Home Maoni Sitamani Zitto aununue ‘ugomvi’ wa Assad na Ndugai

Sitamani Zitto aununue ‘ugomvi’ wa Assad na Ndugai

1070
0
SHARE

Jimmy Charles

KATIKA mambo ambayo kwa sasa sitamani yatokee ni kumuona Zitto Kabwe akiununua ‘ugomvi’ wenye sura binafsi kati ya Job Ndugai na msomi Mussa Assad.

Watatu hawa kila mmoja ana nafasi yake ya kiuongozi, Assad (Profesa) yeye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ndugai (Mbunge) yeye ni Spika wa Bunge na Zitto (Mbunge) yeye ni kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mvutano wa maneno ambao binafsi naupa sura isiyo rasmi ya ugomvi, kati ya Assad na Ndugai.

Mvutano wa wawili hawa ambao kwa upande mmoja umepewa sura ya ugomvi wa Bunge zima, eti, umesababishwa na neno dhaifu.

Kwamba Assad akiwa nchini Marekani katika moja ya mahojiano yake aliyopata kuyafanya huko alijibu swali aliloulizwa kwa kutumbukiza kibwagizo cha kuwapo kwa udhaifu wa kushughulikia mambo kitalani.

Hapa ndipo nongwa ilipoanzia, Assad ambaye tangu kuanza kwa vuguvugu hili amekuwa akisimama upande wa Katiba, alianza kwa kuitwa kwenye Kamati ya Bunge ya Maadili.

Kuitwa kwake kuliwaibua wengi wanaojua na wasiojua kubwata na kubwatuka, kusema na kunena, kuteta na kutetea, kupongeza na kubagaza, miongoni mwao ni Zitto.

Zitto yeye alikuwa upande wa Assad ambao nafikiri upande huo ndiko Katiba ya nchi imeegemea. Salama ya suala lile ilikuwa ni uamuzi wa  Assad kwenda mbele ya Kamati na kuipa nafasi imuhoji.

Kwa fikra zangu naamini tamaa ya Zitto katika kuununua ugomvi ule haikufanikiwa maana nafikiri Assad alitumia busara kulimaliza jambo lile kwa njia iliyosahihi.

Bahati mbaya waliolianzisha jambo lile hawakutaka kuiona busara ya Assad, badala yake wakaenda mbali zaidi kwa kukoleza moto wa kumsusa msomi huyo ambaye kumteua ni rahisi, kumtumbua ni mbinde, kutokana na kulindwa na Katiba ya nchi.

Uamuzi huu wa kumsusa Assad umepokelewa vibaya, kundi kubwa la wajuaji wa mambo hawakubaliani nao, jambo la kufurahia ni kitendo cha Bunge kuipokea ripoti ya Assad (CAG).

Nilifikiri hatua ya kuipokea ripoti na kuwa na utayari wa kuifanyia kazi kwa hoja kuwa watafanya kazi na ofisi ya CAG, lakini sio CAG mwenyewe, ingetosha na bila shaka ilitosha kumaliza msuguano ule.

Jambo la kusikitisha ni Ndugai (Spika) pamoja na kusema hana ugomvi binafsi na Assad, kuliamsha dude upyaa kwa kutoa kauli na lugha zenye sura tata dhidi ya mteule huyo wa Rais.

Miongoni mwa kauli hizo ni ile ya kuhoji kama Assad anajua mambo au anajua kutoa na kujumlisha tu!

Hapa ndipo hoja yangu ya kutamani Zitto asiununue ugomvi huu inaposimama, sitamani hilo kwa sababu mwanasiasa huyu kijana ana nongwa mbaya na kila ugomvi anaoununua au anaouanzisha haumwachi mpinzani wake salama.

Kisarani cha Zitto dhidi ya wapinzani wake nje na ndani ya Bunge kilianza kitambo hasa  kwenye Bunge lake la kwanza ambalo ni , Bunge la tisa lililokuwa chini ya hayati Samuel Sitta.

Wengi waliomgusa mguso wa kiuonevu walianguka na baadhi yao hawakusimama kabisa kwenye majukwaa ya kisiasa ama kiuongozi.

Miongoni mwa waliopotea kwenye majukwaa ya kisiasa kwa sababu kadha wa kadha, huku wakimwacha Zitto akiendelea kutamba na kushamiri kwenye siasa ni Nazir Karamagi, ambaye alitajwa kwenye sakata la Buzwagi.

Karamagi alipoteza uwaziri na baadae mwaka 2010, kura za kuteuliwa kuwania ubunge ndani ya chama chake hazikutosha na  ndio ulikuwa mwisho wake wa kisiasa.

Februari 2008, Karamagi aling’oka Wizara ya Nishati na Madini baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu. Vilevile aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha alijiuzulu. Wote hao ni kutokana na kashfa ya Richmond.

Charles Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliondolewa kwenye wizara hiyo kwa madai ya ulevi ikiwa ni kipindi kifupi mara baada ya kuingia katika vita ya maneno na Zitto.

Zitto alisema Kitwanga amekuwa akiwatumia vijana wa UVCCM kumshambulia kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sehemu ya hujuma kwa Rais John Magufuli. Kwa upande wake Kitwanga alisema hapendi maneno ya Kiswahili.

Aliyekuwa mwanasiasa machachari wa upinzani, David Kafulila sasa si mbunge tena, kabla ya kujikuta nje ya Bunge aliingia kwenye malumbano na Zitto.Kafulila alimwita Zitto ‘Simba wa kwenye boksi’, kwamba hang’ati, kwa hiyo hana athari yoyote kisiasa, Zitto nae alimwita Kafulila ‘manamba’.

Zitto bado ni mwanasiasa wa upinzani  mwenye mvuto, Kafulila amepotea kwenye medani za kisiasa na tayari ameshajisalimisha CCM. Zitto!!!
Mtu mwingine ambaye mara baada ya kulumbana na Zitto amepotea kabisa ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Maswi alikuwa mbabe haswa hakuwa na hofu walka woga kwa wanasiasa, alipambana na Zitto na sasa jina lake limepotea kabisa masikioni mwa waliomjua.

Mwaka 2012, katika Bunge la Bajeti, kuelekea bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Bodi ya Tanesco ilimsimamisha kazi, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, William Mhando. Baada ya uamuzi huo, ikaibuka kashfa kuwa bodi ilifanya makosa ya kukiuka sheria ya manunuzi katika kununua mafuta ghafi.

Ikabainika kuwa pamoja na makosa ambayo Mhando anatajwa kuwa nayo, yapo maelezo kuwa tofauti yake na bodi, ilisababishwa na yeye kupinga ukiukwaji wa makusudi wa sheria ya manunuzi. Kwamba mshindi wa zabuni ananyimwa halafu anapewa aliyeshindwa.

Zabuni imetangazwa, makampuni kadhaa yamejitokeza kuwania tenda. Kila moja inatangaza ofa yake, baadaye baada ya kupima vigezo kampuni moja ikashinda. Ajabu iliyopewa tenda ikawa kampuni tofauti na ile iliyoshindaa. Hiyo ni kashfa, na kulikuwa na sura ya wazi kwamba rushwa ilichukua nafasi.

Zitto akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) wakati huo, akamwandikia barua Spika Anne Makinda, kuomba kamati yake iruhusiwe na Bunge kuhoji pande zote mbili, Mhando na bodi ya Tanesco.

Haraka sana picha likageuka; Ikaelezwa kuwa Zitto alihongwa na makampuni ya mafuta kwa ajili ya kumtetea Mhando. Hali ilikuwa mbaya sana mpaka akaita mkutano na waandishi wa habari kujitetea lakini haikusaidia. Ilisababisha mpaka baadhi ya wabunge kuomba uongozi wa POAC uondolewe.

Spika Makinda alipoiagiza Kamati ya Ngwilizi (Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi) kufanya uchunguzi, ikabainika kuwa Maswi na Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, walisema uongo kwa lengo la kushawishi bajeti yao ipite na kuwadhibiti waliokuwa wakiipinga kwa kupitia kashfa ya ununuzi wa mafuta ghafi.

Kipindi hicho, Zitto alimtumia ujumbe Maswi akamwambia: “Maswi sijawahi kugombana na wewe kwa kuwa nakuheshimu sana. Tuhuma ambazo wewe na waziri wako mnazitoa dhidi yangu ni uongo, uzushi na za kupikwa.

“Mwambie waziri wako na wewe binafsi, sijawahi kushindwa vita ya kulinda credibility yangu, sipendi ujinga hata kidogo, mimi nina uhuru wa kusema ninachokiamini, sina bei, tupambane tu tuone nani ataumia.”

Turejee kwenye sentensi hiyo, “tupambane tuone nani ataumia.” Jiulize nani ameumia kati ya Zitto na Maswi? Zitto bado yupo bungeni na anendelea kuthibitisha viwango vyake, Maswi yupo Manyara.

Vita ya Maswi na Muhongo upande mmoja na Zitto iliishi kwa wapinzani wake kuanguka, aidha aliingia kwenye vita ya maneno na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, walilumbana hadi kufikia hatua ya kutoleana viapo. Zitto alisema kuwa Mkullo ni fisadi, kisha akalinyooshea kidole Baraza la Mawaziri kwamba lilihongwa ili kulifuta Shirika Hodhi la Rasilimali za Mashirika ya Umma (CHC) kwa sababu za kifisadi.

Mawaziri wakawa wakali, wakamtaka Zitto athibitishe, yeye aliwasilisha uthibitisho wake na kuanzia hapo ikawa kimya.

Mkullo alisema Zitto anatumika na kwamba anahongwa. Zitto akatoa uwanja huru, kila mmoja aruhusu kuchunguzwa ikibainika amewahi kuhongwa, atajiuzulu uenyekiti wa POAC, ubunge na ataacha siasa.

Akamtaka Mkullo kutangaza kuwa tayari kuuacha uwaziri endapo itathibitika amehusika na ufisadi akiwa Waziri wa Fedha.

Mkullo alinywea lakini ripoti ya CAG ya mwaka 2012, ilimng’oa Mkullo pamoja na mawaziri wengine saba.

Kabla ya kung’oka, mawaziri walikuwa wabishi, Zitto akaanzisha mchakato wa kukusanya saini 70 ili zihalalishe hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Mambo kabla hayajawa mabaya, Rais aliwaondoa mawaziri wote waliokumbwa na kashfa.

Mlolongo wa matukio haya unanifikirisha na kuniaminisha kutotamani hata kidogo Zitto aununue ugomvi wa Ndugai na Assad, kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa kwa yule atakayepingwa.