Home Tukumbushane TATIZO LA TAKUKURU NI KUKOSA UHURU

TATIZO LA TAKUKURU NI KUKOSA UHURU

2461
0
SHARE

NA HILAL K. SUED


Mapema mwezi huu (Septemba) Rais John Magufuli alimteua Kamishna wa Polisi Diwani Athumani kuwa

Mkurugenzi Mkuu mpya wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akichukua nafasi ya Valentino Mlowola ambaye ameteuliwa kuwa balozi.

Ni uteuzi wa pili wa Rais Magufuli wa mkuu wa taasisi hiyo nyeti nchini katika kipindi kisichozidi miaka mitatu – kwa maneno mengine Takukuru imeendeshwa na wakurugenzi wakuu watatu tofauti tangu rais huyo aingie madarakani.

Akizungumza baada ya kumuapisha Diwani Ikulu ya Dodoma Rais Magufuli alitoa sababu kwa nini amemuondoa Mlowola – kwamba alishindwa  ‘kuisafisha’ taasisi hiyo kutokana na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watendaji wake, kushindwa kuongeza kasi ya kushughulikia rushwa nchini na kushindwa kuhakikisha kuwa watu wanaokabiliwa na tuhuma wanafikishwa mahakamani.

Hakuwataja kwa majina ni watuhumiwa gani hao wa ufisadi walioshindikana kufikishwa mahakamani lakini kutokana na hotuba zake katika hafla mbali akizungumzia ufisadi uliojitokeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi na nyinginezo kama vile sekta ya uchimbaji madini, na tukio la suala la Akaunti ya Tegeta Escrow aligusia kuna watu waliotakiwa kufikishwa mahakamani,

Maagizo haya ni kama marudio tu ya yale aliyoyatoa kwa mtangulizi wake Valentino Mlowola alipomteua Desemba 2015 na ni kielelezo tosha kwamba  mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi hapa nchini ni zaidi ya ubora/umahiri wa watendaji wananaoiongoza Takukuru. Ukweli ni kwamba mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi hayataweza kuwapo kwa sababu taasisi hiyo imekuwa ikikosa ‘uhuru.’

Huwezi, kwa mfano, kulinganisha ‘uhuru’ wa Takukuru na taasisi za nchi nyingine kama vile Pakistan, Brazil, Korea ya Kusini, Afrika ya Kusini na hata jirani zetu Kenya. Lakini pengine tatizo hapa kwetu limetokana na ‘makosa’ ya kihistoria, ingawa wakati ule huenda yalifanyika kwa nia njema. Nitaeleza.

Ufisadi na changamoto za kupambana na kansa hiyo hapa nchini vilianza tangu wakati wa utawala wa Awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya 70.

Mwaka 1971 serikali ilipitisha Sheria ya Kuzuia Rushwa (Anti Corruption Act, 1971) lakini sheria hii ilikuja kuanza kutumika miaka mitano baadaye – mwaka 1976 baada ya kuundwa kwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa – Anti Corruption Squad (ACS). Haikueleweka kwa nini ilichukua muda mrefu hivyo kuanza kutumika.

Hata hivyo ingawa sheria hiyo ilikuwa kali na yenye meno, lakini haikuuma sana – kwa maana kwamba haikuwahi kuibua kesi iliyotikisa nchi – sana sana ilikuwa inakimbizana na ‘vidagaa’ tu vya rushwa kama ilivyo tu katika miongo ya sasa.

Mfano mmoja wa ukali wa meno wa sheria ile ni pale ambapo mtumishi wa umma anayetuhumiwa kumiliki mali nyingi yeye ndiye alikuwa na jukumu la kuieleza mahakama uhalali wa kumiliki mali hizo, huku ikitiliwa maanani kipato chake halali akiwa mtumishi wa umma.

Mwishoni mwa miaka ya 70 Kikosi hicho kilihamishwa kutoka Jeshi la Polisi kilichokuwa kama moja ya taasisi chini yake na kupelekwa kuwa chini ya ofisi ya Rais. Nadhani makosa yalianzia hapo.

Hatua hii ilisababisha watu kuinua kope zao na kuibua maswali na kuhoji lengo lilikuwa nini hasa, huku wachunguzi wa mambo wakiona kwamba ni njia ya kuinyima taasisi hiyo uhuru – hasa kutokana na ukweli kwamba mafisadi wakubwa wako katika Mhimili wa Utawala (Executive Branch) ambayo kiongozi wake ni rais wa nchi.

Lakini wengi hawakuamini iwapo Nyerere alikuwa ana nia ya kuwalinda mafisadi, bali mafisadi ndiyo walianza kuwa werevu mno katika kuvinyamazisha vyombo dola husika, hususan Kikosi cha Kuzuia Rushwa chenyewe, polisi na Idara ya Mahakama kwa kutoa milungula kwa watendaji wao.

Ilidaiwa kwamba iwapo wakati ule kulikuwa mtuhumiwa wa ufisadi ambaye alionekana ana uwezo mkubwa wa kifedha, basi Nyerere alikuwa anaomba ushauri wa Mwanasheria Mkuu iwapo serikali inaweza kushinda kesi hiyo kama itapelekwa mahakamani. Na baada ya uchunguzi na iwapo Mwanasheria Mkuu atasema kuna uwezekano serikali kushindwa kesi, basi Nyerere humweka mtuhumiwa huyo kizuizini kwa kutumia Sheria ya Kuweka watu Kizuizini (Preventive Detention Act).

Aidha inasemekana changamoto kama hizi dhidi ya kupambana na ufisadi kipindi kile ndizo zilimsukuma Mwalimu Nyerere, mapema miaka ya 80, kuanzisha, kwa kupitia sheria ya Bunge, mahakama maalum ya wahujumu uchumi, nje ya mfumo wa mahakama rasmi uliokuwapo Kikatiba.

Hata hivyo alikumbana na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa tasnia ya sheria, wakiwemo majaji, wanasheria, makundi mbali mbali ya wanaharakati wa haki za binadamu kutoka ndani na nje ya nchi – hasa pale sheria hiyo ilipopitishwa baada ya watuhumiwa kutiwa mbaroni sehemu mbali mbali nchini.

Na hata taasisi iliyorithi ACS katika miaka ya 90 – yaani TAKUKURU – ilibakia kuwa chini ya Ofisi ya rais – hadi leo hii, hali ambayo bado imekuwa ikiibua manung’uniko hayo hayo ya kukosa uhuru kamili pamoja na kuwepo kwa sheria mpya iliyopitishwa mwaka 2007.

Na hiki ni kitu kimekuwa kinajionyesha wazi kabisa hasa kutokana na kuongezeka kwa matukio ya tuhuma ya ufisadi dhidi ya maafisa wakuu wa Utawala na kwa TAKUKURU kuonekana iko katika likizo ndefu isiyoisha.

Kwa maoni yangu tatizo kubwa la taasisi hii si kukosa meno, au kukosa mahakama maalum ya mafisadi, bali ni kukosa uhuru. Namshauri Rais John Magufuli aliangalie suala hili na kuiondoa kutoka Ikulu na kuwa taasisi ya kujitegemea isiingiliwe na chombo chochote kile.

Lakini hili ni shughuli kubwa kuibadilisha kwani uteuzi wa mkuu wa taasisi hiyo na maafisa wengine usifanyike na mtu mmoja (rais wa nchi) kama ilivyo sasa, bali nyadhifa hizo ziwe za kuombwa na uwepo mchakato maalum wa kusaili waombaji kupitia tume maalum pamoja na kamati za bunge na hatimaye rais hupewa jina tu kutangaza, kama vile ilivyo kwa Kenya. Bila ya hivyo tutaendelea kuzilea changamoto zile zile.

Kusema kweli majukumu ya taasisi hii huwa yananichanganya sana, hasa katika mwenendo wake ule wa “kutenda” na “kutotenda” (acts of commission and omission).

Tukiachia mbali ule udhaifu wake unaoeleweka na uliowahi kuanikwa kwa shukrani ya mtandao wa Wikilileaks – wa kushindwa kuwafikisha vigogo wa ufisadi mahakamani (“kutotenda”), kuna hili la taasisi hiyo muhimu mara kadha kukubali kutumiwa katika malengo ya kisiasa (“kutenda”).

 

Mara kadha chama tawala – CCM – kimekuwa kikitumia chombo hiki katika kuwekana sawa katika safu zake za uongozi hasa wakati wa chaguzi zake za ndani. Mfano ni chaguzi za ndani katika chama hicho mwaka 2007 mkoani Arusha na pia katika chaguzi za kuteua wagombea ubunge Tabora, Iringa na kwingineko mwaka 2010). Kadhalika katika chaguzi za ndani za chama hicho mwaka 2012. Lakini Takukuru imekuwa haijishughulishi na chaguzi za ndani kwa vyama vya upinzani.

Kwa ujumla changamoto kama hizi zipo katika nchi mbali mbali Barani Afrika ingawa kumetokea wakuu wa taasisi kadha za kupambana na ufisadi, ambao tunaweza kusema walikuwa mashujaa wa vita dhidi ya ufisadi katika nchi zao.

Hawa ni John Githongo wa Kenya na Nuhu Ribadu wa Nigeria. Wawili hawa wsalilazimika  kuzikimbia nchi zao kutokana na mikwara na vitisho kutoka kwa viongozi wakuu pamoja na watawala waliokuwa chini ya chunguzi zao na wao kukuosa kulindwa na serikali.

Taasisi yetu iliyopewa kazi hiyo – TAKUKURU – nikisema kwamba imekwenda likizo ndefu pengine itakuwa nimesema kidogo. Pamoja na kwamba taasisi hiyo hujigamba kuwa karibu kila wilaya hapa nchini katika ofisi za kisasa lakini haina habari na ufisadi unaoendelea katika maeneo yao – kama vile alivyosema Rais Magufuli kuhusu ufisadi katika Mkoa wa Mara.

Huwa siachi kujiuliza: Hivi maafisa wa TAKUKURU katika wilaya hizo wanafanya kazi gani hasa? Tuache huko wilayani na turudi Dar es Salaam ambayo ni makao makuu ya TAKUKURU.

Miaka mitatu iliyopita kabla ya ujio wa kimbiza-kimbiza ya rais John Pombe Magufuli, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aligundua madudu yasiyosemeka katika Mamlaka ya Bandari (PTA), wizi na ufisadi wa kutisha hadi kupelekea maafisa wengine kusimamishwa na baadaye kufukuzwa kazi. Huyo ni mtu mmoja tu aliyefanya kazi hiyo kubwa.

TAKUKURU walikuwa wapi? Si hapa hapa Dar es Salaam? Bado mnabisha hawakuwa likizo ndefu? Itashangaza kusikia kwamba taasisi kubwa kama hiyo hawana watu wanaowabonyeza (informers) kuhusu madudu yanayoendelea kule bandarini.