Home Habari TANZANIA MPYA YASHIKA KASI

TANZANIA MPYA YASHIKA KASI

1288
0
SHARE
Na JOHANES RESPICHIUS  |  

RAIS Dk John Magufuli tayari ameshazindua awamu ya pili ya ujenzi wa Reli ya kisasa ya  umbali wa kilometa 336, itakayokuwa na uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa.

Uzinduzi wa ujenzi wa reli hiyo, ulifanyika jana katika Stesheni ya Ihumwa mkoani Dodoma hatua inayoashiria kasi ya ujio wa Tanzania mpya.

Ujenzi wa reli hiyo ya kisasa unakadiriwa kugharimu dola za Marekani bilioni 1.923 sawa na Sh trilioni 4.3.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi wa Reli ya Kisasa kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Maizo Mgedzi, alisema kuwa reli hiyo itajengwa usiku na mchana ili kuhakikisha inakamilika katika kipindi cha miaka mitatu.

Alisema kupitia mradi wa ujenzi wa reli hiyo, zitapatikana ajira za moja kwa moja  kwa wafanyakazi takribani 4,000 wakiwamo wafanyakazi 3,000 sawa na asilimia 80 kutoka maeneo ambayo reli hiyo itapita na wageni 1,000 ambao watakuwa ni asilimia 20.

“Pamoja na kupatikana kwa fursa za ajira lakini pia Kampuni ya Yapi Markezi ya Uturuki ambayo ndiyo yenye kandarasi ya kujenga reli hiyo itasaidia na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kama kujenga barabara, shule, zahanati na miundombinu ambayo itaendesha reli hiyo,” alisema Mgedzi.

Kukamilika kwa reli hiyo ya mwendo kasi kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barani Afrika nyuma ya Morocco ambayo tayari ina kilometa 1,300 zilizounganishwa kwa reli ya Standard Gauge, yenye uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 320 kwa saa.

Huku Nigeria, Afrika Kusini na Ethiopia zikiwa na reli za kiwango cha Standard Gauge zenye uwezo wa mwendokasi wa kilometa 120 kwa saa.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 1964 Serikali ya Japani kupitia Kampuni ya Japan Railways Group Ilitengeneza reli za mwendokasi wa kilometa 442.57 kwa saa na mwaka 1992 Ufaransa kulikuwa na reli yenye mwendokasi wa kilometa 379.8 kwa saa.

Mwaka 2003 katika mji wa Shanghai, nchini China kulikuwa na reli ya mwendokasi wa kilometa 500.5 kwa saa ambapo 2010 nchi hiyo ilianza kutumia reli nyingine ya mwendokasi wa kilometa 486 kwa saa.