Home Makala Sintofahamu ya trafiki, madereva inachangia ajali barabarani

Sintofahamu ya trafiki, madereva inachangia ajali barabarani

1327
0
SHARE

NA FRANKLIN VICTOR

BARABARANI unahisi furaha katika mwendo wa magari huku yakichekeana kupitia taa za mbele. Madereva walio nyuma ya sukani hawakaukiwi tabasamu, bashasha inang’arisha nyuso zao wakijihisi huru na wakizifuata sheria za usalama barabarani pasi shurti.

Abiria wanaziona raha zilizowasheheni madereva. Naam, ukiona hivi jua hakuna askari wa usalama barabarani maarufu kama trafiki katika barabara mbalimbali zinazotumiwa na madereva hawa. Ile hofu waliyoizoea ya kukutwa na makosa haipo kwa muda husika.

Ukizitazama takwimu za ajali za barabarani na wingi wa fedha zinazokusanywa kupitia faini na tozo mbalimbali wanazolipa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto unagundua uwepo wa tatizo linalohitaji mabadiliko ya lazima ya mbinu katika kukabiliana nalo, kukabiliana na ajali za barabarani ili kunusuru maisha ya viumbe, mali na rasilimali.

Tangu mwaka huu uanze imeshuhudiwa migomo kadhaa ya madereva wakilalamikia vitendo wanavyoviita uonevu wanavyofanyiwa na mamlaka zinazosimamia usafiri na usafirishaji, miongoni wakitajwa askari wa usalama barabarani. Migomo hii si ya kuidharau na kuisahau bila kuitafutia dawa itakayotumika kama kinga dhidi ya utitiri wa ajali.

Ukiona watu kama dereva wa daladala na konda wake wanakataa fedha za nauli na kuamua kuegesha gari kimgomo ujue iko namna inayohitaji utatuzi wa kudumu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini, yenye Watanzania maskini, hohehahe wa kipato. Serikali ya awamu ya tano inaendeleza jitihada za kuhakikisha nchi inauingia uchumi wa viwanda ili iwe katika kundi la nchi za uchumi wa kati, na Watanzania wawe watu wa kipato cha kati.

Mchango wa kila mtu ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Tanzania kufikia uchumi wa kati hivyo watendaji wa umma, wakubwa kwa wadogo, hawatarajiwi kukwamisha jitihada zinazofanyika kwa aidha kufanya kazi kimazoea, kutumia nafasi za kimamlaka ndivyo sivyo na kukatisha tamaa wananchi.

Kama tunajua nchi bado ni maskini na Watanzania ni maskini, inakuwaje dereva anaandikiwa kirahisi tu faini ya sh 30,000/= kwa kuwa taa ya upande wa kushoto katikati ya gari la mkopo analoliendesha haiwaki, ina ufa kidogo kwa pembeni na muda wa tukio ni saa saba na nusu mchana katikati ya jiji au mji. Jambo kama hili ndilo hufanya madereva kuwa na hofu isiyoisha wakijua wakati wowote watapatwa na kosa hata kama si kosa.

Mbwembwe na kujiamini kunakoonwa pale trafiki wanapokosekana barabarani kunadhihirisha madereva wengi wa Kitanzania wanaogopa sana askari wa usalama barabarani pengine kuliko wanavyoogopa ajali.

Pengine madereva wangeambiwa wachague wanachotaka kitokee barabarani wangechagua kusiwe na trafiki. Yaani dereva anatetemeka anapomuona trafiki utadhani kuna uhasama badala ya usalama barabarani! Hii si sawa kama isivyo sawa kwa raia kuogopa kituo cha polisi.

Madereva kujihisi wako hatarini kupatwa na makosa au kupatwa kimakosa barabarani kunafanya wakose umakini, wasitulie ipasavyo hivyo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata au kupatwa na ajali.

Ningekuwa mimi ndiye mwenye mamlaka ya juu ya ukuu wa kitengo cha usalama barabarani ningefanya nini cha tofauti kuleta utofauti? Swali zuri, majibu mengi. Ningekuwa ndiye ningeanza kwa kuhakikisha watendaji wote chini yangu wanawajali wateja, yaani watumiaji wakuu wa barabara hasa wale wanaoendesha vyombo vya moto. Ningehuisha vilivyo dhana stahiki ya usalama barabarani na kuutowesha uhasama barabarani unaokua kila kukicha.

Ningepunguza sana idadi ya trafiki katika barabara na kupiga marufuku vitendo vyote vinavyosababisha usumbufu usio na mantiki kwa madereva wawapo barabarani, hasa mtindo wa trafiki kuwasimamisha madereva pengine bila kuwapo sababu mahsusi ya kufanya hivyo, kung’ang’ania leseni, kupoteza muda na yafananayo. Wingi wa trafiki barabarani hausaidii, zaidi unaongeza hofu na kutojiamini kwa madereva achilia mbali usumbufu kadha wa kadha.

Kama ningekuwa na ukuu nisingesubiri kujuta baada ya ‘kutumbuliwa’ bali ningekuwa makini na kuwaelekeza wenzangu tusifanye kazi kwa mazoea, kukomoa wala kuonea wateja wetu wanaofanya sisi trafiki tuwepo.

Ningesihi pamoja na kuzitumia vizuri sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani tutambue uwepo muhimu wa busara na ubinadamu kwenye utendaji hasa kwa mambo yanayohitaji elimu kwa wateja wetu, maelekezo au maonyo badala ya kukimbilia kuwaandikia faini au kuwaweka mahabusu.

Katika kuhakikisha wateja wetu wanashirikishwa, ningehakikisha kunakuwa na njia nyingi za kuwasilisha maoni, malalamiko, kero na ushauri kuhusu kazi zetu na utendaji wetu.

Ningetlilia mkazo matumizi ya teknolojia mpya tulizo nazo katika ukaguzi na ufuatiliaji ili kuondoa kero zitokanazo na matumizi ya mbinu zilizopitwa na wakati za kuvizia, kusimamisha madereva kila mara na kulazimisha makosa.

Yaani kuna baadhi ya trafiki wanajulikana kwa sifa mbaya tu za ukali, kusimamisha magari (madereva wa daladala wanasema ‘kupiga bao’), kuandika faini (au ‘kupiga cheti’), kusweka mahabusu na kadhalika.

Vile vile ningeelekeza shughuli zetu zisiingilie wala kuingiliwa na shughuli zisizo zetu. Ningewaelekeza wenzangu na tungeelewana kufanya yetu kwa weledi na kuwaachia wenzetu kina TRA, Sumatra na mamlaka nyinginezo wafanye yao. Mara nyingine trafiki wanalalamikiwa kutokana na kutekeleza majukumu nje ya wigo wao.

Mwisho kwa kutaja ningewataka watendaji wangu wote kutokimbilia kutuhumu, kuhukumu bila kujiridhisha kupitia uchunguzi. Mambo kama kudai chanzo cha kila ajali ni mwendokasi ningeyasitisha jumla ili matamko yanayotolewa kuhusu majukumu yetu hasa baada ya ajali kutokea yawe sahihi kutokana na uwepo wa uchunguzi wa kitaalamu tulio nao.

Binafsi nahisi dereva yeyote akipewa wasaa wa kulitambua kosa, akipata nafasi ya kurekebisha dosari anayokutwa au kupatwa nayo, akielekezwa, kukumbushwa na kuonywa huku busara ikipewa nafasi muhimu linapatikana funzo kubwa la utii wa sheria bila shurti na uwezekano mkubwa wa kulikabili kwa pamoja janga la ajali barabarani.

Inawezekana kuuhuisha ushirikiano baina ya wadau wa usalama barabarani kwa kutumia mbinu mpya zisizojumuisha sana shurti wala ukali kama baadhi nilizozitaja. Mbinu mbadala zikitumika zitaondoa hata hofu ya kupatwa na makosa halali au ya kubambika inayokua kwa kasi kwa madereva. Tanzania ni ya Watanzania, itafanywa bora na Watanzania wote kwa umoja wao.