Na Sosthenes Nyoni
Mjadala mkubwa ambao umetawala mazungumko ya wadau wa soka hapa nchini kwa sasa ni kuhusu kipigo ilichokipata timu ya Taifa’Taifa Stars’.
Stars haikuzindua vizuri kampeni zake za fainali za mataifa ya Afrika zinazoendelea kupigwa nchini Misri, baada ya kuchapwa mabao 2-0 na timu ya Taifa ya Senegal maarufu Simba wa Terenga.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja Juni 30, Stars ilionekana kuzidiwa kila idara na wapinzani wao hao walionekana imara kiasi cha kutosha.
Baada ya mchezo huo, wadau wengi wa soka hapa nchini wameonekana kukosoa uwezo wa kikosi cha Stars na hasa kocha wa timu hiyo, Emmanuel Amunike.
Wengi wanaolaumu wamekuwa wakidai kuwa, Amunike alipanga kikosi kilichokuwa na uwezo wa kupambana na kupata matokeo.
Hii ndiyo sababu kubwa inayoelezwa na wadau wa soka wanaomlaumu Amunike.
Lawama hizi dhidi ya Amunike hazijaanza sasa, zilikuwepo tangu kikosi cha Stars kilipokuwa kinashiriki mechi za kuwania kufuzu fainali hizo na hata baada ya uteuzi wa kikosi cha mwisho cha wachezaji 23.
Ukirejea kuangalia viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Senegal inakamata nafasi ya 22, wakati kwa Afrika inaongoza kwa ubora ikiwa nafasi ya kwanza.
Tanzania iliyocheza na Senegal, inakamata nafasi ya 136, duniani na nafasi ya 36 kwa Afrika.
Takwimu hizi zinaonyesha jinsi mataifa haya mawili yalivyotofautiana kwa mbali kwa nafasi zao katika viwango vya soka vya FIFA.
Ukiangalia mchezo wa Stars na Senegal utagundua kwanini mataifa haya mawili yanatenganishwa kwa mbali.
Hakukuwa na usawa katika ubora wa vikosi, Senegal iliionekana kuundwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa tofauti tofauti na Stars, ambayo wachezaji wake walionekaana kucheza huku wakiwa wamejaa hofu.
Hofu waliyokuwa nayo wachezaji wa Stars haikuja hivi hivi tu, ilitokana na sifa tofauti ya vikosi hivyo viwili, kubwa ikiwa na ligi ambazo wachezaji wake wanacheza.
Katika kikosi cha Senegal, idadi kubwa ya wachezaji wake wanacheza soka la kulipwa katika ligi kubwa za mataifa mbalimbali ya Ulaya.
Na sio kucheza Ulaya pekee, huko walipo wanapata nafasi ya kucheza na baadhi wanategemewa.
Hali ni tofauti katika kikosi cha Stars wachezaji wake wengi wanacheza ligi ya ndani, wachache nje ya Tanzania na Ulaya.
Hii ilikuwa ni sababu kubwa ya kwanza kwa Stars kuwa katika nafasi duni ya kuweza kupata matokeo mazuri dhidi ya Senegal.
Mchezaji anapocheza katika ligi kubwa anapata fursa ya kuimarika zaidi tofauti na yule anayecheza ligi yenye ushindani mdogo kama ya Tanzania ambayo imetawaliwa na klabu mbili, Simba na Yanga.
Kwa mantiki hiyo, kwanza ni lazima mamlaka zinazosimamia mchezo wa soka nchini, zihakikishe ligi zetu na hasa Ligi Kuu Tanzania Bara, inakuwa na ushindani wa kutosha tofauti na sasa.
Yapo madai ya kuwepo upendeleo wa wazi wazi ambayo yamekuwa yakitolewa na klabu nyingi hususani za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF).
TFF inalaumiwa kuzibeba baadhi ya klabu na zinazolengwa zaidi ni Simba na Yanga na kidogo Azam.
Kama hizi shutuma zina ukweli ndani yake, ni wazi tunakuwa tunajimaliza wenyewe kwani kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunaandaa wachezaji wasioweza kujipigania wenyewe badala yake wanasubiri kubebwa.
Bahati mbali wadau wengi wa soka wanaomlaumu Amunike wamesahau changamoto hizi zilizoko kwenye ligi zetu, ambazo mwisho wa siku ndiyo inayotoa wachezaji wanaokuja kuichezea timu za taifa.
Baadhi ya wapenzi wa soka wamefikia hatua ya kuhusisha kukosekana kwa wachezaji fulani na kipigo ilichokipata, lakini ukweli ni kwamba uwezo wa kikosi cha Stars ulionekana kuwa mdogo ukilinganisha na ule wa kikosi cha Senegal.
Kingine kilichoonekana kuiathiri Stars ni makuzi yasiyojitosheleza ya wachezaji wanaounda kikosi hicho.
Katika mchezo dhidi ya Senegal, baadhi ya wachezaji wa Stars walionekana kukosa misingi ya mchezaji wa soka kuanzia wakiwa wadogo.
Mapungufu haya yaliionekana katika umiliki wa mpira ambapo baadhi walioenekana kushindwa kuudhibiti pale walipopigiwa pasi hivyo kujikuta wakimpa adui.
Hili liliifanya Stars muda mwingi kuwa watumwa mbele ya wapinzani wao Senegal.
Na kwakutambua hilo,Senegal ilizidisha presha ili kuifanya Stars kufanya makosa na katika hilo ilifanikiwa na kufanikiwa kufunga mabao mawili huku washambuliaji wake wakikosa mabao mengine mengi.
Suluhisho la mapungufu hayo ya Stars ni kurejea katika kuwajenga wachezaji wetu kuanzia umri mdogo kupitia akademi za soka. Ni jambo lisilowezeka kwa kocha wa timu ya Taifa kumfundisha mchezaji namna ya kutuliza mpira na kupiga pasi.
Kama hili hatulioni kama tatizo la msingi, ni wazi tutaendelea kumlaumu Amunike na wachezaji wenyewe, hata kama tutaamua kumfukuza na kumleta mwingine halitakuwa suluhisho.