Home Latest News TAASISI HII IJITUTUMUE KUPAMBANA NA UFISADI

TAASISI HII IJITUTUMUE KUPAMBANA NA UFISADI

500
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Ni takriban miezi miwili imepita tangu niandike makala katika gazeti hili kuhusu utendaji wa taasisi muhimu nchini – Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) – nikisema kwamba bado haijaonyesha makucha yake hasa pamoja na kuwepo ahadi na maneno mengi.

Ilikuwa ni kipindi kile Rais John Magufuli alipomuapusha Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU. Wakati wa hafla ya kuapishwa afisa huyo Rais Magufuli aliwataka viongozi wote nchini kushirikiana katika jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ili kuepusha madhara ya tatizo hilo katika uchumi na ustawi wa jamii.

Alisema mambo makubwa utawala wake unapambana nayo yanasababishwa na rushwa ambayo alisema

imesambaa kila mahali. Akitoa mfano alisema watumishi hewa chanzo ni rushwa, dawa za

kulevya ndani yake kuna masuala ya rushwa, vyeti feki ndani kuna rushwa, mikataba mibovu ndani kuna rushwa na kadhalika.

Katika makala yangu nilitoa hoja kwamba changamoto kubwa iliyokuwa inaikabili taasisi hiyo katika kupambana na ufisadi ni kukosa uhuru kamili na ari katika kuendesha vita hiyo na nilishauri kwamba ingefaa taasisi hiyo iondoke kuwa taasisi chini ya Ofisi ya Rais (Ikulu) na ijitegemee kama ilivyo katika nchi nyingine kadha – mfano Afrika ya Kusini, Pakistan, Brazil, Korea ya Kusini n.k.

Nilisema uanzishwaji wa mahakama maalum ya mafisadi ni wazo jema lakini haikuwa changamoto kubwa kuliko ile ya TAKUKURU kukosa uhuru kamili. Kwani Mahakama hiyo pia inatarajia ipelekewe kesi za wahusika wa ufisadi, na kama haipelekewi basi mambo yanakuwa yale yale.

Na hapa ninamaananisha kesi kubwa kubwa za ufisadi zinazohusu wakubwa ndani ya utawala ambazo baadhi yake zimekuwa hazifikishwi mahakamani kutokana na idadi ya kashfa zilizokuwa zinaibuliwa zikiwemo zile zilizotinga Bungeni na kutolewa maelezo kwamba wahusika washitakiwe.

Mfano mmoja ni ile kashfa kubwa ya Akaunti ya Tegeta Escrow. Nakubali kuna watu wawili wamefikishwa mahakamani, lakini kwa upande wa utawala je? Wako wapi wale waliokuwa ndani ya utawaka waliofanikisha ufisadi huo? Kuna methali ya Kiingereza isemayo “It takes two to Tango” yaani mchezo wa dansi wa aina ya Tango huchezwa na watu wawili wawili.

Kwa ujumla ufisadi unauhusisha zaidi Mhimili wa Utawala kuliko ile miwili mingine. Mifano mingi kuhusu kusambaa kwa rushwa ambayo rais Magufuli alitolea mfano ilionyeshwa hapo juu – kama vile vyeti feki, mikataba mibovu, watumishi hewa, ugawaji tata wa pembejeo n.k.  inawahusisha zaidi watendaji wa Mhimili wa Utawala (Executive Branch).

Hivyo baadhi ya kashfa kubwa za ufisadi zimekuwa hazianzii na TAKUKURU yenyewe na mara kadha umekuwa wa kutonywa na watu wengine pamoja na uwezo wake mkubwa uliopewa chini ya sheria iliyoiunda taasisi hiyo.

Tuliliona hilo katika kashfa kadha — kama ile ya Wizara ya Maliasili ya utoroshaji wa twiga, ya ufisadi katika Wizara ya Nishati na Madini iliyomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wake David Jairo, ile ya ufisadi iliyotetemesha Bunge hadi ikapelekea mawaziri kadha kuondolewa katika nafasi zao, akiwemo Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo na ile ya mabilioni ya fedha yaliyowekwa katika akaunti za vigogo katika mabenki ya Uswisi.

Kashfa zote hizi hazikugunduliwa na Takukuru, bali na taasisi au watu wengine hususan Wabunge. Kwa mfano ilishangaza kuona Mbunge tu wa kawaida akipeperusha Bungeni nyaraka (barua) iliyoonyesha ufisadi katika Wizara ya Nishati na Madini (kashfa ya Jairo). Takukuru hawakuwa na nyaraka hiyo wakati ina bajeti yake mahsusi, wakaguzi kila wilaya, na maafisa wengine na ‘manusanusa’ kila kona na katika ofisi za umma wakishindwa kuipata hati kama hiyo na kuifanyia kazi.

Isitoshe Takukuru inawezeshwa na sheria, ambayo maafisa wake wanaweza kuomba na kupewa mara moja nyaraka yoyote wanayotaka kutoka wizara na ofisi za serikali.

Tulifikiri mambo haya yote yalikuwa yanatokea katika awamu zilizopita za utawala, lakini ukweli ni kwamba yamekuwa yakiendela hadi sasa.

Wiki iliyopita taasisi hii ilitangaza kumtafuta mhasibu wake Godfrey Gugai kwa tuhuma za (hakuna haja ya kushangaa) ufisadi – tena ufisadi mkubwa. Gugai anatuhumiwa kujilimbikizia mali nyingi, yakiwemo majumba sehemu mbali mbali nchini, ambayo inadaiwa alizipata kwa njia siyo za halali.

Yumkini ilimchukua muda mrefu kwa mtuhumiwa huyo kujilimbikizia mali hizo huku akiendelea kufanya kazi taasisini hapo bila jinai yake hiyo kugundulika. Isitoshe awali hakuweza kutiwa mbaroni mara moja hadi ‘kutoweka’ kwake kulipotangazwa na kuwekewa dau la sh 10 milioni kwa yeyote atakayemkamata, hadi mwenyewe alipojitokeza na hivyo kutiwa nguvuni na kufikishwa mahakamani.

Aidha itakumbukwa kwamba miaka kadhaa iliyopita Mkurugenzi wa zamani wa TAKUKURU Edward Hosea aliwahi kujitetea mbele ya vyombo vya habari kwamba hana tatizo kiutendaji kwa taasisi hiyo kuwa Ikulu kwani wanafanya kazi kwa uhuru kabisa bila kuingiliwa na yeyote.

Lakini haikupita muda kauli hiyo ilikuja kumsuta sana mwenyewe pale mtandao wa Wikileaks ulipomnukuu yeye mwenyewe akimwambia afisa mmoja wa ngazi ya juu kutoka Ubalozi wa Marekani hapa nchini kwamba alikuwa anapata vizingiti ‘kutoka juu’ kuhusu azma yake ya kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wa ufisadi ambao ni vigogo wa serikali.

Ingawa baadaye Dk Hosea alikanusha kutamka hayo na/au kusema alinukuliwa vibaya, lakini wengi waliona alichosema kilikuwa ni kweli tupu, kutokana na hali halisi ilivyo.

Na mara kadha baada ya Takukuru kufanya uchunguzi kuhusu kesi, hasa zile dhidi ya wakubwa kinakuja kile kipindi cha kutupiana mpira kati ya taasisi hiyo na ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa serikali (DPP) ambaye ndiye hasa mwenye mamlaka kamili ya uamuzi wa mwisho iwapo kesi iende mahakamani au la.

Utupianaji huu wa mpira mara nyingi huleta tafsiri kwamba lao ni moja tu – kulinda wakubwa katika tuhuma za ufisadi.

Pamoja na kwamba taasisi hiyo imefungua ofisi za kisasa mikoani na karibu kila wilaya hapa nchini, — tena ofisi za kisasa kabisa lakini haina habari na matukio makubwa makubwa ya ufisadi yanayoendelea katika maeneo yao.

Waziri wa serikali anayekwenda kuhutubia mikutano huko wilayani huwa anapata tabu pale wananchi wanapotoa vilio vyao kuhusu ufisadi uliokithiri wa watendaji wa halmashauri yao (mkurugenzi na maafisa wengine) na kwamba wanaomba serikali iwaondoe.

Ni hivi karibuni tu Waziri Mkuu alipokuwa ziarani Mbeya alitoa agizo la kufikishwa mahakamani kwa waliokuwa maafisa wakuu wa halmashauri ya jiji hilo kutokana na ufisadi katika ujenzi wa soko jipya la Mwanjelwa.

Inakuwaje TAKUKURU haikuweza kugundua ufisadi huo mkubwa?