Home Makala Tanzania ya Magufuli inaweza kuifikia Rwanda

Tanzania ya Magufuli inaweza kuifikia Rwanda

887
0
SHARE

NA FRANKLIN VICTOR

HOTUBA ya Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa ndege mbili mpya za Shirika la Ndege Tanzania – ATCL aina ya Bombardier Dash 8 – Q 400 NextGen Septemba 28 mwaka huu ilinifurahisha kwa kubeba kauli ya msisitizo kwamba nchi hii (yaani Tanzania) ni tajiri.

Nikupongeze Rais Magufuli kwa kuuona na kuukiri utajiri wa nchi ambao kwa kipindi cha kutosha umekuwa ukifujwa na kufubazwa kupitia ulafi wa watu wachache wabinafsi, wafitini, warasimu na wapenda uheshimiwa pasi kuufanyia kazi. Rais mwenyewe anajua namna nchi ilivyokuwa imefikishwa pabaya.

Naendelea kumuelewa Rais Magufuli kuwa si wa mazoea na mchezo mchezo tu; akisema hataki uzembe wa kimazoea unaomkwamisha kuharakisha maeneleo anamaanisha. Agizo la kuwataka viongozi wote wa umma walioalikwa na kulipwa posho ili kuhudhuria tamatisho la mbio za Mwenge wa uhuru uliozimwa Ijumaa Oktoba 14, 2016 (Nyerere Day) wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu kutohudhuria na kubaki katika vituo vyao vya kazi ni mojawapo kati ya maamuzi mengi ya msingi na manufaa yanayofanyika.

Ikiwa imetimu miaka 17 tangu afariki Babu ambaye kwa Tanzania ni Baba wa Taifa wa kujivunia Hayati Julius Nyerere, mabadiliko mengi yaliyoonwa ndoto yanaelekea kutimia yakifanywa na rais Magufuli, mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kilichoasisiwa naye baba wa taifa.

Kazi aliyoifanya baba wa taifa ilibadilisha nchi kwa wakati wake, kipindi cha kudai na kupata uhuru, wakati wa siasa za ujamaa na kujitegemea. Kazi anayolazimika kuifanya rais Magufuli yapasa ilete mabadiliko yanayotarajiwa ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano bila kujilazimisha kurejea ama kurejesha yaliyopita.

Dk. Magufuli mwenyewe anakiri dunia imebadilika, mazingira yamebadilika na watu wamebadilika. Mabadiliko haya si maneno pekee, yalazimu kuakisiwa katika kiwango cha ufikiri, maendeleo na matakwa ya watu hawa wa sasa, wengi tukiwa vijana.

Si dhambi kuyaacha mambo ya zamani kwa amani ili kwenda murua na fikra mpya za sasa, malengo mapya, mipango mipya, mambo mapya yanayokidhi usasa. Si kosa kuliacha lilivyo Azimio la Arusha au lile la Zanzibar na kuzipa wasaa fikra mpya kuenea kwa uhuru kama zilivyoenea fikra za vipindi vilivyopita ambazo zilikidhi kwa usahihi wake nyakati husika.

Siasa na sera kivitendo za ujamaa na kujitegemea za serikali ya baba wa taifa zilifaa zaidi enzi zake kuliko ambavyo zingeweza kufaa hata kama zingetumika katika kipindi hiki chenye utofauti mkubwa kwenye kila Nyanja nchini na kimataifa.

Hayati Nyerere, licha ya mengi mengineyo, alikuwa na dhana ya kufikirisha juu ya upatikanaji wa maendeleo; akitaja umuhimu wa kuwa na watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Nchi nyingi za Afrika zinakwama kuendelea kwa kukosa siasa safi na uongozi bora. Tanzania kama zilivyo nchi nyenza 53 ziundazo Umoja wa Afrika – AU ina utajiri mkubwa wa ardhi yenye neema nyingi; na watu (Watanzania) wa kutosha wenye ukarimu, amani na utulivu. Hata vikwamishi vya maendeleo; yaani kutokuwepo siasa safi na uongozi bora, havijakithiri Tanzania.

Siasa safi kwa maana ya demokrasia huru, kati ya mengineyo, si haba Tanzania ukilinganisha na nchi nyingi nyingine za Kiafrika. Uongozi bora kwa maana ya uwajibikaji unaofuata msingi wa Katiba na sheria zisizo kandamizi za nchi, uendeshaji nchi unaoridhiwa na waongozwa, viongozi wanaojali utu wa watu wao kati ya mengineyo kwa dalili zilizopo unarejea mahali pake. Hivyo hakuna sababu kubwa inayofanya nchi ishindwe kuendelea, ichelewe kufanikiwa.

Ndani ya mwaka mmoja ikulu, Rais Magufuli amejitahidi kuidhihirisha azma yake ya kuyafikia mabadiliko aliyoahidi wakati wa kampeni zake. Nia ya rais kuwa na Tanzania ya viwanda haijatetereka. Hatua za serikali hii ya awamu ya tano zinanikumbusha moja ya Makala nilizowahi kuandika juu ya mbuga zilizokuwa zikichanjwa na Jenerali Paul Kagame, Rais wa Rwanda kuyaelekea mafanikio hasa ya kiuchumi.

Rwanda ya enzi Rais Kagame akiingia ikulu na Rwanda iliyofikiwa sasa kuna hatua kubwa sana zimetembewa. Mafanikio yanayofikiwa na Wanyarwanda si ya kubeza, hayakuzuka tu kwa bahati mbaya bali mipango ilisukwa na bado inasukwa, ubunifu unachochewa, kazi inafanyika na malengo yanafikiwa.

Kwa mfano; shirika la ndege la Rwanda la sasa limefika mbali sana kimafanikio hivyo kuchangia vilivyo maendeleo mapana ya nchi tangu serikali ya Kagame ifanye maamuzi magumu kuhusu RwandAir. Umaarufu wa RwandAir kutokana na uwekezaji wa kimalengo, huduma zitolewazo, weledi wa watendaji, kujitangaza vilivyo na kujitanua kwake kitaifa na kimataifa unaongezeka. Wateja wanavutika, biashara inafanyika kitaifa na kimataifa.

RwandAir iko pazuri ikiwa na umiliki wa ndege za kisasa kama Airbus A330 – 200, na 300; Boeing 737 – 700, na 800; Bombardier CRJ 900 NextGen, na Bombardier Dash 8 – Q400 NextGen kama za ATCL.

Kama rais Kagame kaweza kuipaisha Rwanda iliyokumbwa na janga la mauaji ya kimbari, kwa nini rais Magufuli mwenye nchi tajiri, kubwa, tulivu na iliyo katika eneo zuri kimipango asiweze kuipaisha Tanzania tena maradufu ya kasi na mpao vilivyotumiwa na Rwanda?

Najiaminisha kwa kasi hii ya Rais Magufuli asiyetania pale anaposisitiza ulazima wa nchi kubadilika na kuwa bora istahilivyo, Rwanda itasogelewa punde si punde.

Kwa utendaji usioendekeza urasimu, usiolea mazoea ya kiutendaji, unaotekeleza miradi kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha, sina shaka hatua za kufika walikofika Wanyarwanda ziko pazuri.

Kwa ufuatiliaji wake Rais Magufuli, makamu wa rais na waziri mkuu baada ya kauli au maagizo kutolewa; mafanikio ya rais Kagame, serikali yake na Wanyarwanda yanaweza kufikiwa mapema zaidi na Tanzania hii ya Magufuli.

Hatua za kuipa uhai ATCL na kuichangamsha ijiendeshe kwa faida na kishindani ni moja ya mipango muafaka itakayochochea maendeleo ya haraka ya Tanzania ya viwanda, na kuifikia kama si kuipiku Rwanda yake rais Kagame.

Kwa namna mfumo wa Kikatiba na kisheria wa uendeshaji nchi ulivyo, rais mtendaji na mthubutu kama alivyo Dk. Magufuli anaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kihistoria Tanzania hasa katika sekta muhimu ya uchumi wa taifa. Muda utaamua.