Home Latest News SIMULIZI YA KAROLINE NA TAMADUNI ZA UKEKETAJI

SIMULIZI YA KAROLINE NA TAMADUNI ZA UKEKETAJI

799
0
SHARE

Na PETER KASERA, Mara

Tamaduni zinazotaka watoto wa kike kufanya tohara ni maarufu sana mkoa wa Mara hasa wilaya ya Tarime. Wilayani hapa, ukeketaji licha ya kwamba umepungua lakini bado unafanyika. Athari zake zipo katika maeneo mengi na kubwa ni saikolojia ya Yule anayekeketwa bila ridhaa yake. Tena hata Yule aliyefanya kwa kuridhia, hukutwa na athari hizo hizo pale anapotakiwa kuwa na wajibu kwa mumewe.

Tohara kwa watoto wa kike ina historia katika makabila haya. Historia hii mara nyingi haifafanui nini hasa ilikuwa maana ya tohara hii. Wapo wazee wanaosimulia kuwa, ilifanyika kwa lengo la kutoa ulinzi kwa watoto hao ili wasijihusishe na tendo la ndoa kabla ya kuolewa. Dai hili halijawahi kuwa na uthibitisho na hivyo halina mantiki kabisa.

Katika safari yangu wilayani Tarime, nafanikiwa kukutana na uongozi wa Asasi isiyo ya Kiserikali ijulikanayo kwa jina la Association for Termination of Female Genital Multilation (ATFGM). Asasi hii inajihusisha na kuelimisha jamii kuhusu unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kukabiliana na vitendo vinavyoashiria unyanyasaji huo hasa utamaduni wa kukeketa watioto wa kike.

Meneja Miradi wa ATFGM Valerian Magani anaeleza kuwa wanaendesha mafunzo yao katika kata za Nyanungu, Goronga, Nyansicha na Mariba. Kinachonipa simanzi katika safari hii ni simulizi kutoka kwa Karoline Kizito (15).

Binti huyu amenufaika na asasi ya ATFGM katika utekelezaji wake wa mradi huu uliopata ruzuku kutoka kwa The Foundation for Civil Society. Binti huyu mzaliwa wa kijiji cha Masanga Kata ya Gorong`a wilaya ya Tarime, anasimulia kwamba katika vipindi tofauti vya miaka ya 2013, 2014, 2015 na 2016 alifanikiwa kukimbia baada ya kuambiwa na wazazi wake kuwa muda wake umefika, hivyo ni lazima akeketwe.

Alikimbilia katika kambi ya ATFGM ambapo alikaa kwa kipindi chote hadi ukeketaji ulipoisha. Katika kipindi chote ambapo alikuwa anakimbia ATFGM, shirika hilo lilikuwa linaendelea elimu na ushauri kwa wazazi juu ya madhara ya ukeketaji kwa watoto. Awali zoezi hilo lilikuwa gumu lakini kadri siku zilivyoendelea hali ya uelewa iliongezeka.

Karoline anaelezea kuwa mwaka 2016, Mama yake alifika na kuingia ndani ya kambi aliyotorokea na akafanya vurugu kubwa akitaka kumchukua kwa nguvu ili aende kukeketwe. ATFGM walifanya kazi ya kumkamata kwa kushirikiana na polisi na kisha akapelekwa kituo cha polisi.

Baada ya kutoka polisi, mama wa Karoline aligoma kabisa kuendelea kumsomesha mtoto wake ambaye wakati huo alikuwa anasoma kidato cha pili. Kwa kuwa dhumuni kubwa la ATFGM ni kusimamia haki za watoto, shirika hilo lilitafuta fedha na kumsaidia mtoto huyu aendelee na masomo yake.

Shirika bado linaendelea kutoa ushauri kwa wazazi lakini pia kuendelea kumpatia ushauri wa kisaikolojia mtoto huyu, kwani ameathirika baada ya mzazi wake kukataa kumsomesha. Koroline kwa sasa ametengwa na wazazi wake pamoja na ukoo wake.

Kamanda wa polisi kanda maalum Tarime Rorya ACP Benedick anatoa wito kwa jamii kuacha mara moja kukandamiza watoto na anaitaka jamii ielewe kwamba haki mojawapo kubwa ya mtoto ni kupata elimu.

Kamanda huyo amepongeza kazi kubwa inayofanywa na ATFGM na kuiomba asasi hiyo kutoishia kufanya kazi katika wilaya hiyo tu, bali wasaidie mkoa mzima wa Mara. Ukiwa kama mkoa wenye tatizo hilo kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wa vijana waliokuwa wakitoa elimu katika vijiji, wameeleza kufurahishwa na mradi huo kwa sababu umewapa upana na masuala ya jinsia ambayo kwa vijijini  ni vigumu kuonekana na kutekelezeka. Pia wanaeleza kuwa, mradi huu umewaandaa kujijengea familia bora zenye mwendelezo wa kizazi chenye elimu ya kutosha.

Uchunguzi wetu katika kaya mbalimbali wilayani humo umebaini mabadiliko makubwa hasa kwenye kata ya Nyanungu. Katika kata hiyo kulikuwa na tabia ya kulazimisha watoto wa kike hata walio chini ya miaka 10 kukeketwa kwa nguvu. Kupitia elimu inayotolewa na ATFGM jambo hili limeonekana kueleweka na jamii kukubali kubadilika,” anasema Sunday Mwabe kutoka katika kata ya Nyanungu.

Chacha Barnaba ni Mkufunzi kutoka kata ya Nyasincha, yeye anaeleza kuwa suala la ukeketaji kwa wanawake kwenye kata yake sasa hivi halipo. “Hakuna anayetaka kusikia suala hilo kwa sasa hapa kwenye kata yangu. Lakini huko nyuma jambo hili lilikuwa ni nyeti sana. Ilikuwa ni mila iliyoheshimiwa na wengi,” anasema na kuongeza:

“Tulianza na wazee wanaoheshimika katika jamii yetu ambao kwao ni rahisi kuwakataza kutekeleza mila hii. Lakini pia tulitumia viongozi wa dini ambao wanaheshimika sana katika jamii.”

Kutokana na kuwepo kwa vitendo vya ukeketaji, wasichana wengi walijikuta wakikimbia makazi yao kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine. “Tuna imani kwa elimu tunayoendelea kuitoa itafanya jamii ya Tarime kuwa salama zaidi kwa kila mtu na vijana watabaki vijijini na kuleta maendeleo,” anasema Chacha

Kutokana na asasi ya ATFGM kuanzishwa na hatimaye asasi hiyo kuanzisha kituo cha kutoa malezi kwa watoto wanaonyanyaswa, asasi hiyo imekuwa ni kimbilio kwa watoto wengi wanaopita katika unyanyasaji wa aina mbalimbali.