Home Michezo Stars ya Amunike ina uwezo wa kufika mbali zaidi ya 1980

Stars ya Amunike ina uwezo wa kufika mbali zaidi ya 1980

1631
0
SHARE

NA HENRY PAUL

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, ilijihakikishia kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya pili baada ya kuifunga Uganda ‘The Cranes’ mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo uliochezwa Machi 24 mwaka huu, uliiwezesha Stars kushika nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi nane katika Kundi I nyuma ya vinara Uganda waliovuna pointi 13.

Katika kampeni ya kuwania tiketi ya AFCON 2019 inayotarajiwa kuanza Juni 21 mwaka huu nchini Misri, Stars ilianza kwa sare ya bao 1-1 na Lesotho kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, kabla ya kutoka sare ya kutofungana na Uganda ugenini.

Katika mchezo uliofuata, Stars ilichapwa mabao 3-0 na Cape Verde ugenini, kabla ya kulipiza kisasi kwa wapinzani wake hao kwa kuwafunga mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Stars ilifunga safari hadi Lesotho kuvaana na wenyeji wao hao na kupokea kipigo cha bao 1-0, matokeo yaliyoonekana kuififisha matumaini ya Watanzania kuiona timu yao ikifuzu michuano hiyo ya Afrika.

Hapo ndipo Watanzania walipoanza kukesha wakiomba timu yao ishinde mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda, huku pia wakipiga dua ili Cape Verde ishinde au itoke sare na Lesotho.

Mwisho wa siku, ndoto ya Watanzania ilitimia kwasababu Stars iliichapa Uganda mabao 3-0 wakati Lesotho na Cape Verrde zikitoka sare ya kutofungana na kutoa nafasi kwa Taifa Stars kufuzu fainali hizo za AFCON kwa mara ya pili tangu wafanye hivyo mwaka 1980.

Ikumbukwe mara ya mwisho Taifa Stars kushiriki fainali hizo zilipigwa jijini Lagos, Nigeria, walipangwa Kundi A pamoja na wenyeji Super Eagles, Misri na Ivory Coast.

Tangu mwaka huo wa 1980, takriban miaka 39 imepita, Taifa Stars ikijitahidi kupambana kufuzu michuano hiyo bila ya mafanikio, hali iliyokuwa ikiwasononesha wapenzi wa soka nchini.

Wakati fulani, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, alidiriki kuiita Tanzania katika soka ni ‘kichwa cha mwendawazimu’ kutokana na mwendendo mbaya wa timu uwanjani.

Tayari kikosi cha Stars chini ya kocha wake, nyota wa zamani wa Nigeria, Emmanuel Amunike, kimeanza kambi kujiandaa na michuano hiyo huku Watanzania wakiwa na matumaini makubwa ya vijana wao, wakiongozwa na Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, kufanya vema huko Misri. 

Amunike alichagua kikosi cha wachezaji 39 ambao tayari wapo kambini kabla ya kuchuja na kubaki na wachezaji 23 ambao watakwenda Misri kushiriki Kombe la Afrika inatarajiwa kumalizika Julai 19 mwaka huu.

Licha ya Taifa Stars kutokuwa na maandalizi ya muda mrefu, ubora wa wachezaji waliyoitwa kikosini ulionekana kwa namna walivyocheza wakiwa na timu zao hivyo wanaweza kufanya vizuri endapo watajituma na kucheza kwa bidii.

Kikosi cha Taifa Stars kilichochaguliwa hivi karibuni kabla hakijachujwa na Amunike, ni kizuri na chenye wachezaji mahiri waliyo na vipaji vya hali ya juu, hivyo wanaweza kufanya vizuri na kuvunja rekodi ya mwaka 1980.

Ikumbukwe kwamba mwaka 1980 wakati Taifa Stars inashiriki michuano hiyo ya Afrika pamoja na kuwa na kikosi kizuri, lakini haikufanya vizuri.

Katika mchezo wa kwanza, Stars ilifungwa na wenyeji Nigeria mabao 3-1 kabla ya kupoteza kwa Misri mabao 2-1 kisha kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Ivory Coast.

Wakati Taifa Stars inashiriki Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza 1980, ilikuwa na washambuliaji mahiri kama Peter Tino, Mohamed Salim, Thuwen Ali na Omar Hussein ‘Keegan’, huku viungo wakiwa ni Mohamed Rishard ‘Adolp, Hussein Ngulungu na mabeki wakiwa ni Jella Mtagwa, Leodger Tenga, Leopold Taso na Ahmed Amasha ‘Mathematicians’.

Ukiangalia kikosi hicho kwa wakati huo, kilikuwa ni kizuri mno, kwasababu wachezaji wote walikuwa na vipaji vya hali ya juu na walikuwa mahiri mno katika timu zao walizotoka.

Lakini kutokana na kucheza na timu zilizokuwa na viwango vikubwa barani Afrika, ilishindwa kufika mbali na kuishia hatua ya makundi.

Mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 1980, Tanzania pia ipo katika kundi gumu, ikipangwa na timu za Kenya, Algeria na Senegal, ambazo zote zina viwango vikubwa vya soka.

Mbali na ubora wa nahodha Samatta anayetesa Ulaya akiwa na Genk, yupo Mtanzania mwingine anayesumbua huko Morocco katika kikosi cha Difaa El-Jadida, Simon Msuva, ni wazi safari hii huenda timu hiyo ikafanya vema zaidi ya 1980.

Wachezaji wanaocheza timu ya Taifa Stars hivi sasa wengi wao wameng’ara katika ligi za nje kama Samatta, Msuva, Thomas Ulimwengu anayechezea timu ya JS Saoura ya Algeria, Shabani Chilunda anayekipiga Tenerife ya Hispania, Himid Mao (Petrojet FC, Misri), Rashid Mandawa (BDF X1, Botswana), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia) na Shiza Kichuya (ENPPI, Misri).

Wachezaji hawa wanaowika katika ligi za nje, wakiungana na wenzao wanaocheza Ligi Kuu Tanzania Bara kama John Bocco, Mudathir Yahaya, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Jonas Mkude, Aggrey Morris na Gadiel Michael, wanaweza kutoa ushindani mkubwa kwa timu watakazocheza nazo huko Misri iwapo watacheza kwa kujituma kama wanavyofanya wakiwa na klabu zao.  

Kilichobaki kwa sasa ni Watanzania kuipa Stars sapoti ya hali na mali, ikiwamo kuwaombea wachezaji waweze kufanya maandalizi yao ipasavyo bila kupata majeraha yoyote na mwisho wa siku, waende kuiwakilisha vema Tanzania huko Misri.

Kikosi cha Stars kina mahitaji mengi mno kiasi kwamba kila Mtanzania ana wajibu wa kusaidia pale anapoweza kulingana na nafasi na uwezo wake, hili si jukumu la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Serikali pekee, bali ni la Watanzania wote.