Home Michezo Siri Madrid ilivyogeuka chungu kwa Zidane

Siri Madrid ilivyogeuka chungu kwa Zidane

1467
0
SHARE
Real Madrid's French coach Zinedine Zidane looks on during the Audi Cup football match between Real Madrid and Tottenham Hotspur in Munich, on July 30, 2019. (Photo by Christof STACHE / AFP)

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

IKIWA ndiyo mechi ya kwanza ya hatua ya makundi msimu huu, hali ni tete kwa kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ‘Zizou’. Kichapo cha mabao 3-0 katika mechi yao dhidi ya PSG kule Ufaransa kimekiweka hatarini kibarua chake Santiago Bernabeu.

Ukiachana na matokeo ya mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Sevilla, mchezo wa La Liga, tayari kulikuwa na makocha waliokuwa wakitajwa kwenda kukalia kiti chake, orodha ikiwa pia na jina la Jose Mourinho.

Je, nini kilicho nyuma ya Zidane kuonekana amechemsha miezi michache tu tangu aliporejea kuliongoza benchi la timu hiyo baada ya kuachia ngazi msimu uliopita? Makala haya yanakuchambulia.

Kwa jicho la haraka, tatizo linaanzia dirisha la usajili la kiangazi lililofungwa hivi karibuni, Septemba 2, mwaka huu. Ukikitazama kikosi cha Madrid alichonacho Zidane, sehemu kubwa ya nyota wake wapya hawajaanza kuonesha ubora wao.

Eden Hazard, ambaye alitua akitokea Chelsea, aliumia nyama za paja kabla ya Madrid kuvaana na Celta Vigo, mchezo uliokuwa wa ufunguzi wa msimu huu wa La Liga. Dhidi ya PSG ulikuwa mchezo wake wa kwanza kumaliza dakika 90 na hakuwa kwenye kiwango chake, ikionesha ana kazi kubwa mbele yake kuthibitisha Madrid walimuhitaji.

Ukitazama eneo la beki wa kushoto, unamkuta Ferland Mendy aliyeigharimu Madrid kiasi cha Pauni milioni 43 akitokea Lyon. Hata hivyo, bado hajaonesha kuwa anaweza kutegemewa katika nafasi hiyo, mfano mzuri ukiwa ni namna alivyovurunda dhidi ya PSG.

Pia, kinachoweza kuwa kinamuumiza kichwa Zidane kwa sasa ni kwamba iko hivyo kwa mlinzi wa kati aliyetokea Porto, Eder Militao. Aidha, bado Rodrygo aliyechukuliwa Santos kwa Pauni milioni 40 hajathibitisha kuwa ilikuwa sahihi kwa mashabiki wa Madrid kumfananisha na Neymar.

Unaweza kumtupia jicho hata Luka Jovic aliyekuwa moto wa kuotea mbali akiwa na Eintracht Frankfurt msimu uliopita, ambaye licha ya Madrid kumsajili kwa Pauni milioni 54, ameshindwa kuwa tegemeo ndani ya muda mfupi huu, akiwa ameingia kikosi cha kwanza mara moja pekee (dhidi ya Villarreal).

Zidane anatembea akifahamu wazi kuwa eneo la ulinzi ni tatizo kubwa. Ukiuweka kando mchezo uliopita dhidi ya Sevilla, Madrid waliruhusu nyavu zao kutikiswa katika mechi zote tano za mashindano msimu huu.

Wakati huo huo, safu ya kiungo nayo ni pasua kichwa na katika hilo, huenda kinachoweza kumfanya Zidane ajutie kwa sasa ni kuwaonesha mlango wa kutokea mastaa Dani Ceballos (Arsenal) na Marcos Llorente (Atletico Madrid).

Mbaya zaidi, hao wametimka, huku kiungo tegemeo wa Madrid akiwa na umri wa miaka 34, tatizo likionekana wazi dhidi ya PSG, ambapo Wafaransa hao walilitawala vilivyo eneo hilo la katikati ya uwanja, ‘wakiwazima’ Toni Kroos, James Rodriguez na Casemiro.