Home Makala Taifa Stars ianze kuandaliwe sasa

Taifa Stars ianze kuandaliwe sasa

1295
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

BADO wiki haijapita tangu makundi ya michuano ya Kombe la Afrika yapangwe lakini gumzo mitaani ni kundi walilopo timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, na hatima yao ya kufanya vizuri. 

Droo za michuano hiyo mikubwa ya soka barani Afrika ilifanyika Pyramids Giza jijini Cairo na Misri walichagua eneo hilo mahususi kuutangaza utalii wao. Hili nalo ni soma kwetu kuhusu namna tunavyoandaa michuano inayoleta watu kutoka sehemu mbalimbali nje nchi. 

Mfano mzuri ni michuano ya Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 inayoendelea katika Uwanja wa Taifa na Azam Complex jijini Dar es Salaam. Hii ni heshima kubwa ambayo nchi tumepewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). 

Michuano hiyo inayoshirikisha mataifa nane yaliyogawanywa kwa makundi mawili na kushuhudia timu zitakazotinga nusu fainali kucheza Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 baadaye mwaka huu nchini Brazil yanatazamwa na maelfu ya Waafrika. 

Kilio cha Watanzania ilikuwa ni namna wadau katika sekta hususan ya utalii wanavyotumia michuano hiyo kutangaza utalii wa nchi ukizingatia kuna mashabiki wa soka watakaopenda kutembelea vivutio vya utalii siku ambapo hamna mechi au michuano itakapokamilika. 

Tuyaache hayo ya Kombe la Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 na tuiangazie Taifa Stars iliyoweka rekodi ya kucheza Kombe la Afrika baada ya kuikosa kwa miaka 39. Taifa Stars chini ya Emmanuel Amunike wamepangwa Kundi C na majirani Kenya, Senegal na Algeria katika michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu nchini Misri. 

Katika droo hiyo iliyotizamwa na watu wengi duniani, wawakilishi kutoka Tanzania ukiacha Amunike walikuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, na Meneja wa Timu, Danny Msangi. 

Kwa mara ya kwanza Kombe la Afrika itashirikisha timu 24 huku wawakilishi kutoka Afrika Mashariki mbali na Tanzania na Kenya ni Uganda waliopangwa Kundi A inayojumuisha wenyeji Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zimbabwe huku Burundi wakitupwa Kundi B yenye Nigeria, Guinea na Madagascar. 

Droo hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka ndani na nje ya Afrika ilishuhudia burudani nzuri kutoka makundi mbalimbali na aliyeleta kombe ukumbini ni gwiji wa soka kutoka Cameroon, Rigobert Song. 

Kundi D linatabiriwa ndilo kundi gumu likihusisha Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini na Namibia wakati mabingwa watetezi, Cameroon, wapo Kundi F pamoja na Ghana, Benin na Guinea Bissau. 

Miongoni mwa wachezaji nyota katika kundi la Taifa Stars wanaokipiga soka katika Ligi Kuu England na wataitumikiwa Senegal ni Sadio Mane (Liverpool), Idrissa Gueye (Everton) na Cheikhou Kouyate (Crystal Palace) huku kutoka Algeria ni Riyad Mahrez ambaye anaichezea Manchester City na Kenya wanajivunia Victor Wanyama anayekipiga na Tottenham. 

Maandalizi ya Taifa Stars yanapaswa wawe yalianza siku ile tu walipowafunga Uganda Cranes na kufuzu kucheza Kombe la Afrika. Amunike anahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa TFF na Serikali ili Taifa Stars iende Misri kufanya maajabu. 

Ni dhahiri idadi kubwa ya wachezaji watatoka katika timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara hivyo TFF kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inapaswa kuhakikisha ligi inakamilika kwa wakati mzuri ili wachezaji wapate muda wa kupumzika na kujiunga na timu ya taifa. 

Aidha kambi inayoendana na hali ya hewa ya Misri ni muhimu ili wachezaji watakoitwa kuunda kikosi cha Stars wasipate taabu. Taifa Stars inahitaji kucheza mechi za kirafiki hususan an mataifa yaliyofuzu Kombe la Afrika kama sehemu ya wachezaji kujipima nguvu na kocha kuelewa aina ya mfumo atakayotumia.