Home Habari kuu Tamu na chungu za miaka mitatu ya JPM

Tamu na chungu za miaka mitatu ya JPM

2071
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA

Novemba 5, mwaka huu Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli, itatimiza miaka mitatu  tangu kuingia madarakani rasmi, Novemba 5, 2016.

Katika kipindi hicho cha miaka mitatu kumekuwa na mambo mengi matamu na machungu yaliyojitokeza.

Miongoni mwa mambo hayo matamu na machungu ni jitihada za serikali kuboresha huduma za jamii, kama vile elimu, afya, miundombinu, maji na ongezeko la viwanda, hata hivyo yapo machungu ambayo hayaigusi serikali moja kwa moja kama vile lakini mauaji ya Kibiti yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana huku yakiwalenga zaidi maofisa wa serikali.

MATAMU

Baadhi ya mambo matamu ni Serikali kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (standard gauge) kati ya Dar es Salaam na Mwanza yenye urefu wa kilometa 1219, itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni inayokwenda kwa kasi ya zaidi ya kilometa 160 kwa saa.

Ujenzi wa mradi huo ulianza Mei mwaka jana, kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilometa 300 ikiwamo kilometa 205 huku 95 zikiwa ni njia za kupishania treni.

Ujenzi huo unajumuisha uzio na vivuko vya watembea kwa miguu na wanyama na unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh trilioni 2.6 hadi utakapomilika.

Pia mkataba wa ujenzi wa kipande cha pili cha reli hiyo kati ya Morogoro hadi Makutupora Dodoma chenye urefu wa kilometa 336, ulisainiwa mwaka jana na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza rasmi Machi mwakani na utagharimu zaida ya Sh trilioni 4.3.

Kuwezeshwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambalo ni kama lilikufa baada ya kuandamwa na mzigo mkubwa wa madeni yaliyosababisha kufutiwa uanachama katika Chama cha Usafiri wa Anga Kimataifa (IATA).

Katika kulifufua shirika hilo ndege nne zimewasili nchini zikiwamo tatu aina ya Bombardier Q 400 –Dash 8 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ndege nyingine kubwa aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262, huku ikiendelea na mpango wa kuongeza ndege hizo kufikia saba.

Katika azima ya Serikali ya kujenga nchi inayojitegemea kiuchumu imefanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato, kutoka Sh trilioni 9.9 hadi trilioni 14 kwa mwaka.

Serikali imeweza kuboresha huduma za afya kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, hususan eneo la dawa na vifaa tiba ambao imepanda kutoka Sh bilioni 30 wakati inaingia madarakani hadi bilioni 270 za sasa.

Katika kutekeleza mpango wake wa kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, Serikali inatoa Sh bilioni 23 kila mwezi ili kuwezesha mpango huo, ambao pamoja na changamoto mbalimbali umewezesha idadi kubwa ya wanafunzi kuandikishwa.

Utawala wa Dk. Magufuli umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhamishia shughuli za Serikali mkoani Dodoma jambo ambalo lilishindikana tangu wakati wa utawala wa Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda  iko baadhi ya miradi ya viwanda vikubwa  ambavyo vimejengwa na kuanza uzalishaji kama vile vya vigae vya Goodwill kilichopo Mkuranga na Twyford cha Chalinze (Pwani), kiwanda cha Juice cha Sayona, sabuni na vipodozi cha Keds, na kiwanda cha nondo cha Kilua.

Serikali imeongeza udhibiti katika sekta ya madini kamati mbalimbali zimeundwa kuchunguza mikataba ya madini ikiwamo ile iliyoundwa kuchunguza kiasi cha dhahabu kwenye makinikia, ambapo ilibaini kuwa katika makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini kulikuwa na tani saba za dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.147, na kupendekeza hatua kadhaa kuchukuliwa ikiwamo kusitisha usafirishaji wa mchanga nje ya nchi, kusimika mitambo na kusafisha makinikia hapa nchini.

Baadae kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemiah Osoro, kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kwenye makinikia pamoja na kuibua uozo uliokuwa katika mikataba ya madini, ikiwamo baadhi ya kampuni kutosajiliwa hapa nchini pia ilibaini kuwa katika makontena hayo 277 yalikuwa na madini yenye thamani ya Sh billion 829.4 kwa kutumia viwango vya wastani na sh trillioni 1.44 kwa kutumia viwango vya juu.

Serikali imejenga ukuta wenye urefu wa kilomita 24.5 na urefu wa mita tatu kwenda juu kuzunguza mgodi ya Tanzanite huko Mererani Mkoani Manyara kama hatua ya kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo.

TUMBUA TUMBUA

Katika kuhakikisha Rais anaboresha baadhi ya mambo alitengua na kutumbua watendaji wote waliokuwa wakizembea kwenye maeneo yao.

Mei 20 mwaka 2016, Rais Dk. John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Charles Kitwanga, kutokana na kitendo cha kuingia bungeni akiwa amelelwa.

Baadae June 11 mwaka huo huo alimteua alimhamisha aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo wakati huo, Mwigulu Nchemba, nafasi ambayo ameihudumia kwa muda wa miaka miwili tu kabla ya kuenguliwa na kuteuliwa aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Kangi Lugola kushika wadhifa huo huku nafasi ya Lugola ikijazwa na Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima.

Aprili 11 mwaka 2016, Dk. Magufuli alimtumbua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyaga, Anna Kilango Malecela, kwa kile alichodai kuwa alidanganya kuwa Mkoa wake haukuwa na watumishi hewa lakini baada ya kutuma watu kuchuza kwa muda wa wiki mbili walibainika kuwapo zaidi ya watumishi hewa 45.

Desemba 17 mwaka huo huo Rais Magufuli alimtumbua Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binaadamu (NIMR) Dk. Mwele Malecela kutumbuliwa.

Mei 24 mwaka jana Rais Dk, Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ikiwa umepita muda mfupi baada ya kumtaka ajitafakari na ikiwezekana ajiuzulu mwenyewe.

Dk. Magufuli alifikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya tathamini ya kiuchumi na kisheria katika sakata la makontena 277 ya mchanga wa madini yaliyozuiliwa kusafirishwa nje ya nchi.

Februari Mosi mwaka huu Dk. Magufuli alitengua uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji George Masaju na kumteua kuwa Jaji wa Mahama Kuu na Dk. Adelardus Kilangi, kuchukua nafasi hiyo.

Pia Dk. Magufuli alitengua uteuzi wa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG), Gerson Mdemu, na kumteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa masuala ya sheria wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Paul Ngwembe.

Utenguzi  wa viongozi hawa ulifanyika usiku wa saa chache baada ya Rais kulihutubia Taifa katika maadhimisho ya siku ya sheria na kueleza kutoridhishwa kwake na utendaji wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Machi 15, mwaka jana aliyekuwa  Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Uledi Mussa, uteuzi wake ulitenguliwa kutokana na kinalichodaiwa kuwa ni kutozingatiwa kwa taratibu zinazotakiwa katika kushughulikia masuala ya uwekezaji,

Machi 23, 2017  JPM alitenguea uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kumteua Dk. Harrison George Mwakyembe kushika nafasi hiyo huku  nafasi yake ya Waziri wa Katiba na Sheria ikichukuliwa na Profesa Palamagamba Kabudi.

Wizara ya Fedha na Mipango ni miongoni mwa wizara za mwanzo kutikiswa ambapo Septemba Mosi mwaka 2016,  Dk. Magufuli alimwondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Servacius Likwelile na kumteua Doto James kuchukua wadhifa huo.

Oktoba 21 2016 Dk. Magufuli alisimamisha kazi Kaimu Katibu wa Tume ya Mipango wa Wizara ya Fedha na Mipango, Florence Mwanri, aliyedaiwa kuidhinisha kuanza kwa awamu ya pili ya ujenzi wa jengo jipya la abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) (Terminal 3) kabla ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.

Rais alifikia uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya na kuagiza shughuli za ujenzi wa uwanja huo ziendelee, baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa kampuni ya BAM international inayojenga jengo hilo kutaka kusitisha shughuli zake kutokana na kutiolipwa.

Mwingine aliyekumbwa na tumbuatumbua hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga Emmanuel Mkumbo, ambaye alitumbuliwa  Oktoba 16 mwaka 2016.

Julai Mosi mwaka jana aliyekuwa Mkurugenzi Mtenaji wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mshandisi Felchesmi Mramba, aliondolewa katika nafasi hiyo, huku kuondolewa kwake kukihusishwa na taarifa ya kupanda kwa bei ya umeme iliyotangazwa na Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA).

Septemba 26 mwaka  huu aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suzan Kolimba, aliingia katika orodha ya waliotumbuliwa baada ya uteuzi wake kutenguliwa na nafasi yake kujazwa na Mbunge wa Songea Mjini, Damas Ndumbaro.

Wengine waliotumbuliwa ni Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama, Solomoni Ngiliule,  Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Mark Mwandosya, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Profesa Wakuru Magigi aliyeondolewa hivi karibuni kwa madai ya kukiuka utaratibu wa uuzaji wa zao hilo.

MACHUNGU

Baadhi ya matukio yaliyobeba uchungu katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya Tano ni pamoja na matukio ya utekaji na mashambulio dhidi ya watu maarufu wakiwamo wabunge.

Moja ya matukio hayo ni pamoja na lile la kushambuliwa kwa risasi zaidi ya thelathini Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Mengine ni kutoweka kwa aliyekuwa msaidizi wa karibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane na  Mwandishi wa Habari wa Kampuni ya Mwananchi Communication (MCL), Azory Gwanda aliyetekwa na watu wasiojulikana Novemba 21 mwaka jana wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani.

Aidha, Mei 10 mwaka huu askari wa jeshi la polisi aliyetambulika kwa jina moja la PC Ali, alitekwa kisha kupigwa na kuumizwa vibaya na watu wasiojulikana kabla ya kutupwa kwenye vichaka, mkoani Singinda.

Novemba mwaka jana mwanachama wa Chadema aliyetajwa kwa jina moja la Linus alitekwa na watu wasiojulikana waliojihami kwa silaha za moto mkoani Iringa.

Katika tukio jingine Mwenyekiti wa Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, alidai kutekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Machi 7, mwaka huu na baadae aliripotiwa kupatikana Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akiwa hajitambui.

Hata hivyo, taarifa za kutekwa kwake ziligubikwa na utata baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, kudai kuwa Nondo hakutekwa bali alijiteka mwenyewe na kwamba alikwenda mkoani humo kwa mpenzi wake.

Miongoni mwa matukio machungu ni la kutekwa kwa mfanyabiashara na bilionea kijana, Mohamed Dewji ambaye alikuja kupatikana siku tisa baadae.

HAMA HAMA

Pia katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya JPM madarakani imeshuhudia takruibani wabunge tisa wa vyama vya upinzani wakivihama vyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile walichodai kuwa ni kuunga mkono juhudi za Dk. Magufuli.

Wabunge waliofanya hivyo ni Maulid Mtulia na Zubery Kuchauka (CUF) Godwin Ole Mollel, Mwita Waitara, James Ole Milya,  Pauline Gekul ,  Marwa Ryoba, Juliasi Kalanga na Joseph Mkundi (wote Chadema)

na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM Lazaro Nyalandu ambaye alikwenda Chadema.