya Afrika isaidie kuzidisha kujenga umoja

Siku ya Afrika isaidie kuzidisha kujenga umoja

115
0
SHARE
Mwalimu Nyerere akiwa na Rais wa kwanza wa Ghana Hayati Kwame Nkuruma

NA DK. HELEN KIJO-BISIMBA

MEI 25 mwaka huu ni siku ya Afrika. Siku hiyo inatambuliwa katika nchi za Afrika na hata za nje ya Afrika. 

Umuhimu wa siku ya Afrika unatokana na kuundwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) siku kama hiyo yaani Mei 25 mwaka 1963 ambapo nchi za kiafrika zilizopata uhuru ziliamua kuwa na umoja kama mwendelezo wa nia ya nchi hizo kuungana ili kukuza uhuru wao kufikia uhuru wa kiuchumi katika jamii ya Kiafrika na kuondokana na kutawaliwa na mataifa ya kigeni kwa kuondokana na ukoloni na hata ukoloni mambo leo. 

Wazo la Rais wa kwanza wa Ghana, Hayati Kwame Nkuruma ambalo lilijitokeza wakati huo na kuungwa mkono na waasisi wenzake kama Mwalimu Julius Nyerere, ni kuwa na Afrika moja. 

Miaka 38 baadaye umoja huo ulibadilishwa kuwa Umoja wa Afrika (AU) kutoka kwenye jina la asili  la Umoja wa Nchi Huru za  Afrika kuwa Umoja wa Afrika.

Umoja huo pamoja na changamoto nyingi inazokumbana nazo  kiuchumi, kijamii na  vinginevyo bado ni umoja ambao unaweza kuleta majibu mengi mazuri kwa watu Waafrika hasa katika vipindi kama hiki kigumu cha ugonjwa huu wa Corona.  

Umoja wa Afrika una mikakati mizuri mingi ukiwepo ule wa Agenda ya Afrika 2063, ambayo inajiangaliza Afrika katika miaka 50 ijayo. Agenda namba moja katika mpango huo wa 2063 unahusu nia ya kubainisha juhudi za kuwa na umoja wa watu wa Afrika ili kujiepusha na kutawaliwa kiuchumi na kijamii.  

Kila mwaka nchi za Afrika huadhimisha siku hii ambapo zipo nchi ambazo siku hii huwa ni ya mapumziko kabisa ili kujipa muda wa kushereheka. Nchi hizo ni kama vile Ghana, Zimbabwe, Lesotho, Mali na Zambia. Siku hiyo husherehekewa kama njia ya kujikumbusha umbali wa tulikotoka kama nchi za Afrika, wakati tukijiangaliza umbali wa huko tuendako na umbali uliosalia kufikia umoja halisi wa nchi hizi za Afrika zilizojikomboa kutoka ukoloni.

Kila mwaka ipo kauli mbiu inayoongoza siku yenyewe. Mwaka jana 2019, kauli mbiu ilihusu’ mfumo wa maisha kiafya, huongeza uhai’. Msisitizo ulihusu kuishi kwa kuzingatia kanuni za kiafya ni muhimu katika kuendeleza uhai. 

Kauli mbiu hii ni muhimu hata sasa hasa kwa kuzingatia hali iliyopo ya ugonjwa huu wa Corona na magonjwa mengine mengi nyemelezi mengi yakichangiwa na jinsi watu wanavyoishi kiasi cha kuruhusu afya kutetereka.

Umoja wa Afrika hakika ulitakiwa uwe umeshatengemaa na Afrika kama bara kuwa nchi moja ambayo inajiongoza kimaamuzi, kiuchumi na vinginevyo. Yapo mambo yanayofanyika katika umoja kwa jinsi ulivyo sasa, lakini utekelezaji wake unategemea kila nchi na utashi wake kwani kila nchi ni huru na inaweza kuamua lolote bila kuingiliwa na nchi nyingine.  

Mfano mzuri ni jinsi umoja huo ulivyoamua kujiangaliza au kufuatiliana ili kusaidiana kujenga utawala bora barani kwa mkakati ujulikanao kama NEPAD. Huu mpango nchi inaamua kukaribisha wafuatiliaji na wao wakifika watakutana na makundi mbalimbali wakifuata vigezo walivyoviweka kisha kutoa taarifa kwa nchi husika ya hali waliyoibaini ya utawala katika nchi ile. 

Nchi husika itapokea na itaweza kufanyia kazi mapendekezo  yatakayotolewa, ila isipofanyia kazi hakuna kinachofanyika na hata isipotaka kuwaalika wafuatiliaji hao hali haibadiliki zaidi ya kutazamana tu.

Mwaka 2013 wakuu wa nchi za Afrika katika mkutano wao wa Abuja uliokuwa maalumu kuzungumzia suala la Ukimwi, Kifua Kikuu na malaria waliona umuhimu wa kuwa na taasisi  maalumu ya kuzisaidia nchi za Afrika  kupambana na kuzuia maradhi. 

Ilipofika mwaka Januari mwaka 2006, taasisi hiyo iliundwa na mwaka 2017 ilizinduliwa rasmi ikijulikana kama Africa CDC yaani vituo vya Afrika vya kudhibiti na kuzuia magonjwa. Nia yake ni kuweka njia za kufuatilia na  kushughulikia athari katika eneo la  Afya ya  umma barani Afrika. Kwa kutambua kuwa  Afya ni suala la kimaendeleo linalogusa uchumi, jamii na usalama wa nchi, chombo hicho kilianzishwa.

Katika kushughulikia magonjwa ya milipuko kama Ebola na Ukimwi chombo hiki na vituo vyake vimejibidiisha kutambua na kutafuta suluhisho. Kwa Covid-19, pia kimeweza kuwa mstari wa mbele kutoa elimu na mwelekeo wa ugonjwa. Changamoto ambayo ipo ni pamoja na kuwa ni chombo cha Umoja wa Afrika, bado  nchi moja moja za barani Afrika zinafanya mambo yake kivyake vyake. Utaona Madagascar imesema imepata dawa dhidi ya Corona, Tanzania imeifuata dawa na inasema inaichunguza. 

Nimejaribu kuona jinsi Afrika CDC inavyohusiana na ugunduzi huo wa Madagascar. Nimemsikia msemaji wa CDC akionekana kuwa nao wameisikia dawa hiyo ikitangazwa na serikali ya Madagascar na kwa hivyo walikuwa nao wanataka wafuatilie ili wajue ilivyopatIkana na wajihakikishie kuwa imefuata taratibu zote za kiusalama na za viwango na manufaa ya kitabibu. 

Jambo ambalo ungetegemea ni kuwa kwa vile hiki ni chombo cha kiafrika na pia kimeunda kikosi kazi kuhusu Corona, nchi ilipofahamu ugunduzi huo ingekishirikisha kikosi kazi hicho na kisha chombo hicho kingeweza kuchukua jukumu la kuitangaza dawa hiyo iliyogundulika Madagascar baada ya wao kujiridhisha ili ikianza kugawiwa si tena kila nchi iende kwao kwenda kuifanyia majaribio. 

Hapa utaona hilo suala la Umoja wa Afrika na mkakati wake wa afya haujatumika ipasavyo.

Kwenye masuala ya kiuchumi matatizo ni dhahiri kwani hakuna njia moja tunayoitumia kama Afrika ili kukabiliana na athari za kiuchumi zitokanazo na Corona kama bara moja. Tumeanza kuona nchi jirani kuamua kujifungia kuepusha maambukizi wakati nchi nyingine kama ya kwetu haikuona hiyo kama njia ya kufuata. Baadaye tunaona nchi jirani zikifunga  mipaka ili Watanzania wasiingie huko. Tanzania  nayo inajipanga na yenyewe kurudisha au kujibu mapigo.  Hapa kuna athari kubwa za kiuchumi kwa nchi zote zinazohusika ambazo ni jamaa, ni nchi za Afrika, ni ndugu. 

Kama nchi hizi za kiafrika zingekuwa na huo umoja ambao ulikusudiwa tungekuwa bara moja hivyo utatuzi wa tatizo kama hili ungehusu wote walio barani humu na hivyo basi iwapo upande wa mashariki ndiko athari ilipo kubwa, ungewekwa mkakati wa kusaidia kupunguza athari na iwapo ni kaskazini au kusini hivyo hivyo. 

Kama ilivyo kwa nchi moja moja, kwa mfano hapa Tanzania, iwapo Dodoma ndiko shida ilipo kubwa nguvu zinaelekezwa huko na kuikinga mikoa mingine.  Kwa hali ilivyo sasa kila nchi inajiamulia itakavyo na mwisho wa siku athari zitawagusa karibu wote wakati tunajitanabahisha kuwa tu wamoja katika bara hili la Afrika.

Hii siku ya Afrika itukumbushe nia na lengo la waasisi wake kuiweka na ikiwezekana malengo hayo yawekewe mikakati ili kufikia pale ambapo palitegemewa na tuweze kukabili changamoto kwa pamoja. Mungu ibariki Afrika na watu wake. 

0713337240