Home Habari Siku ya sheria isaidie kutoa majibu kuliko kuacha maswali

Siku ya sheria isaidie kutoa majibu kuliko kuacha maswali

1107
0
SHARE

DK. HELLEN KIJO BISIMBA

KILA mwaka tumekuwa na maadhimisho ya siku ya sheria nchini. Siku hii kwa sasa imeongeza njia za kuadhimisha na inaelekea kuitwa wiki ya sheria ambapo shughuli za mahakama, husemekana ndio huanza rasmi katika mwaka husika.

Katika wiki ya sheria yapo mambo mengi yanayotendeka na wahusika wakuu wa maandalizi haya huwa ni mahakama ikiwa ni moja ya mihimili mitatu ya dola.

Mwaka huu katika wiki hii ya sheria pamekuwa na mambo mbalimbali yaliyoendelea katika mikoa mingi hapa nchini, ikiwemo maonyesho katika viwanja kama ilivyokuwa hapa Dar es Salaam katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Kwenye maonyesho hayo wapo waliokuwa wanatoa elimu ya mambo na uendeshwaji wa kesi mahakamani na vyombo vingine vya utoaji haki na wapo waliokuwa wanatoa msaada wa sheria na mengine mengi.

Siku ya sheria ina umuhimu sana kwani katika siku hii kama nilivyomsikia Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk. Rugemeleza Nshala akizungumza, akisema ni inayohusu kujikumbusha mambo mbalimbali ya kisheria.

Kwa upande wake aligusia suala la uhuru wa mahakama kuwa mahakama kikiwa ndicho chombo kilichowekwa na Katiba kuwa muamuzi wa mwisho wa masuala ya migogoro ya kisheria.

Kwa mujibu wa ibara 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mahakama ndicho chombo cha mwisho katika utoaji haki na hakuna chombo kingine chochote kinachoweza kukiingilia chombo hiki, si serikali ya Jamhuri wala Bunge na kwa Zanzibar hata serikali ya mapinduzi haipaswi kukiingilia chombo hiki.

Katiba na hata sheria ziko wazi kabisa kuhusu uhuru huo wa mahakama na siku ya sheria ni mahali pake kujikumbusha na kuangalia iwapo ipo hali ya uhuru huo kuingiliwa au kutokuwepo na hivyo kutafuta njia za kurekebisha.

Katika kipindi kuelekea siku ya sheria sijui ni bahati mbaya au ilikusudiwa tuliona kwenye mitandao kauli iliyotolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, akiwa anahojiwa na moja ya vyombo vya habari na alionekana akiangaliza suala la ucheleweshwaji wa kesi za jinai kwa sababu ya upelelezi kutokamilika kwa muda unaotakiwa. 

Siku hiyo ya sheria pia suala hilo liliibuka kwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, naye kulizungumzia na aliyekuwa mgeni rasmi wa siku hiyo kitaifa, Rais Dk. John Magufuli naye alilizungumzia na hata kuonyesha kuwa ni jambo lisilokubalika na linaumiza watu.

Hapo utaona kuwa wote waliozungumza walionekana wanazungumzia tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi. Ni kweli na wengi ni mashahidi wapo watu wengi walioko magerezani kwa muda mrefu wengine hata miaka nane au zaidi wakisubiri upelelezi ukamilike na wengi wao kesi zao hazina dhamana hivyo hukaa tu kesi ikitajwa na kurudishwa rumande.