Mawazo Lusonzo
KILA anayefanya vizuri anastahili pongezi. Kinachoendelea hivi sasa ndani ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuhusiana na juhudi za kuweka katika soka la vijana linastahili kuungwa mkono na kupongezwa.
Tangu kuingia kwa awamu hii ya uongozi mpya ndani ya TFF chini ya Rais Wallace Karia kuna jambo linaonekana kama juhudi ya kuendeleza soka la vijana wa kila rika. Tunapongeza katika hili.
Tunapongeza kwasababau kuna mwanga unaonekana, ikiwa ni pamoja na kuona namna shirikisho linavyoandaa timu za taifa za vijana, lakini pia msisitizo uliopo wa kuwa na mashindano mengi ya vijana wetu.
Kokote duniani ambako mataifa yaliyoendelea kupitia soka, hawakupata mafanikio ya njia ya mkato, bali ni kupitia jitihada kama hizi ambazo ndizo zilizoifanya timu yetu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ilipofanikiwea kutwaa ubingwa wa CECAFA mwaka huu.
Wakati huu wa kupongeza kinachoendelea juu ya soka la vijana, lazima turejee pia namna ambavyo soka la umri mdogo ili iwe dira ya kufika huko ambako mataifa mengine yamepiga hatua kwa mikakati hii.
Pamoja na mikakati hii, tunachoendelea kusisitiza kama ushauri kwa TFF ni kujikita pia katika kupambanua falsafa ya taifa itakayotufikisha katika mafanikio. Hili ni jambo lingine la msingi.
Kupitia Falsafa kama hii pia iendane na sera ya pamoja ambayo ndiyo itakayozaa matunda kwa wanasoka vijana tunaowaibua katika mashindano mbalimbali waweze kucheza soka la mfumo wa pamoja kwa nchi nzima.
Mfumo huo wa mashindano ya watoto lazima ufanane kote nchini, ukienda Mbeya, Mwanza, Lindi, Pemba uone mfumo mmoja wa mashindano ili ukipata wachezaji wafanane kiuchezaji.
Kupatikana kwa falsafa sahihi ya kisoka itarahisisha ngazi yote ya kusimamia soka la vijana kwa marika tofauti, kwa maana ya kwamba, kijana aliyetoka Zanzibar, Pemba, Manyara, Lindi kufundishwa mpira wa aina moja kwasababu tayari kuna falsafa ya nchi ambayo pia itaingia moja kwa moja kwenye timu za ligi kuu.
Kwa mfano ukiangalia ligi ya Ujerumani, Bundesliga, ukiangailia ligi ya Hispania, La Liga au Uholanzi, inavyocheza timu ya taifa ukienda kwenye klabu utaona wanacheza vilevile, mathalani, wanavyocheza Barcelona, Real Madrid, Valencia utaona wanacheza hivyo hivyo kwenye timu ya Taifa ya Hispania.
Ukienda Ujerumani ‘Staili’ ya uchezaji wa klabu inaendana na timu ya taifa. Hii ndio maana ya falsafa, kama taifa mnaamua kwamba hii ndio staili yetu ya uchezaji, kufundisha wachezaji na hapo ndipo unapata urahisi wa kufundisha mpira.
Kabla ya kukimbilia kwenye mashindano kwanza ni kukaa chini na wataalamu ili kutengeneza falsafa ya mpira wa Tanzania.
Hatua nyingine muhimu ni hii ya kutengeneza mfumo Lazima tuendeleze mikakati ya kuwa na mashindano ya vijana yafanyike chini ya mfumo mzuri wa kimashindano wa kubaini vipaji na mfumo wa kuviendeleza vipaji hivyo, kama hatutilia mkazo hatua hii basi lengo la kupata mafanikio ya juu halitafanikiwa.
Ukiachana na mikakati iliyotajwa hapo juu, kuna haja pia kwa shirikisho kuendelea kubuni mikakati ya kuzalisha makocha wa kutosha, angalau kuwepo uwiano wa kocha mmoja kufundisha vijana 30, hapa inategemeana na bajeti yake.
Uanzishwe pia mpango madhubuti wa kuzalisha makocha wengi ili kuwa na uwiano wa timu za vijana zinazotakiwa kuanzishwa kuanzia ngazi ya chini.
Kama nilivyogusia hapo juu , kama unataka kuwa na idadi kubwa ya vijana pia unatakiwa kuwa na wataalamu wengi wa kung’amua vipaji na kuviendeleza, usipokuwa na wataalamu utaishia kutengeneza kundi la wachezaji wa zamani na kuwagawa kwa maeneo wakati utaalamu wenyewe wa kubaini wachezaji hawana.
Pia suala la kuwapo kwa miondombinu ya mpira na utawala kwenye ngazi zote ni eneo kubwa na lililohitaji kupewa kipaumbele kwa viongozi wajao.
Kipaumbele kingine muhimu kwa soka ni suala la kufanya utafiti na kubaini mbinu sahihi za kufundishia, kuna mabadiliko makubwa sana ya kiufundishaji, kabla ya kuanzisha mashindano ya kupata vijana, lazima tukae chini kufanya utafiti mzuri kupata njia sahihi za kufundishia mpira.
Lazima utengenezwe mfumo mzuri wa kisayansi wa kuweza kufundisha soka. Pia miundombinu bora ya kitabibu kwa ajili ya kuwapatia wachezaji tiba nzuri, waweze kupewa ushauri mzuri wa vyakula, sio kukimbia tu na kucheza mpira.
Haya yakifanyika kwa ufanisi, nina imani kubwa kuwa, ndoto ya Tanzania kufanya vyema katika michuano ya kimataifa kupitia mkakati wa soka la vijana linaloambatana na falsafa ya pamoja ya mfumo tunaotaka kuutumia kwa timu zetu za taifa ya marika yote.