Home Makala TANZANIA INA MAZINGIRA BORA YA  SOKO LA  SIMU

TANZANIA INA MAZINGIRA BORA YA  SOKO LA  SIMU

1427
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE


RIPOTI zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa manane barani Afrika, ambayo yana soko kubwa la simu za mkononi.

Hivi karibuni kulizinduliwa ripoti iliyopewa jina la ‘Uchumi wa simu za mkononi Afrika 2016,’ uzinduzi ambao ulihusisha mkutano wa siku tatu uliopewa jina la ‘2016 Mobile 360 Series – Africa’ ukihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano na pia kuhusisha  nchi za Ethiopia na Nigeria ambazo kwa pamoja zimekuwa zikijinyakulia zaidi ya theluthi ya soko la mawasiliano Afrika.

Kwa mujibu wa utafiti wa Umoja wa wadau wa Mawasiliano ya simu za mikononi Duniani GSMA,   kwa sasa  takribani zaidi ya  watu nusu bilioni barani Afrika wanatumia huduma za simu za mkononi, huku kukiwa na uwiano huo huo kwa watumiaji wa intaneti,  mawasilino yanayoshika nafasi kwa sasa.

Mbali na tafiti za mawasiliano, pia ripoti hiyo imebainisha faida ambazo zimechangiwa na uwepo wa huduma hizo za mawasiliano hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

Faida nyingine ambazo ripoti hiyo imebaini ni pamoja na kurahisha mawasiliano na kukuza uchumi, ikiwemo ajira, ufadhili kwa umma (Public Funding) pamoja na ukuaji wa digitali na ushirikishwaji wa kifedha.

“Ni wazi kuwa zaidi ya Waafrika nusu bilioni kwa sasa wamejiunga na huduma ya simu za mikononi, hatua ambayo si tu inawaunganisha bali pia inatoa fursa kwao kuweza kupata huduma nyingine kama vile huduma za afya, utambuzi wa kidigitali na huduma za kifedha,’’ anabainisha Mats Granryad, Mkurugenzi Mkuu wa GSMA.

Ni wazi kuwa nguvu kubwa inayowekezwa kwenye eneo la mtandao (Network) na simu za kisasa (Smartphones) kunachochea uhamiaji zaidi kwenda kwenye matumizi ya intaneti ya simu.

Miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa na masoko makubwa ya simu Afrika ni pamoja na Misri, Nigeria na Afrika Kusini  ambazo zote zimekuwa zikichukua zaidi ya theluthi moja ya jumla ya watumiaji wote barani Afrika idadi ambayo inategemewa kupaa mpaka milioni 725 mwaka 2020 sawa na asilimi 54.

Inatajwa kuwa matumizi ya teknolojia za simu na huduma zake kote Afrika kulizalisha dola bilioni 153 kwenye uchumi mwaka jana, sawa na asilimia 6.7 ya mapato ya nchi za bara la Afrika.

Mchango huo unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia dola bilioni  214 ifikapo 2020. Asilimia 7.6 ya mapato ya nchi (GDP) yanayotarajiwa, wakati mataifa ya Afrika yakiendelea kunufaika kutokana na ongezeko la uzalishaji na ufanisi ulioletwa na kushamiri kwa huduma za simu.

Ni wazi kuwa simu za mkononi zimekuwa mstari wa mbele katika kuchochea ubunifu wa kwenye ujasiriamali Afrika.

Kushamiri kwa bidhaa za simu nchini Tanzania, kunatajwa kuchangiwa moja kwa moja na kuwapo kwa soko kubwa la bidhaa hiyo japo linatajwa kutetereka katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, kama wanavyobainisha wawakilishi wa makampuni makubwa duniani ambayo yamekuwa yakijishuhgulisha na utengenezaji simu hapa nchini.

Meneja wa Huawei nchini Tanzania,  Hu Xiangyang Jacko, anasema kuwa licha ya kwamba mwaka huu haukuwa wa kibiashara kwenye bidhaa za simu,  anakiri kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimekuwa na soko kubwa la bidhaa za simu, jambo ambalo linawafanya kufikiria kuwekeza zaidi hapa nchini ikilinganisha na maeneo mengine.

“Ni wazi kuwa kwa mwaka huu, biashara ya simu ilishuka kwa kiwango cha juu jambo ambalo lilichangiwa  na watu kutokuwa na fedha, hata hivyo kama Huawei hatujaathirika sana na hili kwani tumekuwa nafasi ya tatu sokoni kwa mujibu wa ripoti mbalimbali.

“Hivyo utaona kuwa kwa mwaka huu soko limeyumba kwa asilimia 30 hadi 40,  jambo ambalo linatulazimu kuwaambia mawakala wetu kuwa na idadi ndogo ya bidhaa ikilinganishwa na hali, kwani siyo Huawei pekee iliyoanguka bali ni karibu makampuni yote yamepitia kwenye dhoruba hii, lakini hata hivyo hisa zetu zimepanda kutoka asilimia 19 mwaka jana mpaka 23 mwaka huu hivyo hatujatikisika sana,” anasema Jacko.

Jacko anaweka wazi kuwa kusuasua huko kwa soko hakujawakatisha tamaa ya kuendelea kuwekeza hapa nchini, kwani kumekuwa na mazingira rafiki ya kufanyia biashara ikilinganishwa na maeneo mengine.

“Licha ya kwamba kwa mwaka huu soko la Tanzania ndilo pekee kwa Afrika Mashariki limeonekana kutetereka, ni ukweli usiopingika kuwa hapa nchini kumekuwa na mazingira mazuri zaidi ya kufanya biashara kuliko nchi nyingine na hivyo kutufanya tufikirie kujiimarisha zaidi.

“Ndiyo maana kwa kuona umuhimu wa kuitumia Tanzania kibiashara tumeanza kushirikiana na serikali kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya Tehama, Teknolojia, Afya, Kilimo, kufadhili wanafunzi na mambo mengine, lengo likiwa ni  kusaidiana katika maendeleo ya jamii yetu na serikali kwa ujumla kupitia kile tunachokipata,” anasema Jacko.

Inaelezwa kuwa awali Serikali ilikuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na kukosekana kwa udhibiti wa wafanyabiashara wasio waaminifu, ambao walikuwa wakiutumia mwanya huo kuingiza simu bila kulipia ushuru.

Hatua hiyo ilionekana kuyaumiza makampuni yanayohusika na kuingiza simu kwa njia za halali kama anavyobainisha, Aqil Kurji ambaye ni Afisa mauzo wa kampuni ya Elite inayouza bidhaa za Apple zikiwamo simu za iPhone nchini.

“Kweli kuna wafanyabiashara wadogo wadogo wanaoleta simu mkononi, kutoka Dubai, China, UK na USA jambo ambalo linaharibu soko la simu kwa kuwa hawatozwi ushuru ndiyo maana hata risiti pindi mtu anaponunua bidhaa zao hawatoi kwani biashara zao siyo halali.

“Na hii inatokana na urahisi wa tiketi za ndege kwenda Dubai ambapo mtu akiwa na dola 500 anaenda na kujaza begi simu za kutosha kisha analeta,” alisema Kurji.

Hata hivyo, Kurji aliitaka serikali kuweka mkazo kwenye njia hizo zote jambo ambalo huenda likawa limedhibitiwa kabisa kwani ndiyo iliyokuwa njia ya kuingiza simu feki zilizozimwa hivi karibuni.

Simu hizo za njia ya panya zilikuwa zikipitishwa kwa njia mbalimbali zikiwamo zile za maeneo ya mipakani kama njia kuu ya kuingiza simu ambayo haya yanahusisha viwanja vya ndege vya Mwl. Julias Nyerere kwa Dar es Salaam na Kilimanjaro(KIA) kwa Kaskazini na kubaini namna ubebaji huo unavyofanyika.

“Wafanyabiashara wa simu hubeba mizigo kama abiria wa kawaida (simu 100 mpaka 200), inamaana hulipia mzigo wa ziada kwa shirika la ndege husika, wakifika Airport za Tanzania hulipishwa kwa kukadiliwa uzito wa mzigo bila kuangalia thamani ya mzigo husika zoezi hilo huwa rahisi zaidi kwao kutokana kwamba simu hutolewa kwenye boksi lake, chaja pia huwekwa pembeni-

“Kwa namna hii TRA wakiambiwa ni simu za kutoka China hutoa kadirio la kodi, huku wakiwa wamebeba simu za kisasa za SmartPhone kutoka Dubai, HongKong na Guanzou za bei ya juu ambazo ushuru wake ulistahili kuwa mkubwa, na hii ndiyo imekuwa njia inayotumiwa na wafanyabiashara wanaouza simu za Smartphone kwenye maeneo ya Samora, Kariakoo, Mwanza na Arusha ambao huingiza mzigo kila wiki,” kilibainisha chanzo hicho.