Home Makala TAMICO; SHERIA HAZIWABANI WENYE MIGODI YA KATI

TAMICO; SHERIA HAZIWABANI WENYE MIGODI YA KATI

1191
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE


INAELEZWA kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi hasa wa migodini, wanaokabiliwa na changamoto ni wale ambao wamekuwa hawako katika vyama vya wafanyakazi, jambo linalopelekea kushindwa kupata msaada wanapopata matatizo wakiwa kazini.

Itakumbukwa hivi karibuni tumeshuhudia takribani wafanyakazi 15 wakifukiwa mgodini kwenye machimbo ya dhahabu mkoani Geita katika mgodi wa RZ Union uliopo Nyarugusu na hivyo kujikuta wakishindwa kupata msaada wa haraka kutokana na kuwapo kwa mgodi ambao hata wafanyakazi wake hawako kwenye vyama.

Unapozungumzia wafanyakazi wa migodini ni wazi kuwa lazima utahusisha Tamico ambacho ni chama cha wafanyakazi wa migodi, nishati, ujenzi na kazi nyinginezo, chama hiki kimekuwa na lengo moja tu la kulinda, kutetea na kuboresha masilahi ya wanachama wake.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Thomas Sabai, anabainisha kuwa chama hicho kinatambulika na Serikali na kimekuwa kikifanya kazi kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Sisi kama Tamico tunaamini kuwa kila mfanyakazi anastahili haki ya jasho lake, heshima na kuthaminiwa kwa utu wake, hivyo kupitia mshikamano wa dhati wa wafanyakazi, ndio ngao pekee wa kukuza umoja na uwezo wa kulinda masilahi yao kwani tunatambua kuwa wafanyakazi wote duniani ni sawa na kila mfanyakazi na ana haki ya kujiunga na chama,” anasema Sabai.

Anabainisha kuwa, suala la afya na usalama kazini kwa Tamico ni moja ya vipaumbele vyao na kwamba inasikitisha kuona kwamba Serikali inaweza ikaruhusu shughuli za uchimbaji kufanyika pasipokuzingatia kanuni na masharti ya usalama wa wafanyakazi.

“Hii ina maana kuwa Serikali ya Tanzania bado haijaridhia mkataba wa kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 176 unaohusika na afya na usalama migodini, ambao pamoja na mambo mengine unautaka mgodi kuwa na milango miwili ili hata inapotokea tatizo kwenye mlango mmoja, watu waweze kutokea kwenye mlango wa pili.

“Hivyo, kwenye kile kinachotokea kwenye mgodi kama ule wa Geita, ni migodi ambayo ni sawa na kuingia shimoni ambapo ikitokea dharura kama iliyotokea, unaweza kuona namna gani shughuli za uokoaji zilivyo ngumu lakini iwapo kungekuwa na mlango mwingine, basi madhara yasingekuwa makubwa kama hivi,” anasema Sabai.

Anafafanua kuwa hali hiyo inaonyesha kuwa kama nchi imeshindwa kuwalinda wananchi wake dhidi ya wawekezaji hususan hawa Wakichina ambao kwao suala la afya na usalama si kipaumbele, jambo ambalo linahatarisha usalama wa Watanzania na kujikuta ikipeleka kuwapo kwa walemavu na hata kupoteza maisha.

“Tangu mwaka 2004, Serikali ya haijaridhia mkataba wowote wa kimataifa; mfano kuna mkataba namba 161 unaohusiana na usalama kwa wafanyakazi wa huduma za afya, pia kuna ule wa 165 unaohusiana na usalama na afya mahala pa kazi na ule wa 102 unaohusiana na hifadhi za jamii ambayo hii yote haijaridhiwa.

“Kwa ujumla ni kwamba kwa sasa hakuna sheria zinazowabana wawekezaji hasa wa sekta ya madini, jambo ambalo linapelekea wao kufanya wanachotaka, kwa mfano mgodi kama huu wa juzi binadamu hakutakiwa kuwa mle ndani na hata kama alikuwamo hakutakiwa kwa mujibu wa haki za binadamu, naamini Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka katika kuhakikisha kuwa usalama na afya za wafanyakazi unapatikana,” anasema Sabai.

Anasema waajiri wengi kwa sasa kutoa mikataba kwa wafanyakazi imekuwa ni changamoto kwani wengi wao hawako tayari kutoa mikataba kwa wafanyakazi, jambo linalopelekea wafanyakazi hao kukosa ajira ambayo ni ya staha na stahiki zake na hivyo wengi kutokuwa kwenye vyama vya wafanyakazi.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunahamasisha wafanyakazi kujiunga kwenye vyama ambavyo ni rasmi, kwani wafanyakazi wengi wa migodi isiyotambulika wamekuwa wakishindwa kupata msaada kutakana na kutokuwa kwenye chama.

“Wamiliki wengi wa migodi wamekuwa wakifanya kazi na wafanyakazi wao bila ya kuzingatia mikataba, kwa maana kwama wanasema kuwa mtu akifanya kazi, kitakachopatikana wanagawana, jambo ambalo ni hatari,” anasema.

Anasema kama Tamico wanaomba sheria zilizopo ziwafikie wachimbaji wadogo wadogo kwani wamekosa chombo chenye kusimamia masilahi yao na hivyo kujikuta wakihangaika bila ya kuwa na mtetezi.

“Kwa sasa tumejipanga kuboresha huduma kwa wanachama wetu tulionao, ikiwamo pia kuongeza wanachama wengi zaidi ili Watanzania wengi waweze kufurahia umuhimu wa chama hiki.

“Hivyo kwa wafanyakazi wote walioko kwenye sekta ambazo chama kinahusika nazo, tuna lengo la kuhakikisha kuwa wanafikiwa na mpango huu wa kuwasajili na hivyo ili kulifanikisha hilo, tumekuwa katika harakati za kufufua na kuimarisha matawi, ambapo kila tawi la Tamico ni lazima liwe na mkataba wa haki bora hadi kufikia mwishoni mwaka huu,” anasema.

Anasema wamejipanga kuwachukulia hatua waajiri wote watakaokiuka sheria zinazohusiana na kazi kwa maeneo ambayo wapo, ikiwamo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Hatutakubali kuona haki za wanachama wetu zinapotea au kudhulumiwa na sisi tupo, hivyo tutahakikisha kuwa tunachukua hatua stahiki na madhubuti kwa ajili ya kuwapigania,” anasema.

Anasema wamejipanga katika kuhakikisha kuwa kila mmoja anawajibika kwenye nafasi yake, hii ikijumuisha watumishi na viongozi wa chama hicho kufanya kazi kwa kuheshimu katiba na kanuni za chama, ikiwamo kuzingatia maazimio yaliyowekwa ambapo atakayekiuka atachukuliwa hatua mbalimbali.

Anaongeza kuwa wao kama Tamico wamefurahishwa na hatua mbalimbali za utendaji wa Rais John Magufuli katika kipindi cha mwaka mmoja madarakani licha ya kuwapo kwa changamoto chache.

“Ni wazi kuwa kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja, rais anaenda vizuri isipokuwa kwamba kumekuwa na baadhi ya watendaji wake wa chini ambao wamekuwa wakichukua maamuzi yanayotia doa utendaji kazi wake,” anasema.