Home KIMATAIFA Tanzania ijifunze hili kwa mashtaka ya Trump

Tanzania ijifunze hili kwa mashtaka ya Trump

293
0
SHARE

Andrew Msechu

JUMATANO ya Februari 5 mwaka huu, Bunge la Seneti lilihitimisha mchakato wa karibu wa miezi mitano kwa kumwondolea rasmi mashtaka ya kutokuwa na imani naye, Rais Donald Trump, baada ya waliokuwa wakimtuhumu kushindwa kupata idadi ya kura zilizohitajika kumwondoa madarakani.

Mchakato huo uliokuwa ukifuatiliwa kwa karibu katika nchi nyingi duniani, ulimalizika kwa kuondoa mashtaka hayo, baada ya kura 52 za wabunge wa chama tawala cha Republican katika Baraza la Seneti kuzipiku kura 48 za wajumbe wa chama cha Democrats, walioungwa mkono na Mitt Romney kutoka Republican kumpinga Trump kushindwa kufikia idadi ya kura iliyotakiwa.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa anasema kura ya kutokuwa na imani na rais hapa nchini pia ipo lakini si rahisi namna hiyo, kwa kuwa inapotakiwa kutekelezwa atashambuliwa zaidi waziri mkuu na huwa rais haguswi moja kwa moja.

“Kwa hiyo wao wana utaratibu ambao ni mzuri tofauti na wa kwetu, cha kujua hapa ni kwamba wao wanakwenda moja kwa moja na cha kujifunza ni kwamba hawa watu vifungu vizito namna hiyo wanavitumia.

“Kwa hiyo na sisi kama kuna chochote kizito kinachogusa mamlaka ya Rais tujifunze kwamba hatupaswi kumwogopa kwa sababu yeye ni mtumishi kama watumishi wengine, ingawa yeye ana mamlaka kubwa.

“Lakini akifanya kinyume, ambacho ni kinyume na Katiba na Sheria, Bunge lifanye kazi yake, ndiyo maana ya check and balance (mihimili kusimamiana), ndiyo maana ya kuwa na mihimili mitatu tofauti,”anasema.

Anasema kwa Wamarekani, wao wamefanya hicho kwamba kuna taasisi ya urais huku kuna Bunge ambalo linaweza kumshughulikia Rais na kwamba ingawa hiyo ni nzuri na nchi inaihitaji endapo Rais anakengeuka, lakini kama vile Rais anavyoweza kukengeuka, hata anayesimamia chombo kingine cha maamuzi anaweza akakengeuka vile vile.

“Kwa hiyo cha kujifunza ni kwamba huo unaweza kuwa utaratibu ambao ni strong (imara), ambao wanautumia lakini tujifunze pia kuwa huo utaratibu sio wa ku-abuse (kuutumia vibaya), lazima utumike kwa haki. Usipoutumia kwa haki unaweza kuumiza mtu ambaye hahusiki.

“Na ingawa ni utaratibu mzuri utaona kwamba una ugumu wake, lazima upite ngazi ya kwanza, uende ngazi nyingine na ngazi nyingine na kama ngazi zote zikifanana basi hapo inakuwa hamna namna isipokuwa kumuondoa Rais,” anasema.

UJASIRI WA ROMNEY

Dk. Kahangwa anasema jambo jingine muhimu ni kwamba wamefanya maamuzi ki-vyama na huo ni ukweli kuwa kwa Taifa ambalo limestaarabika, maamuzi yalitakiwa yasimamie ukweli na hicho ndicho, kinachoweza kuonekana kwamba hata katika nchi zetu kuna tatizo kama hilo.