Home Makala SMARTPHONE ZIMEBADILI MWENENDO WA SEKTA YA SIMU

SMARTPHONE ZIMEBADILI MWENENDO WA SEKTA YA SIMU

658
0
SHARE

Na SHERMARX NGAHEMERA


SEKTA ya mawasiliano ya simu za mkononi imefikia ukomavu  kwa kuanza kushindanisha mazao badala ya kampuni na hivyo kuleta ahueni kwa wateja kwa kupata vunja bei.

Sekta hiyo imejipambanua kuwa ina ushindani mkali  sokoni  na bado inakua na kufurahia kile wanachokifanya, kwani kila siku kuna zao jipya kwa wateja wao.

Ili kuendelea kubaki kwa maana kwenye soko, wadau wameendelea kubuni  mazao mbalimbali na wateja  wamekuwa wakiyumbishwa kutoka programu moja kwenda  nyingine. Kuna mienendo minne ambayo itatawala mwaka huu 2017 wote, nayo ni:

Uimarishaji wa huduma ya 4G –LTE, kukua kwa  mahitaji ya data kwa matumizi mengi badala ya sauti (voice), kushamiri kwa biashara ya miamala ya fedha  na

kuongezeka kwa matumizi ya simu za kufuta (‘smartphones’).

Hayo yameainishwa na kuthibitishwa na ripoti ya mwisho wa mwaka 2016 ya TCRA, ambayo ilisema wazi mapambano ya ushindani sasa ni kwenye data ambako kumeongezeka wateja na shughuli.

Kwenye  Ripoti hiyo ya TCRA, watumiaji  walikuwa milioni 18 kwa intaneti, ikiwa ni asilimia 90 ya shughuli za intaneti kwa simu za mkononi, ukifananisha kuwapo watumiaji milioni 3.7 mwaka 2011. Hilo ni ongezeko lisilo kifani.

Imedhihirika kuwa idadi ya intaneti au vifaa vya intaneti vimeongezeka kwa kuchupa kutoka milioni 5.3 mwaka 2011 na kufikia milioni 19.86 mwaka jana mwishoni.

Picha hiyo ni tofauti kabisa na kile kinachoendelea kwenye  idara ya sauti ambapo ukuaji wa shughuli sio mkubwa sana kama Ripoti ya TCRA inavyoonesha.

Kwenye sauti hali imekuwa tete, kwani mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na ongezeko la wateja  wapya  63,596 kwa idadi ya SIM card zilizouzwa nchini kote. Hali hiyo ilifanya soko la simu liwe na wateja milioni 40.17 mwishoni mwa mwaka kutoka milioni 40.11 wa awali.

Hata Halotel ambayo ni mgeni kwenye shughuli inafanya vizuri na idara yake ya data kwa kuwapa data isiyo na kikomo kwa kifurushi chake kwa ajili ya wanafunzi kwa kutumia  huduma ya 3G na kuifanya iwe kampuni inayokua kwa kasi sana nchini, ingawa haijaanza kupata faida kwa shughuli zake.

‘Iliweza kupata wateja wa SIM card wapya 344,661  mwishoni mwa mwaka na hivyo kufikia kima cha wateja  milioni 3.439 na kuwa wa nane  kwa ukubwa kwenye soko,” inasema ripoti ya TCRA.

Ujio wa smart phones umeleta mabadiliko makubwa  kwenye soko, kwani watu wengi wako kwenye data na kupunguza kuongea kwa sauti na hivyo kukua kwa idara hiyo ya “apps”.

Kampuni za simu nazo zimeelekeza nguvu zake huko kama kauli, sera na vitendo vinavyoonesha kwenye shughuli zenyewe.

Ushindani sasa umeelekezwa kwenye data na ndiko ziliko fedha na maisha ya baadaye ya kampuni hizo, kwani  mapato kwenye sauti yameanza kunywea kutokana na ujaji wa simu za smartphone kwenye soko zenye kivutio cha data na huduma kedekede za apps, zikiwamo tweeter, instagram, facebook, u-tube, ebay na nyinginezo nyingi. Kila mtu kwa kile kinachomfaa na kumfurahisha kusikia na kuona kwa macho.

 Kutokana na  kuendelea kukamilika kwa utandazaji  wa mkongo wa Taifa, maeneo mengi yameanza kunufaika na matumizi ya intaneti na kufanya kweli dunia kuwa kijiji, kwani matukio yanaonekana kutoka duniani kote.

Takwimu nazo haziko nyuma, kwani  ufikiwaji wa  intaneti umeongezeka kwa kasi kutoka asilimia 12 kwenda 34 na kufikia asilimia 40 kwa miaka ya 2011, 2015 na 2016  sawia.

Uwekezaji wa kampuni za simu unatoa mwelekeo huohuo, ambapo data ni kipaumbele na kutoa nafasi kwa kampuni mpya kama Halotel kusajili wateja wapya wa sauti.

 TCRA inasema kati ya kampuni saba zilizoko, tano zinawekeza kwenye data  na hususan teknolojia ya 4G-LTE, yaani 4th Generation Long Term Evolution yenye intaneti kwa kutumia mwendo kasi  ulioko kwenye mfumo huo kama kigezo na kivutio cha ubora. Wengi wamenasa kwa mbinu hiyo ya spidi kubwa.

TCRA inasema 4G-LTE kama teknolojia ina mwendo kasi mara tano zaidi kuliko 3G, ambayo ilianzishwa kwenye soko miaka michache iliyopita.

Kampuni za Tigo, Vodacom,  Zantel na  Airtel  zimewekeza kwenye teknolojia ya 4G.

Vodacom Tanzania ilianzisha 4G katikati ya mwaka jana na kauli ya Meneja Mkuu wake,  Ian Ferrao, alisema kuwa kampuni yao kuanzia mwaka jana imeipa kipaumbele  huduma za data ili kuongeza mapato yake na hivyo kuongeza mchango wake kwa uchumi wa wananchi ya Tanzania.

Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez, aliahidi wakati wa uzinduzi wa 4G kuwa kampuni itawekeza zaidi ya dola milioni 120 kwa mwaka jana katika masuala mbalimbali, yakiwa na lengo la kuongeza wateja wa data  na kufikisha huduma ya 4G kwa mikoa yote.

Mkuu wa Masuala ya Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia, alisifia hatua ya kuelekea kwenye data, kwani takwimu zinashauri hivyo.

 Mworia alitamba kuwa, data imethibitisha kuwa Vodacom ni kampuni inayoongoza kwa kila kitu na imejizatiti kuipeleka nchi hii kwenye ulimwengu wa kidijitali na kuihusisha jamii yote kwenye mfumo wa mwenendo wa fedha wa kisasa kupitia programu yake ya M-Pesa.

Kuonesha mambo yamenoga kwenye data, TIGO nayo haikubaki nyuma na kuanzisha kifurushi kinachotisha hapa mjini cha ‘Halichachi’ kwenye huduma zake ambapo mteja hutumia bando yake hadi nukta ya mwisho ya matumizi bila hofu ya data kupokwa kwa muda kwisha au wakati wake kukoma; ndiyo maana ya kutochacha ili kuwazingua washindani wake kwenye soko.

Meneja Chapa wa Tigo, William Mpinga, alisema kwenye uzinduzi kuwa ‘Halichachi’ ni ubunifu wao kukabili ushindani uliopo katika utoaji huduma na inadhihihirisha kuwa Kampuni yake inaongoza katika kubuni mambo ambayo yanawafaidisha wateja wao kuishi vizuri.

“Ni ukweli usiopingika kuwa, soko la mawasiliano la Tanzania linajiendeleza na kukomaa kwenye ununuzi wa vifurushi na hivyo bando la Halichachi litakuwa suluhisho la mahitaji ya wateja wao waaminifu na kudhihirisha kuwa katika ubunifu hakuna mshindani zaidi yao,” alisema.

Mpinga alisema huo ni mwendelezo wa kile kinachofanyika mara zote, yaani kuwafanya wateja wao kuishi maisha bora kwa kupata wanachohitaji, ikiwamo kuwapa huduma za mitandao ya bure kwenye mitandao ya jamii kama face book.

Ilipofika Septemba mwaka jana, Zantel ilizindua huduma zake za 4G na hasa za intaneti na kusema wazi siku za usoni zitatawaliwa na data; kama meneja wa chapa wa kampuni hiyo, Rukia Mtingwa, alivyothibitisha na kuainisha.

Kampuni hiyo inaelezwa iko kidedea kwenye masuala ya data, kwani  iliwahi kwenye  gateway yake  kule Zanzibar  na Etisalat  na sasa inapandisha huduma hiyo kwenye mtandao wake wote ili kupitisha mwenendo wa 4G .

Kama kawaida yake, Vodacom inaongoza kwa kupata wateja wapya 64,946 mwishoni mwa mwaka jana na hivyo kufikisha wateja wote kuwa ni milioni 12.419 kutoka milioni 12.354 Septemba mwaka jana.

 

Matumizi ya data kwenye miamala ya fedha

 Matumizi ya simu katika masuala ya fedha ni makubwa nchini na kufanya nchi hii kuongoza katika masuala ya uhusishaji ( financial inclusion) kwenye masuala ya fedha kuwa mkubwa kuliko.

Katika ripoti ya utafiti iliyotolewa na Taasisi ya Uchumi (EIU) ya mwaka 2014 Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kufanikiwa katika utoaji wa huduma za kifedha kwa kutumia mitandao ya simu za mkononi.

Katika ripoti hiyo ilibainika kuwa Tanzania  ni nchi ya sita duniani katika matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya kiteknolojia.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya simu yameongezeka  zaidi ya maradufu kutoka asilimia 17 mwaka 2011 hadi asilimia 40 kwa mwaka 2014.

Kwa sasa Tanzania ina mawakala wa huduma ya mitandao ya simu zaidi ya 270,000 waliosambaa maeneo mbalimbali nchi nzima.

Hadi mwisho wa mwezi Julai mwaka jana takribani Watanzania milioni 21.5 nchi nzima wanatumia huduma za kifedha kwa njia ya mitandao ya simu. Ni mafanikio makubwa.

Tangu kuanzishwa kwa huduma za kifedha kwa njia ya simu mwaka 2008 kumerahisisha maisha ya Watanzania kwa asilimia kubwa mijini na vijijini.

Ripoti ya TCRA imeonesha kuwa kwa miezi miwili ya mwaka jana simu za mkononi wamefanikiwa kufanya miamala ya thamani ya Sh trilioni 13.07.

Novemba kulikuwa na miamala ya Sh trilioni 6.47 na Desemba Sh trilioni 6.60  na hivyo kutoa ushindani mkubwa kwa mabenki nchini kama mtoa huduma  mbadala.

Asilimia kubwa ya mzunguko wa fedha nchini hupitia kwenye simu za mkononi ambapo watu wengi wanafanya huduma kwa njia ya mtandao kwa kutuma na kupokea pesa na kulipia huduma mbalimbali za umeme, maji, ada za shule na huduma nyinginezo.  TCRA inasema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya simu hapa nchini, ikiwa tofauti na miaka ya nyuma na kumerahisisha huduma.

Imedhihirika kuwa, malipo ya fedha kwa njia ya simu yanasaidia kupunguza gharama  za maisha,  hivyo kuwa kichocheo cha maendeleo, kwani  wafanyakazi na  wakulima wanaotumia huduma za bima, wanaonunua bidhaa hulipa kwa kutumia simu za mkononi na hivyo kukimbiza mambo na kufanya matumizi sadifu ya muda na kuleta tija kwenye  shughuli  zinazofanyika.

Isitoshe, watu wengi na hasa vijana wameajiriwa kama mawakala kwa makampuni ya simu na kuleta mafanikio makubwa kiutawala.