Home Makala Sogea  nikuume sikio

Sogea  nikuume sikio

655
0
SHARE

Sogea nikuume sikio maana ninayo mengi niliyohifadhi kwa ajili yako. Nimekuona siku nyingi na sikutaka kukusumbua kwa ghani zangu ziumizazo moyo.

Nitatumia muda huu leo katika safu yangu kukuuma sikio. Nitakuuma bila haya maana niliyobeba kifuani ni mengi. Yapo uliyoyasababisha wewe na mengine yanatokana na matukio yaliyofanywa na nduguzo. Nani alikwambia maisha ni kusaka ufalme na kwamba ufalme ni kukaa kiti cha juu?

Tazama sasa kla nikipita nakutana na watu wakilia kuhusu masaibu ya maisha. Wanasema baadhi yake umeyaleta wewe. Tena wanasema umesababisha mkwamo? Unajua mkwamo wewe?

WhisperMkwamo wa maisha ni ishara inayomaanisha kwamba maisha yana nguvu iliyo nje ya uwezo wa mwanadamu. Pia mkwamo hubainisha uwepo wa mamlaka nje ya nguvu ya kiumbe anayeishi. Mamlaka hiyo, ina nguvu kubwa ambayo haiwezi kuelezeka. Yeyote aliyepata kibali cha kuishi katika uso wa dunia hii katu hawezi kuwa na uwezo wa kukabiliana na nguvu ya mamlaka hiyo.

Mswahili akaja na methali isemayo: “yeye anayedhani amesimama aangalie asianguke.” Methali ambayo inabainisha udhaifu wa mwanadamu katika maisha yake ya kila siku. Methali inayoakisi hali ya maisha kuwa tegemezi na kuonesha kuwa maisha hayana njia moja na kamwe katika maisha hakuna mshindi bali wapo washindi.

Washindi hupatikanaje? Washindi hupatikana pale shindano liandaliwapo na kisha kutolewa fursa ya watu kushindanishwa. Tena mshindi halali ni yule atokanaye na mashindano yasiyo na chembe za udanganyifu. Lakini pia, yawezekana vipi kuwe na mashindano kama hakuna maandalizi?

Kukosekana kwa maandalizi kumesababisha mashindano kadhaa kukosa ladha. Tena kumesababisha baadhi ya magwiji kukataa kushindana. Nani akubaliye kushindana katika eneo lisilotoa fursa sawa kwa kila anayeshindana

Hapa sasa ndipo ninapotaka kabisa kukusogolea ili nikuuume sikio. Unataka tushindane pamoja wakati timu zetu hutaki zifanye mazoezi? Mbona wewe licha ya kuwa na Waamuzi wa mchezo katika timu yako bado unapita huku na kule kuandaa timu yako?

Wenzako wamekukosea nini au nini mantiki ya uoga ulikijaza kifua chako? Unaweza sasa usitazame lakini siku si nyingi utafahamu kuwa maji hata yazibwe vipi yatatafuta upenyo wa kupita. Hii ni sawa na mvua, huwezi kuizuia isinyeshe. Itanyesha tu kama si leo ni kesho na pia kama si Mamlaka iliyo juu, wewe huna hata nukta ya uwezo wa kupanga kiasi cha maji kiletwacho na mvua.

Eti wasema change chako na chako chako. Hivi tabia hii mbaya ya unyimi umeipata wapi? Unawezaje kutaka kula kila sahani ya chakula iagizwayo hotelini? Kwani hufahamu kuwa kumuiga Tembo kwaweza kukusababishia kupasuka msamba? Angalia msamba wenyewe usikukute ukiwa katikati ya halaiki.

Kuna kipindi nakutazama nashindwa hata kupata picha ya wapi ulitokea au wawapi waliokuleta. Natazama kila kona na kuangalia njia hizi mpya ambazo natakiwa kupita wakati hazioneshi kunifiisha niendapo.

Nalalama tu na njia hizi zilizojaa mawe yaliyochongoka ilhali sina viatu katika miguu yangu iliyochoka. Tena umemwaga vumbi zito katika njia tupitazo ili kurahisisha hila zako mbaya zilizojificha katika sura ya Msalaba wa Bwana. Nimeamua kukuuma sikio na kamwe usithubutu kabisa kunizuia maana kufanya hivi kutasababisha nipayuke. Si tabia yangu kupayuka na sitafanya hivyo kama utaendelea kuwa mtulivu na kunisikiliza hadi nitakapomaliza.

Nikupe mfano mmoja ambao nimekutana nao siku chache zilizopita. Najua utakukera kiasi maana hupendi kusikia yale ambayo hayatoki katika kinywa chako. Naanza mfano huu endelea kuweka sikio.

Nimekutana na Video moja iliyoibua hisia mpya katika kubaini faili ya maisha. Msimulizi wa Video ile akatoa simulizi aliyoipata kutoka kwa Naibu Waziri mmoja wa Ulinzi wa Marekani ambaye amekwisha kustaafu (jina akalihifadhi) aliyealikwa kutoa hotuba katika mji mmoja nchini humo.

Naibu Waziri yule alizungumza haya: “mwaka jana nilikuja katika mji huu na nilihutubia katika ukumbi huu huu. Kabla sijatoka Washington, tayari tiketi yangu ya ndege ilishalipiwa katika daraja la Biashara. Nilipotua tu uwanjani tayari kulikuwa na watu wa kunipokea na gari rasmi kwa ajili yangu.

Nilipelekwa hadi hotelini na nilipofika pale tayari chumba change cha kulala kulikuwa kimeshaandaliwa na nilipelekwa moja kwa moja nchumbani.

“Nilipotoka kesho yake tayari nilikuwa na watu wakinisubiri na walinichukua hadi katika ukumbi huu na kuniingiza chumba maalum. Huko nako nilikutana na watu ambao walinihudumia kahawa na viburudisho vingine. Walinielekeza kuja hapa na kuanza kutoa hotuba yangu.

Lakini leo nilipofika kwanza nilipaswa kukata tikti za ndege mwenyewe. Nilipotua nilipaswa kutafuta teksi na kisha kwenda kwenye hoteli na kuanza taratibu za kupewa chumba. Nilipoamka hakukuwa na mtu wa kunisubiri, ilinibidi mimi mwenyewe kujiandaa na kuchukua taksi ili nije katika ukumbi huu.

Nilipofika hapa sikupitishwa tena katika chumba maalum bali nilitumia mlango wa nyuma. Nilipokuwa kule nyuma kabla ya kuingia ukumbini hakukuwa na mtu wa kunipatia kahawa na hata nilipouliza kuhusu wapi kahawa ipo, mtu mmoja alinionesha palipo mashine za kahawa ili nijihudumie.”

Nukuu hii inatupa funzo gani? Maisha yana hali mbalimbali. Kwamba kilichokuwa kikitoa fursa za kupewa huduma nyingi hakikuwa mtu bali nafasi yake. Matajiri na wenye mamlaka hupata huduma nyingi kutokana na uwezo wao wa fedha au nafasi za madaraka walizonazo.

Inapotokea vitu hivyo vinatoweka maisha ya uhalisia yanarejea. Mantiki nyingine ni kuwa, heshima na stahili nyingi unazopewa baada ya kuwa na mamlaka fulani, havitokani na wewe bali nafasi unayoishikilia kwa wakati huo.

Siku ikitokea nafasi hiyo si yako tena, basi heshima na stahili zile huenda kwa mwingine mwenye kushikilia nafasi ile ile. Utaziona stahili zile namna zinavyohama na namna ambavyo hazitarejea kabisa kwako. Hautaumia kama ulifahamu maana ya nafasi na nadharia ya umuhimu wa kupokezana vijiti.

Itaendelea toleo lijalo

0767531303